Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aapishwa

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameapishwa kwa muhula wa pili huku kukiwa na ulinzi mkali, kufuatia uchaguzi uliokumbwa na maandamano yenye ghasia na kukataliwa na upinzani kuwa sio huru na wa haki.
Suluhu, mwenye umri wa miaka 65, alikula kiapo chake mbele ya Jaji Mkuu Ibrahim Hamis Juma, akiahidi "kulinda na kutetea Katiba na umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."
Sherehe ya kuapishwa kwake imefanyika katika uwanja wa kijeshi katika mji mkuu wa Dodoma katika hafla iliyofungwa kwa umma lakini iliorushwa hewani moja kwa moja na kituo cha serikali cha TBC.
Samia alitangazwa mshindi Jumamosi kwa asilimia 98 ya kura. Alikabiliwa na upinzani mdogo huku wagombea wakuu waliokuwa wakishindana naye wakifungiwa au kuzuiwa kugombea.
Mtandao ulisalia kuzimwa nchi nzima wakati rais huyo alipokuwa akila kiapo, huku vikosi vya usalama vikitumwa katika miji muhimu kuimarisha usalama.
Waangalizi wa kimataifa wameibua wasiwasi kuhusu uwazi wa uchaguzi huo na madhara yake ya kukumbwa na ghasia, huku mamia ya watu wakiripotiwa kuuawa na kujeruhiwa.
Mamlaka imejaribu kupuuza ukubwa wa ghasia na vilevile imekuwa vigumu kupata habari kutoka nchini humo au kuthibitisha idadi ya watu waliofariki, baada ya mtandao kuzimwa kote nchini tangu siku ya uchaguzi.
Katika hotuba yake ya ushindi, Samia alisema uchaguzi ulikuwa "huru na wa kidemokrasia" na kuwaelezea waandamanaji kama raia "wasio na uzalendo".

Viongozi wa upinzani na wanaharakati wanasema mamia waliuawa katika mapigano na vikosi vya usalama.
Chama cha upinzani cha Chadema kiliambia shirika la habari la AFP kwamba kimerekodi vifo "si chini ya 800" kufikia Jumamosi, wakati chanzo cha kidiplomasia nchini Tanzania kiliiambia BBC kuwa kuna ushahidi wa kuaminika kwamba takriban watu 500 walifariki.
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa hapo awali ilisema kulikuwa na ripoti za kuaminika za vifo vya angalau watu 10 katika miji mitatu.
Kufuatia machafuko hayo, bei ya vyakula, mafuta na vitu vingine muhimu imeongezeka zaidi ya maradufu au mara tatu katika maeneo mengi. Shule na vyuo vimefungwa na usafiri wa umma umesimamishwa.
Chadema - ambayo ilizuiwa kushiriki - inakataa matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi, ikisema "hayana msingi wowote kwani ukweli ni kwamba hakuna uchaguzi wa kweli uliofanyika Tanzania". Chama hicho sasa kinataka uchaguzi mpya kufanyika.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais
Siku ya uchaguzi, vituo vya kupigia kura vilisalia tupu - lakini mamlaka ya uchaguzi baadaye ilisema waliojitokeza walikuwa 87%.
Siku ya Jumapili, msemaji wa polisi David Misime aliwalaumu waendesha pikipiki na raia wa kigeni kwa maandamano hayo yenye vurugu na uharibifu.
Alisema wapo watu ambao "wameingia nchini kinyume cha sheria kwa nia ya kuleta fujo" katika majimbo ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Songwe.
Isipokuwa kwa jiji la bandari la Dar es Salaam, maeneo yaliyotajwa yapo karibu na mipaka ya Kenya, Uganda, Zambia, na Malawi.
Misime amewataka Watanzania kutoa taarifa kwa mamlaka kuhusu "mgeni yeyote ambaye hajulikani wala ambaye shughuli zake hazieleweki Tanzania" kwa mamlaka.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Tanzania
Matamshi yake yanakuja huku kukiwa na ripoti kwamba raia kadhaa wa Kenya wametoweka nchini Tanzania.
Mwanaharakati wa Kenya Hussein Khalid alisema kwenye X kwamba amepokea taarifa za kuuawa kwa mwalimu Mkenya na wengine bado hawajulikani waliko.
Hali nchini Tanzania imezua wasiwasi duniani, ambapo Papa Leo wa 14 siku ya Jumapili alitoa wito wa maombi, akisema ghasia za baada ya uchaguzi zilizuka "na wahasiriwa wengi".
Mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas aliitaka serikali ya Tanzania kujizuia ili kuokoa maisha, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akisema "ana wasiwasi mkubwa" na hali hiyo "ikiwa ni pamoja na ripoti za vifo na majeruhi".











