Clemence Mtenga: Mwanafunzi Mtanzania aliyefariki Israel alikuwa 'kiongozi' kwa wanafunzi wenzake

Chanzo cha picha, MASHAV ISRAE
Clemence Mtenga alipaswa kuhitimu elimu ya chuo kikuu wiki hii, badala yake mwili wake unasafirishwa kwa ndege kutoka Israel hadi kwa familia yake nchini Tanzania.
Bado haijafahamika alikufa vipi lakini mwanafunzi huyo wa kilimo mwenye umri wa miaka 22 alifariki wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7, wapiganaji wa wa Hamas walipoanzisha shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel kutoka Ukanda wa Gaza.
Mwili wake unatarajiwa jijini Dar es Salaam leo Jumamosi saa mbili usiku kwa saa za Afrika mashariki, utapelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti kabla ya kusafirishwa kijijini kwao wilayani Rombo karibu na Kilimanjaro kwa mazishi.
Familia yake iliambia BBC kwamba hatimaye atazikwa siku ya Jumanne katika hafla iliyohudhuriwa na familia na marafiki.
Bw Mtenga alikuwa nchini Israel kama sehemu ya mpango wa masomo, alifika mwezi mmoja tu kabla ya shambulio hilo.
Wiki hii alitunukiwa shahada yake kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo nchini Tanzania.
Mmoja wa wanafunzi wenzake waliohudhuria sherehe za kuhitimu, Cleopatra Mluge, aliambia BBC kwamba Bw Mtenga "alikuwa kama kiongozi kwa sababu alikuwa mnyenyekevu na yuko tayari kusaidia na kuwashauri marafiki".
Mwanafunzi mwingine, Irene Chaboma, alimkumbuka kuwa "mchapakazi darasani na mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri. Roho yake ipumzike kwa amani."
Inakadiriwa kuwa karibu watu 1,200 waliuawa wakati wa shambulio la Hamas huku watu wenye silaha wakiwachukua mateka 240, miongoni mwao watu kadhaa kutoka mataifa ya kigeni.
Awali Israel ilisema kuwa Bw Mtenga na Mtanzania mwenzake Joshua Loitu Mollel walikuwa miongoni mwa mateka hao. Hata hivyo, Bw Mtenga si mmoja wa mateka wawili ambao miili yao imeopolewa kutoka Gaza, kwa hivyo bado haijafahamika alifia wapi na jinsi gani.
Israel imejibu mashambulizi ya Hamas kwa mashambulizi ya anga ya mara kwa mara huko Gaza na kuanzisha mashambulizi ya ardhini. Takriban watu 13,300 wameuawa huko Gaza, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas. Pande hizo mbili zimekubaliana kusitisha mapigano kwa siku nne.
Watanzania hao wawili walikuwa wakiishi Israel kama sehemu ya programu ya mafunzo ya kilimo. Walitarajiwa kukaa nchini kwa miezi 11 zaidi. Jumla ya Watanzania 260 wanasomea kilimo nchini Israel.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Revocatus Kimario, mkuu wa Sugeco, ambaye aliendesha programu ya mafunzo ya ndani ya chuo hicho alisema: "Kwetu sisi, Clemence ni shujaa kwa sababu alienda nje ya nchi kutafuta ujuzi wa kubadilisha na kuendeleza kilimo katika nchi yake. Tunaiombea familia yake."
Mwanafunzi mwenza katika programu ya mafunzo ya kazi, Ezekiel Kitiku, amechagua kubaki Israel. Aliambia BBC kwamba Bw Mtenga alikuwa akiishi Kibbutz Nir Oz na alikuwa akitoka kufanya kazi katika shamba la ufugaji ng'ombe wa maziwa katika eneo hilo saa za mchana wakati liliposhambuliwa na wapiganaji wa Hamas.
Kitiku alimpongezi kwa rafiki yake, akimkumbuka kama mpenda mazoezi ya viungo.
"Rafiki yangu ndiye aliyependa kufanya mazoezi, kwa hivyo ilikuwa utaratibu wetu wa kila siku jioni kufanya mazoezi pamoja," aliambia BBC.
"Tungeenda kwenye mazoezi kwa kutumia baiskeli pamoja. Alikuwa rafiki mzuri sana kwangu."
"Muda mwingi tulikuwa pamoja," aliongeza. "Tulipika pamoja na kila mara nyakati za jioni tulikuwa tukizungumza kuhusu siku yetu. Kuondoka kwake ghafla ni chungu sana."
Mara ya mwisho Kitiku alizungumza na Mtenga ilikuwa siku ya shambulio kabla ya kupoteza mawasiliano ya simu ya mkononi. Alisema imani yake ya Kikristo inamsaidia, “na ninaamini nitakutana naye tena siku moja”.
Taarifa ya ziada kutoka Eagan Salla akiwa mjini Morogoro.
Imetafisiriwa na Ambia Hirsi













