Je, kiwanda cha kusafisha mafuta Tanga ni ndoto inayowezekana?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Pendekezo la ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta huko Tanga, Tanzania limeibua mjadala mpana wa kisiasa na kiuchumi Afrika Mashariki, likifufua upya hoja ya utegemezi wa mafuta kutoka nje.

Mjadala huo ulipata nguvu baada ya Rais wa Kenya William Ruto kutangaza wazo hilo siku chache zilizopia, kabla ya kulisisitiza tena katika ziara yake nchini Tanzania na hotuba yake bungeni Dodoma.

Pamoja na kwamba mchakato huo unaanza kwa mguu wa kushoto, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha awali kama hakufahamu tangazo hilo, licha ya kwamba Tanga, eneo lililotajwa, liko ndani ya mamlaka yake, mapokezi yamekuwa na matumaini makubwa.

Katika maelezo yake, Rais Ruto alisisitiza kuwa pendekezo hilo halilengi taifa moja pekee, bali ni mkakati wa kikanda unaoweza kunufaisha Tanzania, Kenya, Uganda na Sudan Kusini, hasa katika kukuza viwanda vinavyotegemea mafuta na bidhaa zake pamoja na mbolea.

Hata hivyo, nyuma ya kauli hizo, kuna swali kubwa ambalo bado halijapata jibu la moja kwa moja: Je, huu ni mpango wa kimkakati unaowezekana, au ndoto nyingine kubwa inayoweza kubaki kwenye makaratasi?

Kwa nini ndoto ya kiwanda cha Tanga ni muhimu sasa?

Kwa miongo kadhaa, Afrika Mashariki imekuwa mnunuzi mkubwa wa mafuta yaliyosafishwa kutoka nje licha ya kuwa na baadhi ya rasilimali za mafuta ghafi ndani ya ukanda. Hali hii imeacha uchumi wake ukiwa katika hatari ya mabadiliko ya bei za kimataifa na upatikanaji wa fedha za kigeni.

Takwimu zinaonyesha ukubwa wa changamoto hiyo. Bidhaa za petroli zilizokwisha kusafishwa zinaongoza kwa thamani ya uagizaji katika ukanda huu, zikifikia takribani dola za Marekani bilioni 11.8 kwa mwaka. Hii ni sehemu kubwa ya fedha za kigeni zinazotoka kila mwaka kugharamia nishati pekee.

Kwa Tanzania, mzigo huo unaonekana wazi zaidi. Mafuta yaliagizwa kwa zaidi ya dola bilioni 2.1 katika mwaka mmoja, sawa na karibu asilimia 13.8 ya bidhaa zote zilizoagizwa kutoka nje. Hata pale bei za mafuta ghafi zinaposhuka, gharama za mafuta yaliyosafishwa hubaki juu kutokana na masuala kama usafirishaji, bima na gharama za kusafisha nje ya nchi.

Athari zake ni pana, ikiwemo kupanda kwa bei za mafuta huongeza gharama za usafiri, uzalishaji wa viwandani na hata bei ya chakula. Kwa lugha ya kiuchumi, huu ni mfumuko wa bei unaoingizwa kutoka nje, hali ambayo serikali za ukanda hazina kisu cha kudhibiti kwa kiwango kikubwa.

Ndipo umuhimu wa kiwanda cha Tanga unapojitokeza. Kwa kusafisha mafuta ndani ya ukanda, nchi zinaweza kupunguza utegemezi huo na kubaki na sehemu ya thamani ya mnyororo wa biashara ya mafuta. Kama anavyoeleza mchambuzi Thomas Kibwana: "Kikijengwa kiwanda hiki, kitasaidia mambo mawili, kuokoa muda na kupunguza gharama."

Je, ndoto hii inawezekana kweli?

Pamoja na faida zake, ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta ni miongoni mwa miradi migumu zaidi ya viwanda duniani. Inahitaji uwekezaji wa mabilioni ya dola, teknolojia ya hali ya juu na mipango ya muda mrefu ya usimamizi.

Mchumi Dk. Hildebrand Shayo anaeleza ukubwa wa changamoto hiyo: "Kiwanda cha aina hii kinahitaji muda mrefu kujenga na uwekezaji wa muda mrefu. Mfano wa Dangote kule Nigeria umechukua zaidi ya miaka 12 kukamilika."

Lakini, changamoto nyingine ni rasilimali fedha. Japo kiwanda cha Tanga kinaonekana kitakuwa na uungwaji mkono kifedha kutoka nchi kadhaa kama Kenya, Uganda zilizoonyesha utayari, miradi hii inagharimu fedha nyingi sana. Kwa mfano kiwanda cha Dangote, Nigeria ujenzi wake umegharimu karibu dola $20 billion. Hizi ni fedha nyingi ni bajeti ya serikali kwa nchi kama Tanzania.

Changamoto nyingine ni uhakika wa malighafi. Kiwanda kinahitaji mafuta ghafi ya kutosha kwa muda mrefu ili kifanye kazi kwa ufanisi. Bila mikataba thabiti ya usambazaji, kiwanda kinaweza kufanya kazi chini ya uwezo wake na kupoteza faida.

Pia kuna suala la siasa na uratibu wa kikanda. Kila nchi zinaendelea na mipango yake ya viwanda vya mafuta, kwa tija tofauti, jambo linaloweza kuleta ushindani badala ya ushirikiano ikiwa mipango haitaratibiwa vyema.

Hata hivyo, fursa bado ni kubwa. Dk. Shayo anaongeza: "Kama kitajengwa, kitaikomboa Afrika Mashariki… tutapunguza utegemezi, bei zitashuka na ajira zitaongezeka." Hapa ndipo mvutano ulipo, kati ya ugumu wa utekelezaji na ukubwa wa faida zinazoweza kupatikana.

Ndoto kama hii imewahi kufanikiwa wapi?

Historia inaonyesha kuwa miradi mikubwa ya kusafisha mafuta mara nyingi huanza kama mawazo yanayopingwa, lakini baadhi yake hubadilika na kuwa nguzo za uchumi wa taifa.

Mfano unaotajwa mara nyingi ni wa mfanyabiashara Aliko Dangote nchini Nigeria, ambaye amewekeza katika moja ya viwanda vikubwa zaidi vya kusafisha mafuta barani Afrika. Licha ya changamoto za kifedha na kisiasa, mradi huo umeanza kubadilisha mwelekeo wa soko la mafuta katika ukanda huo. Kinazalisha karibu mapipa ya mafuta 650,000 kwa siku.

Dangote mwenyewe anasisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ndani ya nchi: "Unapopeleka nje malighafi, unapeleka ajira, na unapoingiza bidhaa ndani, unaingia umasikini." Kauli hii inaonyesha mantiki ya msingi ya viwanda vya aina hii, kujenga ajira na kubaki na thamani ya uzalishaji ndani ya nchi.

Na kwa mfano huo, Dangote anatajwa kuwa muhimili wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta Tanga, na amekubali kuwekeza huko.

Nhi kama India zimefanikiwa kujenga uwezo mkubwa wa kusafisha mafuta na sasa zimekuwa wauzaji wakubwa wa bidhaa za petroli katika soko la kimataifa. Hii inaonyesha kuwa uwekezaji wa muda mrefu unaweza kuzaa matokeo makubwa.

Hata hivyo, si miradi yote imefanikiwa. Baadhi ya nchi zimejenga viwanda vya aina hii ambazo baadaye zilishindwa kujiendesha kutokana na gharama kubwa na ushindani wa kimataifa. Pamoja na ndoto, inahitaji pia utashi, sera, soko, fedha na usimamizi.

Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, somo ni moja tu, ndoto ya Tanga inaweza kufanikiwa, lakini si kwa urahisi, inahitajika mipango makini, fedha, ushirikiano wa kweli na nidhamu ya kiuchumi, vinginevyo utakuw amradi mwingine mkubwa wa kwenye makaratasi.