Rais Goïta kujiteua waziri wa ulinzi waiweka Mali njia panda

    • Author, Abdou Aziz Diédhiou
    • Nafasi, BBC News Afrique
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Uamuzi wa Rais wa mpito wa Mali Assimi Goïta kujiongezea wadhifa wa Waziri wa Ulinzi umeweka nchi hiyo katika njia panda, katikati ya wasiwasi wa usalama unaozidi na mjadala mpana kuhusu madaraka mikononi mwa uongozi wa kijeshi.

Hatua hiyo imetangazwa kupitia amri iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa ORTM, ikithibitisha kuwa Goïta sasa ataongoza moja kwa moja Wizara ya Ulinzi sambamba na nafasi yake ya Rais wa Mpito na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.

Uamuzi huo unakuja muda mfupi baada ya mashambulizi yaliyoratibiwa na makundi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya Mali, ambayo yamesababisha vifo na kuongezeka kwa shinikizo la kiusalama kwa serikali ya mpito. Mashambulizi hayo yamemuua pia Waziri wa Ulinzi Jenerali Sadio Camara, ambapo sasa nafasi yake inachulkuliwa na Rais Goïta.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Jenerali Oumar Diarra ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa ulinzi na masuala ya wastaafu wa Jeshi, akisaidia katika kusimamia sekta hiyo muhimu.

Tangu mapinduzi ya Agosti 2020 yaliyomng'oa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keïta, Assimi Goïta amekuwa mhimili mkuu wa siasa na usalama nchini Mali.

Safari ya Assimi Goïta

Kutoka Koulouba, ambako kuna Ikulu ya rais ambayo aliiteka mwaka 2020, Assimi Goïta sasa akiwa pia Waziri wa Ulinzi, Goïta anaweka chini ya uongozi wake wa moja kwa moja operesheni zote za kijeshi dhidi ya makundi ya kigaidi ambayo yameongeza mashambulizi katika maeneo ya kaskazini na katikati mwa nchi.

Kwa muda mrefu, Goïta amekuwa akihusishwa na mipango ya kijeshi kutokana na historia yake ndani ya jeshi, akihudumu katika maeneo yenye migogoro kama Gao, Timbuktu na Kidal.

Hatua hii inaonekana kama juhudi za kuimarisha amri ya moja kwa moja katika vita dhidi ya ugaidi, lakini pia inaibua maswali kuhusu mkusanyiko wa mamlaka mikononi mwa mtu mmoja.

Akiwa na umri wa miaka 43, Goïta ambaye pamoja na wanajeshi wenzake waliupindua utawala wa Ibrahim Boubacar Keïta, na sasa anachukua udhibiti wa operesheni kitu alichokifanya kwa sehemu kubwa ya maisha yake ya kijeshi.

Kufuata nyayo za baba yake

Jenerali Assimi Goïta ni mtoto wa afisa wa jeshi na alifuata nyayo za baba yake kwa kuingia jeshini mwaka 1992. Baadaye alipelekwa Koulikoro.

Alisoma na akabobea katika matumizi ya silaha za kivita na matumizi ya farasi wa kijeshi, na alipata ufadhili wa mafunzo nchini Marekani, Ufaransa na Ujerumani.

Goïta, ambaye alikuwa mkuu wa kikosi cha jeshi maalum la Mali, alipata uzoefu wake wa kwanza wa mapambano katika maeneo ya kati ya nchi alipokuwa akipambana na wanamgambo wa kijihadi.

Mnamo Novemba 2015 aliteuliwa kuwa mratibu wa operesheni maalum katika Wizara ya Ulinzi, kufuatia shambulio la Al-Qaeda katika hoteli ya Radisson Blu mjini Bamako.

Muhimili wa mapinduzi mawili ndani ya miezi tisa

Ilikuwa kupitia taarifa ya televisheni ya taifa ORTM ambapo wananchi wa Mali walijulishwa kuwa kiongozi huyo wa kijeshi amewafuta kazi viongozi wa mpito waliokuwa wamepangwa kuongoza nchi kuelekea uchaguzi baada ya miezi 18 kufuatia kuondolewa kwa Keïta.

Akiwa Kanali wakati huo, Assimi Goïta aliwalaumu Rais wa mpito Bah N'Daw na Waziri Mkuu Moctar Ouane kwa kushindwa kuzuia migomo ya kitaifa na akawashutumu kwa kuhujumu mchakato wa mpito.

Alisema pia walipaswa kumshirikisha kabla ya kutangaza serikali mpya.

"Baada ya mgogoro wa miezi kadhaa kitaifa, migomo na maandamano ya kijamii na kisiasa, serikali ya Moctar Ouane imeshindwa kuwa mshirika wa kuaminika," ilisema taarifa ya Goïta.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ilikuwa ni dalili ya wazi ya kuvunja katiba ya mpito.

Siku moja kabla ya tukio hilo, viongozi hao wawili walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi mkali wa kijeshi kabla ya baadaye kuachiwa.

Baada ya mapinduzi ya kwanza, alilazimishwa na shinikizo la kimataifa kuunda serikali ya mpito, ambayo baadaye aliipindua tena katika mapinduzi ya pili.

Kusimamishwa kwa vyama vya siasa

Vyama vya siasa na mashirika yanayojihusiha na siasa sasa yamepigwa marufuku nchini Mali.

Baada ya kuingia madarakani kwa mapinduzi alihidi kurejesha utawala wa kiraia ndani ya miaka minne, hata hivyo serikali ya kijeshi imeahirisha kwa muda usiojulikana uchaguzi nchini Mali.

Na ikaenda mbali zaidi, ambapo Mei 13, 2025, serikali yake ya kijeshi ilivunja rasmi vyama vyote vya siasa na mashirika ya kisiasa kupitia amri ya rais.

Hatua hiyo, iliyolenga "kupanga upya maisha ya taifa hilo" na mikutano ya kitaifa, imesimamishapia shughuli zote za kisiasa ikiwa ni pamoja na vyama na mashirika ya kiraia.

Hatua hii kali, inayomaliza mfumo wa vyama vingi vya siasa, imekuja baada ya msururu wa vizuizi dhidi ya sauti pinzani, vyombo vya habari na mashirika ya kiraia. Mali sasa iko njia panda zaidi, matumaini ya mamlaka ya raia yanazidi kupotea, mamlaka ya kijeshi chini ya Assimi Goïta, yanaonekana kujisima zaidi.