Uvamizi wa Ukraine: Ndege za Urusi zinakabiliwa na marufuku kabisa kutumia anga za nchi za magharibi

Mashirika ya ndege ya Urusi yanakabiliwa na zui dhidi ya kutumia anga za nchi za magharibi

Mashirika ya ndege ya Urusi yanakabiliwa na zuio kamili dhidi ya kutumia anga za nchi za magharibi baada ya afisa wa Umoja wa Ulaya kusema kuwa nchi nyingi za Ulaya ziko tayari kuweka marufuku ya safari za ndege.

Uamuzi rasmi unatarajiwa juu ya hatua hiyo baadaye Jumapili.

Nchi kadhaa tayari zilikuwa zimechukua hatua, zikifuatwa na Ujerumani na Ubelgiji, huku mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya yakitarajiwa kuungana nao.

Kukiwa na zuio la kutumia anga ya Ukraine , safari za ndege za Urusi sasa zina njia chache za safari za kuelekea magharibi.

Bodi za kuondoka katika viwanja vya ndege vya Domodedovo na Sheremetyevo huko Moscow zilionyesha kughairiwa kwa safari kadhaa siku ya Jumapili, ikijumuisha safari za ndege kwenda Paris, Vienna na Kaliningrad.

Shirika la ndege la Russia la S7 lilisema kwenye Facebook kuwa litaghairi safari zake nyingi za kwenda Ulaya hadi angalau Machi 13.

Aeroflot, shirika kubwa la ndege la Urusi, lilisema litaghairi huduma zake kwa Latvia na Romania hadi angalau Machi 26, na njia zake za Prague na Warsaw hadi Machi 28.

Wakati huo huo, Urusi imejibu kwa vikwazo vya nipe nikupe kwa nchi zinazopiga marufuku safari zake za ndege.

Ndege zinazomilikiwa na Urusi, zikiwemo ndege za kibinafsi, haziwezi tena kuingia angani juu ya mataifa ya Baltic, Poland, Jamhuri ya Czech, Bulgaria, Romania na Slovenia. Ndege za Urusi pia zimepigwa marufuku kutoka anga ya Uingereza.

Nchi kadhaa zaidi za EU sasa zimejiunga na hatua ya kufunga anga kwa ndege za Urusi:

• Ujerumani inaweka marufuku ya miezi mitatu kuanzia 15:00 (14:00 GMT) siku ya Jumapili.

• Italia itafunga anga yake kwa ndege za Urusi, ofisi ya waziri mkuu ilisema

• Finland, ambayo inashiriki mpaka wa maili 800 (1,300km) na Urusi, "inajiandaa kufunga anga yake dhidi ya trafiki ya anga ya Urusi," Waziri wa Uchukuzi Timo Harakka aliandika kwenye Twitter

•Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo alisema anga za Ulaya "ziko wazi kwa wale wanaounganisha watu, si kwa wale wanaotaka kufanya fujo kikatili", na Uholanzi pia itafunga anga yake kuanzia Jumapili jioni.

•Waziri wa mambo ya nje wa Denmark Jeppe Kofod alisema kwenye Twitter kwamba nchi yake itafunga anga yake na kushinikiza kupigwa marufuku kwa EU kote.

• Ireland na Austria zimeunga mkono marufuku ya EU kote.

Zuio la safari za ndege katika nchi nyingi kuelekea magharibi mwa Urusi litahitaji mashirika yake ya ndege kuchukua njia za mzunguko, na hivyo kusababisha muda mrefu wa safari.

Uamuzi wa Ufini unaweza kuiacha Ghuba ya Ufini - karibu maili 74 (km 120) kwa upana wake - kama njia pekee inayofaa kwa ndege za Urusi zinazosafiri kwenda nchi za Ulaya ambazo bado hazijapiga marufuku safari za ndege.

Mashirika ya ndege ya kibiashara pia yanaepuka anga kuzunguka Ukraine, Moldova na Belarus kufuatia uvamizi wa Urusi.

Nchini Marekani, kampuni ya Delta Air Lines ilisema itasitisha makubaliano ya kuweka nafasi ya ndege na shirika la ndege la Aeroflot la Urusi.

Marufuku ya Uingereza kwa safari za ndege za Urusi ilisababisha Moscow kulipiza kisasi kwa hatua sawa dhidi ya ndege za Uingereza.

Virgin Atlantic alisema kuepuka Urusi kutaongeza kati ya dakika 15 na saa moja kwa safari zake za ndege kati ya Uingereza na India na Pakistan.

Shirika la ndege la Australia Qantas lilisema kuwa litatumia njia ndefu zaidi kwa safari yake ya moja kwa moja kati ya Darwin na London ambayo haipitii Urusi