Kupanda na kushuka kwa Ndugai

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Job Ndugai wiki hii ameweka historia ya kuwa Spika wa kwanza wa Bunge la Tanzania kujiuzulu wadhifa huo.

Ingawa barua yake ya kujiuzulu wadhifa huo ilieleza sababu ya kufanya hivyo kuwa ni "uamuzi binafsi uliozingatia maslahi mapana ya Bunge, Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM)" lakini ni wazi kwamba kilichoharibu kila kitu ni kuzorota kwa uhusiano wake na Rais Samia Suluhu Hassan katika siku za karibuni.

Kwa waliomfahamu Ndugai, anajulikana kama mwanasiasa ambaye ndoto yake kubwa ilikuwa kuja kuwa Spika wa Bunge la Tanzania. Ndoto yake hiyo hatimaye ilitimia miaka 15 baada ya kuingia bungeni kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

Hii, kwa vyovyote vile, haikuwa namna ambayo alitaka kumaliza muda wake wa Uspika.

Hata hivyo, mfululizo wa matukio, kukosea mahesabu ya kisiasa na sadfa (coincidence) za kimaisha, ndiko hatimaye kumehitimisha maisha yake ya ukuu wa mhimili huu wa dola.

Ili kufahamu ilikuwaje Ndugai akapanda kutoka kijana kutoka familia masikini ya Kongwa, Dodoma na kuja kuwa mkuu wa mhimili wa mmojawapo wa dola na mmoja wa wanasiasa watata Tanzania - ni muhimu kwanza kupata historia yake.

Ndugai ni nani hasa?

Ndugai alizaliwa mnamo Januari 22, 1960 wilayani Kongwa mkoani Dodoma akiwa mtoto pekee kwa wazazi wake.

Alisoma katika Shule ya Msingi Matare, Kongwa na kusoma katika shule za sekondari za serikali za Old Moshi mkoani Kilimanjaro na Kibaha mkoani Pwani - wakati huo ikijulikana kwa utaratibu wake wa kuchukua wanafunzi wenye vipaji maalumu kitaaluma.

Mwaka 1986 alisoma Stashahada ya Wanyamapori katika Chuo cha Mweka mkoani Kilimanjaro kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya shahada ya kwanza ya Sayansi.

Mbunge huyu ambaye akimaliza awamu hii atakuwa ametimiza miaka 25 bungeni, ana shahada mbili za uzamili (Masters)- moja kutoka chuo cha ESAMI kilichopo Arusha Tanzania kuhusu Utawala wa Biashara na nyingine kuhusu masuala ya Uhifadhi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Norway.

Kabla ya kuingia katika siasa, Ndugai alifanya kazi serikalini katika Wizara ya Maliasili na Utalii katika idara mbalimbali zikiwamo za Uhifadhi - akiwa amewahi kuwa Meneja wa Hifadhi ya Selous na katika taasisi ya utafiti ya Tawiri.

Ndiyo sababu, alipoingia bungeni mara moja aliwekwa katika Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi na Mazingira iliyomtambulisha katika siasa za kitaifa na ambayo alikuja kuwa Mwenyekiti wake kabla ya kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge mwaka 2010.

Kupanda kisiasa kwa Ndugai

Ndugai anatoka katika kizazi cha wanasiasa wa Tanzania ambao walianza kwa kufanya kazi serikalini kabla ya kuingia kwenye siasa wangali bado wadogo.

Alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2000, aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, Pius Msekwa - mjuzi wa masuala ya kibunge na kiserikali, aliona haraka uwezo, uzoefu na uzeefu (skills) wa mbunge huyo mapema na kumpeleka kwenye kamati itakayofaa.

Haraka, Ndugai akajitambulisha kama mmoja wa wabunge waungwana, wanaopenda kujisomea na wanaozungumza lugha ya kibunge.

Haikuwa ajabu kwamba alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge katika miaka yake ya mwanzoni bungeni - jambo ambalo si la kawaida.

Mbadala wa Msekwa, Samuel Sitta, naye aliona kipaji cha Ndugai na ndiye aliyempa fursa pana zaidi za kuzunguka katika mikutano ya kimataifa na kuongoza baadhi ya shughuli za Bunge.

Mara zote, Ndugai hakuwa mwanasiasa aliyetoa kauli za kukoroga wakubwa wake bungeni au serikalini zaidi ya kutoa hoja za maana akizungumza.

Haikuwa ajabu wakati alipochaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge mwaka 2010, chini ya Spika Anne Makinda na ni wakati huo ndipo hasa alipoanza kujitanabaisha kwa sifa ambayo hakuwa nayo awali. Kwenye Bunge la Spika Sitta, kulikuwa na mijadala mikali ambayo kuna wakati ilisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Serikali haikutaka tena mijadala ya namna ile bungeni na ndiyo sababu ya Sitta kutopitishwa ten ana CCM kuwa Spika kwa hoja kuwa ilikuwa zamu ya spika mwanamke.

Kwa waandishi wa habari na baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya Bunge, ilikuwa imeanza kufahamika kwamba siku ambayo Ndugai alikuwa akiongoza vikao vya Bunge, wabunge walikuwa huru kujieleza na kutoa hoja zao kuliko akiwepo Makinda.

Kukaanza kuwa na minong'ono miongoni mwa "waserikali" kwamba Ndugai alikuwa "mkorofi".

Kulikuwa na dhana bungeni kwamba siku ambayo kulikuwa na jambo ambalo serikali haikutaka lijadiliwe sana au wabunge wasichokonoe, siku hiyo Ndugai hakutakiwa kukaa kwenye kiti.

Kwa sababu hiyo, Ndugai akawa mmoja wa wabunge wa CCM wanaoheshimiwa na wabunge wa pande zote bungeni.

Kwanza kwa sababu ya hoja zake wakati akiwa mbunge wa kawaida na pia kwa sababu ya kutowazuia wabunge kusema wanachotaka wakati wakiwa bungeni. I

likuwa kana kwamba Ndugai alivutiwa zaidi na Bunge la Sitta na angetamani liwe mfano wa vikao na mikutano ya Bunge.

Alipogombea uspika mwaka 2015, Ndugai alikuwa mgombea pekee aliyekuwa akiungwa mkono na wabunge wa pande zote - wa CCM na upinzani. Kimsingi, baadhi ya wabunge wa upinzani walikuwa sehemu ya timu yake ya kampeni; hata kama vyama vya upinzani vilivyokuwa bado vinatembea kwenye kivuli cha Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) vilikuwa vimemsimamisha Goodluck ole Medeye kuwania nafasi hiyo.

Kulikuwa na kiu kubwa ya wabunge kutaka kuona Bunge linalofanana na lile lililokuwa linaongozwa na Sitta na Ndugai alionekana kuwa mwana CCM pekee wakati ule aliyekuwa na sifa na ujasiri wa kuendeleza pale alipoishia Mzee Sitta.

Kwa baadhi ya wabunge waliokuwa wakimfahamu, ushindi wa Ndugai ulionekana kama ushindi kwa taasisi ya Bunge.

Ndugai sasa akawa amekalia kiti alichokuwa akikiota kwenye maisha yake ya kibunge.

Kushuka kwa Ndugai

Ndugai alikuwa na bahati mbaya mbili kumlinganisha na Sitta. Mosi, yeye hakuwa mtu wa ndani miongoni mwa marafiki wa hayati Rais John Magufuli na pili alipata Rais ambaye hakuamini katika uhuru wa Bunge.

Nguzo mbili za Bunge la Sitta zilikuwa kwamba lilipata kiongozi aliyekuwa na uhusiano binafsi na Rais - na pili kulikuwa na Rais aliyeamini katika demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kujieleza yaani Jakaya Kikwete.

Maana yake ni kwamba, kama Ndugai angekuwa Spika wa Bunge wakati wa utawala wa Kikwete, huenda mambo yasingekuwa mabaya kwake kama yalivyokuja kuwa wakati wa Magufuli.

Ninafahamu kwamba kulikuwa na misuguano ya chini kwa chini katika siku za kwanza za uspika wa Ndugai na urais wa Magufuli kwa sababu ya haiba zao tofauti wakati huo.

Ndugai akitamani Bunge lenye kujinafasi na Magufuli akiamini kwamba Serikali ndiyo kila kitu na kwamba kelele za bungeni ni muhimu zikazimwa ili serikali ifanye kazi.

Duru za kibunge zilibainisha kwamba ilibidi serikali impe Dk. Tulia Ackson nafasi ya Naibu Spika wa Bunge - ikiwa ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni mwaka 2015, ili kuondoa uwezekano wa kuwa na Spika na Naibu wenye ushawishi mkubwa bungeni.

Mchezo ulikuwa kwamba Spika na Naibu wake wasije kutokea kuwa kitu kimoja na kuipa serikali taabu katika siku za mbele.

Matukio matatu yaliharibu taswira ya Ndugai. La kwanza lilikuwa ni kuugua kwake miezi michache tu baada ya kuchaguliwa kuwa Spika. Kuugua kwake kulimfanya atibiwe nchini India kwa takribani miezi sita na kama Spika wa Bunge, taasisi yake iligharamia matibabu yake kwa gharama kubwa - jambo lililoonyesha moyo mkunjufu wa Rais Magufuli kwake.

Ni kama vile jambo hilo lilimpa Ndugai "deni" la kuona kwamba naye anatakiwa kufanya vitu kuonyesha shukrani zake kwa Mkuu wa Nchi.

Inaonekana kwamba hakutaka tena migogoro na Magufuli au na serikali mara baada ya kumaliza matiba yanayotajwa kuokoa maisha yake.

Wakati huo, Magufuli tayari alikuwa ameanza kugawa mitazamo ya watu na hatua ya kujihusisha naye ilikuwa kamari ya kisiasa kwa Ndugai.

Jambo la pili lilikuwa namna alivyoshughulika na suala la aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Wakati Rais Samia Suluhu Hassan - wakati huo akiwa Makamu wa Rais, alikwenda hadi Nairobi kumjulia hali baada ya jaribio la kumuua kwa risasi jijini Dodoma, Nduga; ambaye ndiye kiongozi wa Bunge, hakwenda hospitalini Nairobi kumwona.

Mbaya zaidi, Ndugai alikuwa akitoa kauli tata dhidi ya mtu ambaye taifa lilikuwa likihuzunika naye - Lissu na kitendo cha Spika kutoa kauli za kebehi na wakati mwingine zilizoumiza dhidi ya Lissu ikiwamo ile ya masuala ya mafao, huku uongozi wake ukizima ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Ulinzi ya Bunge chini aliyekuwa mbunge wa Muheza, Adadi Rajab, zilimpunguzia wafuasi wa upinzani walioshiriki kumwingiza madarakani.

Hili ni kosa kubwa zaidi la kisiasa alilofanya Ndugai bungeni - kujitenga na wabunge na kuegemea kwa Magufuli.

Mojawapo ya mafanikio makubwa ya Sitta yalikuwa namna alivyojijengea nguvu miongoni mwa wabunge. Kama ungemgusa Sitta, wabunge kama Lucas Selelii, Dkt. Harrisson Mwakyembe, Fred Mpendazoe na James Lembeli wangekuja juu kumlinda.

Hii ni kwa sababu Sitta hakuwabagua wabunge na alijua namna ya kuishi nao.

Ndugai hakujenga uga huu wa kumlinda. Matokeo yake ni kwamba wakati mashambulizi dhidi yake yalipoanza kutokana na hotuba yake kuhusu "nchi kuuzwa kwa madeni", hakuna wabunge wa maana waliojitokeza hadharani kumtetea.

Kimsingi, wabunge wa chama chake walioonekana kuwa rafiki zake kama Livingstone Lusinde, ndiyo waliokuja kutoa kauli za kumtaka aachie ngazi.

Kosa kubwa la tatu lilikuwa ni kumgusa Rais. Katika nchi nyingi za Afrika ambazo kwa mfumo wa chama hodhi (dominant party) kama ilivyo CCM kwa Tanzania, ofisi ya Rais ina mamlaka makubwa na hakuna kiongozi wa mhimili mwingine, chama au serikalini ambaye anaweza kuanzisha mgogoro na ofisi hiyo na kushinda.

Kuna video yake inazunguka mtandaoni ikisema "chezea wengine lakini usimchezee Ndugai" lakini ukweli ni kwamba kauli rasmi inatakiwa kuwa "Chezea wengine lakini usimchezee Rais".

Kuna pia namna ambayo alishughulika na jambo la wabunge 19 wa viti maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wabunge mmoja mmoja kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele.

Mambo haya mawili yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na Imani yake kubwa kwamba ali mradi Rais Magufuli yuko upande wake, hakuna kitakachoharibika.

Kuna mambo mengine mawili madogo yalimsumbua Ndugai kwenye uspika wake. Kisaikolojia, watoto waliozaliwa peke yao huwa na tabia tofauti kidogo na wale waliozaliwa wengi.

Kuna ile kitu ya kupewa kila unachotaka na kutozoea kushindanishwa na wengine. Kihisia na kitabia, inawezekana cheo cha uspika kiliiweka wazi hizi tabia hizi kuliko alivyokuwa na vyeo vidogo.

Lingine ni lugha. Katika mazungumzo niliyowahi kufanya naye huko nyuma, alipata kuniambia kwamba hakuwahi kusikia lugha ya Kiswahili mpaka baadaye sana alipoanza elimu ya msingi.

Kwa maneno yake mwenyewe, mara ya kwanza kusikia watu wakizungumza Kiswahili "alishangaa sana kumbe kuna lugha nyingine kuondoa Kigogo alichozoea".

Huyu ni mtu ambaye Kiswahili hakikuwa lugha yake ya kwanza. Pengine, kuna nyakati ulimi wake ulikuwa unateleza kwa sababu ya kukosa maneno mwafaka ya lugha ya Kiswahili kuzungumza. Ni hotuba yake ya lugha ya Kiswahili - katika mkutano wa jamii ya Wagogo, ndiyo hatimaye ilihitimisha safari yake ya uspika.

Kama angelijua na kuzingatia, angefanya mkutano ule kwa lugha ya Kigogo lakini hilo kwa sasa ni majuto na majuto ni mjukuu, maana huja baadaye.