COP26: Nyaraka ilivyovuja zinaonyesha mataifa yanashawishi kubadilisha ripoti muhimu ya hali ya hewa

Coal power plant chimney

Chanzo cha picha, Getty Images

Uvujaji mkubwa wa nyaraka za mabadiliko ya tabia nchi ambazo BBC imeziona zinaonyesha jinsi nchi kadhaa zinavyojaribu kubadilisha ripoti muhimu ya kisayansi juu ya jinsi ya kukabiliana na mabadiliko tabia nchi. Uvujaji huo unaonyesha Saudi Arabia, Japan na Australia ni miongoni mwa nchi zinazotaka Umoja wa Mataifa kutochukulia kwa uzito uharakishaji wa kuachana na matumizi ya mafuta.

Nyaraka hizo zinaonyesha baadhi ya nchi tajiri zikihoji kuhusu umuhimu wa kuzigharamia nchi masikini kuhamia kwenye matumizi ya teknolojia ya kijani kibichi."Hushawishi huu" unaibua maswali kuelekea mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi (COP26) utakaofanyika Novemba mwaka huu.

Taarifa hiyo inaonyesha baadhi ya nchi zikijaribu kurudisha nyuma mapendekezo ya Umoja wa Mataifa ya kuchukua hatua ikiwa ni siku chache kabla hazijatakiwa kutoa ahadi ya kujitolea katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa joto duniani kufikia nyuzi joto 1.5.

Nyaraka hizo zilizovuja zinahusisha maoni zaidi ya 32,000 yaliyotolewa na Serikali, makampuni na wadau wengine kwa timu ya wanasayansi inayoandaa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu njia bora za kisayansi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ripoti hizi za tathmini zinaandaliwa kila baada ya miaka 6 mpaka 7 na jopo maalumu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (IPCC), chini ya Umoja wa Mataifa jopo lililopewa jukumu la kutathmini kuhusu sayansi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Ripoti hii itatumiwa na serikali za mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuamua kuhusu hatua gani za kuchukua katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na itakua na mchango muhimu kwenye majadiliano yatakayofanyika kwenye mkutano wa COP26 huko Glasgow, Scotland.

Mafuta

Mafuta yanayotajwa na kuzungumziwa katika ripoti hii ni yale yanayotokana na mimea na wanyama wanaoharibika. Mafuta haya hupatikana katika ganda la dunia ama safu ya nje kabisa ya sayari yetu; ni ganda nyembamba ambalo linazunguka dunia nzima. Mafuta haya yana yana kaboni na haidrojeni, ambayo inawezwa kuchomwa na kupatikana nishati. Makaa ya mawe, mafuta, na gesi asilia ni mifano ya mafuta yanayozungumzia hapa na yanayotokana na masalia ya mimea na wanyama yaliyooza.

dg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mabaki yaliyooza ya wanyama ni moja ya vyanzo vya mafuta, baada ya kuoza kwa muda mrefu kwa miondo kwa miongo.

Nyaraka zilizovuja zinaonyesha baadhi ya nchi na mashirika zikieleza kwamba dunia haihitaji kupunguza matumizi ya mafuta ama nishati za aina hii kwa haraka kama rasimu ya ripoti ya sasa inavyopendekeza. Mshauri kwenye wizara ya mafuta ya Saudi anataka "maneno yaliyotumiwa kama 'hitaji la hatua za kupunguza haraka ...' inapaswa kuondolewa kwenye ripoti".

Afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Australia anakataa hitimisho kwamba kufunga mitambo ya umeme inayotumiwa na makaa ya mawe ni muhimu, ingawa kumaliza matumizi ya makaa ya mawe ni moja ya malengo ya mkutano wa COP26.

Saudi Arabia ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani na Australia ni muuzaji mkubwa wa makaa ya mawe nje ya nchi.

Mwanasayansi mwandamizi kutoka Taasisi kuu ya Uchimbaji wa Madini na Utafiti wa Mafuta ya India, ambayo ina uhusiano mkubwa na serikali ya India, anaonya kwamba makaa ya mawe yanaweza kubaki kuwa tegemeo la uzalishaji wa nishati kwa miongo kadhaa kwa sababu ya kile wanachokielezea kuwa "changamoto kubwa" za utoaji umeme kwa bei rahisi. India ni mtumiaji mkubwa wa pili duniani wa makaa ya mawe.

Nchi kadhaa zinapingana na teknolojia zinazoibuka na za bei ghali kwa sasa zilizotengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi hewa chafu ya kaboni chini ya ardhi. Saudi Arabia, Uchina, Australia na Japani - ni wazalishaji wakubwa au watumiaji wakubwa wa mafuta - na vile vile nchi zinazozalisha mafuta kupitia OPEC, zote zinaunga mkono teknolojia ya kuhifadhi kaboni (CCS).

Inadaiwa teknolojia hizi za CCS zinaweza kupunguza uzalishaji wa mafuta kutoka kwa mitambo na sekta zingine za viwandani.

Saudi Arabia, Mzalishaji mkubwa wa mafuta duniani, imeiomba Umona wa Mataifa kuondoa hitimisho kwamba "lengo la juhudi za kuondoa hewa ya kaboni katika sekta ya mifumo ya nishati inahitaji kuwa jambo la haraka la kukomesha kabisa vyanzo vya hewa hiyo na kuondoa matumizi ya mafuta".

Argentina, Norway na Ppec nazo zimelibeba jambo hilo. Norway ikiwataka wanasayansi wa Umoja wa Mataifa kuruhusu uwezekano wa teknolojia ya CCS kama nyenzo muhimu ya kupunguza uzalishaji wa mafuta yanayosababisha uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa.

An offshore gas field

Chanzo cha picha, Getty Images

Sayansi isiyo na upendeleo

Jopo maalumu la wataalamu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (IPCC), chini ya Umoja wa Mataifala linasema maoni kutoka Serikali mbalimbali ni muhimu kwenye mchakato wa mapitio ya kisayansi na kwamba wataalam wake wanaoandika ripoti hawalazimiki kuyajumuisha kwenye ripoti hizo.

"Mchakato na utaratibu wetu umeundwa kujiepusha na kujilinda dhidi ya aina yoyote ya ushawishi - kutoka kila upande ", IPCC iliiambia BBC." Mchakato wa mapitio ni (na umekuwa) msingi kabisa kwa kazi za IPCC na ni chanzo kikuu cha nguvu na uaminifu wa ripoti zetu.

Profesa Corinne le Quéré wa Chuo kikuu cha East Anglia, anayeongoza jopo la wanasayansi ambao wamesaidia kuandaa ripoti tatu kubwa za IPCC, anasema hana shaka kuhusu upendeleo wa ripoti za IPCCs.

Anasema kawaida maoni yote hupimwa kwa kuangalia vigezo vya kisayansi haijalishi yametoka wapi.

Umoja wa Mataifa ulipata tuzo ya Nobel mwaka 2007 kutokana na kazi ya IPCC kuhusu sayansi ya mabadiliko ya tabia nchi na jukumu lake katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko hayo.

Kula nyama kiasi

jkj

Chanzo cha picha, Getty Images

Brazil na Argentina, nchi mbili kubwa wazalishaji wa bidhaa za nyama na mazao ya chakula cha wanyama duniani, zinahoji kuhusu ushahidi katika rasimu ya ripoti kwamba kupunguza ulaji wa nyama ni muhimu katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Rasimu ya Ripoti ya inasema "lishe inayotokana na mimea inaweza kupunguza uzalishaji wa gesi chafu hadi 50%". Brazil inasema hii sio sahihi.

Nchi zote mbili zinatoa wito kwa waandishi wa ripoti hiyo kufuta au kubadilisha vifungu kadhaa katika ripoti hiyo yanayotaja "mlo unaotokana na mimea" una jukumu katika kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, au ambayo inaelezea nyama ya ng'ombe kama chakula kinachosababisha "kaboni nyingi". Argentina pia ilihoji kwamba marejeleo ya ushuru kwenye nyama nyekundu na kampeni ya kimataifa ya "Meatless Monday", ambayo inawataka watu kuacha nyama kwa siku moja, iondolewe kwenye ripoti hiyo.

Fedha kwa mataifa masikini

Maoni mengi yaliyotolewa na Switzerland yamejiegemeza kwenye kurekebisha sehemu za ripoti ambazo zinasema nchi zinazoendelea zitahitaji msaada, haswa msaada wa kifedha, kutoka nchi tajiri ili kufikia malengo ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.

Ilikubaliwa katika mkutano wa hali ya hewa huko Copenhagen mnamo 2009 kwamba mataifa yaliyoendelea yatatoa $ 100bn kwa mwaka katika fedha za hali ya hewa kwa nchi zinazoendelea ifikapo 2020, lengo ambalo bado halijafikiwa.

Australia yenyewe inaungana kimtazamo na Switzerland. Afisa mmoja wa juu kwenye upande wa mazingira ameiambia BBC kwamba : "Ingawa fedha ni muhimu katika kufikia matamanio kwenye mabadiliko ya tabia nchi, lakini isiwe ndio nyenzo pekee ya kutegemewa."

Kuelekea kwenye Nyuklia

as

Chanzo cha picha, Getty Images

Nchi kadhaa za Mashariki mwa Ulaya zinasema rasimu ya ripoti hiyo inapaswa kuwa na mtazamo chanya zaidi juu ya jukumu la nguvu ya nyuklia linaloweza kusaidia katika kufikia malengo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa.

India inakwenda mbali zaidi, ikisema "karibu sura zote zina upendeleo dhidi ya nishati ya nyuklia". Inasema ni "teknolojia iliyoanzishwa" na "ikiungwa mkono na kusaidiwa vyema kisiasa isipokuwa kwa baadhi ya nchi".

Jamhuri ya Czech, Poland na Slovakia zinakosoa jedwali katika ripoti hiyo ambayo inasema nguvu za nyuklia zina jukumu nzuri tu katika moja ya malengo 17 ya Maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa. Wanasema inaweza kuchukua jukumu chanya katika kufikisha ajenda nyingi za maendeleo za Umoja wa Mataifa.