Wabunge Askofu Gwajima, Jerry Silaa kuhojiwa na Bunge la Tanzania kwa tuhuma za utovu wa maadili

Askofu Gwajima

Chanzo cha picha, Askofu Gwajima

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ameamrisha wabunge wawili wa nchi hiyo Askofu Josephat Gwajima na Bw. Jerry Silaa kuhojiwa na kamati ya maadili ya Bunge kwa tuhuma "mbalimbali ikiwemo kusema uongo na kushusha hadhi na heshima ya Bunge."

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya mawasiliano ya Bunge la Tanzania hata hivyo haikueleza kwa undani zaidi kuhusu tuhuma hizo zinazowakabili wabunge hao wote kutoka chama tawala cha CCM.

Askofu Gwajima ambaye ni mbunge wa Kawe anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Jumatatu, Agosti 23 huku Silaa akitakiwa Jumanne Agosti 24.

Jerr

Chanzo cha picha, Twitter-Silaa

Askofu Gwajima katika wiki za hivi karibuni amekuwa akigonga vichwa vya habari pamoja na kuwa gumzo katika mitandao ya kijamii kwa msimamo wake hasi juu ya chanjo za kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona.

Msimamo huo umemfanya aingie kwenye mgogoro na Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Dr Dorothy Gwajima ambaye amevitaka vyombo vya dola kumchukulia hatua Askofu huyo kwa kauli "anazotoa dhidi yake (waziri) na Rais (Samia Suluhu Hassan)."

Maelezo ya video, 'Msimamo wangu kuhusu Corona haujabadilika'

Waziri Gwajima alisema Askofu Gwajima amekuwa akitoa kauli hizo zinazoivuruga serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid 19.

Siku moja baada ya Tanzania kupokea msaada wa dozi zaidi ya milioni 1 ya chanjo aina ya Johnson Johnson mwezi uliopita kutoka Marekani, Askofu Gwajima aliwaeleza waumini wake wakati wa ibada ya Jumapili iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba daktari atakaye'shadadia' suala la chanjo bila kufanya utafiti wa kina ikiwemo madhara yake ya muda mrefu na muda mfupi atakufa.

"Tunalazimisha tena, na mnajiuliza mnalazimishia nini? kama ni hela kiasi gani? kwa ajili yta roho za watu? alihoji Askofu Gwajima na kuongeza 'Sitamnyamazia mjinga yeyote atakayejibu haya maswali bila kufikiri, ntakusemesha mpaka utatafuta taulo ya kuvaa, unachanja watanzania milioni 60 kwa majaribio?" Alihoji Gwajima kwenye ibada kuhusu kile anachodai kuwa chanjo kutofanyiwa utafiti wa kutosha.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) chanjo zote zilizoidhinishwa zimeshafanyiwa majaribio na utafiti wa kutosha na hivyo kwa sasa ni salama kwa matumizi na hazitolewi kwa majaribio.

Mbali na kauli hizo, Askofu Gwajima ameeendelea kusisitiza mara kadhaa kwenye ibada za Kanisa lake jijini Dar es Salaam kwamba yeye hatochanjwa na waumini wake hawatachanjwa kwa imani kuwa chanjo hizo si salama na kufikia hatua ya kudai kuwa yupo radhi kupoteza ubunge lakini si kubadili msimamo wake. Kauli hizo zimekosolewa vikali na wanaounga mkono chanjo wakiwemo viongozi.