Ajali za kivuko cha likoni: Je abiria wa feri ya Likoni mjini Mombasa wako salama?

Chanzo cha picha, BAKARI GOWA
Jumatatu Septemba 30 mwaka 2019, biwi la simanzi lilitanda katika kivuko cha Likoni Ferry mjini Mombasa, Kenya, baada ya mama mmoja na binti yake kutumbukia baharini na kufa maji.
Ni tukio ambalo lilishutumiwa vikali na watumizi wa Ferry pamoja na viongozi mbali mbali, huku mamlaka husika ikiahidi kushughulikia usalama wa abiria wote wanaotumia kivuko hicho.
Lakini mwaka mmoja baadaye, hali iko vipi? Mwanahabari wetu Roncliffe Odit ametoka Likoni kujionea hali ilivyo…
Ilikuwa Septemba 30 mwaka jana katika kivuko cha Likoni Ferry mjini Mombasa, ambapo Mariam Kighenda na binti yake Amanda Mutheu walifariki baada ya gari lao kutumbukia majini.

Kwa mujibu wa mashuhuda, gari lao lilirejea nyuma na kutumbukia baharini, mama na bintiye wakalia, wakaitana, wakawapungia mikono, lakini hakuna mtu wa aliyewasaidia.
Ni ajali ambayo mashuhuda wanasema ingeweza kuepukika, lakini msaada ulichelewa.
Sasa zaidi ya mwaka mmoja baadaye, je, usalama wa abiria umeimarishwa katika kivuko hicho?

Chanzo cha picha, HISANI
Saa kumi na mbili jioni kuna msongamano mkubwa wa watu na magari, kila mmoja anajaribu awahi kabla masaa kupita.
Miongoni mwa abiria wengi hapa ni Hamisi Mbete ambaye ni mtaalam wa masuala ya baharini, anayesema kwamba hali imebadilika kidogo.
'Ile ajali ilipotokea, na kufariki kwa yule mama na mtoto wake, ilileta changamoto kubwa sana. Kila mmoja aliyekuwa amelala kazini sasa ameamka.'
Abiria mwingine hapa, Pamela Johnson ambaye huvuka kwa Ferry kila siku pia anakubali kwamba kuna mabadiliko kidogo tangu ajali hiyo ya mwaka jana.
'Siku hizi tunapokuwa ndani ya Ferry huwa tunatangaziwa kuhusu zile jaketi za kuvaa ili kujisadia wakati wa ajali. Japo ajali ni jamabo la dharura, lakini siku hizi tukiwa ndani ya kivukio huwa tunatahadharishwa.'

Chanzo cha picha, HISANI
Lakini kando na matangazo hayo ya usalama yanayotolewa ndani ya Ferry, nini kingine kinahitajika ili kuwahakikishia abiria usalama wao?
'Kunapaswa kuwa na watu ambao wako pale kila wakati, ikiwa mtu ataanguka baharini wanaweza kupiga mbizi na kumuokoa. Pia lazima kuwe na drills (yaani majaribio) kila mara ili watu wawe na uzoefu', anasema Hamisi Mbete ambaye pia ni baharia.
Aidha wataalam wanasema ni muhimu pia kuwe na boti za kutosha na maboya ya kujiokoa wakati wa ajali.
Lakini Lucy Mwaka ambaye huvuka kwa Ferry kila siku anasema hajui kutumia boya la kujiokoa iwapo kutatokea ajali.
'Hayo maboya sidhani kama kuna mtu hata mmoja anayejua kuyatumia. Hata mimi nikipatwa na shida, sijui nitaanzia wapi.'
Sasa kama yeye hajui ni nani anayejua?

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ferry nchini Kenya Bakari Gowa anasema hilo ni tatizo ambalo wanalishughulikia kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa abiria wa Ferry.
'Tumehakikisha kuwa milango ya Ferry iko katika hali ya sawasawa. Na ndani ya Ferry itakuwa vigumu sana kwa mtu kutumbukia ndani ya maji. Pia tunazungumza na wananchi na kuwasisitizia kwamba wakiingia ndani ya Ferry wazime magari ili kuwa salama.'
Aidha Gowa anasema kwamba sasa abiria wengi pia wamekuwa waangalifu zaidi, licha ya kuwa wamefanyia milango ya Ferry marekebisho.
Zaidi ya mwaka mmoja tangu ajali hiyo ya kusikitisha, familia ya Mariam Kighenda na binti yake Amanda Mutheu imejikokota kurejelea maisha ya kawaida.
Na japo mume wake John Wambua bado hana nguvu za kuizungumzia siku hiyo, hapa kwenye kivuko cha Likoni Ferry, bado abiria wengi wana kumbukumbu ya kilichotokea.
Lakini licha ya kumbukumbu hiyo, abiria wa Ferry wanavuka wakiwa na matumaini kwamba hilo ni wingu lililopita na halitawahi kurudi tena.












