Wakati wengine wanakesha kutafuta watoto wengine hawana hamu ya kuwa na watoto

- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Wanja Kimani hana hamu ya kupata watoto wakati Hazel Gachoka alitumia mamilioni ya fedha ili aweze kujaliwa kupata watoto.
Hazel Gachoka ana umri wa miaka 50 wakati Bi Wanja Kimani ana miaka arobaini, Wanawake hawa wawili wana mitizamo ambayo imetofautiana katika upande wa mwanamke kutaka kupata ujauzito au kutotaka kushika mimba.
Hazel Gachoka ni mama aliyetamani watoto tangu alipokuwa msichana na aliamini kuwa siku moja angepata mchumba wafunge ndoa na kisha wapate watoto.
Kwa hiyo miaka yake ya ujana aliendeleza masomo huku akisubiri kuolewa, hekaheka nyingi za kutafuta mchumba zilipelekea kupata mchumba aliyefunga naye pingu za maisha akiwa na miaka 41.
Bila shaka kwa wengi watakuwa na mtizamo kuwa kwa mwanamke wa umri wake Hazel ulikuwa umesonga mno, lakini kwake hakuwa amekata tamaa
"Kwa hiyo nilipokuwa na miaka 41 ndipo tulianza kujaribu kupata mtoto , lakini ilikuwa ni vigumu kwangu kushika mimba " Hazel alisema

Ilikuwa wazi kuwa Hazel alikuwa na matatizo ya kushika mimba kwa njia ya kawaida ya mume na mke kushiriki tendo la ndoa na kisha mwanamke kushika mimba .
Muda wa Hazel wa kupata mtoto ulikuwa unazidi kuyoyoma , lakini ndoto yake haikuyoyoma wala kutikisika .
Alizidi kuwa na matumaini baada ya kutembelea ofisi za daktari bingwa wa uzazi , ilikuwa dhahiri kuwa Hazel lazima angeanza kuwazia kutumia njia mbadala za kupata mtoto kwa kutumia teknolojia za kisasa .
Njia aliyoichagua Hazel na mumewe inayojulikana sana kama (IVF)In-Vitro-fertilization
"Tuliamua kufuata mchakato wa IVF kwa kuwa tulitaka sana kupakata mtoto wetu na haikujalisha fedha au chochote wakati huo "alisema Hazel
Wakati huo Bi. Hazel alikuwa amehitimu umri wa miaka 45 akianza jaribio la IVF,
Je mfumo wa IVF ni upi?
Kwa mujibu wa watalaam wa afya ya uzazi mfumo wa IVF unahusu yai la uzazi la mwanamke kutolewa na vilevile manii (sperms) au mbegu za mwanaume pia kutolewa - haya mawili hufanyiwa uzalishaji katika maabara nje ya mfuko wa uzazi wa mwanamke , endapo lile yai la mwanamke na mbegu za mwanaume zitashikana kwa minajili ya kuwa mbegu ya mtoto , basi hurejeshwa tena ndani ya nyumba ya uzazi ya mwanamke na hapo ndipo mchakati wa mtoto kuanza kukua huanzia .
Changamoto kuu ya njia hii huwa ni fedha ambazo hutumika kwa Hazel na mumewe amekiri kutumia zaidi ya dola karibia elfu ishirini au shilingi milioni mbili za Kenya kutimiza ndoto ya kujaaliwa watoto wawili .
Hatimaye shughuli ya kwanza ya Hazel ilifanywa na ikafua dafu mara mmoja.
Hazel alijaliwa mtoto wake wa kwanza ambaye ni kijana mwaka wa 2017 - baada ya miaka miwili Hael na mumewe walipitia mfumo wa IVF kwa mara nyengine na wakaajaliwa mtoto wa pili .

Naye Wanja Kimani - ni mwanamke 'asiye wa kawaida' ikiwa tutamtazama kwa kutumia jinsi jamii ya kiafrika inavyotafsiri ndoa na uzazi.
Amekuwa kwenye ndoa kwa miaka 20. Yeye na mumewe waliamua kwamba katu, hawatapata watoto.
Katika Mahojiano na BBC Swahili, Bi Wanja alifunguka kuhusu msimamo wake huku akiutetea sana.
Yeye amezaliwa miongoni mwa ndugu watatu wanawake, malezi yao anasema yalikuwa ya kawaida.
Bi Wanja anasema kuwa hajashawishika kuwa ufanisi wa ndoa au ili iitwe ndoa kamili, ni lazima kuwe na hesabu ya watoto.
Kwa mtazamo wake, ndoa ni kati ya mume na mke, na wawili hao wanaweza kuamua vingine.
Lakini kwa nini akaamua kuishi bila watoto ?
Alisema kuwa haja yake kuu katika maisha hajaiona ama kuitambua kuwa ni kuzaa watoto.
Wanja anasema 'Ninapotembea huko nje unaona kina mama wengine wana watoto wengi lakini hawajali kuhusu watakachokula, watakavyosoma na kadhalika, kwa hiyo najiuliza mbona kazaa na hana huruma na yule mwanawe?'
'Nilipojitathmini kwa undani wangu, ni kana kwamba mimi sina zile hisia za kuwa mama' anasema Wanja Kimani
Anasema kuwa ilibidi ajitazame na kuelewa ikiwa yeye anataka kweli kuwaleta watoto duniani alafu waanze kuteseka.
Bi wanja ameeleza kuwa yeye hawachukii watoto bali haamini kuwa lengo lake kuu duniani linaambatana na kuzaa.
'Nilipojitathmini kwa undani , ni kana kwamba mimi sina zile hisia za kuwa mama, Na sikutaka kuleta watoto duniani kisha nianze kuwatelekeza "
Aliendelea kusema kuwa hata mumewe ana maoni sawa naye.
'Ni kana kwamba Mungu aliufahamu moyo wangu kwani alinipatanisha na mtu ambaye tulikuwa na maoni na msimamo sawa ".
Anasema kuwa ni kama sadfa kwani tangu walipoonana kwa mara ya kwanza, moja ya mambo yaliyowaleta pamoja ni kuwa wote walikuwa hawatamani kuwa na watoto wakiwa kwenye ndoa.
Hatahivyo uamuzi huu si mwepesi na wamekuwa wakikabiliwa na unyanyapaa ambao umeandamana na kauli za watu kuhusu msimamo wake.
Kwa mtazamo wake si kwamba mtu asipozaa mtoto huwa ndio maisha hayajakamilika.

Wanja ni miongoni mwa wanawake wachache, ambao wana uwezo wa kuzaa lakini wao wameamua kuwa hesabu ya watoto haipo katika mpangilio wao wa maisha.
Mila na desturi nyingi miongoni mwa waafrika zinawashinikiza wanawake wanaoolewa kuzaa, ili waonekane wanawake kamili katika ndoa.
Wengi ambao wanakuwa na matatizo yanayowazuia kushika uja uzito wanakuwa na mtihani mkubwa, kutokana na unyanyapaa kutoka kwa jamii na wengine hata ndoa zao kuishia kuvunjika.
Licha ya hali hiyo, Wanja anasema kuwa hajutii uamuzi huo wa kuishi maisha bila ya mtoto.
Taswira yake Bi Hazel na Bi Wanja bila shaka ni tofauti ambazo zinakinzana sana kuhusiana na azma za kila mwanamke , ya iwapo analengo la kushika mimba na kujaaliwa watot , au ataishi maisha yake bila kutamani kuzaa












