Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Coronavirus: Gundogan ataka Liverpool kupewa ubingwa kama ligi itafutwa kwa tishio la virusi vya corona
Itakuwa ni "haki" kuwapa Liverpool ubingwa wa Ligi ya Primia (EPL) msimu huu iwapo ligi itashindwa kukamilika kutokana na janga la virusi vya corona, amesema kiungo wa Manchester City, Ilkay Gundogan.
Ligi ya EPL kwa sasa imesimamishwa walau mpaka Aprili 30, huku Liverpool (maarufu kama majogoo wa jiji) ikiwa kileleni kwa pengo la alama 25 na wanahitaji kushinda mechi mbili tu ili kutangazwa mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.
Alipoulizwa endapo majogoo hao wanastahili kombe endapo ligi itakatishwa, Gudogan ameliambia shirika la habari la ZDF la nchini Ujerumani kuwa: "Kwa upande wangu, hilo litakuwa sawa kabisa, ndio."
"Inakupasa kuwa mtu wa haki ukiwa mwanamichezo," ameeleza mchezaji huyo wa Ujerumani mwenye miaka 29.
Klabu zinazoshiriki EPL zitakutana Aprili 3, ambapo inatarajiwa kuwa Ligi hiyo itaahirishwa tena kwa muda zaidi. Hatua hiyo itafanya tarehe ya awali ya Ligi kuisha Mei 17 kupita bila ligi kurejea.
Rais wa bodi ya uendeshaji wa mpira ya Shirikisho la Mpira Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin, amesema kuwa msimu wa Klabu Bingwa Ulaya wa 2019-20 utapotea endapo ligi hiyo haitarejea kufikia mwishoni mwa mwezi Juni.
Gundogan amekiri kuwa viongozi wa mpira wanatakiwa kufanya maamuzi magumu kwa sababu kukufuta msimu wa EPL utakuwa na gharama kubwa kwa timu za juu na za mkiani pia.
"Kuna maoni tofauti. Kwa klabu ambazo zimekuwa na msimu mzuri, haitakuwa jambo jema kwao kwa msimu kufutwa kwa sasa," ameeleza Gundogan.
"Kwa upande mwengine, kwa klabu ambazo zimekuwa na msimu mbaya, hususani zile ambazo zipo chini ya mstari wa kushuka daraja kufutwa kwa msimu kutakuwa jambo jema kwao."
Gundogan pia amesema yu tayari kukatwa mshahara endapo klabu za England zitafikia hatua kama zinazochukuliwa na klabu za Juventus na Borussia Dortmund kupunguza mishahara ya wachezaji wao ili kulipa wafanyakazi wengine.
"Ni jambo sawa kabisa, hilo wala halihitaji maswali - [lakini] bado hakuna majadiliano ya jambo hilo hayajaanza England," ameeleza.