Ole Gunnar Solskjaer: Kocha wa Man United 'hajajikatia tamaa' licha ya kuwa na rekodi mbaya

Ole Gunnar Solskjaer and Paul Pogba

Chanzo cha picha, Getty Images

Ole Gunnar Solskjaer anasisitiza kwamba yeye ni mtu sahihi wa kuiongoza Manchester United, licha ya kwamba timu yake ipo alama tatu tu juu ya mstari wa kushuka daraja.

Tangu Solskjaer apewe rasmi usukani wa kuinoa klabu hiyo mwezi Machi, Man United wameshinda mara tano tu katika mechi 18.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 46, anapigiwa upatu kuwa miongoni mwa makocha wawili wa ligi ya Primia waliopo kwenye hatari ya kupoteza ajira zao muda wowote pamoja Marco Silva wa Everton .

"Mimi mwenyewe sina wasiwasi, kama sitajiamini mwenyewe basi dunia yote itakosa imani nami" amesema kocha huyo.

United inatarajia kucheza na Arsenal usiku wa leo baada ya kupoteza mechi ya nyumbani dhidi ya Crystal Palace na ugenini dhidi ya West Ham katika msimu huu.

Klabu ipo nyuma ya vinara Liverpool kwa pointi 13 na kuwa na pointi tatu tu mbele ya Aston Villa iliyopo nafasi ya 18, ambayo ndipo mstari wa kushuka daraja huchorwa.

"Tulikuwa na mjadala mkubwa sana, lakini tunaamini kile tunachokifanya," alisema Solskjaer said.

Mechi dhidi ya Arsenal inakuja siku chache baada ya kuondoka kwa kocha wa walinda mlango Emilio Alvarez.

Alvarez, ambaye alikuwa na uhusiano mzuri wa kazi na David de Gea tokea klabu ya Atletico Madrid, alipoteza nguvu yake baada ya klabu hiyo kumleta Richard Hartis kuwa kocha mkuu wa magolikipa hivi karibuni.

Hartis, alishawahi kufanya kazi klabuni hapo kwa mwongo mmoja na awali alifanya kazi na Solskjaer huko Molde na Cardiff.

'Kuna umuhimu gani kuwa na wachezaji ambao hawataki kuwa katika klabu hiyo?'

Lukaku

Chanzo cha picha, Getty Images

Siku ya Jumanne, Makamu Mwenyekiti wa Man United Ed Woodward alisema kuwa Solskjaer atapewa muda kuweka mipango yake katika utekelezaji.

Hii ikiwa inamaanisha kuwa wataendelea kuwa na Solskjaer ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo hata kama watashindwa kumaliza katika nafasi nne za juu kwa msimu wa pili mfululizo.

Hata hivyo Solskjaer, haoni kama timu yake itakosa vigezo vya kushiriki michuano ya ligi kuu.

"Timu mbili zilizokuwa zinaongoza zilikuwa mbali zaidi yetu," alisema.

"Lakini nadhani msimu huu tutakaribia. Chelsea pia inakabiliana na changamoto kama yetu ya kujijenga. Kuna sisi ,Arsenal, Tottenham na Leicester.

"Kuna timu nyingi zinataka hizo nafasi na hapo ndipo na sisi tunataka kuwa."

United imehangaika sana kufunga magoli msimu huu mpaka sasa. Toka walipoifunga Chelsea goli nne katika mechi ya ufunguzi wa msimu, wameshindwa kufunga zaidi ya goli moja katika mechi saba zilizofuata.

Majeraha waliyoyapata Anthony Martial na Marcus Rashford ambayo yatawafanya waukose mchezo dhidi ya Arsenal kumemfanya kinda Mason Greenwood, 17, kuwa mshambuliaji kinara wa United.

Alexis Sanchez

Chanzo cha picha, Getty Images

Greenwood alifunga mara mbili dhidi ya Astana na Rochdale - lakini wapo wanaohoji kuwa inakuwaje mzigo huo mkubwa kupewa mchezaji wadogo na kuhoji maamuzi ya kutolewa kwa Romelu Lukaku na Alexis Sanchez kwenda Inter Milan, ambapo tayari wote wamefunga.

"Rom hakutaka kubaki hapa ,kuna umuhimu gani kuwa na wachezaji ambao hawataki kuwa hapa?"amesema Solskjaer.

"Kuna washambuliaji wengine wengi lakini sio hao ndio tunawahitaji. Kama washambuliaji tunaowataka wangekuepo tungewasajili".

"Kuondoka kwa Rom na Alexis , sio lazima mtu uwe mwanasayansi wa roketi kuona kuwa tunatafuta ubunifu na magoli" alisema kocha huyo.