Fifa yamteua Fatma Samoura kama mjumbe wake kwa Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirikisho la soka duniani Fifa limethibitisha kuwa katibu mkuu wake Fatma Samoura ameteuliwa kuwa 'Mjumbe mkuu wa Fifa kwa Afrika' katika jitihada ya kuimarisha utawala katika mchezo wa soka barani Afrika.
Shirikisho la soka barani Afrika (Caf) hivi karibuni limekuwa likichunguzwa katika masuala tofuati yanayohusisha uongozi na usimamazi.
Fatma, raia wa Senegal atachukua usukani kwa miezi sita kuanzia agosti mosi, huku wadhifa huo 'ukiwa na uwezo wa kuidhinishwa upya kwa makubaliano ya taasisi zote mbili'.
"Makubaliano yamefikiwa pia kwamba Fifa na Caf zitaidhinisha haraka iwezekanavyo uchunguzi wa ushahidi wa Caf," taarifa hiyo iliongeza.
Samoura, mwenye umri wa miaka 56, atasalia kuwa katibu mkuu wa Fifa lakini ataelekeza baadhiya majukumu kwa wengine katika shirikisho hilo.
Kwanini uamuzi huu, na una maana gani?
Fifa limeutaja uamuzi huu kama 'hatua ya kipekee na ya muda mfupi' wakai likibaini wazi majukumu atakayokuwa nayo afisa huyo wa zamani wa Umoja wa mataifa.
Wakati Fifa imezoea kuziteua kamati ambazo zinaendesha muungano wa waanchama yanayohitaji usaidizi, sio kawaida kwake kusaidia shirikisho zinazokuwa katika maatizo kama hayo.
Rais wa Caf Ahmad amekuwa akichunguzwa hivi karibuni katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kuhojiwa na maafisa wa Ufaransa mjini Paris mapema mwezi huu kabla ya kuachiliwa huru pasi kushtakiwa.
Hili lilikuwa "sehemu ya uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi, ukiukaji wa imani na udanganyifu" - huku kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59 anayetoka Madasgascar akisema tuhuma zote zinazomuandama ni za uongo.
Masuala mengine ya hivi karibuni ni pamoja na mzozo kuhusu fainali ya ligi ya mabingwa Afrika na kupangwa upya muda wa fainali za mashindanoya kombe la mataifa bingwa Afrika 2019, 2021 na 2023.

Chanzo cha picha, Getty Images
Anachunguzwa pia na kamati ya maadili ya Fifa ambayo uchunguzi wake utaendeshwa kwa kujitegemea na sambamba na jukumu la samoura, ameeleza duru aliyefahamu kuhusu mpangilio huo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Ahmad amependekeza kuwa wataalamu wa Fifa 'waichunguze hali iliopo katika shirikisho hilo la uongozi Afrika … kuhakikisha kuwa Caf inaendeshwa kwa uwazi na uwajibikaji wakati likifuata uongozi wa juu.'
Majukumu ya Samoura ni yapi?
Kwa usaidizi wa wataalamu kadhaa 'katika taswira ya ushirikiano na rais Ahmad na kikosi chake', Samoura anatarajiwa:
- Kusimamia shughuli za Caf, ikiwemo mipango ya uongozi na usimamizi
- Kuhakikisha maandalizi ya mashindano yote ya Caf yalio na uwajibikaji na ya kitaalamu
- Kuhimiza ukuwaji na maendeleo ya soka katika nchi zote na maeneo ya Caf
Majukumu haya, yanayoendelea mpaka Januari 31 yalikubaliwa kwa pamoja na kamati tendaji ya Caf, taarifa hiyo iliongeza.













