Uefa League: Arsenal yaicharaza Valencia 7-3 huku Chelsea ikiilaza Frankfurt 4-3 kupitia mikwaju ya penalti

Washambuliaji hatari wa Arsenal Alexandre Lacazette na Aubameyang

Chanzo cha picha, Getty Images

Mshambuliaji wa Arsenal Pierre-Emerick Aubameyang aliifungia timu yake hat-trick na kuisaidia kutinga fainali ya kombe la Uefa dhidi Chelsea baada ya kuilaza Valencia 7-3 kwa jumla ya magoli.

The Gunners sasa wanasubiri ushindi mmoja ili kujikatia tiketi ya kushiriki katika michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya, huku Unai Emery akiweka historia ya kushinda taji la nne la Uefa barani Ulaya.

Wakati huohuo Eden Hazard alifunga penalti ya mwisho na ya ushindi akiisaidia Chelsea kuilaza Eintracht Franfurt 4-3 kwa mikwaju ya penalti na hivyobasi kukutanisha timu mbili za Uingereza katika fainali ya Uefa.

Eden akifunga mkwaju wake wa penalti

Chanzo cha picha, Getty Images

Hazard ambaye huenda angecheza mechi yake ya mwisho katika uwanja wa Stamford Bridge , alifunga penalti ya mwisho baada ya kipa Kepa Arrizabalaga kuokoa mikwaju miwili ya penalti kutoka kwa Hinteregger na Goncalo Paciencia.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu nne za Uingereza kuingia katika fainali za makombe mawili ya Ulaya.

Huku ikiwa magoli ni 1-1 baada ya mkondo wa kwanza, Chelsea ilichukua uongozi katika kipindi cha pili baada ya Reuben Loftus Cheek kucheka na wavu kunako dakika ya 28 lakini usiku huo ulikuwa mrefu sana kwa Chelsea.

Kepa Arrizabalaga aliokoa mikwaju miwili ya penalti

Chanzo cha picha, Getty Images

Frankfurt ilisawazisha dakika nne tu baada ya kipindi cha pili wakati Luka Jovic alipomfunga Arrizabalaga kufuatia pasi nzuri kutoka kwa Mijat Gacinovic.

Bao la Jovic iliiadhibu Chelsea baada ya kuanza vibaya katika kipindi cha pili huku the Blues wakizidi kushindwa kujimudu.

Valencia vs Arsenal

Aubameyang akisawazisha goli la kwanza

Chanzo cha picha, Getty Images

Wakiwa nyuma 3-1 kutoka katika mkondo wa kwanza , mjini London, bao la Kevin Gameiro lilikuwa limewapatia wanyeji hao muamko mpya.

Hatahivyo, goli la Aubameyang kutoka maguu 20 lilisawazisha kabla ya Alexandre Lacazette kuiweka kifua mbele Arsenal baada ya kufunga goli la kiwango cha juu.

Gameiro ambaye ameshinda taji hilo mara nne na klabu ya Sevilla na Atletico Madrid , aligusa bao la pili kabla ya Aubemayang kufunga goli la tatu.

Mshambuliaji huyo wa Gabon aliteleza na pasi ya Ainsley Maitland-Niles hadi wavuni kabla ya kufunga bao la nne na kukamilisha hat-trick yake huku akiisaidia Arsenal kuilaza Valencia 4-2 nyumbani.

Mchezaji bora wa mechi kati ya Arsenal dhidi ya Valencia- Aubameyang

Mchezaji bora Aubameyang

Chanzo cha picha, Getty Images

Hatua hiyo inamaanisha kwamba Arsenal ambayo ilicheza mechi yake ya kwanza dhidi ya klabu ya FK Qarabag nchini Azerbaijan itaurudi katika taifa hilo katika mechi ya fainali dhidi ya kikosi cha Maurizio Sarri siku ya Jumatano tarehe 29 mwezi huu.

Itakuwa fainali ya kwanza inayoshirikisha mataifa mawili ya Uingereza tangu Tottenham iilaze Wolves katika mikondo miwili mwaka 1972, wakati mashindano hayo yalipokuwa yakiitwa Uefa Cup na itakua mara ya kwanza kwamba timu zote nne zilizofuzu katika mashindano mawili ya Yuropa yanatoka katika taifa moja.