Watoto walimsaidia Wilfried Bony kurejea Swansea

Wilfried Bony amesema watoto wake wawili wa kiume walisaidia kumshawishi arejea Swansea City kwa sababu klabu hiyo "ni kama familia".

Mshambuliaji huyo wa Ivory Coast alirejea uwanja wa Liberty siku ya mwisho ya kuhama wachezaji £12m baada ya kuondoka Manchester City mwaka 2015 kwa mkataba wa £28m.

Bony alifungia Swansea mabao 34, lakini baada ya kuhama alifanikiwa kufunga mabao 12 pekee.

"Nafikiri wavulana wangu waliamua. Walisikia kwamba nilikuwa natafutwa (na Swansea) na wakaniambia 'Baba, lazima urudi Swansea'. Hivyo, wavulana wangu walichagua Swansea."

Mchezaji huyo wa miaka 28 aliongeza: "Kulikuwa na klabu nyingine - Lille, Fenerbahce na wengine - lakini muhimu zaidi ilikuwa yaliyosemwa na watu wa familia yangu."

Bony alikuwa mshambuliaji miongoni mwa waliotafutwa zaidi Ligi ya Premia kabla yake kuhamia Etihad na amesema hajutii uamuzi wake ingawa alianza mechi 15 pekee City.

Msimu uliopita alitumwa Stoke kwa mkopo.