Kylian Mbappe ahamia Paris St-Germain kutoka Monaco

Kylian Mbappe

Chanzo cha picha, Getty Images

Paris St-Germain wamemchukua mshambuliaji chipukizi ambaye amekuwa aking'aa sana Kylian Mbappe kwa mkopo kwa kipindi cha msimu mmoja kutoka Monaco.

Kwenye makubaliano kati ya klabu hizo mbili, PSG wanaweza kuufanya uhamisho wake kuwa wa kudumu kwa kulipa £165.7m.

Iwapo PSG watamchukua mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwa mkataba wa kudumu, badi mkataba wake utakuwa wa hadi Juni 2022.

Ununuzi wowote wa Mbappe, 18, unaweza kuzidiwa tu na ununuzi wa Neymar ambaye alinunuliwa na PSG kwa euro 222m (£200m).

"Nilitaka sana kuwa sehemu ya mpango wa klabu hii, ambayo ni moja ya klabu zenye ndoto kuu zaidi Ulaya," alisema Mbappe.

Kucheleweshwa kwa usajili wake kwa mkataba wa kudumu kunadaiwa kutokana na haja ya PSG kutaka kuheshimu sheria za uchezaji haki kifedha za Uefa.

Mchezaji huyo alifunga bao lake la kwanza katika timu ya taifa ya Ufaransa wakati wa ushindi wao wa 4-0 dhidi ya Uholanzi mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia Alhamisi na kucheza mchezaji wa umri mdogo zaidi kufungia taifa hilo bao tangu 1963.

Rais wa PSG Nasser Al-Khelaifi alisema: "Ni muhimu sana kwa soka ya Ufaransa kwamba tuhifadhi na kukuza vipaji adimu kama yeye katika ligi yetu.

"Miongoni mwa wachezaji wa umri wake, bila shaka ni yeye anayetoa matumaini zaidi duniani kwa sababu ya uwezo wake mkuu kiufundi, kimwili na kiakili.

"Tangu alipochomoza katika soka ya ngazi ya juu, amepata sifa sana kama kijana mwenye kipaji ambaye ana heshima, uwazi, ndoto kuu na mtu ambaye tayari amekomaa."

Mbona kwa mkopo?

Kylian Mbappe

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kylian Mbappe alifungia Monaco mabao 26 mashindano yote msimu uliopita

PSG wenyewe hawangeweza kutangaza kwamba ni mkopo ambao baadaye utabadilishwa na kuwa mkataba wa kudumu kwa sababu pesa walizotumia sokoni kipindi cha sasa cha kuhama kwa wachezaji zingekuwa juu sana.

Kwa hivyo, walichosema ili kuheshimu Sheria za Uchezaji Haki Kifedha za Uefa, ni kwamba wana fursa ya kumnunua kwa mkataba wa kudumu baadaye.

Hata hivyo, inatarajiwa kwamba bado watachunguzwa na Uefa.

Mbappe alifunga mabao 26 katika mechi 44 alizowachezea Monaco msimu uliopita na kuwasaidia kufika nusufainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na pia kushinda Ligue 1.

Real Madrid, Liverpool, Manchester City na Arsenal wote walitaka kumnunua.

Mbappe ni nani?

  • AlizaliwaBondy, viungani mwa Paris, 20 Dsemba 1998
  • Alifanyiwa majaribio Chelsea lakini akajiunga na Monaco mwaka 2013 baada ya kukaa miaka miwili kituo cha soka cha taifa cha Ufaransa Clairefontaine
  • Alicheza mechi yake ya kwanza ya kulipwa Desemba 2015 - na kuvunja rekodi ya Thierry Henry iliyodumu miaka 21 na kuwa mchezaji wa umri mdogo zaidi kuchezea Monaco akiwa na miaka 16 na siku 347.
  • Msimu uliopita alifunga mabao 10 katika mechi 10 alizocheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya
  • Alikuwa mchezaji wa kwanza kfuunga katika kila mechi kati ya mechi nne zake za kwanza mechi za muondoano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya
  • Alifunga mabao 15 mechi 29 za Ligue 1 msimu wa 2016-17
  • Baada ya kufunga mabao 26 na kusaidia ufungaji wa mabao 11 katika mechi 44 msimu uliopita, kimsingi alifunga au kusaidia ufungaji wa bao katika kila dakika 71 alizocheza

PSG timu hatari zaidi kwa sasa?

Potential PSG XI

Mchanganuzi wa BBC John Bennett anasema PSG sasa ni kama 'matajiri kupindukia' upande wa wachezaji nyota. Utachezeshaje Edinson Cavani, Neymar na Kylian Mbappe timu moja?

Walianza msimu wakicheza 4-3-3, na huenda wakaacha kumchezesha Angel Di Maria badala yake wamtumie Mbappe. Lakini Neymar na Mbappe hupenda kucheza kutoka kushoto.

Wanaweza pia kutumia mfumo wa 4-4-2 - ambao Mbappe alizoea kucheza Monaco. Lakini meneja Unai Emery atakosaje kumchezesha Cavani, aliyefunga magoli 35 mechi 36 za Ligue 1 msimu uliopita?

Wachanganuzi Ufaransa wamebashiri kwamba huenda pia wakacheza kwa mpangilio wa 4-1-3-2 Neymar akiwa namba 10 nyuma ya Mbappe na Cavani. Ukiongeza Dani Alves kulia, Julian Draxler kushoto na Marco Verrati mbele ya mabeki.

Tatizo kwa Unai Emery ni kwamba atakuwa na shinikizo sana kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Monaco departures