Somalia yaamuru balozi wa Ethiopia kuondoka nchini humo ndani ya saa 72

Balozi wa Ethiopia nchini Somalia, Mukhtar Mohamed Ware, aamriwa kuondoka nchini humo ndani ya saa 72 zijazo.

Moja kwa moja

Ambia Hirsi and Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri

  2. Somalia yaamuru balozi wa Ethiopia kuondoka nchini humo ndani ya saa 72

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alihutubia wabunge kufuatia makubaliano ya Ethiopia na Somaliland

    Balozi wa Ethiopia nchini Somalia, Mukhtar Mohamed Ware, amearifiwa kuondoka nchini humo ndani ya saa 72 zijazo.

    Vile vile, balozi za Ethiopia katika maeneo ya Hargeisa na Garowe zinahitajika kufungwa ndani ya siku 7.

    Aidha, Somalia imefunga balozi zake ndogo katika maeneo ya Puntland na Somaliland siku ya Alhamisi.

    Katika taarifa yake, Somalia imeishutumu serikali ya Ethiopia kwa kuingilia masuala ya ndani ya Somalia.

    Hisi Ganni, waziri wa serikali ofisi ya waziri mkuu alisema:

    ‘’Kuanzia leo, tarehe 04 Aprili 2024, Serikali ya Somalia imefunga na kubatilisha kibali cha kuendesha balozi ndogo za Serikali ya Ethiopia katika miji ya Garowe na Hargeisa, na lazima ifungwe ndani ya wiki moja. Wanadiplomasia na wafanyakazi wa serikali ya Ethiopia wanaofanya kazi katika balozi mbili katika miji iliyotajwa lazima waondoke nchini humo ndani ya wiki moja”.

    Haya yamejiri siku moja tu baada ya jimbo linalojitawala la Puntland kutangaza makubaliano mapya ya ushirikiano na Ethiopia.

    Maafisa kutoka Somalia walithibitisha hatua hizi zimechukuliwa kujibu kuhusika kwa Ethiopia katika makubaliano hayo yenye kuhusisha eneo linalozozaniwa la Somaliland.

    Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ameshutumu makubaliano hayo kuwa ni kinyume cha sheria, akionya kuhusu hatua za kujihami iwapo Ethiopia itaendelea.

    Kufungwa kwa ubalozi wa Ethiopia kunaonyesha mpasuko mkubwa uliopo kati ya nchi hizo mbili, na athari zinazowezekana kutokea kwa wanajeshi wa Ethiopia waliopo Somalia chini ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika.

    Soma zaidi:

  3. Myanmar: Mji mkuu unaotawaliwa kijeshi washambuliwa na ndege zisizo na rubani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Upinzani nchini Myanmar umedai shambulio la nadra la ndege zisizo na rubani dhidi ya serikali ya kijeshi ya nchi hiyo katika mji mkuu wenye ulinzi mkali, Nay Pyi Taw.

    Serikali ya Umoja wa Kitaifa (NUG) - ambayo inajiita serikali iliyo uhamishoni - ilisema ilipeleka ndege 29 zilizokuwa na vilipuzi kwenye uwanja wa ndege, kambi ya jeshi la anga na makao makuu ya jeshi.

    Jeshi hilo lilisema lilikamata ndege hizo zisizo na rubani, na kuaangusha saba, ikiwa ni pamoja na moja ambayo ililipuka kwenye njia ya kupaa ndege.

    Hakukuwa na majeruhi, walisema,

    NUG inawakilisha serikali ya kiraia iliyochaguliwa hapo awali iliyoongozwa na Aung San Suu Kyi, ambayo ilipinduliwa katika mapinduzi ya 2021.

    Tangu wakati huo serikali hiyo na makundi mengine ya upinzani yamekuwa yakipambana na utawala wa kijeshi, ambao umeanza kupoteza udhibiti wa maeneo makubwa ya nchi.

    Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitatu nchini humo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwakosesha makazi takriban watu milioni 2.6 kulingana na Umoja wa Mataifa.

    Mashambulizi ya Alhamisi asubuhi kwenye mji mkuu yanaashiria uvamizi mwingine wa kijasiri, na nadra wa makundi ya upinzani ambayo yanazidi kuwa na upinzani dhidi ya utawala wa kijeshi.

    Nay Pyi Taw ni kitovu cha mamlaka ya utawala wa kijeshi ambao uliuita mji mkuu, ukichukua nafasi ya Yangon, baada ya kuchukuwa utawala.

    Soma zaidi:

  4. Bobrisky: Mtu maarufu nchini Nigeria akamatwa kwa kurusha pesa juu

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Mmoja wa watu mashuhuri nchini Nigeria, mwanamke aliyebadili jinsia anayefahamika kwa jina la Bobrisky, amekamatwa kwa tuhuma za kutumia vibaya pesa.

    Bobrisky, ambaye jina lake halisi ni Idris Okuneye, anadaiwa kutumia vibaya na kukata noti za naira wakati wa onyesho la kwanza la filamu mjini Lagos, mamlaka iliambia BBC.

    Wanasema "alimwaga" noti, kumaanisha kwamba alizirusha hewani kwa ishara ya kushukuru.

    Mtindo wa "Kumwaga pesa" aina hiyo kwa kawaida hufanywa katika harusi na sherehe za Nigeria.

    Hili kitaalamu ni kosa kwani noti huanguka chini ambapo zinaweza kukanyagwa.

    Bobrisky alidaiwa kumwaga pesa katika onyesho la kwanza la Ajakaju, filamu iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mwigizaji na mtayarishaji Eniola Ajao, katika Film One Circle Mall, katika soko kuu la Lagos wilaya ya Lekki mwezi uliopita.

    Video za tukio hilo zilisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

    Mtu huyo maarufu, ambaye ana wafuasi zaidi ya milioni tano kwenye Instagram, bado hajatoa maoni.

    Msemaji wa Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha (EFCC) Dele Oyewale aliambia BBC kwamba Bobrisky atashtakiwa mahakamani punde tu uchunguzi utakapokamilika, bila kutoa muda uliopangwa.

    Mnamo Februari, mwigizaji Oluwadarasimi Omoseyin alihukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani kwa kumwaga pesa na kukanyaga noti mpya za naira.

  5. Nosiviwe Mapisa-Nqakula: Spika wa bunge la Afrika Kusini ashtakiwa kwa makosa 12 ya rushwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika Kusini Nosiviwe Mapisa-Nqakula ameshtakiwa kwa makosa 12 ya rushwa na moja la utakatishaji fedha.

    Alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza baada ya kujisalimisha kwa kituo cha polisi Alhamisi asubuhi.

    Mwanasiasa huyo anatuhumiwa kuomba hongo ili kutoa kandarasi wakati alipokuwa waziri wa ulinzi.

    Alikanusha kutenda kosa lolote mahakamani na kusema: "Sina tabia ya kufanya uhalifu."

    Lakini mwendesha mashtaka Bheki Manyathi aliiambia Mahakama ya Pretoria kulikuwa na "ushahidi wa kutosha" dhidi ya Bi Mapisa-Nqakula.

    Ameachiliwa kwa dhamana.

    Baada ya wiki kadhaa za uchunguzi, Bi Mapisa-Nqakula alijiuzulu siku ya Jumatano, lakini akasema hii sio "dalili au kukubali hatia".

    Alisema kutokana na "uzito wa suala hilo" na katika uchunguzi hawezi kuendelea na jukumu lake.

    Mwezi uliopita kitengo maalum cha polisi kilivamia nyumba yake Johannesburg kuhusiana na uchunguzi wa ufisadi.

    Mama huyo mwenye umri wa miaka 67 wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi alikua spika mwaka wa 2021. Kabla ya hapo, alihudumu kama waziri wa ulinzi kwa miaka saba.

    Soma zaidi:

  6. Togo yaahirisha uchaguzi baada ya mzozo wa katiba mpya

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Togo imechelewesha uchaguzi wa bunge na kikanda huku kukiwa na mvutano kufuatia mageuzi ya katiba yenye utata.

    Mageuzi hayo yaliyoidhinishwa na wabunge wiki jana yalibadilisha mfumo wa urais na kuwa wa bunge.

    Pia inakabidhi madaraka ya utendaji kwa waziri mkuu, na kupunguza mamlaka ya urais.

    Vyama vya upinzani vimekataa mageuzi hayo, kwa kuhofia kuwa yanaweza kumwachia Rais Faure Gnassingbé kusalia madarakani.

    Alimrithi babake, Gnassingbé Eyadéma, aliyefariki mwaka 2005 baada ya kutawala nchi hiyo kwa miaka 38.

    Ofisi ya rais ilitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo siku ya Jumatano, lakini haikutoa tarehe mpya ya uchaguzi huo, ambao awali ulipaswa kufanywa tarehe 20 Aprili.

    Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki wa Togo limemtaka Rais Gnassingbé kutotia saini mabadiliko ya katiba kuwa sheria, likitaja haja ya "mashauriano mapana na mjadala wa kitaifa unaojumuisha mengi zaidi".

  7. Uingereza yatangaza msada wa pauni milioni 27 kwa mipango ya kuokoa maisha ya wanawake na wasichana Tanzania

    .

    Uingereza imetangaza kifurushi cha pauni milioni 27 ili kuboresha uzazi wa mpango na kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

    Usaidizi wa ziada wa £5.5 milioni utaongeza ufikiaji wa nishati ya kijani na itasaidia biashara katika uwekezaji mpya.

    Ufadhili huo unaashiria mwanzo wa ziara ya siku 4 ya Waziri Andrew Mitchell Afrika Mashariki, ambapo pia atasafiri hadi Rwanda kuadhimisha miaka 30 ya mauaji ya halaiki.

    Mpango huo unalenga kuwalinda akina mama na watoto wachanga, kukabiliana na magonjwa, na kuongeza upatikanaji wa nishati ya kijani.

    Mpango huo wa miaka mitano wa pauni milioni 15 utasaidia kuboresha mfumo wa afya wa Tanzania na kuokoa maisha, hasa ya akina mama na watoto wachanga.

    Ufadhili huo utatoa msukumo unaohitajika kwa mfumo wa afya wa Tanzania, huku Uingereza ikifanya kazi pamoja na serikali kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, kukabiliana na milipuko ya magonjwa, na kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za afya ya msingi.

    Hii itasaidia kuimarisha uwezo wa Tanzania wa kugundua, kuzuia na kukabiliana na matishio ya kiafya.

    Tanzania inaendelea kukabiliwa na kiwango kikubwa cha umaskini, unaochangiwa na ongezeko kubwa la watu.

    Uwekezaji katika afya na haki za wanawake na wasichana ni kipaumbele cha Uingereza na Serikali ya Tanzania.

    Waziri wa Maendeleo na Afrika Andrew Mitchell alisema:

    "Kila mwanamke ana haki ya kuchagua kama ana watoto, na kupata mimba salama na kuzaa.

    "Vitisho vya magonjwa mbalimbali na ongezeko kubwa la watu nchini Tanzania vinaleta matatizo makubwa katika mfumo wake wa huduma za afya, ambayo ina maana kwamba wanawake wengi hawawezi kupata huduma za uzazi wa mpango wanazotaka na wanazohitaji, na hivyo kuwafanya kuwa katika hatari ya utoaji mimba usio salama - na kuweka afya zao na maisha hatarini.

    Soma zaidi:

  8. Wanandoa wa Ufaransa waliofuga paka 159 wapigwa marufuku kufuga wanyama tena

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanandoa wa Ufaransa wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kwa kuwaweka wanyama kadhaa katika mazingira ya ukatili.

    Wanandoa hao, kutoka Nice, walikuwa wamefuga paka 159 na mbwa saba katika gorofa yao ya ukubwa wa 80sqm (861sqft).

    Wanyama waligunduliwa mwaka jana wakiishi katika mazingira ya uchafu, wengi wakiwa wamepungukiwa na maji, wakikabiliwa na utapiamlo au kuambukizwa vimelea.

    Hakimu alisema wanandoa hao walikosa kuwatunza wanyama hao ipasavyo.

    Wanandoa hao, mwanamke, 68, na mwanamume mwenye umri wa miaka 52, pia walipewa marufuku ya kudumu ya kufuga wanyama nyumbani.

    Waliamriwa kulipa zaidi ya €150,000 (£128,000) kwa mashirika ya misaada ya haki za wanyama na vyama vya kiraia.

    Mwaka jana, polisi waliingia katika nyumba ya wanandoa hao na kugundua makumi ya wanyama katika kila chumba.

    Mamlaka ziliripoti uwepo wa kinyesi cha wanyama kila mahali.

    Baadhi ya paka na mbwa hao walikufa kwa sababu ya afya mbaya.

    Wachunguzi walipata miili ya paka wawili na mbwa wawili katika bafuni.

    Mmiliki wa orofa hiyo aliiambia mahakama kwamba wanyama hao walikuwa "kipenzi cha maisha yake" lakini kwamba alikuwa "amezidiwa na malezi".

    Inaonekana alikuwa amechukua paka watatu na mbwa watatu wa wazazi wake mnamo 2018, kabla ya kuleta karibu paka 30 wanaoishi katika jengo lililotelekezwa kwenye gorofa yake. Wanyama hawa baadaye walizaana.

  9. Nosiviwe Mapisa-Nqakula: Spika wa bunge la Afrika Kusini ajiwasilisha kwa polisi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Nosiviwe Mapisa-Nqakula, 67, ni mkongwe wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

    Spika wa Bunge la Afrika Kusini Nosiviwe Mapisa-Nqakula amejisalimisha kwa polisi siku moja baada ya kujiuzulu kwa tuhuma za rushwa.

    Bi Mapisa-Nqakula alifika katika kituo cha polisi huko Centurion, kilomita 40 kutoka Johannesburg siku ya Alhamisi.

    Anatarajiwa kufika kortini kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Pretoria kwa tuhuma za ufisadi.

    Mwanasiasa huyo anatuhumiwa kuomba hongo ili kurudisha kandarasi wakati alipokuwa waziri wa ulinzi.

    Baada ya wiki kadhaa za uchunguzi, Bi Mapisa-Nqakula alijiuzulu siku ya Jumatano, akisema hatua hiyo haikuwa "ishara au kukubali hatia".

    Alisema kutokana na "uzito" wa uchunguzi hawezi kuendelea na jukumu lake.

    Hapo awali alikana kosa lolote.

  10. Luke Fleurs: Mchezaji wa Kaizer Chiefs Afrika Kusini auawa kwa kupigwa risasi

    .

    Chanzo cha picha, Kaizer Cheifs

    Mwanasoka wa Afrika Kusini Luke Fleurs ameuawa kwa kupigwa risasi katika utekaji nyara wa gari, timu yake inasema.

    Ufyatulianai huo ulifanyika katika kituo cha mafuta usiku wa kuamkia leo katika kitongoji cha Johannesburg, Florida.

    Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 alikuwa akisubiri kuhudumiwa alipofikiwa na watu wasiojulikana wenye silaha, ambao walimwamuru ashuke nje ya gari.

    Mmoja wa washukiwa alikimbia eneo la tukio na gari la Fleurs baada ya kumpiga risasi.

    "Washukiwa walimnyooshea bunduki na kumtoa nje ya gari lake, kisha wakampiga risasi moja kwenye sehemu ya juu ya mwili," msemaji wa polisi wa Gauteng Luteni Kanali Mavela Masondo aliambia vyombo vya habari vya ndani.

    Timu yake, Kaizer Chiefs, inasema kifo hicho kilikuwa "cha kusikitisha". Ilisema polisi wanashughulikia suala hilo na taarifa zaidi zitawasilishwa kwa wakati unaofaa.

    Beki Fleurs alijiunga na Kaiser Chiefs mwaka jana. Hapo awali alichezea SuperSport United. Katika tovuti yake, Kaiser Chiefs inaeleza Fleurs kama "beki wa kiwango cha juu" na "uwezo mkubwa wa kiufundi".

    Alianza kazi yake mnamo 2013 katika Chuo cha Ubuntu Cape Town, kulingana na vyombo vya habari vya ndani. Mashabiki wa soka wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kumuomboleza.

  11. ‘Mawe yaliporomoka kama risasi’ – manusura wa tetemeko Taiwan

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waokoaji nchini Taiwan wanafanya kazi ya kuwaokoa takribani watu 100 ambao wamekwama, siku moja baada ya kisiwa hicho kukumbwa na tetemeko kubwa zaidi la ardhi katika kipindi cha miaka 25.

    Mtu mmoja aliyenusurika anasimulia jinsi tetemeko hilo lilivyoporomosha mawe “kama risasi” katika eneo la mgodi wa makaa ya mawe anakofanya kazi.

    Tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.4 lilipiga karibu na eneo la mashariki la Hualien, na kuua watu tisa na kujeruhi zaidi ya 1,000.

    Wengine waliokwama chini ya mahandaki na karibu na mbuga ya taifa wameokolewa na helikopta, lakini watu 34 bado hawajulikani walipo.

    Ugawaji wa chakula umefanyika kupitia angani kwa watu kadhaa walionasa katika maeneo yaliyoathirika, ripoti za ndani zinasema.

    "Mlima ulianza kuporomosha mawe kama risasi, hatukuwa na mahali pa kukimbilia, kila mtu alikimbia kando ya mifuko ya mchanga ili kujificha," manusura, aliyetambuliwa kwa jina lake la pili Chu, aliambia Shirika la Habari la Taiwan.

    Watatu kati ya tisa waliofariki walikuwa wasafiri kwenye njia ya kongoro inayoelekea Hifadhi ya Kitaifa ya Taroko, nje kidogo ya Hualien.

    Katika mji wa Hualien, mji mkuu wa eneo hilo - juhudi za kutoa msaada zinaendelea, huku wafanyakazi wakitumia vifaa kubomoa majengo kadhaa yaliyoharibiwa.

  12. Kwa nini Marekani inataka kuunda mfumo wake wa kutambua wakati Mwezini?

    .

    Chanzo cha picha, ISLAM DOGRU/ANADOLU VIA GETTY IMAGES

    Ikulu ya Marekani imeiagiza Shirika la Anga za Mbali NASA kuunda kiwango kimoja ya kutambua muda Mwezini. Huu hautakuwa mfumo wa saa kama wa Duniani, lakini utakuwa mfumo wa kuweka saa kwa Mwezi pekee.

    Ukweli ni kwamba nguvu ya mvuto kwenye Mwezi ni ya chini kuliko Duniani, na wakati unasonga haraka huko, mbele ya Dunia na microsekunde 58.7 kwa siku. Hiyo ni, tofauti ya sekunde moja inayojilimbikiza kati ya miaka 46-47.

    Kwa mtazamo wa kawaida, si tofauti kubwa, lakini kwa safari za anga, hata tofauti kama hiyo inaweza kuwa muhimu.

    Duniani, muda hupimwa kwa mamia ya saa za atomiki zilizo kwenye sayari yote, ambazo hutambua mabadiliko ya hali ya nishati ya atomi na kurekodi muda kwa usahihi wa nanosecond.

    Ikiwa saa hizi za atomiki zingewekwa kwenye Mwezi, basi baada ya nusu karne zingekuwa na sekunde moja kwa kasi zaidi kuliko zile za Duniani.

    NASA sio shirika pekee linalotaka kuweka wakati wa mwezi. Shirika la Anga za Juu la Ulaya pia linatengeneza mfumo wake wa kuweka muda.

    Kwa hivyo bado tutalazimika kukubaliana juu ya wakati mpya na kuunda shirika la kuratibu, kazi ambazo kwa sasa zinafanywa na Ofisi ya Kimataifa ya Uzani na Vipimo.

    Marekani ingependa kufanikisha hilo ifikapo 2026, kwa wakati kwa ajili ya misheni iliyopangwa kufanywa na watu kwenda Mwezini.

    Ujumbe wa Artemis 3 unaahidi kuwa wa kwanza kutua kwenye uso wa mwezi tangu misheni ya Apollo 17 mnamo 1972. Inapangwa kupeleka timu ya wanaanga kwenye ncha ya kusini ya Mwezi, ambapo inaaminika kuwa kuna hifadhi kubwa ya maji ya barafu kwenye volkeno ambapo mwanga wa jua hauingii kamwe.

    Mafanikio ya misheni hii yatahitaji upangaji sahihi kabisa hadi kwenye nanosekunde, kwani tofauti yoyote inaweza kupeleka chombo kwenye obiti isiyo sahihi.

  13. Majaji wakuu waitaka Uingereza kusitisha uuzaji wa silaha kwa Israel

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Majaji watatu wa zamani wa Mahakama ya Juu wameungana na zaidi ya wataalam 600 wa kisheria katika kuitaka serikali ya Uingereza kukomesha mauzo ya silaha kwa Israel.

    Katika barua kwa Waziri Mkuu Rishi Sunak, wanasema uuzaji wa silaha lazima ukomeshwe kwa sababu Uingereza iko katika hatari ya kukiuka sheria za kimataifa.

    Bwana Sunak tayari anakabiliwa na shinikizo la vyama vingi baada ya wafanyikazi saba wa misaada kuuawa na vikosi vya Israeli.

    Siku ya Jumanne, alisema Uingereza ina serikali "makini sana" ya kutoa leseni ya silaha.

    Mauzo ya Uingereza ni ya chini kuliko yale ya nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Ujerumani na Italia, na yamepunguzwa na mabilioni yanayotolewa na msambazaji mkubwa wa silaha, Marekani.

    Lakini marufuku ya Uingereza itaongeza shinikizo la kidiplomasia na kisiasa kwa Israel, wakati ambapo mwenendo wake katika mzozo wa Gaza unachunguzwa upya kimataifa.

    Aliyekuwa rais wa Mahakama ya Juu Lady Hale ni miongoni mwa mawakili zaidi ya 600, wasomi na majaji wakuu waliostaafu ambao wametia saini barua ya kurasa 17.

    Inasema "hatua kali" inahitajika "kuepuka ushiriki wa Uingereza katika ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari".

    Inaongeza kuwa uuzaji wa silaha na mifumo ya silaha kwa Israel "unakiuka’’ majukumu ya serikali chini ya sheria za kimataifa na kuonya juu ya "hatari inayowezekana ya mauaji ya kimbari" huko Gaza.

  14. Israel yasema mashambulizi ya anga ya Gaza hayakuwa makusudi

    xx

    Waziri nchini Israel amekanusha madai kuwa wanajeshi wa Israel waliwaua kimakusudi wafanyakazi saba wa shirika la World Central Kitchen (WCK) huko Gaza.

    Mwanzilishi wa WCK José Andrés ameishutumu Israel kwa kuwalenga wafanyakazi wake "kiutaratibu, gari kwa gari".

    Lakini Nir Barkat, mjumbe wa baraza la mawaziri la vita la Israel, aliiambia BBC kwamba maoni ya Bw Andrés ni "upuuzi".

    Israel inasema mashambulizi yaliyowaua wafanyakazi hao ilikuwa "kosa kubwa" na imeahidi kufanya uchunguzi Kulingana na WCK, msafara wa misaada uligongwa wakati ukiondoka kwenye ghala la Deir al-Balah, "ambapo timu hiyo ilikuwa imepakua zaidi ya tani 100 za chakula cha msaada wa kibinadamu kilicholetwa Gaza kupitia baharini".

    Msafara huo ulikuwa na magari matatu, yakiwemo mawili yasiyopenya risasi, ambayo yalionyesha wazi nembo ya mhisani. Magari hayo yalikuwa umbali wa kilomita 2.5 na yote matatu yalishambuliwa wakati wa shambulio hilo.

    Miili sita ya wafanyakazi wa kigeni wa WCK imepelekwa Misri ili kurejeshwa nyumbani na mwenzao Mpalestina mwenye umri wa miaka 25 alizikwa katika mji wa Rafah, kusini mwa Gaza, siku ya Jumanne.

    WCK ilitangaza kuwa imesitisha shughuli zake siku ya Jumanne, na hivyo kuweka huduma ya misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza mashakani.

    Umoja wa Mataifa pia ulitangaza kuwa unasitisha harakati usiku kwa angalau saa 48 ili kutathmini hali ya usalama.

    Na shirika la pili la msaada, la the American Near East Refugee Aid (Anera), ambalo lilikuwa likifanya kazi kwa karibu na WCK, liliiambia BBC kuwa pia limesimamisha shughuli zake huko Gaza.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametaja shambulizi hilo kuwa lisilo la kukusudia.

    "Inatokea vitani, tunaichunguza hadi mwisho, tunawasiliana na serikali, na tutafanya kila kitu ili jambo hili lisitokee tena," Bw Netanyahu alisema Jumanne.

    Mkuu wa jeshi la Israel Herzi Halevi alitaja tukio hilo kuwa "kosa kubwa" na kusema "halikupaswa kutokea,".

    Rais wa Marekani Joe Biden alilaani shambulizi hilo, akiishutumu Israel kwa kutofanya vya kutosha kuwalinda wafanyakazi wa misaada na raia.

    Zaidi ya wafanyakazi wa misaada 196 wameuawa huko Gaza tangu Oktoba, kulingana na data ya Usalama ya Wafanyakazi wa Misaada inayofadhiliwa na Marekani, ambayo inarekodi matukio makubwa ya ghasia dhidi ya wafanyakazi wa misaada.

  15. Video: Tazama mtu aliyekuwa akiogelea katika bwawa alivyotikishwa na tetemeko Taiwan

    Maelezo ya video, Tazama: Tetemeko la ardhi la Taiwan lilivyomtikisa mtu kwenye bwawa

    Mwanamume mmoja alinaswa na tetemeko la ardhi la Taiwan wakati akiogelea kwenye bwawa la juu la paa la hoteli katika mji mkuu wa Taiwan, Taipei.

    Tetemeko hilo la ukubwa wa 7.4 lilisababisha uharibifu mkubwa na takriban watu tisa wamethibitishwa kufariki.

    Tetemeko hilo ndilo lenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Taiwan katika kipindi cha miaka 25.

  16. Mgonjwa aliyepandikizwa figo ya nguruwe atoka hospitali

    vv

    Chanzo cha picha, Massachussets General Hospital

    Mwanaume wa kwanza kupandikizwa figo iliyobadilishwa vinasaba kutoka kwa nguruwe ameruhusiwa kutoka hospitalini.

    Mtu huyo mwenye umri wa miaka 62 aliruhusiwa kwenda nyumbani, wiki mbili baada ya upasuaji wa dharura katika Hospitali Kuu ya Massachusetts (MGH).

    Upandikizaji wa viungo kutoka kwa nguruwe waliobadilishwa vinasaba haukufanikiwa siku za nyuma.

    Lakini mafanikio ya utaratibu huu hadi sasa yamesifiwa na wanasayansi kama hatua ya kihistoria katika uwanja wa upandikizaji.

    Katika taarifa, hospitali ilisema mgonjwa, Richard "Rick" Slayman wa Weymouth, Massachusetts, alikuwa akipambana na ugonjwa wa figo na alihitaji kupandikizwa kiungo hicho ili kuokoa maisha yake.

    xx

    Chanzo cha picha, Massachussets General Hospital

    Madaktari wake walifanikiwa kupandikiza figo ya nguruwe iliyobadilishwa vinasaba katika mwili wake katika upasuaji ulifanyika kwa saa nne tarehe 16 mwezi Machi.

    Walisema figo ya Bw Slayman sasa inafanya kazi vizuri na kwamba hahitaji kufanyiwa tiba ya dialysis.

    Katika taarifa, Bw Slayman amepokwa kwa furaha uamuzi wa madaktari kumruhusu kuondoka hospitalini.

    Ni "mojawapo ya nyakati za furaha" maishani mwake, alisema.

  17. Spika wa Bunge la Afrika Kusini ajiuzulu

    Nosiviwe Mapisa-Nqakula

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Nosiviwe Mapisa-Nqakula

    Spika wa Bunge la Afrika Kusini Nosiviwe Mapisa-Nqakula amejiuzulu baada ya polisi kuvamia nyumba yake wakati wa uchunguzi wa rushwa.

    Bi Mapisa-Nqakula anatuhumiwa kuitisha hongo ili kupeana kandarasi wakati alipokuwa waziri wa ulinzi.

    Amekana mashtaka na kusema kujiuzulu kwake "hakumaanishi kukubali hatia".

    Alisema kutokana na "uzito" wa uchunguzi hawezi kuendelea na jukumu lake.

    Bi Mapisa-Nqakula mwenye umri wa miaka 67 na mwanaharakati mkongwe wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi aliteuliwa kuwa spika mwaka wa 2021.

    Kabla ya hapo, alihudumu kama waziri wa ulinzi kwa miaka saba.

    Wiki iliyopita mawakili wa Mapisa-Nqakula waliwasilisha ombi la kutaka amri ya mahakama izuie kukamatwa kwake, wakisema ingevunjia heshima yake.

    Siku ya Jumanne, majaji walikataa ombi hilo kwa msingi kwamba suala hilo halikuwa la dharura na hawakuweza kukisia juu ya kukamatwa ambako bado hakujafanyika.

    Bi Mapisa-Nqakula anashtakiwa kwa madai kadhaa ya kuomba hongo ya kiasi cha dola 120,000, kutoka kwa mmiliki wa kampuni ili kupata zabuni ya kusafirisha vifaa vya jeshi nchini Afrika Kusini kutoka kwingineko barani, gazeti la Business Day linaripoti. .

    Kujiuzulu kwakekunajiri kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, ambao baadhi wanaamini unaweza kuwa mgumu kwa chama tawala cha African National Congress (ANC).

    Chama hicho ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1994, kimekuwa kikikabiliwa na tuhuma za mara kwa mara za rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma, jambo ambalo limekuwa suala kuu la uchaguzi.

  18. Hofu kwa wakazi wa Gaza huku mashirika ya misaada yakisitisha shughuli

    XX

    Chanzo cha picha, EPA

    Wapalestina wengi katika Ukanda wa Gaza wanajiuliza jinsi watakavyolisha familia zao baada ya shsirika la misaada la World Central Kitchen (WCK) kusitisha shughuli zake kufuatia mauaji ya wafanyakazi wake saba katika shambulio la anga la Israel.

    Shirika lingine la hisani la Marekani linalofanya kazi nalo, Anera, pia limesitisha huduma zake kwa sababu ya hatari zinazowakabili wafanyakazi wake wa ndani na familia zao.

    Kwa pamoja, walikuwa wakihudumia milo milioni mbili kwa wiki katika eneo lote la Palestina, ambapo Umoja wa Mataifa umeonya kwamba takriban watu milioni 1.1 - nusu ya idadi ya watu - wanakabiliwa na janga la njaa kwa sababu ya vikwazo vya Israel katika utoaji wa misaada, uhasama unaoendelea na kuvunjika kwa mazungumzo ya usitishaji vita.

    Uamuzi wa WCK kusitisha kazi yake pia ulisababisha "kufungiwa" kwa ukanda wa misaada ya baharini kutoka Cyprus, ambao shirika la misaada lilisaidia kuanzisha mwezi uliopita ili kuongeza njia ya misaada kuingia kaskazini mwa Gaza na kuepusha njaa iliyokuwa ikitarajiwa.

    Msafara wa WCK ulishambuliwa Jumatatu usiku ulipokuwa ukisafiri kuelekea kusini kando ya njia ya usaidizi ya pwani iliyoteuliwa na Israel, baada tu ya kupakua zaidi ya tani 100 za chakula kutoka kwa mashua huko Deir al-Balah.

    Soma zaidi:

  19. Hujambo na karibu