‘Mawe yaliporomoka kama risasi’ – manusura wa tetemeko Taiwan
Waokoaji nchini Taiwan wanafanya kazi ya kuwaokoa takribani watu 100 ambao wamekwama, siku moja baada ya kisiwa hicho kukumbwa na tetemeko kubwa zaidi la ardhi katika kipindi cha miaka 25.
Mtu mmoja aliyenusurika anasimulia jinsi tetemeko hilo lilivyoporomosha mawe “kama risasi” katika eneo la mgodi wa makaa ya mawe anakofanya kazi.
Tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.4 lilipiga karibu na eneo la mashariki la Hualien, na kuua watu tisa na kujeruhi zaidi ya 1,000.
Wengine waliokwama chini ya mahandaki na karibu na mbuga ya taifa wameokolewa na helikopta, lakini watu 34 bado hawajulikani walipo.
Ugawaji wa chakula umefanyika kupitia angani kwa watu kadhaa walionasa katika maeneo yaliyoathirika, ripoti za ndani zinasema.
"Mlima ulianza kuporomosha mawe kama risasi, hatukuwa na mahali pa kukimbilia, kila mtu alikimbia kando ya mifuko ya mchanga ili kujificha," manusura, aliyetambuliwa kwa jina lake la pili Chu, aliambia Shirika la Habari la Taiwan.
Watatu kati ya tisa waliofariki walikuwa wasafiri kwenye njia ya kongoro inayoelekea Hifadhi ya Kitaifa ya Taroko, nje kidogo ya Hualien.
Katika mji wa Hualien, mji mkuu wa eneo hilo - juhudi za kutoa msaada zinaendelea, huku wafanyakazi wakitumia vifaa kubomoa majengo kadhaa yaliyoharibiwa.
Pia unaweza kusoma: