Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Wanajeshi wa Israel waliojifanya kuwa madaktari wavamia hospitali na kuwaua wanamgambo 3

Wanajeshi wa Israel wamewauwa wanamgambo watatu ndani ya hospitali ya Jenin, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

Moja kwa moja

Asha Juma and Abdalla Seif Dzungu

  1. Kwa picha: Mazishi ya Wapalestina 3 waliouawa kwa kupigwa risasi na jeshi la Israel huko Jenin

    Duru za kimatibabu za Palestina zimesema kuwa kikosi maalumu cha Israel kimewaua Wapalestina watatu asubuhi ya leo ndani ya hospitali ya Ibn Sina katika mji wa Jenin.

    Habari zilieleza kuwa vijana hao watatu waliuawa baada ya kikosi hicho maalum kuvamia orofa ya tatu ya hospitali hiyo wakiwa wamevalia kiraia na kutumia silaha zilizokuwa na vifaa vya kuzuia sauti.

    Vijana hao watatu ni ndugu wawili Muhammad na Basil Al-Ghazawi na Muhammad Jalamna.

    Jeshi la Israel lilithibitisha kuwa vijana hao watatu ni wa "seli ya kigaidi" yenye uhusiano na Hamas, na operesheni hii ni ya kwanza ya aina yake nchini humo.

  2. Waziri wa Ulinzi wa Israel: Jeshi litahamia mpakani na Lebanon hivi karibuni

    Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Galant alisema jana usiku kwamba jeshi la Israel "litaanza hivi karibuni" harakati kwenye mpaka wa kaskazini na Lebanon.

    Gallant aliwafahamisha wanajeshi walioko karibu na mpaka na Gaza kwamba wangeondoka eneo hilo na kuelekea kaskazini, na akasema kwamba askari wa akiba wataondolewa hatua kwa hatua "kujiandaa kwa operesheni zijazo.

    "Hapo jana, Hezbollah ilitangaza kulenga maeneo 12 ya Israel, na pia kuwaomboleza wanachama wake wawili.

    Mpaka kati ya Lebanon na Israel unashuhudia mashambulizi ya mabomu kati ya jeshi la Israel na Hezbollah.

    Inafaa kukumbukwa kuwa jeshi la Israel lilitangaza mapema kwamba litafanya mazoezi ya kijeshi kwenye mpaka na Lebanon ili kuongeza utayari wake, kwa kuzingatia hali ya wasiwasi inayoendelea na hivi karibuni Hezbollah kuongeza kasi ya mashambulizi yake.

  3. Polisi wa Uingereza wamemkamata mtu aliyehusika na mauaji ya kimbari ya Rwanda

    Mwanamume mmoja amekamatwa huko Gateshead na polisi wanaochunguza mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu yaliyotokea miaka 30 iliyopita nchini Rwanda.

    Mzee huyo mwenye umri wa miaka 69 alihojiwa kuhusu mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambapo watu 800,000 waliuawa.

    Wataalamu kutoka Timu ya Kukabiliana na Uhalifu wa Kivita wa Kupambana na Ugaidi walifanya kazi na Polisi wa Kukabiliana na Ugaidi Kaskazini Mashariki ili kukamata watu hao Alhamisi iliyopita.

    Maafisa walisema kuwa mwanamume huyo ameachiliwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea.

    Timu ya Uhalifu wa Kivita ni kitengo cha kitaifa kinachoendeshwa ndani ya afisi Kupambana na Ugaidi ya Polisi wa mijini.

    Kamanda Dominic Murphy alisema uchunguzi huo unafuatia "tuhuma za makosa makubwa zaidi unaweza kufikiria" na yeyote aliyefanya ukatili huo "atakabiliwa na haki popote alipo duniani".

    Aliongeza: “Kukusanya ushahidi wa kuunga mkono uwezekano wa kufunguliwa mashitaka siku za usoni ni mchakato mgumu unaohitaji bidii na usahihi.

    "Wakati kukamatwa ni hatua muhimu katika uchunguzi wowote, maafisa wataendelea kufanya kazi ili kuendeleza uchunguzi huu."

    Uchunguzi huo hauhusiani na uchunguzi unaoendelea wa uhalifu wa kivita ambao ulizinduliwa mnamo 2018, ukiangazia watu wengine watano wa Uingereza.Kati ya Aprili na Juni 1994, inakadiriwa kuwa Wanyarwanda 800,000 waliuawa katika muda wa siku 100.

  4. Habari za hivi punde, Video: Tazama jinsi Wanajeshi wa Israel waliojifanya kuwa madaktari walivyovamia hospitali na kuwaua wanamgambo 3

    Wanajeshi wa Israel wamewauwa wanamgambo watatu ndani ya hospitali ya Jenin, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

    Kanda za CCTV zilionyesha washiriki wa kitengo cha siri wakiwa wamejigeuza kama matabibu na raia wengine wakipita kwenye korido wakiwa na bunduki zilizoinuliwa.

    Jeshi la Israel lilisema wanamgambo hao walikuwa wamejificha katika hospitali hiyo, na kwamba mmoja alikuwa karibu kutekeleza shambulio hilo.

    Wizara ya afya ya Mamlaka ya Palestina iliishutumu Israel kwa kutekeleza "mauaji mapya ndani ya hospitali".

    Hamas, kundi la Wapalestina wenye silaha ambalo linapigana vita na Israel huko Gaza vilivyochochewa na mashambulizi yake dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba, lilisema kuwa jeshi la Israel "limewaua wapiganaji watatu", akiwemo mmoja wa wanachama wake.

  5. Angola yakanusha kuhusika na meli iliyoshambuliwa na wapiganaji wa Houthi

    Kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Angola ya Sonangol imepuuza ripoti kwamba meli iliyolengwa na wapiganaji wa Houthi wiki iliyopita katika Ghuba ya Aden ilikuwa sehemu ya meli zake.

    Meli hiyo yenye uhusiano na Uingereza iliwaka moto kwa saa kadhaa Ijumaa iliyopita katika Ghuba ya Aden baada ya kushambuliwa kwa kombora lililorushwa na Wahouthi.

    Kundi hilo lenye kuungwa mkono na Iran ambalo makao yake yako Yemen, limesema lililenga meli hiyo kwa jina Marlin Luanda kama hatua ya kujibu "uchokozi wa Marekani na Uingereza".

    Taarifa ya kukana kuwa na uhusiano nayo imewadia baada ya vyombo vya habari vya Angola kuhusisha meli hiyo na Sonangol.

    "Sonangol inaarifu umma kwamba meli ya Marlin Luanda, iliyoshambuliwa hivi majuzi na kombora katika Bahari ya Shamu, si sehemu ya meli zinazomilikiwa na kampuni au za kukodi," kampuni hiyo ilisema katika taarifa iliyoonekana na vyombo vya habari vya ndani.

    Marlin Luanda, inayoendeshwa kwa niaba ya mfanyabiashara wa bidhaa mwenye makao yake Singapore Trafigura, inapeperusha bendera ya Visiwa vya Marshall.

    Trafigura ni mmoja wa wasambazaji wakuu wa dizeli na dizeli ya baharini nchini Angola.

    Pia ni mbia katika kampuni ya Puma Energy, ambayo inadhibiti vituo vya mafuta vya Pumangol nchini Angola.

    Wanahisa wengine katika kampuni ya Puma Energy ni pamoja na Sonangol.

  6. Tazama Video: Afisa wa trafiki anasurika kifo kimiujiza baada ya gari alilolisimamisha kugongwa

    Video ya Dashcam iliyotolewa na Polisi wa barabara kuu ya Oklahoma nchini Marekani inaonyesha mmoja wa maafisa wake akinusurika kifo baada ya gari alilolisimamisha kugongwa

    Katika video hiyo, askari Gregory anaonekana akizungumza na dereva wa gari lililoegeshwa wakati gari lingine linapowagonga, na kumpelekea afisa huyo kuruka.

    "Natumai hii ni hofu yangu ya kazi," Gregory alisema.

    Hakuna aliyepata majeraha mabaya.

    Katika chapisho kwenye Facebook, Doria ya Barabara Kuu ya Oklahoma ilionya dhidi ya "uendeshaji mbaya" na kuwataka madereva kupunguza mwendo na kusogea ikiwa watasimamishwa na trafiki.

  7. CHADEMA: Maoni yetu yamepuuzwa

    Katibu wa chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema, John Mnyika amesema kuwa maoni yao na ya wadau juu ya kushughulikia miswada ya uchaguzi nchini Tanzania yamepuuzwa.

    Moja ya agenda ya maandamano yaliyofanywa na chama hiko siku chache zilizopita ni kushinikiza miswada hiyo kuondolewa bungeni.

    Kupitia ujumbe alioweka katika mtandao wa X, Mnyika ameelezea ratiba iliyowekwa kwenye tovuti ya Bunge, akisema kuwa ‘’miswada mibovu ya uchaguzi na vyama itajadiliwa kuanzia leo mpaka tarehe 2 Februari 2024’’.

    ‘’Inakwenda kupitishwa bila kuanza na mabadiliko au marekebisho ya katiba’’ Mnyika alisema.

    Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wiki iliyopita alisema maandamano hayo yalilenga kuishinikiza serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali kuhusu masuala ya uchaguzi.

    Vilevile chama hicho kiliitaka serikali iondoe Bungeni miswaada inayohusu vyama vya siasa na uchaguzi, ambayo ni muswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya siasa na Sheria ya gharama za Uchaguzi.

    Badala yake, Chadema iliitaka serikali iwasilishe muswada wa kukwamua mchakato wa Katiba mpya kwa kuzingatia mwafaka wa kitaifa.

    Kadhalika, Chadema iliitaka serikali iwasilishe bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpito ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na ule mkuu wa 2025 uwe huru na haki.

    Katika taarifa ya Bunge la Tanzania, mkutano huo umeongezewa wiki moja ya ziada ili kujadili kwa uzito miswada hiyo.

    ‘’Mkutano huu umeongezewa wiki moja kutokana na uzito wa majukumu yaliyopangwa ikiwemo uzito wa Miswada itakayoshughulikiwa”

    Soma zaidi:

  8. Habari za hivi punde, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Imran Khan afungwa jela kwa kuvujisha siri za serikali

    Aliyekuwa waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela katika kesi ambayo alishtakiwa kwa uvujaji wa siri za serikali.

    Bw Khan, ambaye alitimuliwa na wapinzani wake kama Waziri Mkuu mnamo 2022, tayari anatumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi.

    Ametaja mashtaka yote dhidi yake kuwa ya kisiasa.

    Hukumu chini ya sheria ya siri inawadia wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu ambapo amezuiwa kugombea.

    Waziri wa zamani wa mambo ya nje Shah Mahmood Qureshi - makamu mwenyekiti wa chama cha Bw Khan cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) - pia alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na mahakama maalum.

    Kinachojulikana kama kesi ya siri inahusu madai ya uvujaji wa barua za siri za kidiplomasia zilizotumwa na balozi wa Pakistan mjini Washington kwenda Islamabad wakati Bw Khan alipokuwa waziri mkuu.

    Inahusiana na kuonekana kwake katika mkutano wa Machi 2022, mwezi mmoja kabla ya mchezaji huyo wa zamani wa kriketi kuondolewa mamlakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye. Imran Khan alionekana jukwaani, akipunga karatasi ambayo anasema ilionyesha njama za kigeni dhidi yake.

    Alisema ilieleza kwa kina kwamba "wote watasamehewa ikiwa Imran Khan ataondolewa madarakani". Hakutaja nchi hiyo - lakini aliikosoa sana Marekani.

    Upande wa mashtaka ulisema kwamba hatua za Bw Khan ni sawa na kuvujisha waraka wa siri na kuharibu uhusiano wa kidiplomasia.

    Shtaka la mwisho linaweza kusababisha kifungo cha maisha au hata adhabu ya kifo.

    Kesi hiyo imesikilizwa kwa muda wa miezi michache iliyopita ndani ya mahakama maalum iliyoundwa ndani ya jela ambayo Bw Khan amekuwa akishikiliwa tangu Agosti. Vyombo vya habari vya kimataifa havikuruhusiwa kuhudhuria.

    Vyombo vya habari vya eneo viliripoti kwamba hakimu aliambiwa hivi majuzi kuharakisha kesi hiyo.

    Chama cha Bw Khan cha PTI kilisema kitapinga uamuzi wa mahakama na kuuita dhihaka.

    Uchaguzi mkuu utafanyika tarehe 8 Februari, huku kukiwa na madai kuwa PTI inazuiwa na mamlaka kufanya kampeni. Bw Khan anapambana na kesi nyingine nyingi za kisheria.

    Soma zaidi:

  9. Zimbabwe yaanzisha kampeni ya chanjo ya nyumba hadi nyumba ya kipindupindu

    Zimbambwe imeanzisha kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa kipindupindi wakilenga zaidi ya watu milioni mbili dhidi ya ugonjwa huo unaoenezwa kupitia maji.

    Mlipuko wa sasa ambao ulianza mapema mwaka jana umehusishwa na zaidi ya vifo 400 huku zaidi ya watu 21,000 wakisemekana kuambukizwa. Takriban nusu ya idadi hiyo ilihusisha watoto.

    Kampeni ya chanjo inafanywa nyumba hadi nyumba kwa ushirikiano na mashirika ya Umoja wa Mataifa na inalenga raia kuanzia umri wa mwaka mmoja na zaidi.

    Maafisa wa Afya wanatoa kipaumbele kwa wilaya 26 zinazochukuliwa kuwa kitovu cha ugonjwa huo.

    Mlipuko huo umesababisha zaidi ya maambukizi 188,000 na zaidi ya vifo 3,000, hasa Zimbabwe, Msumbiji na Zambia, Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu, Ocha, linasema.

  10. Ecowas: Nigeria yazikosoa nchi zilizojiondoa kutoka jumuiya ya kikanda

    Nigeria imezishutumu Mali, Burkina Faso na Niger kwa kuwakatisha tamaa watu wao baada ya kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas).

    Ni maoni ya kwanza kutoka kwa mwenyekiti wa bodi ya kiuchumi na kisiasa tangu serikali tatu kutangaza uamuzi wao wa kuondoka kwenye Jumuiya hiyo siku ya Jumapili.

    Nchi hizo tatu tayari zilikuwa zimesimamishwa kuendesha shughuli zake kwa Ecowas baada ya mapinduzi ya hivi majuzi.

    Watawala wao wa kijeshi wamejitenga na ukoloni wa zamani wa Ufaransa na kuimarisha uhusiano na Urusi.

    Wakisema kwamba walitaka kurejesha usalama kabla ya kuandaa uchaguzi, waliunda makubaliano ya ulinzi wa pande zote mnamo Septemba yaliyoitwa Muungano wa Nchi za Sahel.

    Wanaishutumu Ecowas kwa kushawishiwa na mataifa ya nje na kushindwa kuwasaidia kukabiliana na ghasia za wanajihadi katika nchi zao.

    Ripoti kutoka Niger siku ya Jumatatu zilisema watu 22 wameuawa katika shambulio linaloshukiwa kuwa la wanajihadi kwenye kijiji karibu na mpaka na Mali.

    Afisa wa eneo hilo alisema watu walikuwa wamewasili Motagatta katika eneo la Tillaberi kwa pikipiki na kuanza kuwafyatulia risasi raia.

    Kujiondoa kwao kutakuwa na madhara makubwa ikizingatiwa kwamba jumuiya inahakikisha usafiri bila visa na haki ya makazi na kufanya kazi katika nchi wanachama, kulingana na uchambuzi wa shirika la habari la AFP.

    Mali, Burkina Faso na Niger zote zilikuwa wanachama waanzilishi wakati Ecowas ilipoanzishwa karibu miaka 50 iliyopita.

    Uhusiano kati ya nchi hizo tatu na Ecowas ulikuwa wa wasiwasi baada ya mapinduzi yaliyofanyika Niger mwezi Julai, Burkina Faso mwaka 2022 na Mali mwaka 2020. Ecowas ilitoa wito kwa nchi zote tatu kurejea kwenye utawala wa kiraia.

    Katika taarifa yake kuhusu kuondoka kwa nchi hizo tatu, wizara ya mambo ya nje ya Nigeria ilizishutumu kwa kutochukua hatua kwa nia njema na kuwakosoa viongozi wao wa kijeshi.

    Wiki iliyopita, Burkina Faso ilitangaza kupokea tani 25,000 za ngano ya bure kutoka Urusi, ambayo ilifungua tena ubalozi wake huko mnamo mwezi Desemba. Ubalozi huo ulikuwa umefungwa tangu kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti.

    Soma zaidi:

  11. Mauzo ya silaha ya Marekani nje ya nchi yafikia rekodi ya juu zaidi 2023, yakiimarishwa na vita vya Ukraine

    Mauzo ya silaha ya Marekani katika nchi za nje yaliongezeka kwa kasi, na kufikia rekodi ya jumla ya $238bn (£187bn), huku uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ukizidisha mahitaji.

    Serikali ya Marekani ilifanya majadiliano ya moja kwa moja ya $81bn katika mauzo, ikiwa ni nyongeza ya 56% kutoka mwaka 2022, Idara ya Ulinzi ilisema.

    Mengine yalikuwa mauzo ya moja kwa moja ya makampuni ya Idara ya ulinzi ya Marekani kwa mataifa ya nje.

    Jirani ya Ukraine, Poland, ambayo kwa sasa iko kwenye harakati za kupanua jeshi lake, ilifanya ununuzi mkubwa zaidi.

    Poland ilinunua helikopta za Apache kwa $12bn, na pia ililipa $10bn kwa mifumo ya makombora ya (Himars) na $3.75bn kwa vifaru vya M1A1 Abrams, idara hiyo ilisema katika ripoti ya mwaka wa fedha wa serikali ya Marekani uliomalizika Oktoba.

    Pia ilitumia $4bn kwa mifumo ya silaha zilizounganishwa za ulinzi wa angani.

    Waziri Mkuu Donald Tusk ameapa kuendeleza kuboresha mpango wa kisasa wa kijeshi wa serikali ya awali ya kihafidhina, ambao ulilenga kuifanya Poland kuwa "kikosi chenye nguvu zaidi cha ardhini barani Ulaya".

    Soma zaidi:

  12. Afcon 2023: Mashabiki walivyosherehekea ushindi wa Ivory Coast dhidi ya Senegal

    Shuhudia nyuso za watu zikipatwa na furaha baada ya mikwaju ya penati kupigwa ambapo iliwapelekea Ivory Coast kushinda 5 kwa 4 dhidi ya Senegal.

    Hawa ni mashabiki kutoka katika mji wa San Pedro waliokuwa wakifuatilia mpira kupitia runinga kubwa zilizowekwa kwenye eneo lililotengwa kwaajili ya mashabiki kuangalizia mpira bure.

    Mataifa hasimu haya kisoka yalishuka dimbani katika uwanja wa Charles Konan Banny katika mji wa Yamoussoukro.

    Mwandishi wa BBC @frankmavura aliyepo nchini Ivory alishuhudia shangwe hizo.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Polisi wawakamata wanaume watano juu ya miili iliyopatikana katika jangwa la California

    Polisi wamewakamata watu watano baada ya miili kadhaa kupatikana imepigwa risasi katika eneo la mbali kusini mwa Jangwa la Mojave huko California.

    Miili sita ilipatikana baada ya mwathiriwa aliyepigwa risasi aitwaye 911, kutuma helikopta ya polisi kwenye eneo la uhalifu mbaya.

    Wachunguzi wa Ofisi ya San Bernardino Sherriff walisema Jumatatu kwamba mzozo huo unaonekana kuhusishwa na uzalishaji haramu wa bangi.

    Wanne kati ya waathiriwa sita wametambuliwa hadi sasa, polisi walisema.

    Miili hiyo - yote ya wanaume - ilipatikana mnamo Januari 23 nje ya barabara kuu karibu na mji wa El Mirage, ulioko katika Kaunti ya San Bernardino. Waathiriwa wote sita walifariki kutokana na majeraha ya risasi, polisi walisema.

    Wanne kati ya waathiriwa pia walikuwa wameungua vibaya sana, Sgt Michael Warrick aliwaambia wanahabari siku ya Jumatatu.

    Uchunguzi ulianza wakati wahudumu wa dharura wa 911 walipopokea simu kutoka kwa mmoja wa waathiriwa akiripoti kwamba alikuwa na jeraha la risasi.

    Helikopta ya polisi ilitolewa na kuwapata waathiriwa, pamoja na SUV na gari dogo lililojaa risasi saa 20:15 saa za eneo (04:15 GMT), takriban 144km kaskazini mashariki mwa Los Angeles.

    Wanaume wanne kati ya hao walipatikana karibu na kila mmoja, huku mwingine akiwa ndani ya gari. Maafisa waligundua mwili wa mwisho umbali mfupi.

    Picha za angani za eneo la tukio zilionekana kuonyesha gari hilo aina ya SUV likiwa na risasi na alama ya madirisha yaliyopasuka na mabaki ya moto.

    "Kulingana na nia, tuna imani kuwa huu unaonekana kuwa mzozo kuhusu bangi," Sgt Warrick alisema.

    Katika taarifa ya habari, ofisi ya sheriff ilisema kwamba "wachunguzi walidhania waathiriwa walikuwa wamepanga kukutana katika eneo hilo kwa mabadilishano ya bangi".

    Wanaume watano ambao wamekamatwa "walifika katika eneo hilo, na kwa sababu ambazo bado zinachunguzwa, waliwapiga risasi waathiriwa sita".

    Bunduki nane zimetwaliwa na wachunguzi na zinafanyiwa uchunguzi kubaini iwapo zilitumika katika mauaji hayo.

    Maafisa walikataa kutoa maoni yao iwapo mauaji hayo yalihusiana na genge, badala yake waliyahusisha na "uhalifu uliopangwa".

    Bangi imehalalishwa kununuliwa na watu wazima na kwa matumizi huko California tangu 2016, lakini soko haramu bado linaendeleza bangi isiyotozwa ushuru.

    Soma zaidi:

  14. Elon Musk atangaza kipandikizi cha kwanza kwenye ubongo wa binadamu kisichotumia nyaya

    Bilionea wa kiteknolojia Elon Musk amesema kwa mara ya kwanza kampuni yake ya Neuralink imefanikiwa kupandikiza kifaa maalum cha eletroniki kwenye Ubongo wa binadamu kisichotumia nyaya.

    Inatarajiwa kuwa kifaa hicho kuwa kiunganishi cha ubongo na kitawasaidia watu waliopooza viungo vyote kudhibiti vifaa kwa kutumia mawazo yao pekee.

    Akiandika kwenye mtandao wake wa X, Musk alisema matokeo ya awali yamegundua kuimarika kwa mishipa ya neva na kwamba mgonjwa aliyefanyikwa upasuaji huo aliripotiwa kupona vizuri kutokana na operesheni ya Jumapili.

    Lengo la kifaa hicho ni kutenda kama kiunganishi na ubongo kwa kusaidia kukabiliana na hali matatizo ya neva, kama vile kuruhusu watu waliopooza kudhibiti vifaa kama simu na kompyuta wakitumia fikra zao.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Wenyeji Ivory Coast wawaondoa mabingwa watetezi Senegal kutoka Afcon

    Wenyeji Ivory Coast waliwaondoa mabingwa watetezi Senegal kwa mikwaju ya penalti ili kujikatiatiketi ya robo-fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 kufuatia sare ya 1-1 baada ya muda wa ziada mjini Yamoussoukro.

    Franck Kessie, ambaye alifunga mkwaju wa penalti dakika nne kabla ya mechi kukamilika muda wa kawaida, na kuwapatia wenyeji ushindi muhimu, ambaouliwawezesha kujikomboabaada yamwanzo mbaya katika hatua ya makundi na kupelekea kushindwa mara mbili.

    Senegal walikuwa wamenzavizuribaada ya Habib Diallo kufunga dakika ya nne kutoka kwa krosi ya Sadio Mane.

    Robo fainali ya The ElephantsJumamosi (17:00 GMT) itawakutanisha na Mali au Burkina Faso, ambao watacheza mechi yao ya hatua ya 16 bora huko Korhogo Jumanne (17:00 GMT).

    Pia unaweza kusoma:

  16. Wanajeshi watatu wa Marekani waliouawa katika shambulizi la Jordan watambuliwa

    Serikali ya Marekani imetoa majina ya wanajeshi watatu waliouawa katika shambulizi la ndege isiyo na rubani huko Jordan siku ya Jumapili.

    Sgt William Jerome Rivers, 46, Mtaalamu Kennedy Ladon Sanders, 24 na Mtaalamu Breonna Alexsondria Moffett, 23 waliuawa wakati ndege isiyo na rubani iliposhambulia eneo lao la makazi.

    Marekani imelaumu makundi yanayoungwa mkono na Iran kwa shambulio hilo na Pentagon na kusema limefuata "nyayo" za Hezbollah.

    Pentagon pia ilisisitiza kuwa Marekani haitaki vita na Iran.

    "Hatutafuti vita, lakini tutachukua hatua, na kujibu mashambulizi dhidi ya vikosi vyetu," alisema msemaji wa Pentagon Sabrina Singh.

    CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani, alisema iliambiwa na afisa wa Marekani kwamba ndege isiyo na rubani iliyotumiwa katika shambulio hilo inaonekana kuwa ya Iran.

    Afisa huyo alisema ni "aina ya ndege isiyo na rubani ya Shahed," droni ambayo Iran imekuwa ikitoa kwa Urusi.

    Hata hivyo, Iran imekanusha shutuma za Marekani na Uingereza kwamba inaunga mkono makundi ya wanamgambo wanaolaumiwa kwa shambulizi hilo.

    Pentagon ilisema wanajeshi watatu waliouawa Jumapili asubuhi walitoka katika kitengo cha wanajeshi wa akiba kilichopo Fort Moore, katika jimbo la Georgia.

    Lt Jenerali Jody Daniels, Mkuu wa Hifadhi ya Jeshi na Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Akiba ya Marekani, alitoa pongezi kwa wanajeshi waliofariki.

    "Kwa niaba ya Jeshi la Akiba, ninashiriki katika majonzi waliyonayo marafiki, familia, na wapendwa wao. Utumishi na kujitolea kwao havitasahaulika, na tumejitolea kusaidia wale walioachwa nyuma kutokana na mkasa huu". Alisema Gen Daniels.

    Shambulio hilo la ndege zisizo na rubani lilifanyika Rukban, kaskazini-mashariki mwa Jordan, karibu na mpaka wa Syria. Kituo hicho kilitajwa baadaye na maafisa wa Marekani kama Tower 22.

    Soma zaidi:

  17. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 30/01/2024.