Kuna 'uwezekano mkubwa' mateka walikuwa katika hospitali ya Al-Shifa - Netanyahu

Maafisa wa Israel wanasema wanajeshi walipata mwili wa Yehudit Weiss mwenye umri wa miaka 65 karibu na hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza.

Moja kwa moja

  1. Mamlaka ya barabara kuu Kenya yatoa ushauri wa trafiki baada ya barabara kuzama na mafuriko Mjini Kilifi

    .

    Chanzo cha picha, Courtesy/Kenha

    Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA) imetoa ushauri wa trafiki kufuatia mafuriko yaliosababisha na kusababisha mafuriko makubwa katika eneo la kinamasi la Kwa Kadzengo karibu na Mtwapa katika Kaunti ya Kilifi.

    Kulingana na KeNHA, barabara hiyo kwa sasa haipitiki baada ya kuzama kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo na nchi kwa ujumla.

    “Mamlaka inawashauri madereva wa magari kujizuia na kuwa waangalifu wanaposubiri viwango vya maji vipungue kabla ya magari kurejea katika hali ya kawaida. Eneo hilo kwa sasa linajengwa,” ilisema taarifa Ijumaa jioni.

  2. Mbwa wa rais wa Moldova amng'ata mkono rais wa Austria

    Maelezo ya video, Mbwa wa rais wa Moldova akimng'ata mkono rais wa Austria

    Marais hao wawili walikuwa wakitembea wakati wa tukio hilo

  3. Sudan: Waasi wa Jem huko Darfur wajiunga na jeshi kupigana dhidi ya RSF

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Jeshi la Sudan limepoteza udhibiti wa vituo muhimu katika wiki chache zilizopita

    Makundi mawili ya waasi kutoka eneo la Darfur nchini Sudan yanasema yatapigana pamoja na jeshi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

    Haya yanajiri baada ya wanajeshi wa (RSF) kupata mafanikio makubwa huko Darfur, ambako wameshutumiwa kwa mauaji ya kikabila.

    Kiongozi wa waasi Gibril Ibrahim aliiambia BBC Newsday "wanataka kuwatetea raia wao" kutoka kwa RSF, ambayo anasema imekuwa ikiwazika watu wakiwa hai.

    Alisema uamuzi wa kujiunga na jeshi si jambo rahisi.

    Kiongozi wa vuguvugu la Justice and Equality Movement (Jem) alisema imechukua miezi saba kufikia muafaka.

    Uhusiano kati ya Jem na jeshi la Sudan ni mgumu. Nduguye Bw Ibrahim aliuawa na jeshi, ambaye hapo awali alikuwa kiongozi wa kundi hilo.

    Jem na Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan (SLM) walichukua silaha huko Darfur mwaka 2003, wakiishutumu serikali kwa kuzitenga jamii za Waafrika weusi wa eneo hilo.

    Kisha serikali ilikusanya wanamgambo wa Kiarabu dhidi yao, na kusababisha kile ambacho kimetajwa kuwa mauaji ya halaiki ya kwanza ya Karne ya 21.

    Wanamgambo hawa wamebadilika na kuwa RSF, ambayo imekuwa ikipigana na jeshi kwa udhibiti wa nchi tangu Aprili.

    RSF imechukua miji kadhaa muhimu huko Darfur katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na jiji la pili kwa ukubwa nchini humo, Nyala.

    Wiki iliyopita, kulikuwa na ripoti kwamba walikuwa wameua mamia ya watu katika mji mkuu wa Darfur Magharibi wa El Geneina.

    RSF imekanusha kuhusika na mauaji hayo, ikisema ni sehemu ya "mzozo wa kikabila".

  4. Snoop atangaza kuacha ‘uvutaji’ baada ya miaka mingi ya matumizi ya bangi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Vibao vya rapa huyo ni pamoja na Who Am I? (What's My Name) na Drop It Like It's Hot

    Msanii wa muda mrefu kutoka nchini Marekani Snoop Dogg, ambaye amejitengenezea umaarufu kutokana na uvutaji wake wa bangi amesema kwamba ameacha kuvuta bangi

    Msanii huyo wa muziki wa Pop, ambaye jina lake halisi ni Calvin Broadus, alitoa tangazo hilo la kushtukiza kwenye mitandao ya kijamii.

    "Baada ya kufikiria na kufanya majadiliano mengi na familia yangu, nimeamua kuacha kuvuta sigara. Tafadhali heshimu faragha yangu kwa wakati huu," alichapisha kwenye mtandao wake wa Instagram, external na X.,

    Hakutaja ni aina gani ya uvutaji anayoacha, au hata ikiwa alikuwa mkweli.

    Baadhi ya mashabiki walikisia kuwa chapisho hilo lilikuwa miongoni mwa harakati zake kukuza kampuni yake ya bangi Leafs by Snoop

    Wengine walijibu kwa kutoamini.

    "Leo sio siku ya Aprili Fools Snoop," alisema mmoja.

    "Snoop bila moshi ni kama ardhi bila maji," aliongeza mwingine.

    Ro Marley, mtoto wa gwiji wa reggae Bob Marley, alitoa maoni: "Hakuna BBQ tena kwa uncle's... grill imezimwa kwa msimu huu."

    Matumizi ya bangi ya Snoop yamethibitishwa vyema katika muziki wake na mahojiano.

    Rapa huyo mwenye umri wa miaka 52, alitamba kwa mara ya kwanza kwenye albamu ya Dr Dre ya mwaka 1992, The Chronic, ambayo jina lake ni jina la mzaha la bangi ya hali ya juu.

    Kwa miaka mingi, maneno yake yamekuwa na marejeleo mengi ya tabia hiyo.

    "Tutavuta moshi kidogo," alirap kwenye wimbo wake wa pekee wa Gin And Juice. Ushirikiano wa Dr Dre The Next Episode - ambao ulifungua onyesho wakati wa mapumziko ya mechi ya Super Bowl mnamo 2022 - ulibeba maoni: "Vuta bangi kila siku."

    Mnamo 2013, akizungumza na jarida la GQ, msanii huyo alisema alikuwa akivuta bangi 80 kwa siku.

    Alianzisha Leafs By Snoop miaka miwili baadaye. Kampuni hiyo ina utaalam wa kutengeneza aina zake za bangi.

    Ruka Instagram ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa Instagram ujumbe

  5. Blinken arudia msimamo wa Marekani kwamba 'Gaza haiwezi kukaliwa tena na Israel'

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Antony Blinken

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anasema kuwa Hamas "inahatarisha kila mtu, kwa kujichanganya na raia katika hospitali, shule na makazi ya raia".

    Akizungumza na kituo cha Habari cha Marekani ABC siku ya Alhamisi, Blinken aliulizwa ikiwa ana uhakika kwamba kulikuwa na vituo vya amri kwenye mahandaki vilivyo chini ya hospitali ya Al-Shifa. Alisema kwa uthabiti: "Ndiyo."

    Pia aliulizwa kama Marekani inaunga mkono Israel kuwa Gaza baada ya kumalizika kwa vita, na akajibu: "Hatuungi."

    Blinken aliendelea: "Hakuwezi kuwa na eneo litakalokaliwa na Israel Gaza. Vile vile Gaza haiwezi kuendelea kutumika kama jukwaa la kuanzisha mashambulizi ya kigaidi.

    "Tunapaswa kusonga mbele ambapo Wapalestina wana haki za kisiasa na wana uwezo wa kujitawala katika jimbo lao."

  6. Rais wa Kenya atajwa kuwa miongoni mwa watu wanne wanaokabiliana na mabadiliko ya tabianchi Afrika

    .

    Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais

    Rais wa Kenya William Ruto ametajwa na Jarida la Time Magazine kuwa mmoja wa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani wanaochagiza mabadiliko ya tabianchi duniani.

    Uorodheshaji huo unajiri katika wiki ambayo aliongoza likizo ya kitaifa iliyolenga kupanda miti milioni 100 kwa siku moja.

    Bw Ruto alitajwa pamoja na meya wa mji mkuu wa Sierra Leone Freetown, Yvonne Aki-Sawyerr.Msanifu wa Burkinabe-Ujerumani Francis Kéré na mjasiriamali wa hali ya hewa wa Ethiopia Kidus Asfaw ni miongoni ya walioorodheshwa

    Orodha hiyo, inayojulikana kama "Time 100 Climate", ilitolewa Alhamisi, na ni jaribio la uzinduzi wa jarida hilo kutaja wale inaowaona kuwa muhimu katika kuangazia na kufanya kitu kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa kote ulimwenguni.

    Time Magazine ilisema ilichagua wale walioorodheshwa kwa "kufanya maendeleo makubwa katika kupambana na mabadiliko ya tabainchi ".

    Jarida hilo pia lilisema kuwa washindi hao walichaguliwa kwa sababu ya juhudi zao katika kupambana na mabadiliko ya hali ya anga

    Bw Ruto amekuwa na sauti katika kujaribu kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa nchini Kenya na Afrika.

    Likizo ya upandaji miti iliyofanyika tarehe 13 Novemba ilikuwa sehemu ya azma yake kubwa kwa Kenya kupanda miti bilioni 15 katika miaka 10.

    Mnamo Septemba, aliandaa Mkutano wa kwanza kabisa wa hali ya hewa barani Afrika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambao ulimalizika kwa tamko la pamoja la kutaka wachafuzi wa mazingira watoe rasilimali zaidi kusaidia mataifa maskini.

    Lakini baadhi ya wanamazingira wamemtaja Bw Ruto kuwa mnafiki kwa kutetea upandaji miti huku akikosa kudhibiti ukataji miti ovyo katika misitu ya umma.

    Mwezi uliopita, mahakama ya mazingira ilisitisha agizo ambalo Bw Ruto alitoa mnamo Juni kuondoa marufuku ya 2018 ya ukataji miti.

  7. Kwa picha: Operesheni ya wanajeshi wa Israeli huko Gaza

    Wakati wanajeshi wa Israel wakiendelea na operesheni zao kaskazini mwa Gaza, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limetoa picha za wanajeshi wake wanaoendesha operesheni katika eneo hilo.

    Hakuna waandishi wa habari wa BBC kaskazini mwa Gaza, na hatujaweza kufikia mawasiliano huko kutokana na kukatika kwa mawasiliano.

    .

    Chanzo cha picha, IDF

    .

    Chanzo cha picha, IDF

    .

    Chanzo cha picha, IDF

  8. Mzozo wa Israel na Palestina: Netanyahu akiri Israel 'haijafanikiwa' kupunguza vifo vya raia

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema juhudi za vikosi vyake kupunguza vifo vya raia mjini Gaza "hazijafanikiwa" - ingawa alimlaumu adui yake.

    Netanyahu alisema jeshi la Israel linafanya kila iwezalo kutokomeza Hamas, lakini kundi hilo linatumia raia kama "ngao".

    Wakati huo huo Jeshi la Ulinzi la Israel linasema limewauwa watu karibu watu watano wenye silaha katika mapigano usiku kucha.

  9. Israel- Gaza: Jeshi la Israel latoa picha za 'mahandaki chini ya hospitali' Gaza

    BBC haiwezi kuthibitisha mara moja picha hii, ambayo Israel inadai kuonyesha vichuguu vinavyoendeshwa na Hamas kwenye uwanja wa hospitali ya Al-Shifa.

    Chanzo cha picha, IDF

    Maelezo ya picha, BBC haiwezi kuthibitisha picha hii, ambayo Israel inadai kuonyesha mahandaki ya Hamas kwenye uwanja wa hospitali ya Al-Shifa.

    Katika saa chache zilizopita, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limechapisha picha na video kwenye X (zamani ikijulikana kama Twitter) ambazo wanasema zinaonyesha mahandaki ya Hamas chini ya hospitali za Gaza.

    BBC haiwezi kuthibitisha picha hizi mara moja.

    "Handaki la magaidi wa Hamas limepatikana ndani ya jengo la Hospitali ya Shifa," ilitweet IDF katika taarifa iliyoambatana na video ambayo, walidai, ilionyesha lango la njia ya chini kwa chini katika uwanja wa hospitali ya Jiji la Gaza.

    IDF pia ilishiriki picha kutoka kwa kile walichosema ni ndani ya "handaki lingine la magaidi" katika hospitali kuu ya watoto ya Gaza, Al-Rantisi.

    Mapema wiki hii, IDF pia ilitoa video kutoka hospitali hiyo hiyo ikidai kupatikana kwa silaha na vilipuzi katika kituo hicho cha matibabu.

    Maelezo zaidi:

  10. Fury v Oleksandr: Mabondia ambao hawajawahi kupigwa wanakutana kuzichapa

    xx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bondia wa Uingereza Tyson Fury (35), atamenyana na Oleksandr Usyk (36) wa Ukraine mjini Riyadh, Saudi Arabia tarehe 17 Februari.

    Fury anajivunia rekodi ya kutopigwa na kushinda mara 34 na sare moja.

    Usyk, 36, ndiye bingwa wa WBA, WBO na IBF huku Fury akishikilia mkanda wa WBC.

    Pambano hili litafanyika miezi michache tangu Fury kupata ushindi mwembamba dhidi ya Francis Ngannou huko Saudi Arabia mwezi Oktoba.

    Usyk naye ameshinda mapambano yake yote 21 na mwezi Agosti alimpiga Daniel Dubois kutoka London.

  11. Matokeo ya uchaguzi wa Liberia: George Weah na Joseph Boakai katika kinyang'anyiro kikali

    Rais George Weah n Kiongozi wa upinzani nchini Liberia Joseph Boakai

    Chanzo cha picha, AFP/REUTERS

    Kiongozi wa upinzani nchini Liberia Joseph Boakai anaongoza kwa asilimia 50.58 dhidi ya Rais George Weah aliye na asilimia 49.42 katika matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais.

    Asilimia tisini ya kura zimeshahesabiwa na tume ya uchaguzi nchini humo.

    Katika duru ya kwanza ya kura, wagombea hao walishindwa kupata zaidi ya asilimia hamisini ya kura.

    Katika duru hii ya pili, mshindi atakayepata kura nyingi kumliko mwenzake hata bila ya kufikisha zaidi ya asilimia hamsini, ndiye atatangazwa mshindi.

    Rais Weah anatafuta muhula wa pili madarakani kwa ahadi za kuboresha elimu,ajira na kukabiliana na ufisadi huku bwana Boakai akiahidi kuinusuru Liberia kutoka kwa uongozi mbovu na usimamizi mbaya wa raslimali za nchi unaofanywa na Weah.

  12. Kuna 'uwezekano mkubwa' mateka walikuwa katika hospitali ya Al-Shifa - Netanyahu

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema kuna "uwezekano mkubwa" kwamba mateka wanaoshikiliwa na Hamas walikuwa katika hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza.

    Ilikuwa "sababu mojawapo iliyotufanya tuingie hospitalini", anasema katika mahojiano na CBS Evening News.

    Israel imewashutumu Hamas mara kwa mara kwa kuwa na kambi kubwa chini ya Al-Shifa - jambo ambalo Hamas inakanusha.

    Vikosi vya Israel vilivamia hospitali ya Al Shifa siku ya Jumatano, lakini Netanyahu anasema walipofika, mateka hawakuwapo tena.

    "Kama walikuwa [huko], walitolewa nje," anasema. Anasema serikali yake ina "intelijensia kuhusu mateka," lakini anaongeza "kadiri ninavyosema kidogo juu yake, bora zaidi".

    Maelezo zaidi:

  13. Mwimbaji Cassie amshutumu Puff Daddy kwa ubakaji na unyanyasaji

    Ventura anasema alikutana na rapa huyo 2005

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ventura anasema alikutana na rapa huyo 2005

    Msanii wa muziki wa rap Sean "Diddy" Combs ametuhumiwa kwa ubakaji na biashara ya ngono na mwimbaji wa kike.

    Katika kesi iliyoonekana na BBC, mpenzi wa zamani Casandra Ventura alisema alikuwa amenaswa kwa muongo mmoja katika mzunguko wa unyanyasaji na vurugu.

    Bw Combs - ambaye pia amejulikana kwa jina la kisanii Puff Daddy - anakanusha madai hayo, akimshutumu mwimbaji huyo kwa kujaribu kumlaghai.

    Wakili wake alisema madai hayo ni "ya kuudhi na ya kuchukiza".

    Bi Ventura - mwimbaji wa muziki wa R&B anayejulikana kwa jina la kisanii Cassie - anadai kuwa nyota huyo wa rap alimbaka na kumpiga kwa zaidi ya miaka 10 kuanzia alipokuwa na umri wa miaka 19.

    "Baada ya kuwa kimya kwa miaka mingi, hatimaye niko tayari kusimulia hadithi yangu," alisema katika taarifa siku ya Alhamisi.

  14. Israel yasema imepata mwili wa mateka huku mawasiliano yakikatizwa Gaza

    Yehudit Weiss

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Israel limesema limepata mwili wa mwanamke ambaye alichukuliwa mateka na wanamgambo wa Hamas karibu na hospitali ya Al Shifa katika ukanda wa Gaza.

    Jeshi hilo limesema walimpata Yehudit Weiss ameuawa walipokuwa wakifanya opresheni yao Al Shifa lakini hawakutoa maelezo zaidi.

    Hayo yanajiri huku mkuu wa hospitali hiyo Muhammud Abu Salmiya akisema wanakabiliwa na janga baada ya kuishiwa maji na gesi ya Oxijini.

    Kuna wagonjwa 650,wahudumu mia tano na takriban watu elfu tano waliotafuta hifadhi ndani ya hospitali hiyo.

    Mawasiliano ya simu na intaneti yamezimwa kote katika Ukanda wa Gaza kwa sababu ya ukosefu wa mafuta.

    Tamara Al-Rifai, wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA ameiambia BBC kuwa kutatizwa huko kwa mawasiliano kutawaathiri mno watu wa Gaza.

    Unaweza pia kusoma:

    • Hezbollah yaonya vita vya kikanda ikiwa mashambulizi Gaza yataendelea
    • Mtoto mmoja huuawa kila baada ya dakika kumi Gaza
    • Nchi ya Amerika Kusini ambayo ina jamii kubwa zaidi ya Wapalestina nje ya Ulimwengu wa Kiarabu na Israeli
    • 'Ninapiga simu kutoka shirika la ujasusi la Israel.Tunarusha bomu, una saa mbili kuondoka’
    • Vita vya Israel na Gaza: Je, uhalifu wa kivita unatekelezwa?, sheria inasemaje?
  15. Ikiwa ndio kwanza unautembelea mtandao wetu, huu ndio muhtasari wa habari kuu za dunia

    • Jeshi la Israel limesema limepata mwili wa mwanamke ambaye alichukuliwa mateka na wanamgambo wa Hamas karibu na hospitali ya Al Shifa katika ukanda wa Gaza.
    • Mawasiliano ya simu na intaneti yamezimwa kote katika Ukanda wa Gaza kwasababu ya ukosefu wa mafuta.
    • Jordan imesema haitasiani makubaliano yaliyopangwa kati yake na Israel ambapo ilikuwa iipe Israel nishati nao wapewe maji.
    • Kiongozi wa upinzani nchini Liberia Joseph Boakai anaongoza kwa asilimia 50.58 dhidi ya Rais George Weah aliye na asilimia 49.42 katika matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais.
    • TikTok imesema inaondoa taarifa katika mtandano wake zinazosambaza barua ilioyoandikwa na aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda Osama bin Laden.
  16. Hujambo na karibu.