Watakao tuma 'picha za ngono za wanafunzi' kukabiliwa na kifungo cha miaka 14 Nigeria
Raia wa Nigeria wameonywa kuwa kutumiana picha za ngono za watoto ni kosa litakalosababisha kifungo cha miaka 14 jela, hii inakujabaada ya video inayodaiwa kuwahusisha watoto wa shule kusambaa nchini humo.
Wanafunzi kutoka shule za kifahari za Chrisland walikuwa katika safari ya kwenda Dubai mwezi uliopita wakati tukio hilo linalodaiwa kurekodiwa kutokea.
Mama wa mtoto wa miaka 10 aliyerekodiwa katika video hiyo anasema binti yake alilazimishwa kushiriki.
Serikali katika jimbo la Lagos imeamuru kufungwa kwa shule hiyo ili "kesi inayodaiwa kuwa ya unyanyasaji wa kingono" iweze kuchunguzwa.
Katika video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii, mama huyo anadai binti yake alileweshwa na wanafunzi wa kiume na kushutumu mamlaka za shule kwa kuficha tukio hilo.
Shule za Chrisland, ambazo zinaendesha shule binafsi kadhaa za msingi na sekondari katika jiji la Lagos, zimekanusha kufanya makosa yoyote, zikisema inatekeleza jukumu lake la kutunza kwa uzito na itatoa ushirikiano kwa uchunguzi wowote.
Kwa mujibu wa shule hiyo, watoto walikuwa wakicheza mchezo wa "Ukweli au kuthubutu" (Truth or Dare) uliohusisha wanafunzi watano kati ya 76 waliohudhuria Michezo ya Shule ya Kimataifa kati ya Machi 8 na 14.
Ilisema iliwajulisha wazazi wao juu ya "utovu huo wa nidhamu" na wanafunzi hao wamepewa karipio kwa mujibu wa kanuni za shule.
Lakini mama wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka 10 anasema hakuambiwa uzito wa kile kilichotokea mwanzoni, lakini aligundua baadaye wakati mzazi mwingine alipomtahadharisha kuhusu kanda hiyo ya video, ambayo tangu wakati huo imekuwa ikisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.
Alipomhoji binti yake, aligundua kuwa binti yake alikuwa ameambiwa asizungumze kuhusu kilichotokea.
Kwa mujibu wa mama yake mtoto wake sasa amesimamishwa shule.