Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amejiuzulu

Trudeau amesema atakaa madarakani hadi Chama chake cha Liberal kiweze kuchagua kiongozi mpya, na bunge litaahirishwa - au kusimamishwa - hadi Machi 24.

Muhtasari

Moja kwa moja

Ambia Hirsi, Mariam Mjahid & Rashid Abdallah

  1. Kwaheri hadi kesho

    Na hapa ndio mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, tukutane kesho.

  2. Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amejiuzulu

    Kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa chama chake, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau ametangaza kujiuzulu na kumaliza kipindi chake cha miaka tisa ya uongozi.

    Trudeau amesema atakaa madarakani hadi Chama chake cha Liberal kiweze kuchagua kiongozi mpya, na bunge litaahirishwa - au kusimamishwa - hadi Machi 24.

    "Nchi hii inastahili chaguo bora katika uchaguzi ujao na imedhihirika kwamba ikiwa nalazimika kupigana vita vya ndani, siwezi kuwa chaguo bora katika uchaguzi huo," amesema wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jumatatu.

    Trudeau aliingia madarakani mwaka 2015, akiwa na umri wa miaka 43 wakati huo, aliahidi aina mpya ya siasa inayozingatia sera za wazi juu ya uhamiaji, kuongeza kodi kwa matajiri na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

  3. Rais wa zamani wa Ufaransa afikishwa mahakamani akituhumiwa kupokea pesa kutoka kwa Gaddafi

    Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy amefikishwa mahakamani siku ya Jumatatu, kwa tuhuma za kupokea mamilioni ya euro za ufadhili usio halali katika kampeni za kugombea urais 2007, kutoka kwa hayati Rais wa Libya Muammar Gadaffi.

    Sarkozy amekuwa akikana mashtaka hayo na kesi hiyo itaendelea kwa muda wa miezi mitatu.

    Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha kihafidhina anakabiliwa na mashtaka ya "kuficha ubadhirifu wa fedha za umma, ufisadi, ufadhili haramu wa kampeni na njama ya kufanya uhalifu," imesema ofisi ya mwendesha mashtaka wa fedha.

    Waendesha mashitaka wanasema mwaka 2005, Sarkozy, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa wakati huo, aliafikiana na Gaddafi, ili kupata ufadhili wa kampeni ili kuiunga mkono serikali yake katika uwanja wa kimataifa ambapo ilikuwa imetengwa.

    Gaddafi aliondolewa madarakani kisha kuuawa mwaka 2011.

    Wachunguzi wanadai alifanya mapatano ya kifisadi na serikali ya Libya, yaliyohusisha majasusi wa Libya, gaidi aliyepatikana na hatia, wauzaji silaha na madai kwamba Gaddafi alitoa pesa kufadhili kampeni ya Sarkozy na pesa hizo kusafirishwa hadi Paris katika masanduku.

    Wakili wa Sarkozy amesema kesi dhidi ya rais huyo wa zamani ni uzushi na hakuna ufadhili wa pesa kutoka Libya katika kampeni yake.

    Iwapo atapatikana na hatia, Sarkozy anaweza kufungwa jela hadi miaka 10 na faini ya euro 375,000 ($386,000).

    Sarkozy katika miaka ya hivi karibuni amekabiliwa na safu ya kesi za kisheria. Mwezi Desemba, mahakama ya juu zaidi ya Ufaransa ilikubali hukumu dhidi yake juu ya rushwa na kutafuta upendeleo kutoka kwa jaji.

    Sarkozy ameagizwa kuvaa bangili ya kielektroniki kwa mwaka mmoja badala ya kwenda jela, ikiwa ni mara ya kwanza kwa rais wa zamani wa Ufaransa kuamriwa hivyo.

    Katika kesi nyingine, Sarkozy alipatikana na hatia ya kuficha matumizi haramu ya kampeni, na kesi hiyo inasubiria.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Polisi wanane wauawa katika shambulio huko India

    Takriban polisi wanane na dereva mmoja wameuawa katika mlipuko wa bomu uliotekelezwa na waasi wa kundi la Mao katika jimbo la kati la India la Chhattisgarh, polisi wamesema siku ya Jumatatu.

    Gari la polisi ambalo waathiriwa walikuwa wakisafiria lilikumbwa na mlipuko katika wilaya ya Bijapur katika jimbo hilo siku ya Jumatatu, imesema taarifa ya polisi.

    Hili ni tukio la hivi punde zaidi katika mfululizo wa mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya vikosi vya usalama katika jimbo hilo. Pia kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya vikosi na waasi.

    Chhattisgarh na majimbo yake jirani katikati na mashariki mwa India yameathiriwa na uasi wa miongo kadhaa wa waasi wa Mao.

    Waasi hao wenye itikadi za kikomunisti za kiongozi wa zamani wa China, Mao Zedong, wameendesha mashambulizi ya kuvizia kutokea msituni dhidi ya serikali, na kusababisha mapigano ya mara kwa mara na majeruhi kwa pande zote mbili.

    Wafuasi wa Mao wanasema wanapigania kuwapa wakulima maskini wa India na vibarua wasio na ardhi udhibiti zaidi wa ardhi yao na madini ambayo kwa sasa wanadai yananyonywa na makampuni makubwa ya uchimbaji madini.

  5. Waziri Mkuu wa Canada anatarajiwa kutangaza kujiuzulu - ripoti

    Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau huenda akatangaza kujiuzulu ndani ya siku chache, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

    Anafikiria kujiuzulu kama kiongozi wa chama tawala cha Liberal, na kumaliza miaka yake tisa kama Waziri Mkuu.

    Ni kufuatia miezi kadhaa ya shinikizo kutoka kwa wabunge wa chama chake. Mwezi uliopita, waziri wake wa fedha alijiuzulu, akitoa sababu za kutokuelewana kuhusu jinsi ya kukabiliana na tishio la Donald Trump la kutoza ushuru mkubwa kwa bidhaa za Canada.

    Kura za maoni zinaonyesha Chama cha Liberal cha Trudeau kinpo nyuma ya chama cha Conservatives huku uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu ukikaribia.

    Zaidi ya dazeni ya wabunge wake wamemtaka aondoke madarakani, huku kura za maoni zikionyesha thuluthi mbili ya wapiga kura wanampinga.

    Gazeti la Globe and Mail linaripoti kwamba anaweza kutangaza nia yake ya kujiuzulu kabla ya kikao cha chama chake siku ya Jumatano, ili kuepusha dhana kwamba wabunge wake walimlazimisha kuondoka.

    Vyanzo vyao vinasema haijulikani ikiwa Trudeau ataondoka moja kwa moja au ataendelea kuwa Waziri Mkuu hadi kiongozi mpya atakapochaguliwa. Lakini vyanzo hivyo vimesisitiza kuwa bado hajafanya uamuzi wa mwisho juu ya mustakabali wake.

    Aliingia madarakani mwaka 2015, akiwa na umri wa miaka 43 wakati huo, aliahidi aina mpya ya siasa inayozingatia sera za wazi juu ya uhamiaji, kuongeza kodi kwa matajiri na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Waisraeli watatu wauawa kwa kupigwa risasi katika Ukingo wa Magharibi

    Waisraeli watatu wameuawa siku ya Jumatatu na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la risasi kwenye gari na basi karibu na mji wa Kedumim katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na na Israel, imesema taasisi ya huduma za gari la wagonjwa ya Israeli Magen David Adom (MDA).

    Redio ya Jeshi la Israel imesema jeshi limeweka uzio kuzunguka vijiji vyote vya eneo hilo ili kuwasaka washukiwa hao, ambao inaamini walikimbilia kijiji cha karibu cha Wapalestina.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwafikisha wahusika na yeyote atakayewasaidia mbele ya sheria. "Hakuna atakayesalia," alichapisha kwenye X.

    Hakukuwa na taarifa ya mara moja kutoka kwa mamlaka ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi. Lakini Hamas, kundi la wanamgambo ambalo linaendesha Ukanda wa Gaza, limesifu mashambulizi hayo kama "jibu la kishujaa dhidi ya uhalifu unaoendelea wa uvamizi na mauaji ya halaiki huko Gaza," lakini hawakudai kuhusika.

    Ghasia katika Ukingo wa Magharibi zimekuwa zikiongezeka, huku mamia ya Wapalestina na makumi ya Waisraeli wakiuawa tangu shambulio la Oktoba 7, 2023 la wanamgambo wa Hamas kusini mwa Israel lilipoanzisha vita huko Gaza.

    Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema amewaagiza wanajeshi "kuchukua hatua za nguvu" katika kukabiliana na mashambulizi hayo, na kusema kuwa yeyote atakayefuata njia ya Hamas "atalipa gharama kubwa."

    MDA imesema wanawake wawili wenye umri wa miaka 60 na mwanaume mmoja wa miaka 40 walikutwa wamefariki dunia katika eneo la tukio, huku abiria saba wakijeruhiwa akiwemo dereva mwenye umri wa miaka 63 ambaye hali yake ni mbaya.

    Maelfu ya Waisraeli wameweka makazi katika Ukingo wa Magharibi tangu Israel ilipoteka eneo hilo katika vita vya 1967. Nchi nyingi zinaona makazi hayo kuwa haramu, ingawa Israelil inapinga hilo, ikitoa hoja ya uhusiano wa kihistoria wa kibiblia na ardhi hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Tembo amuua mtalii aliyekuwa akimwogesha nchini Thailand

    Tembo amemuua mwanamke mmoja raia wa Uhispania alipokuwa akimwogesha mnyama huyo katika kituo cha tembo nchini Thailand, wamesema polisi wa eneo hilo.

    Blanca Ojanguren García, 22, alikuwa akiosha tembo katika Kituo cha Kutunzia Tembo cha Koh Yao, siku ya Ijumaa iliyopita alipouawa kwa kupigwa na pembe za tembo.

    Wataalamu wa tembo waliliambia gazeti la lugha ya Kihispania, Clarín kwamba huenda tembo huyo alikuwa na hofu baada kulazimika kutangamana na watalii nje ya makazi yake ya asili.

    García, mwanafunzi wa sheria na mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Navarra nchini Uhispania, alikuwa akiishi Taiwan kama sehemu ya mpango wa kubadilishana wanafunzi.

    Alikuwa katika matembezi nchini Thailand akiwa na mpenzi wake, ambaye alishuhudia shambulio hilo.

    Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania, Jose Manuel Albares, amesema ubalozi mdogo wa Uhispania huko Bangkok unaisaidia familia ya García.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Mwili wa mwandishi wa habari aliyetoweka wapatikana kwenye tanki la maji taka

    Mwili wa mwandishi wa habari wa India ambaye aliripoti kuhusu madai ya ufisadi nchini humo umepatikana kwenye tanki la maji taka katika jimbo la Chhattisgarh.

    Mukesh Chandrakar, 32, alipotea siku ya mwaka mpya na familia yake ilitoa taarifa polisi.

    Mwili wake ulipatikana Ijumaa katika eneo la ujenzi wa barabara katika mji wa Bijapur baada ya maafisa kufuatilia simu yake ya mkononi.

    Watu watatu wametiwa mbaroni kuhusiana na kifo chake, wakiwemo jamaa zake wawili.

    Polisi katika wilaya ya Bijapur hawakupata chochote wakati wa operesheni ya kwanza kwenye eneo hilo tarehe 2 Januari.

    "Hata hivyo, baada ya ukaguzi zaidi tarehe 3 Januari, tuligundua mwili wa Mukesh kwenye tanki la maji taka," amesema afisa mkuu wa polisi wa eneo hilo.

    Polisi wamesema mwili wake ulionyesha majeraha mabaya.

    Bw Chandrakar, ni mwandishi wa habari wa kujitegemea, aliripoti sana juu ya tuhuma za ufisadi katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umma.

    Imeripotiwa katika vyombo vya habari vya India kuwa mmoja wa waliokamatwa kutokana na kifo cha mwanahabari huyo ni binamu yake.

    Waandishi wa habari wa eneo hilo wamefanya maandamano wakitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wanaodaiwa kuwa wahusika.

    Shirika la uangalizi wa vyombo vya habari la Reporters Without Borders linasema wastani waandishi watatu au wanne wanauawa kila mwaka nchini India na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi hatari zaidi duniani kwa vyombo vya habari.

  9. Wakenya wanne kati ya waliopotea wapatikana wakiwa hai

    Takribani Wakenya wanne walioripotiwa kutoweka wamepatikana wakiwa hai, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti leo asubuhi.

    Habari hizi zinajiri huku kukiwa na wimbi la kutoweka kwa watu ambalo limeikumba nchi hiyo ya Afrika Mashariki, huku Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya ikifichua kuwa Wakenya 82 wametekwa nyara katika muda wa miezi sita iliyopita.

    Wengi wa waathiriwa wa utekaji wanaaminika ni wakosoaji vijana wa serikali. Kutoweka huko kumezua hasira kubwa, huku wanaharakati wakipanga duru nyingine ya maandamano leo - ambayo yatakuwa maandamano ya pili ya kupinga utekaji nyara ndani ya wiki mbili.

    Katika taarifa ya Jeshi la Polisi la nchi hiyo imemtaja Bernard Kavuli Musyimi kuwa amepatikana leo baada ya kufika kituo cha polisi, na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

    Wengine watatu waliotajwa katika taarifa ya polisi ni Billy Wanyiri Mwangi, Peter Muteti na Rony Kiplagat, ambao tayari wameungana na famili zao na Polisi inawasiliana nao kwa ajili ya uchunguzi zaid.

    Wiki iliyopita, Chama cha Wanasheria nchini Kenya kiliwasilisha kesi ya kisheria dhidi ya serikali, kikitaka kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa watu saba waliotekwa nyara mwezi uliopita.

    Katika taarifa yake, Rais William Ruto alikiri uwepo wa utekaji nyara na kuapa kukomesha utekaji huo, "tutakomesha utekaji nyara ili vijana wetu waishi kwa amani."

    Hali hiyo inaendelea kuzua hofu kote nchini, huku wazazi wakiwa na wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wao na wanaharakati wakiapa kuendelea na shinikizo hadi watu wote waliopotea wapatikane.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mkuu wa jeshi la Uganda asema anataka kumkata kichwa Bobi Wine

    Mkuu wa jeshi la Uganda Generali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais wa muda mrefu Yoweri Museveni, amesema anataka kumkata kichwa kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo Bobi Wine.

    Kainerugaba mara kwa mara hutoa machapisho yenye utata kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na tishio la 2022 la kutaka kuivamia nchi jirani ya Kenya.

    Katika chapisho kwenye X Jumapili jioni, Kainerugaba alisema babake aliyeitawala Uganda tangu 1986, ndiye mtu pekee anayemlinda kiongozi wa upinzani Bobi Wine dhidi yake.

    "Kama Mzee hakuwepo, ningemkata kichwa leo," ameandika Kainerugaba.

    Bobi Wine, ambaye jina lake ni Robert Kyagulanyi, alimaliza wa pili nyuma ya Museveni katika uchaguzi wa urais wa 2021, alijibu kupitia X kwamba hapuuzi vitisho hivyo, na kusema kumekuwa na majaribio kadhaa ya kuuawa siku za nyuma.

    Kainerugaba alijibu: "Hatimaye! Nimekuamsha? Kabla sijakukata kichwa, uturudishie pesa tulizokukopesha," akidai kuwa hapo awali serikali ilikuwa imemnunua Wine ili kudhoofisha upinzani.

    Wasemaji wa serikali na Kainerugaba mwenyewe hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao. Huku msemaji wa jeshi akikataa kutoa maoni yake.

    Wine, mwanamuziki maarufu aliyegeuka kuwa mwanasiasa ni mpinzani mwenye nguvu dhidi ya Museveni. Alikataa matokeo ya uchaguzi wa 2021, kwa madai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Tanzania: Mtalii wa Israel afariki katika hifadhi ya Ngorongoro

    Mtalii wa Israel ambaye utambulisho wake haujabainishwa (mwanamke) amefariki na wengine watano kujeruhiwa katika ajali ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA)

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumapili Januari 5, 2025 na Kaimu Meneja Uhusiano wa NCAA, Hamis Dambaya, ajali hiyo iliyotokea Jumamosi usiku wa manane ilihusisha gari la watalii.

    "Ajali hiyo ilitokea kati ya eneo la mwonekano na lango kuu la Loduare. Gari hilo lilikuwa na watu saba, sita kati yao wakiwa ni raia wa Israel na Mtanzania mmoja ambaye alikuwa dereva," ilisema taarifa hiyo.

  12. Korea Kaskazini yarusha kombora la kwanza la balestiki katika muda wa miezi miwili: Seoul

    Korea Kaskazini imerusha kombora linaloonekana kuwa la masafa ya kati kuelekea bahari ya mashariki, jeshi la Korea Kusini lilisema, ikiwa ni hatua ya kwanza ya Pyongyang katika kipindi cha miezi miwili.

    Kombora hilo lilipaa kilomita 1,100 kabla ya kuanguka baharini, jeshi lilisema, na kuongeza kuwa "linalaani vikali" "kitendo hiki cha wazi cha uchochezi".

    Hatua hiyo inakuja wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiitembelea Seoul kwa mazungumzo na baadhi ya viongozi wakuu wa Korea Kusini.

    Mapema Jumatatu, Blinken alikutana na kaimu rais Choi Sang-mok, ambapo alielezea muungano kati ya Washington na Seoul kama "msingi wa amani na utulivu kwenye rasi ya Korea".

    Jeshi la Korea Kusini linasema kuwa limeimarisha ufuatiliaji kwa ajili ya kudhibiti hatua za Korea Kaskazini siku zijazo na "linashiriki kwa karibu habari" ya kurushwa kwa kombora la leo na Marekani na Japan.

  13. Hamas waorodhesha majina ya mateka 34 wanaonuia kuwaachia huru

    Afisa mwandamizi wa Hamas ameikabidhi BBC orodha ya mateka 34 ambao kundi la Wapalestina linadai kuwa lipo tayari kuwaachia huru katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel.

    Haijulikani ni wangapi kati ya mateka hao bado wako hai.

    Miongoni mwa walioorodheshwa ni wanawake 10 na wanaume wazee 11 wenye umri kati ya miaka 50 na 85, pamoja na watoto wadogo ambao Hamas ilisema awali waliuawa katika shambulio la angani la Israel.

    Pia kuna baadhi ya mateka waliodaiwa kuwa ni wagonjwa, ambao pia wamo kwenye orodha hiyo.

    Ripoti kutoka Gaza inayosimamiwa na Hamas zinasema kwamba mashambulizi ya angani ya Israel yaliua zaidi ya watu 100 huko mwishoni mwa juma.

    Hata hivyo, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ilikanusha taarifa kwamba Hamas imetoa orodha ya mateka kwa Israel.

    Mazungumzo ya kusitisha mapigano yaliendelea Doha, Qatar, mwishoni mwa juma, lakini mazungumzo hayo hayajafikia mafanikio makubwa hadi sasa.

    “Kufikia sasa, uvamizi unaendelea kuwa mgumu juu ya makubaliano ya masuala ya kusitisha mapigano na kujiondoa, na hakuna hatua iliyochukuliwa,” alisema afisa huyo wa Hamas akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

    Awali, Hamas ilichapisha video ya mateka wa Israeli mwenye umri wa miaka 19, Liri Albag, akihimiza serikali yake kufikia makubaliano. Alikamatwa pamoja na askari wanawake sita wa jeshi kwenye kambi ya Nahal Oz, kwenye mpaka wa Gaza, wakati wa shambulio la Hamas mnamo Oktoba 7, 2023.

    Kampeni ya kijeshi ya Israel ya kukabiliana na kundi la Hamas imesababisha vifo vya watu wasiopungua 45,805 katika Gaza kufikia Jumamosi, kwa mujibu wa wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.

    Chanzo hicho hicho kinadai kuwa mashambulizi ya angani ya Israel yaliua watu 88 Gaza Jumamosi na Jumapili, shirika la habari la Reuters liliripoti vyanzo vya afya vikisema kuwa watu 17 walikufa katika mashambulizi manne tofauti ya Israeli katika eneo hilo.

    Jeshi la Israel limesema Jumapili kuwa ndege zake za kivita zilishambulia zaidi ya maeneo 100 ya “magaidi” katika Ukanda wa Gaza mwishoni mwa juma, na kuua maelfu ya wapiganaji wa Hamas.

  14. Raia wa China wakamatwa DR Congo wakiwa na dhahabu na pesa taslimu $800,000

    Raia watatu wa China wametiwa mbaroni wakiwa na vipande 12 vya dhahabu na dola 800,000 za Kimarekani katika sehemu ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kwa mujibu wa Gavana wa Mkoa wa Kivu kusini Jean Jacques Purusi.

    Dhahabu na fedha hizo zinadaiwa kuwa walizificha chini ya viti vya gari walilokuwa wakisafiria.

    Gavana Jean alisema operesheni ya kuwakamata watu hao ilifanywa kIsiri baada ya kuachiwa kwa kikundi kingine cha raia wa China waliokamatwa kwa tuhuma za kuendesha mgodi haramu wa dhahabu katika eneo hilo.

    Sehemu ya mashariki ya DRC ina hifadhi kubwa ya dhahabu, almasi, na madini yanayotumika kutengeneza betri za simu na magari ya umeme.

    Utajiri huu wa madini umekuwa ukinyakuliwa na makundi ya kigeni tangu enzi za ukoloni na ni moja ya sababu kuu za mzozo unaokumba eneo hilo kwa zaidi ya miaka 30.

    Makundi ya waasi yanadhibiti migodi mingi katika mashariki ya DRC na viongozi wao wanapata utajiri kwa kuuza madini hayo kwa wafanyabiashara wa kati.

    Mwezi uliopita, Gavana Jean aliiambia vyombo vya habari kwamba alishangazwa kusikia kwamba raia 17 wa China, waliokamatwa kwa tuhuma za kuendesha mgodi haramu wa dhahabu, walikuwa wameachiliwa na kuruhusiwa kurejea China.

    Hata hivyo, ubalozi wa China haujatoa maoni kuhusu tuhuma hizo.

    Soma pia:

  15. Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji kurejea nchini wiki hii

    Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji ambaye, amekuwa akiongoza maandamano ya wiki kadhaa kupinga uchaguzi wenye utata kutoka uhamishoni, anasema atarejea nchini siku ya Alhamisi.

    Venancio Mondlane alisema (kwenye mitandao ya kijamii) atawasili kabla ya kuapishwa kwa rais mpya.

    Daniel Chapo wa chama tawala cha Frelimo anatazamiwa kuapishwa wiki ijayo.

    Uthabiti wa Msumbiji umeathiriwa vikali katika wiki chache zilizopita.

    Ikiwa kiongozi wa upinzani Venacio Mondlane atarejea nchini - kama alivyoahidi - msukosuko zaidi unaweza kuendelea.

    Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji zilichochewa na kile ambacho wengi, wakiwemo waangalizi wa uchaguzi, waliona kama kura ya maoni yenye dosari kubwa ambayo iliongeza miaka 49 ya chama cha Frelimo.

    Kuapishwa kwa Daniel Chapo kunatarajiwa baada ya siku kumi.

    Hakuna kitu cha kunachoashiria kupatikana kwa utulivu hivi karibuni nchini Msumbiji.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Katika Picha: Uwanja wa ndege ulivyofunikwa na theluji

    Picha kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muhammad Ali wa Louisville huko Kentucky zinaonyesha ndege zilizofunikwa na theluji huku eneo hilo likikumbwa dhoruba kali ya majira ya baridi.

    Safari za ndege zimesitishwa katika uwanja huo kwa siku nzima - kuzingatia tahadhari iliyotolewa.

    Takribani safari 4,500 za ndege zimecheleweshwa na zingine 2,000 kuahirishwa kulingana na FlightAware.

  17. Mamilioni wakumbwa na baridi kali huku majimbo sita ya Marekani yakitangaza hali ya dharura

    Mamilioni ya Wamarekani wamearifiwa kujiandaa kwa hali ya hewa ya majira ya baridi. Jimbo la West Virginia limejiunga na majimbo mengine matano kutangaza hali ya dharura.

    Kentucky, Virginia, Kansas, Arkansas na Missouri zimetangaza hali ya dharura.

    Majimbo 30 ya Marekani yanayoanzia katikati mwa nchi hadi pwani ya mashariki - ikiwa ni pamoja na miji mikuu kama Washington DC na Philadelphia - yanatarajiwa kushuhudia hali ya baridi kali.

    Watabiri wanasema mgandamizo mkubwa wa hewa kutoka kutoka katika nguzo ya mbili za dunia umeleta baridi kutoka Aktiki hadi katikati ya Marekani na kusababisha hali mbaya ya hewa.

    Maelezo zaidi:

  18. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja.