Ndege isiyo na rubani yarushwa kuelekea nyumbani kwa Waziri Mkuu wa lsrael - msemaji
Netanyahu hakuwa nyumba na hakuna mtu aliyejeruhiwa, msemaji huyo anaongeza kusema.
Muhtasari
- Israel yaanzisha mashambulizi mapya kusini mwa Beirut
- Netanyahu aapa Israel 'itaendelea hadi ipate ushindi'
- Naibu kamanda wa Hezbollah auawa kusini mwa Lebanon
- Raia wa Uingereza, Uturuki 'watekwa' Nairobi
- Viongozi wawili wa upinzani wauawa Msumbuji kuelekea maandamano ya uchaguzi
- Cuba yatumbukia gizani baada ya umeme kupotea nchi nzima
- Makumi ya watu waripotiwa kuuawa katika shambulizi la anga la Israel
- Kiongozi mkuu wa Iran asema Hamas 'itasalia hai'
- Ndege isiyo na rubani yarushwa kuelekea nyumbani kwa Waziri Mkuu wa lsraeli - msemaji
Moja kwa moja
Ambia Hirsi
Israel yaanzisha mashambulizi mapya kusini mwa Beirut

Chanzo cha picha, EPA
Israel imefanya mashambulizi manane ya anga dhidi ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, na kulenga shabaha katika maeneo mengine ya nchi hiyo, hasa kusini mwa bonde la Bekaa.
Baada ya siku tatu za utulivu katika mji mkuu, vitongoji vya kusini mwa nchi vimeanza tena kutikiswa na milipuko ya mashambulizi ya anga ya Israel.
Moshi mkubwa umekuwa ukifuka kutoka vitongoji kadhaa.
Mashabulizi mawili yalilenga karibu na uwanja wa ndege wa Beirut, ambao bado unatumiwa na ndege za raia zilizokodishwa.
Awali IDF iliwataka wakazi katika maeneo ya kusini mwa Beirut kuondoka, ikionya kuwa inapanga kufanya operesheni katika eneo hilo siku zijazo.
Netanyahu aapa Israel 'itaendelea hadi ipate ushindi'
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema hakuna kitakachomzuia na kwamba Israel itaendelea na mapambano yake dhidi ya Hamas "hadi ushindi upatikane".
"Tulimuondoa muuaji mkuu Yahya Sinwar," anasema kwenye video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii.
Sinwar, mbunifu mkuu wa shambulio la 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israeli, aliuawa na wanajeshi wa Israeli siku ya Jumatano.
"Nilisema tuko kwenye vita vya ufufuo na tunaendelea mbele hadi mwisho," Netanyahu anaongeza.
Video hiyo inakuja baada ya msemaji wa Netanyahu kusema ndege isiyo na rubani ilirushwa kuelekea nyumbani kwa Waziri Mkuu huko Caesarea, kaskazini mwa Israel, ingawa hakuwa nyumbani wakati huo na hakuna aliyejeruhiwa.
Soma pia:
Naibu kamanda wa Hezbollah auawa kusini mwa Lebanon
Jeshi la Israel linasema kuwa vikosi vyake vya jeshi la angani vimemuua naibu kamanda wa Hezbollah katika eneo la Bint Jbeil kusini mwa Lebanon.
Kwa mujibu wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), Naser Abed al-Aziz Rashid alihusika katika "shughuli za kigaidi dhidi ya raia wa Israel".
Hezbollah haijatoa tamko lolote.
Huku hayo yakijiri jeshi la Israel limewataka wakazi katika maeneo ya kusini mwa Beirut kuondoka, likionya kufanya operesheni siku zijazo katika eneo hilo.
Muingereza, Waturuki kadhaa 'watekwa' Kenya

Chanzo cha picha, IMAGE SUPPLIED
Maelezo ya picha, Necdet Seyitoğlu aliishi Uingereza kwa miaka 18 kabla ya kuhamia Kenya Raia wa Uingereza ameiambia BBC kuwa yeye na wenzake kadhaa raia wa Uturuki walitekwa nyara na watu waliojifunika nyuso zao siku ya Ijumaa jijini Nairobi Kenya.
Waturuki wanne kwa sasa hawajulikani waliko.
Necdet Seyitoğlu, ambaye aliishi nchini Uingereza kwa miaka 18 kabla ya kuhamia Kenya miaka miwili iliyopita, alisema aliachiwa baada ya saa nane alipowaonyesha wanaodaiwa kumteka nyara nakala ya pasipoti yake ya Uingereza.
Katika taarifa, Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema "wanatoa usaidizi wa kibalozi kwa Muingereza na familia yake kufuatia tukio lililotokea nchini Kenya".
Kulingana na ripoti hiyo, "watu wanane waliokuwa na silaha walitoka kwenye magari hayo mawili, na kuwatoa watu wawili waliokuwa ndani" na kuondoka nao, alisema msemaji wa polisi wa Kenya Resila Onyango.
"Baadaye, Yusuf Kar mmoja, raia wa Uingereza mwenye asili ya Uturuki" aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi kilicho karibu na kuwataja watu waliotekwa nyara kuwa ni Hüseyin Yeşilsu na Necdet Seyitoğlu.
Mamlaka ya Uturuki bado haijatoa maoni yoyote kuhusu tukio hilo.
Tukio hilo linachunguzwa na Mamlaka ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI.
Tawi la Nairobi la Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kuhudumia Wakimbizi pia limethibitisha kwamba “UNHCR imepokea ripoti na itatoa taarifa zaidi pindi tutakapozipata.”
Watu waliopotea walisemekana kuwa chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa jijini Nairobi.
Viongozi wawili wa upinzani wauawa Msumbuji kuelekea maandamano ya uchaguzi

Chanzo cha picha, Reuters
Watu wenye silaha wamemuua mwanasheria wa upinzani wa Msumbiji na afisa wa chama baada ya kufyatulia risasi nyingi gari walimokuwa wakisafiria siku ya Jumamosi, na hivyo kuzua hali ya wasiwasi kabla ya maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi yenye utata, mashirika ya kutetea haki za binadamu yalisema.
Chama kipya cha upinzani cha Podemos cha Msumbiji na mgombea wake wa urais Venancio Mondlane wamekataa matokeo ya awali yanayoonyesha uwezekano wa kushinda kwa Frelimo, chama ambacho kimetawala Msumbiji kwa nusu karne.
Wameitisha maandamano ya kitaifa siku ya Jumatatu. Kundi la waangalizi wa uchaguzi wa mashirika ya kiraia ya Msumbiji More Integrity lilisema shambulio hilo lilitokea katika kitongoji cha Bairro Da Coop katika mji mkuu Maputo, na kuwaua wakili wa Podemos Elvino Dias na mwakilishi wa chama Paulo Guambe.
"Waliuawa kikatili (katika) mauaji ya kinyama," Adriano Nuvunga, mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia na Haki za Kibinadamu cha Msumbiji (CDD), aliiambia Reuters kwa njia ya simu.
Cuba yatumbukia gizani baada ya umeme kupotea nchi nzima

Chanzo cha picha, AFP
Raia Milioni 10 wa Cuba wako gizani baada ya kiwanda chake kikuu cha nishati kukumbwa na hitilafu.
Gridi yake ya umeme iliacha kufanya kazi mwendo wa saa tano usiku (15:00 GMT) siku ya Ijumaa, wizara ya nishati ilitangaza kwenye mitandao ya kijamii.
Maafisa wanasema hawajui itachukua muda gani kurejesha nguvu za umeme.
Taifa hilo la Kisiwani hicho limekumbwa na kukatika kwa umeme kwa muda mrefu, na hivyo kumfanya waziri mkuu kutangaza "dharura ya nishati" siku ya Alhamisi.
Rais Miguel Díaz-Canel Bermúdez alisema hali hiyo inapewa "kipaumbele". "Hatutapumua hadi umeme urejeshwe," aliandika kwenye X.
Mkuu wa ugavi wa umeme katika wizara ya nishati, Lazara Guerra, alinukuliwa baadaye na shirika la habari la AFP akisema mpango wa kurejesha umeme unaendelea.
Makumi ya watu waripotiwa kuuawa katika shambulizi la anga la Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Takriban watu 33 wameuawa na wengine 85 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza siku ya Ijumaa, mamlaka inayoongozwa na kundi hilo la Hamas imesema.
Idadi ya vifo huenda ikafikia 50, taarifa kutoka ofisi ya vyombo vya habari vya serikali ya Gaza inasema, huku watu wakizikwa chini ya vifusi vya majengo.
Vikosi vya Israel vimekuwa vikiizingira kambi hiyo yenye wakazi wengi kwa wiki kadhaa, vikisema mashambulizi yake huko yanalenga kuwazuia wapiganaji wa Hamas kujipanga upya kwa mashambulizi zaidi.
Takriban watu 400,000 wamenaswa ndani ya kambi hiyo wakiwa na chakula kidogo au maji kwa zaidi ya wiki mbili.
Mapigano pia yanaendelea nchini Lebanon, ambapo Israel imekuwa ikifanya uvamizi wa ardhini dhidi ya kundi ya Hezbollah.
Jeshi la Israel linasema kuwa limewauwa takriban wapiganaji 60 wa Hezbollah na kuharibu kituo cha amri cha kikanda cha kundi linaloungwa mkono na Iran kwa shambulio la anga, huku Hezbollah ikisema ilirusha makombora katika mji wa Haifa na maeneo ya kaskazini mwa Israel.
Unaweza pia kusoma:
Kiongozi mkuu wa Iran asema Hamas 'itasalia hai'

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei anasema Hamas ilikuwa "hai na itasalia hai" licha ya kifo cha kiongozi wake, Yahya Sinwar.
Sinwar, mhusika mkuu wa mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israel, aliuawa baada ya wanajeshi wa Israel kushambulia jengo moja mjini Rafah mapema wiki hii.
"Kifo chake bila shaka ni pigo kubwa,lakini harakati za kupigania haki hazitafifia licha ya mauaji ya watu mashuhuri," Khamenei anasema katika taarifa.
"Mhimili wa Upinzani", unaoungwa mkono na Iran, unajumuisha Hamas, kundi la wanamgambo wa Lebanon Hezbollah, pamoja na makundi mengine yenye silaha karibu na Mashariki ya Kati ambayo yameishambulia Israel.
Ndege isiyo na rubani yarushwa kuelekea nyumbani kwa Waziri Mkuu wa lsrael - msemaji

Chanzo cha picha, AP
Ndege isiyo na rubani ilirushwa kuelekea nyumbani kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika mji wa Caesarea kaskazini mwa Israel siku ya Jumamosi, msemaji wake anasema.
Netanyahu hakuwa katika jengo hilo na hakuna mtu aliyejeruhiwa, msemaji huyo anaongeza.
Jeshi la Israel hapo awali lilisema ndege tatu zisizo na rubani zilirushwa kuelekea mji huo wa pwani mapema Jumamosi. Mmoja aligonga jengo,huku zingine mbili zikizuiliwa, liliongeza.
Serikali ya Israel haijasema iwapo jengo hilo lilikuwa sehemu ya makazi ya Waziri Mkuu wala kiwango cha uharibifu.
Netanyahu anatumia nyumba mbili katika miji ya Kaisaria na Jerusalem, na wakati mwingine anatumia muda katika mji wa Beit Aghion, makazi rasmi ya waziri mkuu huko Jerusalem, ambayo kwa sasa yanafanyiwa ukarabati.
IDF inasema jumla ya roketi 55 zilirushwa hadi Israel kutoka Lebanon kufikia Jumamosi.
Soma pia:
Karibu katika matangazo ya moja kwa moja.
