Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Maelfu wakimbia DR Congo huku waasi wakidai kuudhibiti mji wa Goma

Kundi la M23 linadai kuuteka mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lakini jeshi la linasema bado linadhibiti maeneo muhimu.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirs & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Wanasoka wa DR Congo watoa wito wa amani

    Sio wanasiasa na mashirika ya misaada yanayopaza sauti kuhusu mzozo unaondelea nchini DR Congo - wanasoka wa timu ya taifa ya DRC pia wametoa kauli zao.

    Chancel Mbemba, anayechezea klabu ya Marseille Ufaransa, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X: "Solidarity with Goma" kuashiria kuwa anasimama na Goma.

    Pia alichapisha picha ya kikosi cha DR Congo cha mwaka jana, ambapo walionyesha mshikamano na waathiriwa wa mzozo huo kwa kuziba midomo yao kwa mkono wao wa kushoto na kuelekeza vidole kwenye mahekalu yao, wakiiga bunduki.

    Mshambulizi Cédric Bakambu pia alitumia X kuangaziamachafuko yanayoendelea kushuhudiwa mashariki mwa DR Congo.

    "Amani ina nguvu zaidi kuliko vita #PrayForCongo #FreeCongo," aliandika.

  3. Majadiliano ya moja kwa moja na M23 ni muhimu - Rais wa Kenya

    Rais wa Kenya William Ruto ameangazia kuzorota kwa hali ya usalama nchini DR Congo baada ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda kuingia katika mji muhimu wa Goma.

    Ruto amesema kuwa Rais wa DR Congo Félix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame wamekubali kuhudhuria mkutano wa dharura siku ya Jumatano kujadili mzozo huo.

    Ruto aliwaambia waandishi wa habari kwamba: "Hali ilivyo, sioni uwezekano makabiliano ya kijeshi yakiwa suluhisho la changamoto inayokabili mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

    "Majadiliano ya moja kwa moja kati ya kundi la M23 na washikadau wengine mashariki ya mwa DRC ni muhimu."

    Kwa sasa Kenya inaongoza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye wanachama wanane, ikiwemo DR Congo na Rwanda.

    Soma pia:

  4. DR Congo inajitahidi kuepusha mauaji - msemaji

    Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inasema inajitahidi kuepusha "mauaji" mjini Goma, lakini haitaachia eneo lolote baada ya waasi wa M23 kudai kwamba wameuteka mji huo.

    Katika taarifa kwenye mtandao wa X, Waziri wa Mawasiliano Patrick Muyaya aliwataka watu kusalia majumbani kwa usalama wao.

    Pia aliwataka watu kujiepusha na uhalifu au uporaji, na kupuuza "propaganda za Rwanda".

    Muyaya pia alirudia kauli za awali zinazodai kuwa wanajeshi wa Rwanda wako ndani ya DRC na wanashirikiana na waasi wa M23 katika mapigano yanayoendelea mjini Goma.

    "Sisi sote ni walinzi wa eneo letu," Muyaya alisema, akiongeza kuwa "hakuna sentimita moja itakayotolewa".

    Maelezo zaidi:

  5. Katika Picha: Mzozo wa DR Congo

    Zifuatazo ni mkusanyiko wa picha zinazoashiria matukio nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

  6. Belarus: Lukashenko adai kushindi uchaguzi unaotiliwa shaka na mataifa ya Magharibi

    Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amepata ushindi mwingine katika uchaguzi ambao mataifa ya Magharibi yanadai ulikumbwa na udanganyifu.

    Tume ya Uchaguzi ilisema leo Jumatatu kwamba Lukasjenko alishinda asilimia 86.8 ya kura na kwamba waliojitokeza kupiga kura walikuwa karibu asilimia 87.

    Kulikuwa na wagombea wengine nne waliowania urais - waliochaguliwa kwa uangalifu ili kutoa changamoto yoyote dhidi ya uongozi wa sasa - lakini hakuna wagombea wanaoaminika walioruhusiwa kushiriki uchaguzi huo, kwani viongozi wote wa upinzani wamefungwa jela au wamekimbilia uhamishoni.

    Hakuna waangalizi huru waliofuatilia shughuli ya upigaji kura.

    Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisema uchaguzi huo umekuwa ukiukaji wa wazi wa demokrasia, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akichapisha ujumbe kwenye mtandao wa X akisema kwamba "watu wa Belarus hawana chaguo".

    Wakati huo huo, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Rais Vladimir Putin - ambaye ametawala Urusi tangu 2000 - alimpongeza mshirika wake wa karibu Lukasjenko kwa "ushindi wake madhubuti".

    Peskov alisema Moscow inaamini kwamba uchaguzi wa Belarus ulikuwa "uchaguzi halali kabisa, ulioandaliwa vyema na kwa njia ya uwazi" na kuyashutumu "mataifa ya Magharibi" kwa kutilia sha mchakato huo.

    Viongozi wa China, Venezuela na Pakistan pia walitoa pongezi zao kwa Lukashenko.

  7. Baadhi ya wanajeshi wa DRC walijisalimisha kwa vikosi vya UN - Uruguay

    Jeshi la Uruguay ambalo ni sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Goma, linasema kuwa baadhi ya wanajeshi wa DR Congo wamesalimisha silaha zao kwa wanajeshi wake.

    Kikosi cha Uruguay pia kilisambaza picha za wanaume waliovalia sare za kiraia na za kijeshi ambao walionekana kujiandikisha nao.

    Waasi wa M23 walikuwa wamewaamuru wanajeshi kusalimisha silaha zao na walikuwa wametoa makataa ya saa 48 ambayo yalikamilika mapema Jumatatu.

    Waasi hao pia wamewaomba wakazi wa Goma kuwa watulivu na kuvitaka vikosi vya serikali ya Congo kukusanyika katika uwanja wa michezo.

    Shughuli ya kukabidhi silaha hizo kwa wanajeshi wa Uruguay ilifanyika Jumapili jioni kabla ya kukamilika kwa muda uliowekwa na kabla ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda kuingia mjini humo.

  8. Mpaka wa Rwanda na DR Congo waripotiwa kufungwa

    Mpaka kati ya DR Congo na Rwanda umeripotiwa kufungwa baada ya waasi wa M23 kuingia Goma.

    Chanzo cha kidiplomasia kiliiambia shirika la habari la AFP kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia au kutoka kwenye kivuko kikuu kati ya nchi hizo mbili.

    Ni wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa ambao huduma zao sio za dharura na familia zao waliruhusiwa kuvuka walipokuwa wakihamishwa kupitia Rwanda.

    Shirika la utangazaji la Rwanda liliripoti kuwa baadhi ya mabasi yalikuwa yakisubiri kuwahamisha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na familia zao.

    Goma iko wapi na kwa nini ni muhimu?

    Goma ni mji mkuu wa eneo la Kivu Kaskazini na nyumbani kwa zaidi ya watu milioni moja.

    Mji huo ambao uko katika mpaka wa DRC na Rwanda ni kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji ambacho kinaunganisha miji ya uchimbaji madini inayosambaza madini na madini yanayohitajika sana, kama vile dhahabu, bati na coltan, kiungo muhimu katika utengenezaji wa simu za mkononi.

    Kundi la M23 liliichukua udhibiti wa mji wa Goma kwa muda mfupi wakati wa uasi mwaka 2012, lakini wakajiondoa baada ya makubaliano ya amani kufikiwa.

  9. Shirika la Umoja wa Mataifa lasitisha shughuli zake mjini Goma

    Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limelazimika kusitisha shughuli zake mjini Goma na eneo kubwa la Kivu Kaskazini, shirika hilo limesema.

    Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X, WFP ilisema ameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na "kuongezeka kwa ghasia".

    Iliongeza kuwa watu 800,000 katika eneo la Kivu Kaskazini "wanategemea msaada muhimu wa chakula na lishe".

    WFP itarejelea shughuli zake wakati hali itakapotengamaa kwa "jamii" na wafanyikazi wake, ilisema taarifa hiyo.

    Operesheni za WFP katika maeneo mengine ya DR Congo zitaendelea kama kawaida.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Poland yaonya dhidi ya kuanzisha tena usambazaji wa gesi ya Urusi

    Rais wa Poland amesema kwamba usambazaji wa gesi kutoka Urusi hadi Ulaya Magharibi haupaswi kurejeshwa hata kama Urusi na Ukraine zitafikia makubaliano ya amani.

    Andrzej Duda aliambia BBC kwamba mabomba ya gesi ya Nord Stream, ambayo hayajatumika tangu 2022, "yanafaa kuvunjwa".

    Hii, alisema, itamaanisha kuwa Ujerumani haishawishika kurejesha vifaa vya Urusi ili kukuza uchumi wake unaokumbwa na msukosuko.

    "Matumaini yangu ni kwamba viongozi wa Ulaya watajifunza kutokana na uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine na kwamba watazingatia uamuzi wa kutorejesha usambazaji wa gesi kupitia bomba hili," alisema.

    Akizungumza katika Kongamano la Kiuchumi Duniani mjini Davos Uswizi, Rais wa Poland alisisitiza kuwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi vinafanya kazi na nchi za Ulaya zinapaswa kupinga shinikizo kutoka kwa makampuni kuanzisha upya uhusiano wa biashara.

    Mabomba ya gesi ya Nord Stream yalijengwa na kampuni kubwa ya gesi ya Urusi Gazprom na kuendeshwa kati ya Urusi na kaskazini mwa Ujerumani.

    Nord Stream 1 ilifungwa mwaka wa 2022 na Nord Stream 2 haikutumika, kufuatia uvamizi wa Ukraine.

    Mabomba yote mawili yaliharibiwa na milipuko mnamo 2022.

    Bei ya gesi barani Ulaya ilipanda baada ya hatua hiyo, katika miezi ya hivi karibuni, wanasiasa kutoka chama cha AfD cha Ujerumani wamependekeza mabomba ya gesi ya Nord Stream kuanza kufanya kazi tena.

  11. Colombia yakubali kupokea waliofukuzwa baada ya tishio la ushuru wa Trump

    Marekani yasitisha mpango wa ushuru kwa Colombia, baada ya Bogota kukubali kupokea - bila vikwazo - wahamiaji waliofukuzwa Marekani, Ikulu ya White inasema.

    Donald Trump alikuwa ameamuru ushuru wa 25% kwa bidhaa zote za Colombia baada ya rais wake kuzuia safari mbili za ndege za jeshi la Marekani kutua nchini humo siku ya Jumapili.

    Rais wa Colombia Gustavo Petro hapo awali alikuwa amejibu kwa kusema nchi yake ingekubali raia waliorudishwa kwenye "ndege za raia, bila kuwachukulia kama wahalifu".

    Taarifa ya White House inasema Colombia sasa imekubali kuwapokea wahamiaji wanaowasili kwa ndege za kijeshi za Marekani "bila kikomo au kuchelewa". Colombia ilisema mazungumzo yatadumishwa ili "kuhakikisha utu wa raia wetu".

    Soma zaidi:

  12. Wapalestina sasa wanaweza kuelekea kaskazini kwa magari

    Msemaji wa Kiarabu wa jeshi la Israel, Avichay Adraee, awali alitoa muda wa kurejea kwa Wapalestina kaskazini mwa Gaza:

    • Wakazi waliruhusiwa kurejea kwa miguu hadi Ukanda wa kaskazini wa Gaza "kupitia Barabara ya Netzarim na kupitia Mtaa wa Rashid (barabara ya baharini) kuanzia saa 07:00" (05:00 GMT)
    • Magari yataruhusiwa kuhamia upande wa kaskazini "baada ya ukaguzi" kutoka 09:00 (07:00 GMT)
    • "Uhamisho wa wanamgambo au silaha kupitia njia hizi hadi kaskazini mwa Ukanda wa Gaza utazingatiwa kuwa uvunjaji wa makubaliano," Adraee anasema.

    Soma zaidi:

  13. Wakuu wa Nchi za Afrika wakutana Tanzania kujadili kuhusu nishati,

    Wakati Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati ukianza leo jijini Dar es Salaam, ulinzi na usalama umeimarishwa katika maeneo mbalimbali huku shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiendelea.

    Alkadhalika usafiri nafuu yaani bajaji na bodaboba umesitishwa kwa baadhi ya maeneo ya jiji baada ya kuzuiwa kuingia katikati ya jiji kwa siku mbili.

    Kufuatia tamko la juzi, barabara kuu tisa zinazoelekea katika jijini zimefungwa, shule za umma na nyingi za binafsi zimefungwa pamoja na shughuli mbalimbali katika ofisi za umma nazo zimesimama huku watumishi wa umma wakihimizwa kufanya kazi majumbani.

    Kwa mujibu wa wataalamu wa kiuchumi, ujio wa ugenimkubwa waiwemo wakuu wa nchi na viongozi wa taasisi kubwa ulimwenguni utaitangaza Tanzania na fursa zake, hivyo kurahisisha kupatikana kwa wawekezaji na hatimaye kuzalisha ajira.

    Kwa mujibu wa nchi mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, mkutano huo unalenga kuongeza uunganishaji nishati kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.

    Zaidi ya wakuu wa nchi 25 na mawaziri 60 wanatarajiwa kuwa sehemu ya mkutano huo wa siku mbili.

    Tutaendelea kuwapa taarifa ya kile kinachojiri….

  14. Manyoya ya ndege yapatikana katika injini za ndege iliyoanguka ya Jeju Air

    Wachunguzi wamesema wamepata ushahidi wa ndege wa angani aliyeingia katika injini ya ndege ya abiria ambayo ilianguka Korea Kusini mnamo mwezi Desemba na kuwauwa watu 179.

    Manyoya na madoa ya damu kwenye injini zote mbili za ndege ya Jeju ni kutoka kwa jamii ya bata inayoruka kwa kundi kubwa, kulingana na ripoti ya uchunguzi wa awali iliyochapishwa Jumatatu.

    Uchunguzi wa ajali hiyo - mbaya zaidi kuwahi kutokea Korea Kusini - sasa itazingatia kilichotokea baada ya ndege kuingia na muundo uliojengwa kwa saruji mwishoni mwa barabara ya ndege, ambako ndege iligonga.

    Injini za Boeing 737-800 zitabomolewa na muundo wa saruji utachunguzwa zaidi, ripoti hiyo ilisema.

    Ndege ya Jeju Air ilikuwa imetoka Bangkok asubuhi ya tarehe 29 Desemba na ilikuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan kusini-magharibi mwa nchi.

    Mnamo saa 08:57 kwa saa za nchi hiyo, dakika tatu baada ya marubani kuwasiliana na uwanja wa ndege, wadhibiti waliwashauri wafanyakazi kuwa waangalifu na mienendo ya "ndege ya angani".

    Saa 08:59, rubani aliripoti kwamba ndege hiyo imegonga ndege na kutangaza tahadhari.

    Kisha rubani akaomba ruhusa ya kutua kutoka upande mwingine, ambapo ilitua kwa tumbo bila vifaa vyake vya kutua vilivyowekwa.

    Ilipita zaidi ya barabara ya kurukia ndege na kulipuka baada ya kugonga muundo wa zege, ripoti hiyo ilisema.

    Soma zaidi:

  15. Rwanda yasema taarifa za kupotosha kuhusu mzozo wa DR Congo sio suluhisho

    Rwanda imekosoa taarifa zinazotolewa na pande mbalimbali juu ya hali ilivyo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ikisema kuwa taarifa za uwongo na kupotosha hazitoi suluhisho kwa mzozo unaoendelea.

    Wizara ya mambo ya nje ya Rwanda imesema mapigano ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo hasa makabiliano makali katika eneo la Goma yalichochewa na ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha mapigano na wanajeshi wa Congo (FARDC).

    Rwanda imesema mapigano haya yapo karibu na mpaka wa Rwanda na yanaendelea kuwa tishio kubwa kwa usalama wa Rwanda na inailazimu kuchukua hatua za kujilinda.

    ‘’Mchakato wa kutafuta amani wa Luanda baada ya serikali ya DRC kukataa kufanya mazungumzo na kundi la M23 na kuendelea kukataa kuangazia chanzo halisi cha mgogoro wa mashariki mwa DR Congo ndio sababu ya kuendelea kwa mapigano na kuwa tishio kwa mataifa jirani ikiwa ni pamoja na Rwanda,’’ Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Rwanda imesema.

    Rwanda inasisitiza kujitolea kwake kuhakikisha suluhisho la kisiasa linapatikana katika mzozo huo.

    Imeendelea kusema kuwa mchakato wa Luanda na Nairobi unahitaji nguvu mpya kuhakikisha upatikanaji wa amani endelevu na uthabiti kwa nchi zote za eneo.

    Soma zaidi:

  16. Trump anatoza ushuru wa 25% kwa Colombia huku safari za ndege za wahamiaji zikizuiwa

    Haya yanajiri baada ya Rais wa Colombia Gustavo Petro kupinga kuingia kwa ndege za kijeshi za Marekani zilizokuwa zimebeba wahamiaji waliofukuzwa.

    Trump anatoza ushuru wa 25% kwa Colombia huku safari za ndege za wahamiaji zikizuiwa

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema ataiwekea Colombia ushuru wa asilimia 25 na vikwazo baada ya rais wake kuzuia ndege mbili za kijeshi za Marekani zilizokuwa zimebeba wahamiaji waliofukuzwa kutua nchini humo.

    Trump alisema ushuru wa "bidhaa zote" zinazoingia Marekani kutoka Colombia utawekwa "mara moja", na katika wiki moja ushuru wa 25% utapandishwa hadi 50%.

    Rais wa Colombia Gustavo Petro alijibu kwa kusema atatoza ushuru wa kulipiza kisasi wa 25% kwa Marekani.

    Mapema siku ya Jumapili, Petro alisema amekataa kuingia katika ndege za kijeshi za Marekani za kuwafurusha wahamiaji. Alisema "atawapokea raia wenzetu kwenye ndege za kiraia, bila kuwachukulia kama wahalifu" na wahamiaji lazima warudishwe "kwa utu na heshima".

    Maafisa wa Marekani waliambia mshirika wa BBC wa Marekani, CBS News, kwamba ndege mbili za kijeshi kutoka San Diego zilipaswa kutua Colombia siku ya Jumapili na wahamiaji waliofukuzwa, lakini mipango hiyo ilifutiliwa mbali kutokana na sintofahamu iliyojitokeza.

    Akijibu, Trump alitangaza "hatua za haraka na za kulipiza kisasi" katika ujumbe kwenye mtandao wa TruthSocial. Alisema Marekani itaweka marufuku ya kusafiri na "kufuta viza mara moja" kwa maafisa wa serikali ya Colombia, pamoja na washirika wake na wafuasi.

    "Hatua hizi ni mwanzo tu," Trump aliongeza, akisema utawala wake hautaruhusu serikali ya Colombia "kukiuka majukumu yake ya kisheria kuhusiana na kukubalika na kurudi kwa wahalifu waliowalazimisha nchini Marekani".

    Petro alijibu kwenye mtandao wa X kwa kutangaza ushuru wake mwenyewe na kusherehekea urithi na ujasiri wa Colombia.

    Soma zaidi:

  17. Mateka sita kuachiliwa na Wagaza kuruhusiwa kuingia Kaskazini - Israeli

    Hamas itawaachilia mateka sita wiki hii na Israel itawaruhusu raia wa Gaza kurejea makwao kaskazini mwa nchi kuanzia Jumatatu, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema.

    Mateka hao ni pamoja na Arbel Yehud - raia aliye katikati ya mzozo ambao umesababisha Israel kuchelewesha kurejea Gaza kaskazini mwa Gaza.

    Hamas iliwaachilia huru wanajeshi wanne siku ya Jumamosi, lakini sio Bi Yehud. Israel iliishutumu Hamas kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano ambapo raia wa Israel wangeachiliwa kwanza ili kubadilishana na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina.

    Tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa, mateka saba na wafungwa zaidi ya 200 wameachiliwa huru.

    Maelfu ya Wapalestina waliokimbia makazi yao wanaojaribu kufika kaskazini mwa Gaza wamekusanyika kwenye kizuizi cha kijeshi kinachozuia wao kusonga mbele kwa siku mbili.

    Makubaliano ya kusitisha mapigano na mateka na kuachiliwa kwa wafungwa yalianza kutekelezwa tarehe 19 Januari. Mabadilishano yamefanyika mara mbili.

    Israel itaanza kuwaruhusu Wapalestina kuhamia kaskazini siku ya Jumatatu, na pia kuwaachilia wafungwa zaidi wa Kipalestina baadaye wiki.

    Picha zinaonyesha umati mkubwa wa watu wakisubiri kupita.

    Soma zaidi:

  18. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja. Tarehe ni 27/01/2025.