Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump awapa viongozi Hamas makataa ya hadi Jumapili kukubali mpango wa amani wa Gaza
Mpango huo wenye vipengele 20 unapania kukomesha mapigano mara moja na kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel wanaozuiliwa na Hamas na wafungwa wa Kipalestina.
Muhtasari
- Trump awapa viongozi Hamas makataa ya hadi Jumapili kukubali mpango wa amani wa Gaza
- "Côte d'Ivoire haiwahifadhi maadui wa Burkina" - Msemaji wa serikali
- Akina baba wana haki ya kupata likizo sawa ya uzazi, mahakama kuu Afrika Kusini yaamua
- ''Vijana msihadaiwe na wahuni wa kutoka nje kuiharibu nchi'' - Rais Madagascar
- Ni nini kilicho nyuma ya visa vya ndege zisizo na rubani kwenye viwanja vya ndege?
- Askofu Mkuu mteule wa Canterbury Sarah Mullally ni nani?
- Ulaya yaanza kujitayarisha kwa vita vikubwa vinavyoweza kutokea
- Jina la mshambuliaji wa sinagogi la Manchester latangazwa, tukio lililoelezwa kuwa "ugaidi"
- Sarah Mullally ateuliwa mwanamke wa kwanza kuoliongoza kanisa la Kianglikana duniani
- Mtoto wa Robert Mugabe afikishwa mahakamani kwa tuhuma za dawa za kulevya
- Putin aonya Marekani dhidi ya kupeleka makombora Ukraine
- Misri inajitahidi kushawishi Hamas kukubali mpango wa Trump, asema waziri wa mambo ya nje
- Venezuela inaishutumu Marekani kwa kupeleka ndege za kivita karibu na pwani yake
- Ahukumiwa kwa kujaribu kumzamisha mtoto wa Kiislamu
- 'Nilipotea njia' - Diddy amwomba jaji amuhurumie usiku wa kuamkia hukumu yake
- Uwanja wa ndege wa Munich wafungwa baada ya ndege zisizo na rubani kuonekana karibu
- Marekani imetuma pesa kwa Lebanon wakati ikielekea kuipokonya silaha Hezbollah, duru zinasema
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Lizzy Masinga
Trump awapa viongozi Hamas makataa ya hadi Jumapili kukubali mpango wa amani wa Gaza
Rais Donald Trump amewapa viongozi wa Hamas makataa ya kukubali mpango wa amani wa Gaza uliopendekezwa na Marekani la sivyo "watakiona cha mtema kuni".
Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social leo Ijumaa kwamba makubaliano lazima yafikiwe Jumapili hii saa kumi na mbili jioni majira ya Washington (22:00 GMT)
Mpango huo unapendekeza kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka 20 wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas ndani ya saa 72. Mpango huo piaunajumuishwa kuachiwa kwa mamia ya Wapalestina wanaozuiliwa na Israel.
Wapatanishi kutoka mataifa ya Kiarabu na Uturuki wanasadikia kushinikiza Hamas kutoa jibu chanya kwa pendekezo hilo, lakini kiongozi mkuu wa Hamas amesema kundi hilo lenye silaha huenda likakataa mpango huo.
Melezo zaidi:
Katika Picha: Familia ya Diddy yawasili mahakamani kusubiri hukumu ya kesi yake
Hukumu ya kesi dhidi ya mwanamuziki maarufu wa Marekani Sean "Diddy" Combs inatarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia sasa.
Hapo jana Diddy alimwandikia barua jaji anayesimamia kesi yake ya jinai, akiomba ahurumiwe wakati wa hukumu yake akidai kuwa tabia yake ya zamani ilichochewa na uraibu wa dawa za kulevya.
Jamaa zake wamewasili mahakamani kusubiri hukumu dhidi yake.
"Ivory Coast haiwahifadhi maadui wa Burkina" - Msemaji wa serikali
Msemaji wa serikali ya Ivory Coast Amadou Coulibaly amepuuzilia mbali madai ya kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, kwamba maadui wa nchi yake wako Côte d'Ivoire.
Akizungumza na BBC, Bw Coulibaly alisema hakuna maadui wa Burkina Faso katika ardhi ya Ivory Coast.
"Nchi yetu inajulikana kwa ukarimu, na kusema kwamba tunawahifadhi maadui zao, kwa sababu ya kuwakaribisha wageni ni kitu cha kushangaza, Côte d'Ivoire ni mahali ambapo Waafrika wengi wamepata kimbilio," alisema.
Alibainisha kuwa wageni ni 26% ya wakazi wa Côte d'Ivoire ambayo ina takriban watu milioni saba, ikiwa ni pamoja na raia milioni tatu wa Burkina Faso.
"Hatuna nia ya kuyumbisha nchi hii (Burkina Faso), kwa sababu sisi ndio tutaathiriwa pakubwa na msukosuko huo," aliongeza.
Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imekuwa ikidai kwamba imetibua "njama" za mara kwa mara za kumpindua KapteniTraoré, huku wanaodaiwa kupanga njama hiyo wakisemekana kufanya hivyo kutoka nchi jirani ya Côte d'Ivoire.
Kapteni Traoré alichukua mamlaka mnamo 2022 wakati nchi hiyo ilipokumbwa na ongezeko la mashambulizi ya wanamgambo wa kijihadi.
Burkina Faso, pamoja na mataifa mengine mawili yanayoongozwa na kijeshi - Mali na Niger, wamejiondoa kwenye uwanacha wa jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, Ecowas, na kuunda muungano mpya, Muungano wa Mataifa ya Sahel.
Wamekata uhusiano na mkoloni wa zamani Ufaransa na kuungana na Urusi badala yake, na kuituhumu Côte d'Ivoire kuwa na "ajenda ya siri" kwa maslahi ya Ufaransa.
Pia unaweza kusoma:
Akina baba wana haki ya kupata likizo sawa ya uzazi, mahakama kuu Afrika Kusini yaamua
Mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini imeamua kwa kauli moja kuwa wazazi wote wawili wana haki ya kupata likizo sawa ya uzazi - uamuzi wa kihistoria uliopongezwa kama ushindi mkubwa wa usawa wa kijinsia na haki za familia.
Kwa mujibu wa sheria ya sasa, akina mama wanapewa likizo ya miezi minne, huku akina baba wakipokea siku 10 pekee.
Katika uamuzi wake, Mahakama ya Kikatiba ilitangaza sehemu za sheria hiyo kuwa kinyume na katiba, na kuzitaja kuwa za kibaguzi dhidi ya baba, na kuamua kwamba wazazi wote wawili sasa wanaweza kutumia likizo waliyopewa watakavyo.
"Hii ni hatua ya muhimu kuelekea usawa, ustawi wa familia, na mustakabali wa mzazi wa kuime nchini Afrika Kusini," alisema Sthembiso Phakathi, mwanzilishi wa Single Dads Network.
''Vijana msihadaiwe na wahuni wa kutoka nje kuiharibu nchi’’ -Rais Madagascar
Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina, amelaani kile alichokiita jaribio la mapinduzi lililohusishwa na maandamano yanayoendelea nchini humo.
Katika hotuba kwa taifa aliyoitoa kupitia ukurasa wake wa Facebook mapema leo, Rajoelina alisema kuwa maandamano hayo yanayoongozwa na vijana wa kizazi kipya cha Gen Z yamechochewa na watu wenye nia ya kuiangusha serikali kwa nguvu.
Hotuba hiyo pia ilirushwa na televisheni ya taifa, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa ndani.
“Wamechochewa kutekeleza mapinduzi. Ninachotaka kuwaambia ni kwamba kuna watu wanataka kuiharibu nchi,” alisema Rajoelina, kama alivyonukuliwa na shirika la habari la AFP.
Rais alieleza kuwa kulikuwapo na mpango wa kumng’oa madarakani kwa nguvu, ambapo alikumbwa na vitisho vya maisha.
Hata hivyo, amewahakikishia wananchi kuwa yuko salama na serikali iko imara.
Akizungumza akiwa ofisini mwake Rais Rajoelina ameonya kuwa machafuko yanapoendelea, kuna hatari ya kusitishwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Miradi muhimu ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara kuu za kitaifa namba 10 na 13, ipo hatarini kusimama.
Katika hotuba yake pia, Rais amesisitiza kuwa baadhi ya mataifa ya kigeni na mashirika ya kimataifa yanahusika katika njama za kupenya kwenye siasa za ndani kwa lengo la kunufaika na rasilimali za madini za Madagascar.
Akigusia maadamano ambayo yanaendelea kuchacha Rais wa Madagascar ametoa tahadhari kuhusu uwepo wa makundi ya wanamgambo wenye silaha waliopenya kwenye maandamano kwa lengo la kuchochea vurugu na machafuko.
Wakati huo huo, amewasihi vijana na wasanii kutambua adui wa kweli na kutoacha kupoteza dira au malengo yao halisi ya kujenga taifa.
Mnamo Jumatatu, Rajoelina alivunja serikali yake kwa lengo la kupunguza hasira za wananchi, lakini hatua hiyo haikutosha kutuliza hali ya sintofahamu.
Leo hii, polisi wa kutuliza ghasia walifunga sehemu kubwa ya katikati ya jiji la Antananarivo kwa hofu ya maandamano mapya.
Asubuhi ya leo, mamia ya waandamanaji walijaribu kuingia katikati ya jiji lakini polisi waliwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi.
Maandamano hayo, yaliyoanza wiki iliyopita siku ya Alhamisi katika mji mkuu, sasa yameenea hadi miji mingine mikuu nchini.
Soma pia:
Netanyahu afanya mkutano wa usalama leo, huku kukiwa na ripoti zinazokinzana kuhusu msimamo wa Hamas huko Gaza
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kufanya mkutano maalum siku ya Ijumaa na maafisa wakuu wa usalama.
Channel 14 ya Israel imeripoti kuwa, ajenda ya Netanyahu inajumuisha mada kuu mbili: kutathmini hali ya Gaza, ikizingatiwa nia ya Hamas iliyoripotiwa kukataa mpango wa Marekani, na kuongezeka mashambulizi Ukingo wa Magharibi, ambayo inaweza kusababisha operesheni kubwa sawa na mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Mwandishi wa BBC Gaza aliripoti kwamba wapatanishi waliwasiliana na mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas huko Gaza, Izz al-Din al-Haddad, ambaye alionesha kutokubaliana kwake na mpango huo mpya wa Marekani wa kusitisha mapigano.
Izz al-Din al-Haddad anaamini mpango huo "unalenga kuiondoa Hamas, iwe vuguvugu hilo linakubali au la," na ndio maana amedhamiria kuendelea kupigana.
Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas Mohammed Nazzal aliiambia idhaa ya Al Jazeera ya Qatar Alhamisi jioni kwamba vuguvugu hilo lilipokea mpango wa Trump Jumatatu iliyopita na kuanza mashauriano ya "ndani na nje" kuhusu hilo.
Nazzal aliongeza kuwa vuguvugu hilo lina "angalizo" juu ya mpango huo na litatangaza msimamo wake hivi karibuni, akieleza kuwa vuguvugu hilo liliamua kujadili mpango wa Marekani kwa kuzingatia kanuni ya "kusimamisha vita na mauaji," kama alivyoweka.
Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas alieleza kuwa vuguvugu hilo litatangaza msimamo wake kuhusu mpango huo hivi karibuni, na "haitachukua muda mrefu."
Unaweza kusoma;
Ni nini kilicho nyuma ya visa vya ndege zisizo na rubani kwenye viwanja vya ndege?
Uwanja wa ndege wa Munich nchini Ujerumani umefunguliwa tena baada ya kuonekana kwa ndege zisizo na rubani kulazimisha kufungwa na kuahirishwa kwa safari zaidi ya kumi na mbili Alhamisi usiku.
Ni hatua ya hivi punde zaidi katika mfululizo wa uvamizi wa hivi karibuni wa ndege zisizo na rubani kote Ulaya.
Haijulikani ni nani aliye nyuma ya matukio haya, lakini Dk Ulrike Franke kutoka Baraza la Umoja wa Ulaya kuhusu Mambo ya Kigeni aliambia kipindi cha Leo cha BBC Radio 4 asubuhi ya leo kwamba tukio la Munich linaweza kusababishwa na "nchi yenye uwezo''.
"Tumekuwa na visa vya ndege kubwa zaidi katika siku na wiki za hivi karibuni na katika visa vingine ndege kubwa zisizo na rubani zenye uwezo wa kurusha droni ndogo, zikiruka karibu na miundombinu muhimu," alisema.
"Haya ni matukio ambapo tunaweza kuwa na uhakika kwamba hawa si wanagenzi... uwezekano mkubwa ni nchi, kuna uwezekano mkubwa kuwa Urusi.
"Katika kesi ya Munich kwa wakati huu hatuna taarifa za kutosha kuhusu aina ya ndege zisizo na rubani, na jinsi zilivyorushwa, ili kutupa taarifa ni nani alikuwa akiziendesha." Franke alivitaka viwanja vya ndege kujitayarisha na teknolojia ya kupambana na ndege zisizo na rubani ili kukabiliana na ongezeko la uvamizi wa anga.
Alisema kuwa hadi sasa, maafisa "hawajaona hitaji la kiuchumi" la kuwekeza katika teknolojia.
Askofu Mkuu mteule wa Canterbury Sarah Mullally ni nani?
Dame Sarah Mullally, 63, amekuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury katika historia ya Kanisa la Uingereza iliyodumu kwa takriban miaka 500.
Lakini kabla ya kuwa kasisi mnamo 2006, alikuwa muguzi. Mullally ameolewa na ana watoto wawili, na alifanya kazi kwa miaka 35 katika Hudama ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza - na kuwa afisa mkuu wa uuguzi mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea nchini Uingereza mwaka wa 1999.
Japo alikuwa akijitolea katika shughuli za Kanisa wakati huo, miaka michache baadaye aliamua kuwa kasisi na kupewa jukumu la kusaidia kufanya mageuzi katika njia ambayo taasisi hiyo ilishughulikia unyanyasaji.
Alipewa dhamana ya kusimamia sheria katika Kanisa Kuu la Salisbury mnamo 2012, kabla ya kuwa Askofu wa Crediton katika dayosisi ya Exeter mnamo 2015.
Alipoteuliwa kuwa Askofu wa London alionekana kama mtu ambaye alitumia uzoefu wake kama msimamizi wa Huduma ya Kitaifa ya Afya (NHS) kusaidia dayosisi kuwa ya kisasa.
Wakati wa uteuzi huo alisema: "Mara nyingi mimi huulizwa jinsi anavyomudu kuwa na kazi mbili, kwanza katika Sekta ya Afya na sasa Kanisani.
"Siku zote nimekuwa nikihisi kuwa majukumu yote mawili na wito mmoja: kumfuata Yesu Kristo".
Mojawapo ya maeneo ambayo amekuwa akizungumzia zaidi ni kusaidiwa kufa - anapinga vikali suala hilo, kama alivyokuwa mtangulizi wake. Na hatimaye alielezea uamuzi wa kuruhusu makasisi kuwabariki wapenzi wa jinsia moja mwaka wa 2023 kama "wakati wa matumaini kwa Kanisa".
Ulaya yaanza kujitayarisha kwa vita vikubwa vinavyoweza kutokea
NATO inadai kuwa Urusi inaendesha vita vya mseto dhidi ya muungano huo na inajiandaa kwa vita halisi.
Kuongezeka kwa idadi ya matukio yaliyoripotiwa na kuthibitishwa yanayohusisha ukiukaji wa anga ya NATO imesababisha ongezeko la haraka la mivutano barani Ulaya na wasiwasi kuhusu nia ya muda mrefu ya Urusi.
Wataalamu wa Magharibi wanaona kuwa uchumi wa Urusi kwa ujumla unazidi kuhamasishwa kwa mahitaji ya vita, na hii inachangia ukuaji wa jumla wa uwezo wa kijeshi wa Urusi.
Hatahivyo, hakuna dalili dhahiri za kujiandaa kwa uvamizi, kama vile harakati za askari. Kwa hiyo, makadirio mengi yanaonesha muda wa miaka kadhaa, wakati ambapo Urusi inaweza kujiandaa na kuanzisha vita kamili katika Ulaya Magharibi.
Unaweza kusoma;
Jina la mshambuliaji wa sinagogi la Manchester latangazwa, tukio lililoelezwa kuwa "ugaidi"
Polisi wa Uingereza wametangaza kuwa wamemtambua mhusika wa shambulio hilo lililotoka Alhamisi asubuhi ndani ya sinagogi katika eneo la Crumpsall, kaskazini mwa Manchester.
Shambulizi hilo lililosadifiana na Yom Kippur, siku takatifu zaidi katika kalenda ya Kiyahudi, lilisababisha vifo vya watu wawili na wengine watatu kujeruhiwa, akiwemo mlinzi, kwa mujibu wa Polisi.
Polisi wa Uingereza walisema mshambuliaji huyo aliyetambulika kwa jina la Jihad al-Shami, Muingereza mwenye umri wa miaka 35 mwenye asili ya Syria, aliendesha gari lake hadi kwa wapita njia nje ya Sinagogi ya Usharika wa Heaton Park Hebrew kabla ya kuwashambulia kwa kisu. Aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika eneo la tukio.
Polisi walitangaza kukamatwa kwa watu wengine watatu kama sehemu ya uchunguzi, na kuelezea tukio hilo kama "tukio la kigaidi."
Kulingana na polisi, walipokea ripoti saa 9:31 asubuhi kwa saa za huko kuhusu gari lililowagonga waumini nje ya sinagogi, kabla ya mtu mmoja kuendelea kuwachoma visu kadhaa.
Dame Sarah Mullally ateuliwa mwanamke wa kwanza kuoliongoza kanisa la Kianglikana duniani
Kwa mara ya kwanza katika karibu miaka 500 ya historia, Kanisa la Anglikana limemteua mwanamke kuliongoza.
Dame Sarah Mullally, 63, ameteuliwa kuwa Askofu Mkuu Mteule wa Canterbury.
Alikuwa akijenga msingi mpya katika taaluma yake aliyoichagua hata kabla ya kuwa kasisi.
Mwaka wa 1999 akawa afisa mkuu wa uuguzi mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea nchini Uingereza.
Kwa zaidi ya miaka saba amehudumu kama Askofu wa London, mshiriki mkuu wa tatu wa makasisi katika Kanisa na mwanamke wa kwanza kufanya kazi hiyo.
Wanawake wameruhusiwa tu kuwa mapadri katika Kanisa la Anglikana tangu katikati ya miaka ya 1990.
Lakini kuna maaskofu wakuu katika Kanisa la Anglikana ambao wanapinga waziwazi wanawake kujiunga na ukasisi hata kidogo kuongoza taasisi hiyo.
Sheria inawahitaji Maaskofu Wakuu wa Canterbury kustaafu wakiwa na umri wa miaka 70, ambayo labda ni sababu mojawapo kwa nini wengine hawakumwona Dame Sarah Mullally akiwa na nafasi ya kuchaguliwa.
Hata hivyo ameishia kuandikisha historia. Tarehe ya kutawazwa kwakerasmi bado haijatangazwa.
Mtoto wa Robert Mugabe afikishwa mahakamani kwa tuhuma za dawa za kulevya
Mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amefikishwa katika mahakama ya Harare akikabiliwa na shtaka la kupatikana na dawa za kulevya.
Robert Mugabe Jr, 33, alikamatwa Jumatano asubuhi alipokuwa akiendesha gari kwa njia isiyo sahihi katika barabara ya njia moja, kulingana na hati za mahakama.
Polisi walipekua begi jeusi alilokuwa amevaa wakati huo na inadaiwa walipata sacheti mbili ndogo za bangi.
Kufuatia tukio hilo, polisi walisema katika taarifa kwamba watu watano "waliohusishwa naye" pia walikamatwa.
Wakili wa Bw Mugabe aliambia BBC wanapanga kukana mashtaka, na kupinga madai yaliyotolewa na polisi.
Bw Mugabe aliyekuwa amevaa kofia nyekundu huku akiwa anazungumza na simu yake alipokuwa akiongozwa kwenda katika mahakama ya hakimu siku ya Alhamisi. Alizungukwa na watu na hakuwa amefungwa pingu.
Mahakama ilimweka rumande Bw Mugabe akisubiri uamuzi wa dhamana siku ya Ijumaa.
Polisi wamesema wataendelea na uchunguzi.
Putin aonya Marekani dhidi ya kupeleka makombora Ukraine
Rais wa Urusi Vladimir Putin Alhamisi ameonya kwamba kupeleka makombora ya Marekani ya Tomahawk nchini Ukraine kutasababisha "kiwango kipya cha mashambulizi", pamoja na kuharibu uhusiano kati ya Urusi na Marekani.
Akizungumza katika mkutano huko Sochi, Putin alisema hilo halibadilisha hali ilivyo katika mstari wa vita, ambako Urusi inafikia maendeleo yake ingawa kwa mwendo wa taratibu inasonga mbele.
"Utumiaji wa makombora ya Tomahawk bila uwepo wa jeshi la Marekani ni jambo lisilowezekana. Hii itasababisha kiwango kipya kabisa cha mashambulizi, pamoja na uhusiano wa Urusi na Marekani, Putin alisema.
Kiongozi huyo wa Urusi alisema kuwa hata kama makombora ya Tomahawk yatasababisha uharibifu kwa Urusi ikiwa yatapelekwa Ukraine, ulinzi wa anga wa Urusi utaitikia haraka tishio jipya.
Soma zaidi:
Misri inajitahidi kushawishi Hamas kukubali mpango wa Trump, asema waziri wa mambo ya nje
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema Alhamisi kwamba nchi yake inashirikiana na Qatar na Uturuki kuwashawishi Hamas kukubali mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump kumaliza vita vilivyodumu takriban miaka miwili huko Gaza, na kuonya kwamba mzozo huo utaongezeka ikiwa kundi la wanamgambo litakataa.
Akizungumza katika Taasisi ya Uhusiano ya Kimataifa ya Ufaransa mjini Paris, Badr Abdelatty amesema ni wazi kuwa Hamas inabidi iweke silaha chini na Israel isipewe kisingizio cha kuendelea na mashambulizi yake huko Gaza.
"Tusitoe kisingizio chochote kwa upande mmoja kutumia Hamas kama kisingizio cha mauaji haya ya kichaa ya kila siku ya raia. Kinachotokea ni zaidi ya kilichofanyika tarehe saba ya Oktoba," alisema, akimaanisha shambulio la Hamas la 2023 dhidi ya Israeli, ambapo watu 1,200 waliuawa na zaidi ya watu 200 walichukuliwa mateka, kulingana na Israeli.
Mashambulizi ya Israel yameua zaidi ya watu 66,000 huko Gaza, mamlaka ya afya ya Palestina inasema.
"Ni zaidi ya kulipiza kisasi. Haya ni mauaji ya kikabila na kimbari. Kwa hiyo inatosha," Abdelatty alisema.
Ikulu ya White House ilitoa mapema wiki hii mpango wenye vipengele 20 ambao ulitaka kusitishwa kwa mapigano mara moja, kubadilishana mateka wanaoshikiliwa na Hamas kwa wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel, hatua ya Israel ya kujiondoa kutoka Gaza, upokonyaji silaha wa Hamas na serikali ya mpito inayoongozwa na chombo cha kimataifa.
Soma zaidi:
Venezuela inaishutumu Marekani kwa kupeleka ndege za kivita karibu na pwani yake
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Jenerali Vladimir Padrino alisema Alhamisi kwamba ndege tano za kivita zimegunduliwa karibu na pwani ya nchi hiyo, katika kile alichokitaja kuwa tishio la Marekani.
"Ni ndege za kivita za kibeberu ambazo zimethubutu kuja karibu na pwani ya Venezuela," Padrino alisema kutoka kituo cha anga, katika maoni yaliyotangazwa kwenye televisheni ya serikali, akiongeza habari kuhusu ndege hizo zimeripotiwa kwenye mnara wa udhibiti na shirika la ndege.
"Kuwepo kwa ndege hizi karibu na Bahari yetu ya Caribbean ni jambo baya, uchochezi, na tishio kwa usalama wa taifa," Padrino aliongeza.
Ikulu ya Marekani haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni yake juu ya suala hili.
Katika taarifa ya baadaye, serikali ilisema shirika kubwa la ndege la Colombia Avianca, liliripoti ndege hizo takriban kilomita 75 kutoka pwani ya Venezuela.
Avianca haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.
Venezuela "inamtaka Waziri wa Vita wa Marekani Peter Hegseth kusitisha mara moja kutojali, kutafuta msisimko na uchochezi," ambavyo vinavuruga amani ya Caribbean, taarifa hiyo iliongeza.
Marekani imetuma kundi la meli za kivita katika visiwa vya Caribbean katika operesheni ambayo Washington inasema inapambana na ulanguzi wa dawa za kulevya. Marekani pia imeshambulia boti kadhaa inazodai zilikuwa na dawa za kulevya kutoka Venezuela na kuua waliokuwa ndani yake.
Pia unaweza kusoma:
Mwanamke wa Marekani ahukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kujaribu kumzamisha mtoto wa Kiislamu
Mwanamke wa Texas amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kujaribu kumzamisha msichana wa miaka 3 Mwislamu wa Kipalestina na Marekani katika shambulio la 2024 ambalo mamlaka ilisema lilichochewa na ubaguzi wa rangi.
Rekodi za mahakama zilizotajwa na CBS News na Fort Worth Star-Telegram zilionyesha Jaji Andy Porter alitoa hukumu hiyo kwa Elizabeth Wolf, 43, baada ya kukiri kosa la kujaribu kuua na kumjeruhi mtoto.
Wolf alishtakiwa mwaka jana baada ya shambulio hilo, ambalo lililaaniwa na Rais wa wakati huo Joe Biden.
Kulingana na ripoti za polisi, Wolf alizozana na mamake msichana huyo kwenye kidimbwi cha maji kabla ya kuuliza familia hiyo inatoka wapi.
Kisha akajaribu kumzamisha mtoto huyo wa miaka 3 na kujaribu kumshika kaka yake mwenye umri wa miaka 6.
Mama wa watoto alifanikiwa kumvuta bintiye kutoka kwenye maji na watoto waliondolewa baada ya madaktari kuthibitisha kuwa hawakudhurika.
Pia unaweza kusoma:
'Nilipotea njia' - Diddy amwomba jaji amuhurumie usiku wa kuamkia hukumu yake
Mwanamuziki maarufu wa muziki wa kufokafoka Sean "Diddy" Combs amemwandikia barua jaji anayesimamia kesi yake ya jinai, akiomba ahurumiwe wakati wa hukumu yake siku ya Ijumaa na kulaumu tabia yake ya zamani juu ya uraibu wa dawa za kulevya.
Katika barua hiyo yenye kurasa nne, Diddy anaomba radhi “kwa maumivu yote ambayo nimesababisha” na anasema kwamba amebadilika baada ya kukaa kwa miezi 13 katika jela ya Brooklyn.
Barua hiyo ya Alhamisi imetolewa saa chache kabla ya kusikilizwa kwa hukumu yake saa 10:00 ET (15:00GMT) siku ya Ijumaa.
Mnamo mwezi Julai, alipatikana na hatia ya mashtaka mawili ya ukahaba na sasa anakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela.
Waendesha mashitaka wanatafuta kifungo cha angalau miaka 11, lakini wanasheria wa Combs wanaomba kwamba aachiliwe baadaye mwezi.
Soma zaidi:
Uwanja wa ndege wa Munich wafungwa baada ya ndege zisizo na rubani kuonekana karibu
Uwanja wa ndege wa Munich nchini Ujerumani umefuta safari zaidi ya kumi na mbili baada ya ndege zisizo na rubani kuonekana karibu na anga yake.
Takriban safari 17 za ndege zilisitishwa mjini Munich, na kuathiri takriban abiria 3,000.
Uwanja wa ndege wa Munich ulisema ulielekeza safari 15 za ndege kwenda miji ya karibu.
Hakukuwa na uthibitisho wa haraka wa wapi ndege hizo zisizo na rubani zilitoka. Viwanja vya ndege kadhaa kote barani Ulaya vimefungwa katika wiki za hivi karibuni kwa sababu ya ndege zisizo na rubani ambazo hazijatambuliwa.
Uwanja wa ndege wa Munich ulitoa taarifa kwa mamlaka baada ya ndege hizo kugunduliwa.
Safari za ndege kutoka uwanja wa ndege wa Munich "zimesimamishwa", uwanja wa ndege ulisema.
Udhibiti wa trafiki ya anga ulielekeza upya safari za ndege ambazo zilipaswa kutua Munich hadi Stuttgart, Nuremberg, Vienna na Frankfurt.
Kwa sababu kulikuwa na giza, hakuna habari kuhusu aina, ukubwa au asili ya ndege hizo zisizo na rubani zilizothibitishwa, msemaji wa Polisi wa Shirikisho Stefan Bayer aliliambia Gazeti la Bild. Ndege zisizo na rubani zilionekana kwa mara ya kwanza saa 21:30 kwa saa za eneo (19:30 GMT), na kisha tena saa moja baadaye, polisi walisema.
BBC imewasiliana na polisi wa jimbo la Bavaria na polisi wa shirikisho la Ujerumani.
Pia unaweza kusoma:
Marekani imetuma pesa kwa Lebanon wakati ikielekea kuipokonya silaha Hezbollah, duru zinasema
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump uliidhinisha dola milioni 230 kwa vikosi vya usalama vya Lebanon wiki hii huku wakishinikiza kunyang'anya silaha kundi lililokuwa na nguvu la Hezbollah, vyanzo vya habari huko Washington na Beirut vilisema.
Chanzo cha Lebanon kinachofahamu uamuzi huo kilisema ufadhili huo ni pamoja na dola milioni 190 kwa Wanajeshi wa Lebanon na dola milioni 40 kwa Kikosi cha Usalama wa Ndani.
Wasaidizi wa chama cha Democratic Marekani walisema fedha hizo zilitolewa kabla tu ya mwaka wa fedha wa Washington kumalizika Septemba 30. "Kwa nchi ndogo kama Lebanon, hiyo ni muhimu sana," mmoja wa wasaidizi hao alisema kwenye simu na waandishi wa habari, akiomba kutotajwa jina ili kuzungumza kwa uhuru.
Ufadhili huo ulitolewa wakati utawala wa rais wa Republican umekuwa ukipunguza programu nyingi za usaidizi wa kigeni, ukisema kwamba kipaumbele chake katika matumizi ya dola za walipa kodi ni Marekani Kwanza.
Kutolewa kwa fedha hizo kulionekana kuakisi kipaumbele ambacho Trump ameweka katika kujaribu kutatua mzozo wa Gaza na eneo kubwa zaidi.
Pia unaweza kusoma: