Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Makombora ya Israel yashambulia jengo la makazi Beirut kati
Jengo la makazi linasemekana kuharibiwa kabisa, na pia kuna ripoti za watu kadhaa kufariki.
Muhtasari
- Mazungumzo yaelekea kusambaratika COP29
- Mabao 50 ya Harry Kane katika Bundesliga
- Mchezo wa kamari marufuku Kano Nigeria
- Mbowe na wenzake waachiwa huru mkoani Songwe
- Mataifa yanayoinukia kichumi yachemka kuhusu ufadhili katika COP29
- Mpox inasalia kuwa dharura ya kiafya ya umma kimataifa
- Makombora ya Israel yashambulia jengo la makazi Beirut kati
Moja kwa moja
Ambia Hirsi & Maryam Dodo
Mazungumzo yaelekea kusambaratika COP29
Majadiliano yanaonekana kusambaratika Baku Azerbaijan kunakofanyika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi COP29.
Mwandishi wa BBC ameshuhudia wawakilishi wa kundi la mataifa maskini - lililo na ushawishi na linalowakilisha mataifa mengine maskini - wakitoka katika mkutano huo kwa pamoja na rais wa COP29 kujadili pendekezo jipya la fedha kutoka mataifa tajiri.
BBC inafahamu kuwa $300bn zimependekezwa – kiwango ambacho kund hilo linahisi ni kidogo sana na badala yake wanataka $500bn.
Mjumbe mmoja ameiambia BBC kuwa huenda mkutano huo wa COP ukasitishwa kwa muda na kufanyika tena katika tarehe nyingine siku za mbele. Hili limewahi kushuhudiwa katika mkutano wa nyuma mnamo 2000 katika COP6.
Wakati baadhi ya wajumbe wakiondoka katika mkutano huo, baadhi ya wawakilishi na wanaharakati wa mazingira na haki za binaadamu wamesalia.
Wanaendelea kuweka shinikizo kwa mataifa yanayoendelea kushinikiza ufadhili zaidi kutoka kwa mataifa tajiri.
Mabao 50 ya Harry Kane katika Bundesliga
Harry Kane ameandikisha historia kwa kufunga jumla ya mabao 50 kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani maarufu Bundesliga.
Kane amefikia mabao hayo kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa alipofunga hat-trick iliyoipatia Bayern Munich ushindi wa 3-0 dhidi ya Augsburg.
Nahodha huyo wa England alihitaji kufunga mabao matatu tu kuandikisha historia hiyo.
Kane amefunga mabao 50 katika mechi 43 za Bundesliga kumaanisha kuwa amevunja rekodi ya Erling Haaland ya kufunga mabao 50 katika mechi 50 alipokuwa akichezea klabu ya Borussia Dortmund, kabla mchezaji huyo wa Norway kujiunga na Manchester City.
Ushindi huo uliwafanya Bayern kuwa pointi nane mbele ya Leipzig kileleni mwa ligi kabla ya mechi za wikendi.
Wababe hao wa Ujerumani hamepata ushindi mara tisa na kutoka sare mara mbili katika mechi 11 walizocheza.
Pia unaweza kusoma:
Mchezo wa kamari marufuku Kano Nigeria
Maafisa wa polisi wanaosimamia nidhamu katika dini ya Kiislamu kaskazini mwa Nigeria wanasema wataendeleza sera yao ya kufunga maduka yote ya kucheza kamari baada ya uamuzi wa mahakama kuhusu mchezi huo.
Mahakama ya juu zaidi Ijumaa ilitupilia mbali sheria ya mnamo 2005 ilioidhinisha tume ya kitaifa ya mchezo wa bahati nasibu na iliohalilisha mchezo huo wa kamari.
Polisi hiyo ya nidhamu ijulikanayo kama Hisbah imesema uamuzi wa mahakama unamaanisha kuwa misako dhidi ya maduka ya kamari itashinikizwa katika jimbo hilo kwasababu ni kinyume cha sheria za dini ya kiislamu.
Maduka haya yanapatikana kote Kano na huwavutia wateja wengi wanaofika kutazama mechi za soka katika televisheni.
Kano ni mojawapo ya majimbo 12 yalio na idadi kubwa ya waislamu na yanayofuata sheria za dini ya kiislamu na sheria za nchi.
Mbowe na wenzake waachiwa huru mkoani Songwe
Jeshi la polisi Mkoani Songe limemuachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe na wenzake 10 baada ya kuwashikilia kwa saa 12.
Kiongozi huyo alikamatwa jana Alhamisi baada ya kujaribu kuhutubia mkutano wa hadhara kinyume cha utaratibu katika mkoa huo wa Songwe.
‘’Tulivamiwa na jeshi la polisi wakati tunatoka kwenye mikutano vijijini. Polisi hawajaweza kutupatia sababu mahususi ya kwanini wametukamata,’’ alisema Mbowe mara baada ya kuachiwa usiku wa jana akiongeza kuwa polisi hatimaye waliwaambia kuwa kosa lao ni kuharibu taratibu ya mikutano ya kampeni.
Jeshi la polisi lilikuwa limetoa taarifa kuwataka viongozi wa vyama kutii na kufuata ratiba ya kampeni zilizotolewa na wazimamizi wa uchaguzi ilikuepusha vurugu.
‘‘Mtu yeyote ambaye atakiuka taratibu zilizowekwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua,’’ ilisema taarifa iliyotolewa na jeshi hilo Alhamisi tarehe 22.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Jumatano ya wiki ijayo, Novemba 27.
Soma pia:
Mataifa yanayoinukia kichumi yachemka kuhusu ufadhili katika COP29
Mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi Cop29 umeongezeka muda baada ya hapo awali kutarajiwa kumalizika Ijumaa.
Mgawanyiko unaonekana kuongezeka kati ya mataifa tajiri na mataifa yanayoinukia kiuchumi kuhusu fedha zitakazosaidia nchi zilizo katika hatari zaidi ya kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi.
Mataifa tajiri siku ya Ijumaa yalipendekeza kuongeza zaidi ya mara dufu kufika $250bn kwa mwaka - fedha zitakazokwenda kwa mataifa yanayoendelea kila mwaka kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Lakini mataifa maskini yalikataa pendekezo hilo kwa hasira yakisema ni kiwango cha chini cha fedha.
Jitihada za kukabiliana na kupunguza hewa chafu pia zilijadiliwa katika mkutano huo uliopitisha muda wa kumalizika huku kukiwa hakuna ishara ya lini makubaliano yatafikiwa.
Suala la fedha limekuwa donda sugu kwa muda mrefu katika majadiliano kuhusu tabia nchi kimataifa.
Jitihada za awali kuwasilisha $100bn kwa mataifa yanayoendelea zilichelewa na mara nyingi kuishia kuwa mikopo.
Mataifa yanayoendelea yanasema yanahitaji $1.3tn kufikia mwaka 2035 kukabiliana na athari inayoongezeka inayotokana na hali ya ujoto duniani na kuchukuliwa hatua kubwa zaidi kupunguza uzalishaji wa hewa mkaa.
Pia unaweza kusoma:
Mpox inasalia kuwa dharura ya kiafya ya umma kimataifa
Kamati ya dharura ya Shirika la afya duniani (WHO) imethibitisha kuwa Mpox inasalia kuwa dharura ya kiafya ya umma kimataifa (PHEIC)
Hii ni tahadhari kubwa iliowahi kutolewa kwa mlipuko wowote ule uliowahi kutokea. Mkurugenzi mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus, ameidhinisha mapendekezo ya kamati hiyo akitaja visa vinavyoongezeka, kusambaa kwa ugonjwa huo katika maeneo mapya na uhitaji wa dharura wa kuwepo muitikio ulioratibiwa kimataifa.
Ripoti kamili ya mapendekezo ya kamati hiyo inatarajiwa kuchapishwa wiki ijayo.
Visa vya Mpox vimekuwa vikiongezeka Afrika mashariki na kati tangu mapema 2024 huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ikiathirika pakubwa na aina mpya na kali ya ugonjwa huo ijulikanayo kama Clade 1b.
Hii ilichangia tangazo la awali mnamo Agosti la dharura ya kiafya ya umma kimataifa. Mpaka sasa nchi 20 za Afrika zimeripoti visa vya maambukizi huku Angola ikiwa ndio nchi ya hivi karibuni kuripoti maambukizi.
Maelezo zaidi:
Makombora ya Israel yashambulia jengo la makazi Beirut ya kati
Shambulio kubwa la Israeli limeporomosha jengo la makazi Beirut kati nchini Lebanon.
Watu 15 wameuawa na zaidi ya watu 20 wamejeruhiwa kwa mujibu wa wizara ya afya Lebanon.
Jengo hilo la ghorofa nane limeharibiwa kabisa kwa makombora matano yaliofyetuliwa dhidi ya wilaya ya Basta ilio na watu wengi kwa mujibu wa shirika la habari la kitaifa Lebanon NNA.
Shambulio hilo limetekelezwa mwendo wa saa kumi alfajiri Jumamosi huku milipuko ikiutikisa mji.
Wachanbuzi wanaashiria kuwa mlengwa alikuwa afisa wa ngazi ya juu, jeshi la Israel halijatoa tamko lolote.
Katika miezi ya hivi karibuni makombora ya Israeli yamesababisha vifo vya wafuasi wakuu wa Hezbollah mjini Beirut akiwemo kiongozi wa kundi hilo Hassan Nasrallah.
Soma pia:
Karibu katika matangazo ya moja kwa moja leo Jumamosi 23.11.2024