Uchumi wa Kenya umeendelea kusuasua ikilinganishwa na ule wa Tanzania katika eneo la Afrika Mashariki, hasa kutokana na utegemezi mkubwa wa mauzo ya bidhaa ghafi nje ya nchi jambo linalokwamisha ukuaji wa uchumi na kuongeza kiwango cha umaskini.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Ujumuishaji wa Bara la Afrika 2025 iliyotolewa na Umoja wa Afrika (AU).
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla unafanya chini ya wastani wa bara katika juhudi za kuimarisha uchumi wake kupitia ubunifu, uongezaji thamani wa bidhaa na upanuzi wa sekta za uzalishaji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kenya inajipata ikifanya vibaya zaidi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku uchumi wake ukiendelea kutegemea zaidi mauzo ya bidhaa ghafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani.
Hali hiyo, ripoti inasema, imeathiri maendeleo ya viwanda na sekta ya uzalishaji nchini, jambo linalochangia upungufu wa ajira, kipengele muhimu katika kupunguza ukosefu wa ajira na umaskini.
Alama ya utofauti wa biashara katika EAC (0.3920) imebaki chini kidogo ya wastani wa bara la Afrika (0.4072).
Biashara nchini Kenya bado inatawaliwa na mauzo ya bidhaa ghafi (asilimia takribani 68 ya mauzo nje), huku mauzo ya bidhaa za viwandani (0.3420) yakiwa nyuma ya uagizaji wake (0.5986).
Kwa upande wa utofauti wa biashara, Tanzania inaongoza kwa alama 0.4457, ikifuatiwa na Burundi, kisha Kenya.
Nchi zinazofanya vibaya zaidi ni Uganda (0.2848), Rwanda (0.2241) na Sudan Kusini (0.2116), hali inayoonyesha pengo kubwa kati ya wingi wa biashara na kiwango cha ubunifu wa uchumi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa biashara ya bidhaa za kati bado ni dhaifu, huku mitandao ya uzalishaji wa kikanda ikiwa haijakomaa ipasavyo.
Wataalamu wa Umoja wa Afrika wanapendekeza kuwa jumuiya ya Afrika mashariki EAC ichukue hatua mahsusi za kupunguza pengo la biashara kwa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara ndani ya eneo, kukuza uzalishaji wa viwandani, na kuhamasisha uongezaji thamani wa bidhaa.
“Kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda, hasa katika sekta za usindikaji wa mazao na viwanda vidogo, kunaweza kusaidia kupunguza pengo kati ya uagizaji na uuzaji nje. Uboreshaji wa njia kuu za usafirishaji kama vile Mombasa na Dar es Salaam ni muhimu kwa kuongeza ujumuishaji wa kiuchumi,” inasema ripoti hiyo.
Aidha, ripoti inabainisha kuwa nchi dhaifu kama Somalia na Sudan Kusini zinahitaji msaada maalumu unaojumuisha uwekezaji katika miundombinu na ushirikiano wa kiusalama, ili kuwezesha ushiriki wao kamili katika ujumuishaji wa kiuchumi wa bara.