Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Hezbollah yasema 'ina imani' inaweza kuzuia uvamizi wa Israel

Katika taarifa mpya ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas, Hezbollah inasema ina "ujasiri" katika uwezo wake wa "kuzuia uvamizi wa [Israel]", na imeapa kuendelea kupigana.

Muhtasari

  • Hezbollah yasema 'ina imani' inaweza kuzuia uvamizi wa Israel
  • Mwanamume akumbuka maisha 'mazuri' kabla ya vita kuua jamaa wake Gaza
  • Makumbusho yafanyika mwaka mmoja tangu kutokea kwa shambulizi la Hamas
  • 'Mwanaume aliyetekwa nyara Oktoba 7 auawa'
  • Jeshi la Israel lashambulia maeneo ya Hamas kote Ukanda wa Gaza
  • Mwanajeshi wa Israel auawa kwenye mpaka wa Lebanon
  • Mlipuko waua Wachina wawili karibu na uwanja wa ndege wa Karachi, Pakistan
  • Mwanaharakati wa upinzani wa Urusi aliuawa akipigania Ukraine
  • ‘Binti yangu mateka wa Uingereza-Israel amesahaulika’ - mama

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Urusi yamhukumu Mmarekani mwenye umri wa miaka 72 jela kwa kuwa mamluki

    Mahakama ya Urusi imemhukumu raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 72 kifungo cha karibu miaka saba jela kwa madai ya kupigana kama mamluki wa Ukraine.

    Waendesha mashtaka walisema Stephen James Hubbard alikuwa akihudumu katika kitengo cha ulinzi kilichoko katika mji wa mashariki wa Izyum alipokamatwa na vikosi vya Urusi mnamo Aprili 2022, muda mfupi baada ya Moscow kuzindua uvamizi wake kamili wa Ukraine.

    Hubbard "alipokea fidia" kwa ushiriki wake katika vita kwa upande wa Ukraine, taarifa ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Urusi ilisema.

    Sasa amehukumiwa kifungo cha miaka 6 na miezi 10 gerezani.

    Hubbard, mzaliwa wa Michigan, alikiri mashtaka wiki iliyopita, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

    Hata hivyo, dada yake Patricia Fox aliiambia Reuters kwamba Hubbard alikuwa na maoni yanayoiunga mkono Urusi na hangeweza kuchukua silaha katika umri wake.

    "Yeye si mwanajeshi," Bi Fox aliiambia Reuters, akiongeza kuwa kaka yake "hajawahi kuwa na bunduki, kumiliki bunduki, kufanya lolote kati ya hayo... Yeye ni mpiganaji wa amani."

    Kulingana na Bi Fox, Hubbard alihamia Ukraine mwaka wa 2014 na aliishi huko kwa muda na mwanamke, ambaye alinusurika na malipo kidogo ya uzeeni.

    Yeye na mpenzi wake baadaye walitengana lakini aliendelea kuishi Ukraine. Ingawa Hubbard alizuiliwa na vikosi vya Urusi mapema mwaka wa 2022, kesi yake ilitangazwa hadharani tu ilipoanza huko Moscow mnamo Septemba.

  2. Mwandishi kushtakiwa nchini Ufaransa kwa kupuuza mauaji ya kimbari ya Rwanda

    Mwandishi wa Kifaransa na Cameroon, Charles Onana, anatazamiwa kufikishwa mahakamani mjini Paris akituhumiwa kupuuza mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994.

    Takribani Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa ndani ya siku 100.

    Katika kitabu kilichochapishwa miaka mitano iliyopita, Bw Onana alielezea wazo kwamba serikali ya Wahutu ilikuwa imepanga mauaji ya halaiki nchini Rwanda kama "moja wa kashfa kubwa" katika karne iliyopita.

    Wakili wake, Emmanuel Pire, anasisitiza kuwa Bw Onana hahoji kwamba mauaji ya halaiki yalifanyika, au kwamba Watutsi walilengwa haswa.

    Bw Pire aliliambia shirika la habari la AFP kwamba kitabu kinachozungumziwa ni "kazi ya mwanasayansi wa siasa kulingana na utafiti wa miaka 10 ili kuelewa mifumo ya mauaji ya kimbari kabla, wakati wa mauaji na baada".

    Bw Onana, ambaye sasa ana umri wa miaka 60, na mkurugenzi wake wa uchapishaji, Damien Serieyx, walishtakiwa miaka minne iliyopita kuhusu kitabu hicho.

    Kesi hiyo ililetwa na Shirika lisilo la kiserikali la Survie, na Shirikisho la Kimataifa la Haki za Kibinadamu (FIDH) kwa "kupinga hadharani uhalifu dhidi ya ubinadamu".

    Kesi ya Jumatatu ni kesi ya pili tu ya kukana mauaji ya kimbari ya Rwanda kusikizwa nchini Ufaransa.

    Chini ya sheria za Ufaransa, ni kosa kukataa au "kupunguza" ukweli wa mauaji yoyote ya kimbari ambayo yanatambuliwa rasmi na Ufaransa.

    Unaweza kusoma;

  3. Mwanangu si 'shetani' , asema mama Diddy

    Mama yake Sean "Diddy" Combs amesema "amesikitishwa na kuhuzunishwa sana" na tuhuma zinazotolewa dhidi ya mwanaye, zilizo za "uongo".

    Mwanamuziki huyo, anayejulikana kwa vibao kama vile I'll Be Missing You, 1997 alikamatwa kwa tuhuma za ulanguzi wa ngono na ulaghai mwezi uliopita.

    Kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha Manhattan baada ya kunyimwa dhamana.

    Katika taarifa yake, Janice Small Combs alimtetea mwanaye, akisema kwamba ingawa "alifanya makosa siku za nyuma, kama sisi sote ambavyo tumefanya", yeye "sio mnyama ambaye wanamuonesha". "Inasikitisha kuona mwanangu akihukumiwa bila ukweli, lakini kwa simulizi iliyotengenezwa kwa uwongo," aliandika.

    Hatua hiyo Ilikuja siku tano baada ya kufichuliwa kwamba Bw Combs anaweza kukabiliwa na mashtaka kutoka kwa washitaki zaidi ya 100, wanaume na wanawake, kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji. Wakili wa nyota huyo amekanusha mashtaka hayo na mengine yote ya awali, akiyataja kuwa ya "uongo na kashfa".

    Amekabiliwa na kesi kadhaa tangu mwaka jana, wakati mpenzi wake wa zamani Cassie Ventura alipomshtaki kwa ubakaji na unyanyasaji.

    Bw.Combs alikanusha madai hayo, na kesi hiyo ilitatuliwa nje ya mahakama siku moja baada ya kuwasilishwa.

    Unaweza kusoma;

  4. IDF yawataka wakazi wa kusini mwa Gaza na Lebanon kuhama

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limewataka wakazi wa Gaza na Lebanonkuhama.

    Msemaji wa IDF Avichay Adraee anasema watu wa kusini mwa Gaza, karibu na Khan Younis, wanapaswa kuelekea katika eneo la kibinadamu la Al-Mawasi, ukanda mwembamba wa ardhi karibu na Bahari ya Mediterania katika Ukanda wa Gaza.

    Hapo awali, wakazi katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza, ikiwa ni pamoja na Jabalia, Beit Hanoun na Beit Lahia walitakiwa na IDF kuhama.

    Mbali na Gaza, Adraee pia alitoa onyo la dharura kwa wakazi wa vijiji zaidi ya 20 kusini mwa Lebanon, ikiwa ni pamoja na Tayr Harfa na al-Mansouri.

    IDF imewaambia waliohamishwa kuondoka makwao na kuelekea "kaskazini mwa Mto Awali". "Mtu yeyote ambaye yuko karibu na wanachama wa Hezbollah, mitambo au silaha anaweka maisha yake hatarini," IDF inasema.

    Unaweza kusoma;

  5. Habari za hivi punde, Maafisa 10 wa zimamoto wauawa kwa shambulio la Israel-Lebanon

    Tunapata ripoti za shambulio la Israel kusini mwa Lebanon ambalo limewaua maafisa kadhaa wa zima moto, kulingana na wizara ya afya ya nchi hiyo.

    Wizara ya afya inasema uvamizi katika jengo moja huko Baraachit umewaua maafisa 10 wa zimamoto .

    Mamlaka zinasema kuwa zimetoa miili ya watu wanane kufikia sasa, shirika la habari la AFP linaripoti.

    Wizara ya afya ya Lebanon imesema kuwa shambulio hilo lilifanyika kwenye jengo la manispaa huko Baraachit katika eneo la Bint Jbeil, kusini mwa Lebanon.

    Wizara ya afya ya Lebanon inasema uondoaji wa vifusi kutoka kwa jengo lililoharibiwa vibaya unaendelea kwani waliouawa bado hawajatambulika.

  6. Ukraine yashambulia bohari ya mafuta Crimea

    Jeshi la Ukraine limesema limefanya shambulio kwenye kituo kikubwa cha mafuta karibu na rasi ya Crimea inayokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni shambulio la hivi karibuni zaidi katika wimbi la mashambulizi yaliyolenga vituo vya nishati vinavyodhibitiwa na Urusi.

    Maafisa wa Kyiv walisema vikosi vya makombora vya nchi hiyo vilianzisha shambulio usiku kwenye kituo cha Feodosia, kituo kikubwa zaidi cha usindikaji wa mafuta kwenye peninsula.

    Maafisa waliowekwa rasmi na Urusi huko Crimea hawajathibitisha kutokea kwa shambulizi hilo, lakini walikiri kutokea moto katika kituo hicho.

    Hakuna majeruhi walioripotiwa. Hali ya dharura katika ngazi ya manispaa imetangazwa, huku watu 300 wakihamishwa kutoka Feodosia kutokana na moto huo, shirika la habari la serikali la Tass liliripoti.

    Unaweza kusoma;

  7. Hezbollah yasema 'ina imani' inaweza kuzuia uvamizi wa Israel

    Katika taarifa mpya ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas, Hezbollah inasema ina "ujasiri" katika uwezo wake wa "kuzuia uvamizi wa [Israel]", na imeapa kuendelea kupigana.

    Kundi hilo lenye makao yake makuu Lebanon linashirikiana na Hamas, na yote yanaungwa mkono na kufadhiliwa na Iran.

    Hezbollah inayaelezea matukio ya tarehe 7 Oktoba kama "ya kishujaa", ikisema yatakuwa na athari za "kihistoria" katika eneo hilo.

    "Hakuna mahali" kwa Israel huko, inasema, na "lazima iondolewe, haijalishi itachukua muda gani".

    Hezbollah pia inalaumu "Marekani na washirika wake" kwa ghasia huko Gaza na Lebanon iliyofuata shambulio la Hamas la Oktoba 7, wakisema "wanawajibika kikamilifu".

    Soma zaidi:

  8. Mwanamume anakumbuka maisha 'mazuri' kabla ya vita kuwaua mwanawe, mama, na dada yake Gaza

    Maisha katika eneo la Gaza iliyozingirwa kabla ya vita hayakuwa rahisi kabisa, lakini anapokumbuka siku za nyuma huku akiwa ameshika picha za watoto wake wanne wakitabasamu, Ahmed Younis anayakumbuka maisha kuwa "mazuri".

    "Nilikuwa nalenga kujiimarisha. Nilinunua nyumba na nilikuwa na uthabiti wa kifedha," anasema. "Nilikuwa nikipanga maisha bora ya baadaye kwa watoto wangu. Niliwapeleka kwa shule bora za chekechea."

    Familia hiyo iliondoka nyumbani kwao Nuseirat katikati mwa Gaza wakati wanajeshi wa Israel waliposonga mbele, lakini walikuwa wamejisikia salama vya kutosha na kurejea. Kisha, mwezi mmoja uliopita, nyumba yao ilishambuliwa na mashambulizi ya anga ya Israel.

    "Ndani ya sekunde chache tulikuwa tumezungukwa na moto na kunaswa kwenye vifusi," Ahmed anasimulia akiwa kwenye kitanda chake hospitalini.

    Mwanawe mwenye umri wa miaka sita, Hossam - mvulana mchangamfu ambaye alipenda kuendesha baiskeli yake na kumfanya baba yake kuwa na kazi za hapa na pale kwa ajili yake - aliuawa. Jamaa mmoja alibeba maiti yake kwenye shuka nyeupe huku Ahmed akitiririkwa na machozi.

    Mama na dadake Ahmed pia waliuawa. Yeye na mkewe na watoto wao watatu waliosalia waliungua vibaya na binti mmoja kupoteza miguu yake.

    "Nataka kujua ni kwa nini," Ahmed anamwambia mpigapicha wetu wa BBC. "Sisi ni raia, na hatuna tishio lolote."

    Sasa, hamu kuu ya Ahmed ni kuondoka Gaza kutafuta matibabu bora kwa familia yake.

    "Kama ningeweza, ningeondoka, na kuwapeleka kutibiwa nje ya nchi kabla ya kitu kingine chochote," anatuambia. "Natumai kutoka kwa Mungu kwamba [vita] hivi vitakoma leo, kabla ya kesho."

    Israel haiwaruhusu waandishi wa habari wa kimataifa kutoka mashirika ya vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na BBC, ufikiaji huru wa Gaza. Waandishi wa habari wa Palestina wameripoti kutoka ndani ya Gaza tangu kuanza kwa vita, lakini makumi wameuawa, kujeruhiwa au kutoweka.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Makumbusho yafanyika mwaka mmoja tangu kutokea kwa shambulizi la Hamas

    Asubuhi ya leo, watu wamerejea kwenye eneo kulikofanyika shambulio wakati tamasha lilikuwa likiendelea la Supernova huko Re'im, kusini mwa Israel, ambapo zaidi ya watu 350 waliuawa na Hamas mwaka mmoja uliopita leo.

    Wakati huohuo, jamaa walishikilia picha za wapendwa wao waliokuwa kwenye tamasha hilo.

    Wengi katika sherehe hiyo wamevalia fulana zenye picha za wapendwa wao

  10. Mwanaume aliyetekwa nyara Oktoba 7 auawa - Jukwaa la Familia Zilizotoweka limesema

    Idan Shtivi, mmoja wa mateka waliochukuliwa na Hamas kutoka tamasha la muziki la Supernova tarehe 7 Oktoba mwaka jana, ameuawa, Jukwaa la Mateka na Familia Zilizotoweka linasema.

    Kundi hilo ambalo linalenga kuwarejesha waliotekwa nyara nchini Israel, linasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 "alijulikana kwa kujitolea kwa ajili ya wale walio karibu naye".

    Jukwaa hilo limeongeza kuwa wakati shambulio hilo lilipoanza, Shtivi aliamua "kujitolea" kusaidia watu wawili wasiojulikana kutoroka kutoka kwa eneo la tukio, lakini gari lao lilishambuliwa njiani.

    Miili ya watu hao wawili ilipatikana.

    Hamas iliteka nyara watu 251 wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7, kulingana na takwimu za Israel.

    Kabla ya kifo cha Shtivi kutangazwa, 117 kati ya wale waliochukuliwa mateka walikuwa wameachiliwa, 37 walithibitishwa kufariki, na 97 hawajulikani waliko.

    Soma zaidi:

  11. Jeshi la Israel lashambulia maeneo ya Hamas kote Ukanda wa Gaza - msemaji wa jeshi la Israel

    Msemaji wa jeshi la Israel amesema (IDF) sasa inashambulia maeneo ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.

    Makombora manne yamerushwa kuelekea Israel kutoka kusini mwa Ukanda wa Gaza muda mfupi uliopita, jeshi la Israel linasema.

    Makombora matatu kati ya hayo yalinaswa na jeshi la anga la Israel huku moja likitua katika eneo la wazi, jeshi linaongeza.

    Hilo linawadia wakati Israel inaanza kumbukumbu za mashambulizi ya Oktoba 7 wakati watu wenye silaha wa Hamas walipovamia mpaka wa Gaza na kuingia Israel - takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

    Israel ilianza mashambulizi ya anga kwenye maeneo yaliyolenga Gaza kujibu shambulizi hilo, na baadaye kutuma wanajeshi katika eneo hilo.

    Watu kumi wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Hezbollah kaskazini mwa Israel

    Watu kumi wamejeruhiwa na makombora yaliyorushwa kutoka Lebanon katika miji ya kaskazini mwa Israel ya Haifa na Tiberias usiku kucha, kulingana na huduma ya ambulensi ya Israel.

    Majeruhi kadhaa walipata majeraha kutokana na vipande vya makombora, vioo na madirisha, huduma ya ambulensi inaongeza.

    Makombora hayo yalishambulia mgahawa, nyumba na barabara kuu, jeshi la Israel linasema, na kuongeza kuwa linachunguza jinsi makombora ya Hezbollah yalivyoweza kupenya katika mifumo ya ulinzi ya anga ya Israel.

    Hezbollah inasema ilikuwa ikilenga vituo vya kijeshi.

    Soma zaidi:

  12. Mwanajeshi wa Israel auawa kwenye mpaka wa Lebanon

    Jeshi la Israel linasema mwanajeshi mmoja ameuawa katika mapigano kwenye mpaka wa Lebanon na Israel, huku wanajeshi wawili wakijeruhiwa vibaya.

    Jeshi la Israel lilianza uvamizi wake wa ardhini dhidi ya kundi linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah nchini Lebanon Jumatatu iliyopita, kwa mapigano ya mara kwa mara ya kuvuka mpaka tangu wakati huo.

    IDF yashambulia hospitali ya Gaza ambako inasema kuna wanachama wa Hamas

    Wakati huo huo, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema limefanya shambulizi dhidi ya kundi la Hamas waliokuwa wakiendeleza shughuli zao ndani ya hospitali ya al-Aqsa huko Deir al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza.

    IDF inasema vituo hivi vya kamandi vilitumiwa na Hamas kupanga mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa IDF nchini Israel.

    Inasema ilichukua hatua za kuwalinda raia kabla ya shambulizi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya "sahihi ya silaha, uchunguzi wa angani, na taarifa za ziada za kijasusi".

    IDF inaongeza kuwa huu ni "mfano zaidi" wa Hamas wa "utumiaji mbaya wa miundombinu ya kiraia kinyume na sheria za kimataifa".

    Soma zaidi:

  13. Mlipuko waua Wachina wawili karibu na uwanja wa ndege wa Karachi, Pakistan

    Raia wawili wa China wameuawa na takriban watu kumi kujeruhiwa baada ya mlipuko kutokea karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jinnah mjini Karachi, Pakistan.

    Ubalozi wa China nchini Pakistan ulisema kulikuwa na "baadhi ya majeruhi wa eneo hilo" katika kile ulichokitaja kama "shambulio la kigaidi", ingawa jumla ya vifo bado haijulikani wazi.

    Ubalozi umeongeza kuwa mlipuko huo ulilenga msafara wa wahandisi wa China wanaofanya kazi katika mradi wa umeme katika mkoa wa Sindh nchini humo.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, kundi hilo la wanamgambo lilisema "lililenga msafara wa ngazi ya juu wa wahandisi na wawekezaji wa China" unaowasili kutoka uwanja wa ndege wa Karachi.

    Shambulio hilo lilitekelezwa kwa kutumia "kifaa cha vilipuzi kinachobebwa kwenye gari", Reuters ilinukuu BLA ikisema.

    Mlipuko ulitokea mwendo wa 23:00 saa za eneo. Ubalozi wa China ulisema kuwa wahandisi hao walikuwa sehemu ya kampuni inayofadhiliwa na China ya Port Qasim Power Generation Co Ltd, ambayo inalenga kujenga mitambo miwili ya kuzalisha umeme wa makaa ya mawe huko Port Qasim, karibu na Karachi.

    Kiwanda hicho ni sehemu ya ukanda wa uchumi wa China na Pakistan, ambao pia unafadhili miradi kadhaa ya miundombinu na nishati katika jimbo la Balochistan nchini Pakistan, ambalo lina utajiri mkubwa wa maliasili, ikiwa ni pamoja na gesi na madini.

    Jeshi la Balochistan (BLA), ambalo katika miaka ya hivi karibuni limefanya mashambulizi dhidi ya raia wa China wanaohusika na miradi, limedai kuhusika na shambulio hilo.

    Mara kwa mara kundi hilo limekuwa likilenga raia wa China katika eneo hilo, likidai wakaazi wa kabila la Baloch hawakuwa wakipata mgao wao wa mali inayotokana na wawekezaji wa kigeni.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Mwanaharakati wa upinzani wa Urusi aliuawa akipigania Ukraine

    Ildar Dadin, mwanaharakati mashuhuri wa upinzani wa Urusi ambaye alikuwa akipigana nchini Ukraine upande wa Kyiv, ameuawa akiwa vitani kwa mujibu wa kundi lililomsajili.

    Msemaji wa kundi hilo, Baraza la Kiraia, aliiambia BBC kwamba Dadin alifariki, na kuongeza kwamba "alikuwa, na anasalia kuwa shujaa".

    Mwanaharakati huyo aliyegeuka kuwa mpiganaji aliuawa wakati wanajeshi wa kikosi chake cha kujitolea, The Freedom of Russia Legion, walipokabiliwa na shambulio la mizinga ya Urusi katika eneo la Kharkiv kaskazini-mashariki mwa Ukraine.

    Kwa sasa, hakuna maelezo zaidi na Legion yenyewe haitatoa maoni wakati inasema operesheni ya kijeshi bado inaendelea.

    Lakini Ilia Ponamarev, mwanasiasa wa upinzani wa Urusi aliye uhamishoni na ambaye hapo awali alikuwa na uhusiano na Legion, ameiambia BBC kwamba "ana hakika" kwamba Dadin amefariki.

    Chanzo kingine kilifafanua kwamba hii "ilithibitishwa na wale waliokuwa pamoja naye vitani".

    Ujumbe wa hivi punde ambao nimetuma kwenye simu yake bado unaonyesha kuwa "haujasomwa".

    Ildar Dadin alijulikana nchini Urusi muongo mmoja uliopita kwa kuendelea kwake kufanya maandamano ya amani huku ukandamizaji wa kisiasa ukiongezeka.

    Alikuwa mtu wa kwanza kushtakiwa chini ya Kifungu kipya cha 212.1 – kilichopewa jina Sheria ya Dadin - ambayo mwaka wa 2014 ilifanya kuwa kosa la jinai kufanya ukiukaji wa kurudia wa sheria za Urusi zinazozidi kuwawekea vikwazo kwenye maandamano.

    Katika kesi yake, ilisemekana alisimama kwenye mitaa ya Moscow akiwa na mabango.

    Akiwa amehukumiwa miaka miwili na nusu, Dadin aliwekwa kwenye seli ya adhabu na mara moja akagoma kula. Walinzi wake wa gereza kisha wakamtesa ili kusitisha mgomo huo.

    Soma zaidi:

  15. 'Binti yangu aliyetekwa na Hamas amesahaulika' - Mama

    Mama wa mateka pekee raia wa Uingereza na Israel ambaye bado anashikiliwa na Hamas huko Gaza ameuliza kwa nini Uingereza "haipiganii kwa kila namna kuhakikisha kuachiliwa kwake".

    Emily Damari, 28, alipigwa risasi na kuchukuliwa kutoka eneo la kibbutz la Israel na kuvukishwa mpaka hadi Gaza mnamo 7 Oktoba.

    Akizungumza katika hafla ya kumbukumbu ya London kuashiria mashambulizi mwaka mmoja uliopita, mama yake Mandy Damari alisema "shida ya bintiye inaonekana kuwa imesahauliwa".

    Waziri Mkuu Sir Keir Starmer alisema katika taarifa kwamba Uingereza "bila shaka ni lazima isimame na jumuiya ya Wayahudi".

    Binti huyo mwenye uraia mara mbili ni miongoni mwa mateka 97 ambao bado hawajulikani waliko.

    Akiongea kwenye hafla ya ukumbusho ya Hyde Park, mama yake alisema: "[Emily] ni binti wa nchi zote mbili, lakini hakuna mtu anayetaja ukweli kwamba bado kuna mateka wa kike wa Uingereza anayeshikiliwa na Hamas kwa mwaka mmoja sasa. Na mimi wakati mwingine hushangaa kama watu wanajua kuna mwanamke wa Uingereza huko Gaza.

    "Fikiria, kama Emily angekuwa binti yako. Jaribu kuwazia anachopitia.

    "Tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana, amekuwa akishikiliwa na magaidi wa Hamas katika mahandaki ya Gaza, mita 20 au zaidi chini ya ardhi akiwa amefungiwa, kuteswa, kutengwa, kutoweza kula, kuzungumza au hata kusonga bila ruhusa ya mtu mwingine.”

    Soma zaidi:

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 07/10/2024