Urusi yamhukumu Mmarekani mwenye umri wa miaka 72 jela kwa kuwa mamluki
Mahakama ya Urusi imemhukumu raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 72 kifungo cha karibu miaka saba jela kwa madai ya kupigana kama mamluki wa Ukraine.
Waendesha mashtaka walisema Stephen James Hubbard alikuwa akihudumu katika kitengo cha ulinzi kilichoko katika mji wa mashariki wa Izyum alipokamatwa na vikosi vya Urusi mnamo Aprili 2022, muda mfupi baada ya Moscow kuzindua uvamizi wake kamili wa Ukraine.
Hubbard "alipokea fidia" kwa ushiriki wake katika vita kwa upande wa Ukraine, taarifa ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Urusi ilisema.
Sasa amehukumiwa kifungo cha miaka 6 na miezi 10 gerezani.
Hubbard, mzaliwa wa Michigan, alikiri mashtaka wiki iliyopita, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.
Hata hivyo, dada yake Patricia Fox aliiambia Reuters kwamba Hubbard alikuwa na maoni yanayoiunga mkono Urusi na hangeweza kuchukua silaha katika umri wake.
"Yeye si mwanajeshi," Bi Fox aliiambia Reuters, akiongeza kuwa kaka yake "hajawahi kuwa na bunduki, kumiliki bunduki, kufanya lolote kati ya hayo... Yeye ni mpiganaji wa amani."
Kulingana na Bi Fox, Hubbard alihamia Ukraine mwaka wa 2014 na aliishi huko kwa muda na mwanamke, ambaye alinusurika na malipo kidogo ya uzeeni.
Yeye na mpenzi wake baadaye walitengana lakini aliendelea kuishi Ukraine. Ingawa Hubbard alizuiliwa na vikosi vya Urusi mapema mwaka wa 2022, kesi yake ilitangazwa hadharani tu ilipoanza huko Moscow mnamo Septemba.