Iran yasema iko tayari kukabiliana na vikwazo vya Marekani, yajaribu kudhibiti kupanda kwa bei
Iran imesema iko tayari kukabiliana na zuio la Marekani la kijeshi baharini, ikidai kuwa usafirishaji wa bidhaa kupitia mipaka mingine umeongezeka. Hata hivyo, nchi hiyo inakabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei huku gharama za vyakula zikiongezeka.
Muhtasari
- Simu yaibiwa Bungeni Kenya! Mbunge amtaka Spika kumtaja anayedaiwa kuichukua!
- Wamexico watano wakamatwa Nigeria baada ya kukutwa na dawa za kulevya zenye thamani ya dola milioni 227
- Marekani yatangaza ushuru mpya kwa EU, China na nchi nyingine inazofanya nazo biashara
- Wanajeshi 11 wauawa katika shambulizi la Boko Haram nchini Niger
- Iran yasema iko tayari kukabiliana na vikwazo vya Marekani, yajaribu kudhibiti kupanda kwa bei
- IMF yaitahadharisha Tanzania kuhusu mpango wa BoT kununua dhahabu
- Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amewasili nchini Kenya kwa ziara ya siku mbili
- Mwigizaji mkongwe wa Nigeria Pete Edochie afariki dunia akiwa na umri wa miaka 79
- Wahouthi watangaza kuishambulia Ras Tanura, Saudi Arabia yashambulia Hodeidah
- Huawei yakutwa na hatia katika kesi ya inayohusiana na Marekani na Iran
- Mtaala mpya wa Tanzania watoa mfano wa mageuzi ya elimu Afrika
- Theluthi moja vijana hawajahi kufanya ngono ila wanatazama ponografia - Utafiti
- Wanajeshi wa Libya wauawa katika shambulizi la Ukraine bandari ya Benghazi
- Chombo cha Shenzhou-24 cha China charushwa angani na mwanaanga wa kwanza wa Pakistan
- CIA na taasisi ya ujasusi ya Marekani ODNI zadukuliwa
- Rais wa zamani wa Ufaransa na mkewe washtakiwa kwa kuifadhili Libya
- Tetesi za Soka: Arteta asema Arsenal inahitaji bahati zaidi ili kumaliza mechi zake kwa ushindi
- Bajeti ya kuendeleza vita dhidi ya Iran ipo - Trump
- Thomas Markle akabiliwa na mashtaka ya kumiliki picha za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto
- Takriban wanajeshi laki tano wa Urusi wameuawa vitani Ukraine
- Israel yaishutumu Iran kwa kutengeneza silaha za kemikali, yataka Marekani kuanzisha mashambulizi mapya
Moja kwa moja
Beldeen Waliaula & Faidha Ngaga
Simu yaibiwa Bungeni Kenya! Mbunge amtaka Spika kumtaja anayedaiwa kuichukua!

Chanzo cha picha, BUNGE LA KENYA
Sakata la simu iliyodaiwa kuchukuliwa ndani ya Bunge la Kenya limezua mjadala mpya baada ya Mbunge Mteule wa Jubilee, Sabina Chege, kujitokeza na kueleza kwa kina jinsi simu yake ilivyopotea wakati wa vurugu ndani ya Bunge Juni 8, 2023.
Akizungumza Bungeni Jumatano, Novemba 25, 2026, Sabina alisema simu yake aina ya iPhone 16, ambayo ilikuwa na takribani wiki moja tangu kuinunua, ilipotea wakati wabunge walipokuwa wakimkabili kuhusu jaribio la kumwondoa katika nafasi ya Naibu Kiranja wa Wachache (Deputy Minority Whip).
Kwa mujibu wa Sabina, wakati wa vurugu hizo alikuwa amezungukwa na wabunge wa upande mwingine wa Bunge, na anaamini simu yake ilichukuliwa wakati huo. Alisema pia alipata jeraha mkononi kutokana na purukushani hizo.
Sabina alisimulia kuwa aliwaomba waliokuwa karibu naye wamrejeshee simu hiyo, lakini maafisa wa usalama wa Bunge walimshauri kwanza kwenda hospitalini kupata matibabu.
Baadaye, akiwa katika Hospitali ya Nairobi, alijaribu kufuatilia simu hiyo kwa kutumia teknolojia ya kuitambua ilipo. Awali, ilionyesha kuwa ndani ya eneo la Bunge kabla ya kuhamia maeneo ya Protection House na baadaye Donholm jijini Nairobi.
Hata hivyo, licha ya kuripoti suala hilo kwa polisi wa Bunge, Karani wa Bunge na Kamati ya Haki za Wabunge, Sabina alisema hajawahi kuipata simu hiyo hadi leo.
LAKINI SASA AMPA SPIKA WETANG’ULA CHANGAMOTO!
Sabina amemtaka Spika Moses Wetang’ula kumtaja mbunge anayehusishwa na tukio hilo au kuhakikisha simu yake inarejeshwa kabla ya kumalizika kwa muhula wa sasa wa Bunge.
Kauli yake inakuja siku moja baada ya Wetang’ula kufichua kuwa CCTV za Bunge zilinasa mbunge mmoja akiweka simu ya mwenzake mfukoni wakati wa mvutano mkali ndani ya Bunge.
Spika alisema alimwita mbunge huyo ofisini kwake na kumwonyesha ushahidi wa video, lakini akakanusha kuichukua simu hiyo licha ya kujiona kwenye CCTV.
Hata hivyo, Wetang’ula hakumtaja mbunge huyo hadharani.
Wamexico watano wakamatwa Nigeria na dawa za kulevya zenye thamani ya dola milioni 227

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia watano wa Mexico na mfanyabiashara mmoja raia wa Nigeria wamekamatwa baada ya kugunduliwa kwa maabara kubwa ya kutengeneza dawa za kulevya aina ya methamphetamine kusini-mashariki mwa Nigeria.
Shirika la Nigeria la kupambana na dawa za kulevya limesema limekamata dawa hizo zenye thamani ya karibu dola milioni 227.
Zaidi ya tani moja na nusu ya methamphetamine, karibu tani saba za kemikali na vifaa vya viwandani vinavyotumika kutengeneza dawa za kulevya vimekamatwa katika misako iliyofanyika baada ya uchunguzi wa miezi saba uliohusisha nchi kadhaa.
Mamlaka za Nigeria zimesema raia hao wa Mexico walijaribu kuingia nchini humo kwa mara ya kwanza mwezi Agosti, lakini walizuiwa. Baadaye walirejea nchini humo kwa kutumia pasipoti za kughushi.
Hii ni maabara ya nne ya kiwango kikubwa ya kutengeneza methamphetamine iliyogunduliwa nchini Nigeria katika miezi ya hivi karibuni, ikiwa na madai ya kuhusishwa na magenge ya biashara ya dawa za kulevya ya Mexico.
Kumekuwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu mitandao ya uhalifu kuanzisha vituo vya kuzalisha dawa za kulevya katika Afrika Magharibi, kwa lengo la kuhudumia masoko ya ndani na masoko yenye faida kubwa ya nje ya nchi, hususan barani Ulaya na Asia.
Unaweza pia kusoma:
Marekani yatangaza ushuru mpya kwa EU, China na nchi nyingine inazofanya nazo biashara

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imetangaza ushuru mpya wa bidhaa zinazoingizwa kutoka kwa baadhi ya washirika wake wakubwa wa kibiashara.
Ushuru huo umewekwa kufuatia uchunguzi kuhusu uwezo mkubwa wa nchi hizo kuzalisha bidhaa pamoja na kiwango cha uzalishaji wa viwandani. Uchunguzi huo ulifanyika chini ya Kifungu cha 301 cha Sheria ya Biashara ya Marekani.
Nchi zilizofanyiwa uchunguzi ni pamoja na China, Umoja wa Ulaya, Singapore, Uswisi, Indonesia, Malaysia, Cambodia, Thailand, Korea Kusini, Vietnam, Taiwan, Bangladesh, Japan na India.
Viwango vya ushuru vitatofautiana kulingana na nchi husika pamoja na aina ya bidhaa inazozisafirisha kwenda Marekani.
China inakabiliwa na kiwango cha juu zaidi cha ushuru kinachoweza kufikia asilimia 40, ikifuatiwa na Vietnam ambayo inaweza kutozwa hadi asilimia 35. Baadhi ya nchi nyingine zitakabiliwa na ushuru wa asilimia 20 au 25.
Hata hivyo, baadhi ya viwango hivyo vya ushuru vitakuwa chini ya viwango vilivyotajwa, kutokana na makubaliano ya kupunguza ushuru ambayo Rais Donald Trump tayari amefikia na baadhi ya nchi hizo.
Unaweza pia kusoma:
Wanajeshi 11 wauawa katika shambulizi la Boko Haram nchini Niger

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema wanajeshi 11 wameuawa na wengine watano kujeruhiwa katika shambulizi lililolenga kikosi cha doria kusini-mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, shambulizi hilo lilitekelezwa na wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Boko Haram katika eneo la Baroua, mkoani Diffa, siku ya Jumanne.
Katika taarifa yake, wizara hiyo imesema idadi hiyo ni ya awali, huku wapiganaji 22 wa kundi hilo wakidaiwa kuuawa katika mapambano hayo.
“Idadi ya awali ya waliopoteza maisha ni kama ifuatavyo: upande wetu, mashujaa 11 wameuawa na watano wamejeruhiwa. Kwa upande wa adui, magaidi 22 wameangamizwa,” ilisema wizara hiyo.
Mkoa wa Diffa upo katika bonde la Ziwa Chad na unapakana na Niger, Nigeria, Cameroon na Chad. Eneo hilo limekuwa kitovu cha shughuli za makundi yenye misimamo mikali ya kutumia nguvu.
Mipaka isiyodhibitiwa ipasavyo, biashara haramu ya silaha na bidhaa za magendo, pamoja na mabadiliko ya hali ya usalama katika eneo hilo, vimechangia kulifanya kuwa uwanja muhimu wa mapambano ya kudhibiti maeneo.
Eneo la Baroua liliachwa na wakazi wake mwaka 2015 kufuatia mashambulizi ya makundi yenye misimamo mikali. Hata hivyo, takribani wakazi 6,000 walirejea mwaka 2021 katika juhudi za kuwarejesha watu waliokuwa wamekimbia makazi yao.
Wachambuzi wanasema mkoa wa Diffa umekuwa eneo muhimu kimkakati kwa makundi mbalimbali yenye silaha kutokana na jiografia yake, ikiwemo visiwa vyenye vinamasi na njia za maji zinazowapa wapiganaji maficho.
Makundi kadhaa yenye silaha, yakiwemo Islamic State West Africa Province (ISWAP), Boko Haram na JNIM, yamekuwa yakitekeleza mashambulizi nchini Niger na mataifa jirani.
Junta ya kijeshi inayoiongoza Niger tangu mwaka 2023 imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa katika kudhibiti uasi huo.
Unaweza pia kusoma:
Iran yasema iko tayari kukabiliana na vikwazo vya Marekani, yajaribu kudhibiti kupanda kwa bei

Chanzo cha picha, Getty Images
Makamu wa kwanza wa Rais wa Iran amesema Jumatano kuwa Tehran haina wasiwasi kuhusu zuio la Marekani la kijeshi baharini, akieleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la usafirishaji wa bidhaa kupitia mipaka mingine ya nchi hiyo. Amesema serikali pia inachukua hatua kudhibiti kupanda kwa bei.
Marekani ilirejesha zuio lake la kijeshi la baharini dhidi ya bandari za Iran mwezi Julai. Mapema mwezi huu, ilitangaza kuanzishwa kwa operesheni ya kijeshi iitwayo Task Force Iron Gate, inayolenga kuzuia usafirishaji wa silaha na bidhaa zilizowekewa vikwazo kupitia mipaka ya nchi kavu ya Iran na Bahari ya Caspian.
Iran inakabiliwa na moja ya vipindi vibaya zaidi vya kupanda kwa mfumuko wa bei katika miongo kadhaa, hali inayochochewa na vita vya Iran ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa takribani miezi tisa, huku bei za vyakula zikiongezeka kwa kasi zaidi.
“Ongezeko la upakuaji na uondoaji wa bidhaa bandarini kupitia mipaka isiyo ya kusini mwa nchi inatoa ujumbe kuwa hatuna wasiwasi kuhusu zuio la kijeshi la baharini linalowekwa na adui,” amesema Mohammad Reza Aref.
Ameongeza kuwa akiba ya bidhaa muhimu za kimkakati nchini humo iko katika hali nzuri na bidhaa zinapatikana kwa wingi, ingawa hakutaja takwimu zozote kuthibitisha kauli hiyo.
Aref amesema serikali inalenga kuzuia ongezeko la bei za bidhaa muhimu kwa kipindi cha angalau miezi mitatu ijayo.
Katika mkutano tofauti, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema serikali inatafuta namna ya kuelekeza sehemu kubwa zaidi ya rasilimali za bajeti na fedha zitakazookolewa kutokana na matumizi ya nishati katika kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo yenye kipato cha chini.
Kwa mujibu wa Kituo cha Takwimu cha Iran, bei za bidhaa na huduma kwa watumiaji mwezi Oktoba zilikuwa juu kwa asilimia 88.7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Wakati huohuo, wastani wa mfumuko wa bei kwa mwaka uliongezeka hadi asilimia 76.8, huku bei za vyakula na vinywaji zikishuhudia ongezeko la asilimia 112.6 ndani ya mwaka mmoja.
Unaweza pia kusoma:
IMF yaitahadharisha Tanzania kuhusu mpango wa BoT wa kununua dhahabu

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limetoa tahadhari kuwa mpango wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wa kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wa ndani unaweza kuiweka benki hiyo katika hatari ya kupata hasara kubwa iwapo bei ya madini hayo itashuka kwa kasi.
Katika tathmini yake ya uchumi wa Tanzania iliyotolewa Jumanne, Novemba 24, 2026, IMF pia imeeleza kuwa mpango huo unaweza kuongeza changamoto za kiutendaji kwa benki hiyo.
Kupitia mpango huo, BoT hununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wa ndani kwa kutumia fedha za Kitanzania. Lengo ni kuongeza akiba ya taifa ya dhahabu, kupunguza utegemezi wa Dola ya Marekani na kusaidia kuimarisha thamani ya Shilingi.
Hata hivyo, licha ya kutambua mchango wa mpango huo katika kuongeza akiba ya fedha za kigeni, IMF imesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari zaidi ili kupunguza uwezekano wa hasara.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na shirika hilo ni:
- BoT kufanya tathmini ya kina ya hasara zinazoweza kujitokeza kabla ya kuongeza ununuzi wa dhahabu.
- Kuweka wazi mara kwa mara taarifa kuhusu kiasi cha dhahabu kinachonunuliwa pamoja na gharama zinazotumika.
- Kuhamishia jukumu la ununuzi wa dhahabu katika taasisi huru, ili BoT ijikite katika majukumu yake ya msingi ya kusimamia sera ya fedha na kudhibiti mfumuko wa bei.
Wananchi wahoji kutotajwa kwa faida za mpango huo
Hata hivyo, taarifa hiyo imeibua maoni tofauti miongoni mwa wananchi, huku baadhi wakijiuliza kwa nini tahadhari kuhusu mpango huo zimejikita zaidi katika uwezekano wa kupata hasara bila kueleza kwa kina faida zinazoweza kupatikana kutokana na ununuzi wa dhahabu.
Unaweza pia kusoma:
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amewasili nchini Kenya kwa ziara ya siku mbili

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, amewasili nchini Kenya kwa ziara ya siku mbili inayotarajiwa kujikita katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara, uwekezaji na maendeleo ya ujuzi kati ya mataifa hayo mawili.
Steinmeier alipokelewa na Waziri Mkuu Msaidizi wa Kenya, Musalia Mudavadi, mara baada ya kuwasili nchini humo.
Katika ziara hiyo, Rais wa Ujerumani anatarajiwa kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Rais wa Kenya, William Ruto, kujadili masuala yenye maslahi kwa mataifa hayo mawili na kutafuta fursa za kupanua ushirikiano.
Kwa mujibu wa Mudavadi, ziara hiyo inatoa fursa kwa Kenya na Ujerumani kuimarisha zaidi ushirikiano wao wa muda mrefu katika sekta mbalimbali, zikiwemo biashara na uwekezaji, nishati safi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, elimu, teknolojia na maendeleo ya ujuzi.
Alibainisha kuwa kuimarisha uhusiano wa nchi hizo kunaweza kuvutia uwekezaji zaidi nchini Kenya, kuongeza fursa za ajira na mafunzo kwa vijana, pamoja na kuhamasisha ubadilishanaji wa maarifa na teknolojia.
Kenya na Ujerumani zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kwa muda mrefu, unaojengwa katika misingi ya ushirikiano na dhamira ya pamoja ya kuendeleza maendeleo endelevu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Unaweza pia kusoma:
Mwigizaji mkongwe wa Nigeria Pete Edochie afariki dunia akiwa na umri wa miaka 79

Chanzo cha picha, peteedochie/Instagram
Mwigizaji mkongwe wa Nigeria, Pete Edochie, ambaye ni miongoni mwa nyota wanaoheshimika zaidi katika tasnia ya filamu barani Afrika, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79, familia yake imetangaza.
Edochie alifahamika kwa sauti yake nzito, uwezo wake wa kuvutia watazamaji na matumizi yake ya methali za Kiafrika katika uigizaji. Alijijengea umaarufu mkubwa barani Afrika, akijulikana zaidi kwa kucheza nafasi za watawala wa jadi, wafanyabiashara matajiri na viongozi wa familia.
Katika taarifa yake, familia yake imesema Edochie alifariki mapema Jumatano katika mji wa Enugu, kusini mashariki mwa Nigeria, baada ya kuugua saratani ya tezi dume kwa muda mrefu.
Salamu za rambirambi zimeendelea kutolewa na mashabiki pamoja na waigizaji wenzake, waliomkumbuka kama gwiji wa Nollywood aliyechangia pakubwa kuijenga tasnia ya filamu nchini Nigeria.
Edochie alianza safari yake ya kazi kama mtangazaji wa redio mwaka 1967 kabla ya kuingia katika uigizaji.
Alipata umaarufu mkubwa mwaka 1987 baada ya kuigiza katika tamthilia ya televisheni iliyotokana na riwaya maarufu ya Chinua Achebe, Things Fall Apart.
Uigizaji wake wa mhusika Okonkwo, shujaa wa kabila la Igbo mwenye majivuno lakini aliyekuwa akikabiliwa na changamoto mbalimbali, ulimpatia umaarufu wa kimataifa na kumweka miongoni mwa waigizaji wanaoheshimika zaidi nchini Nigeria.
Baadaye, alikuja kuwa mmoja wa waigizaji waliotambulika zaidi katika Nollywood, tasnia ya filamu ya Nigeria ambayo imekua na kuwa miongoni mwa tasnia kubwa zaidi za filamu duniani.
Katika kipindi cha miongo kadhaa ya kazi yake, alishiriki katika filamu nyingi zikiwemo Igodo, Rituals, Billionaire's Club na vichekesho vya kimapenzi vya mwaka 2018 vilivyopewa jina la Lionheart.
Unaweza pia kusoma:
Wahouthi watangaza kuishambulia Ras Tanura, Saudi Arabia yashambulia Hodeidah

Chanzo cha picha, Saudi Press Agency
Kundi la waasi la Wahouthi, Ansar Allah, limetangaza Jumatano kuwa lilishambulia kiwanda cha kusafisha mafuta cha Ras Tanura katika mkoa wa Mashariki mwa Saudi Arabia, pamoja na kituo cha fedha katika Jiji la Kiuchumi la Abdullah, mjini Riyadh.
Kundi hilo limesema mashambulizi hayo ni kulipiza kisasi dhidi ya kile lilichokiita "uchokozi wa Saudi Arabia" dhidi ya mji mkuu wa Yemen, Sana'a na maeneo mengine nchini humo.
Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi, Yahya Saree, aliandika kupitia mtandao wa X kuwa shambulizi dhidi ya kiwanda hicho cha mafuta lilisababisha moto kuzuka.
Alisema pia mashambulizi dhidi ya kituo cha fedha katika mji mkuu wa Saudi Arabia yalitekelezwa kwa awamu tatu na kusababisha uharibifu mkubwa.
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia unaopambana na Wahouthi nchini Yemen ulitangaza kuwa umedungua na kuharibu ndege mbili zisizo na rubani katika mkoa wa Mashariki mwa nchi hiyo mapema Jumatano.
Baadaye, muungano huo ulisema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilidungua na kuharibu ndege nyingine nne zisizo na rubani katika eneo la Ras Tanura.
Muungano huo uliongeza kuwa vipande vya mabaki ya ndege hizo vilianguka ardhini kutokana na operesheni ya kuzidungua, lakini tathmini ya awali haikuonesha kuwepo kwa majeruhi.
Jengo refu zaidi katika mji mkuu wa Saudi Arabia lilishambuliwa kwa mara ya pili ndani ya siku chache siku ya Jumanne, ambapo watu 11 walijeruhiwa.
Muungano huo ulilielezea shambulizi hilo kuwa ni "kitendo cha kigaidi" na kuwalaumu Wahouthi kwa kulitekeleza.
Qatar na Pakistan zililaani shambulizi dhidi ya jengo hilo ambalo lina ofisi za makao makuu ya Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF).
Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya India ilisema raia wake wawili walijeruhiwa katika shambulizi hilo.
Wizara hiyo ilionya kuwa mashambulizi ya aina hiyo yanahatarisha maisha ya raia, yanakiuka mamlaka ya kujitawala ya Saudi Arabia na kudhoofisha usalama na utulivu wa eneo hilo.
Jengo hilo hilo lilishambuliwa Alhamisi iliyopita na ni miongoni mwa maeneo kadhaa muhimu yaliyolengwa katika mashambulizi ya anga tangu mapigano na kundi hilo linaloungwa mkono na Iran yalipoanza tena Julai mwaka huu.

Chanzo cha picha, NASA Worldview
Maelezo ya picha, Picha za satelaiti zaonesha moshi mkubwa ukifuka katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Ras Tanura nchini Saudi Arabia. Unaweza pia kusoma:
Huawei yakutwa na hatia katika kesi ya inayohusiana na Marekani na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Baraza la majaji mjini New York limeikuta kampuni ya China ya vifaa vya mawasiliano ya simu, Huawei, na hatia katika kesi kubwa ya jinai nchini Marekani.
Kampuni hiyo ilishtakiwa kwa kutoa taarifa za uongo kwa benki kuhusu shughuli zake za kibiashara nchini Iran, pamoja na kushirikiana kuiba siri za kibiashara kutoka kwa kampuni za Marekani.
Kesi hiyo ilianza mwaka 2018. Mwezi Desemba mwaka huo, afisa mkuu wa fedha wa Huawei, ambaye pia ni binti wa mwanzilishi wa kampuni hiyo, alikamatwa nchini Canada kwa hati ya kukamatwa iliyotolewa na Marekani. Kukamatwa kwake kulizua mgogoro wa kidiplomasia kati ya Marekani, China na Canada.
Mwaka uliofuata, serikali ya Marekani iliiweka Huawei katika orodha ya kampuni zilizopigwa marufuku kufanya biashara na makampuni ya Marekani kwa sababu za usalama wa taifa. Hatua hiyo iliizuia kampuni hiyo kupata teknolojia za Marekani.
Baraza la majaji katika mahakama ya shirikisho ya Brooklyn limeipata Huawei na hatia katika mashtaka 10 kati ya 12 ya jinai yaliyokuwa yakikabili kampuni hiyo.
Mashtaka hayo yanajumuisha ulaghai wa benki, ulaghai kupitia mifumo ya mawasiliano ya kielektroniki, kukiuka vikwazo vya kibiashara na kula njama ya kuiba siri za kibiashara.
Hata hivyo, majaji wameiondoa Huawei katika mashtaka ya kula njama ya kuzuia utekelezaji wa haki pamoja na kula njama ya kuunda mtandao wa uhalifu.
Unaweza pia kusoma:
Mtaala mpya wa Tanzania watoa mfano wa mageuzi ya elimu Afrika

Chanzo cha picha, Mastercard
Ripoti Mabadiliko yaliyofanywa katika mtaala wa elimu ya sekondari nchini Tanzania yameanza kuwasaidia wanafunzi kuhusisha maarifa wanayopata shuleni na fursa za kujipatia kipato katika siku zijazo, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Mastercard Foundation.
Ripoti hiyo inasema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo uzoefu wake katika kuboresha elimu ya sekondari unaweza kuwa somo kwa mataifa mengine ya Afrika yanayotafuta namna ya kuwaandaa vijana kwa mahitaji ya soko la ajira.
Ripoti hiyo yenye kichwa Secondary Education in Africa: Expanding Pathways to Work, Livelihoods, and Lifelong Learning ilizinduliwa Jumanne mjini Accra, Ghana, katika mkutano uliohudhuriwa na mawaziri wa elimu, taasisi za kikanda na za bara, watafiti, walimu na vijana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu kuanza kutekelezwa kwa mtaala ulioboreshwa mwaka 2023, Tanzania imeanzisha mbinu mpya za ufundishaji zinazomweka mwanafunzi katikati ya mchakato wa kujifunza. Mabadiliko hayo yanajumuisha ufundishaji unaotegemea miradi, elimu ya ujasiriamali, somo la Biashara na mifumo mipya ya upimaji wa wanafunzi.
Ripoti hiyo inasema baadhi ya wanafunzi na walimu wameripoti mabadiliko kutoka katika mfumo wa kukariri masomo kuelekea kwenye mijadala, kukuza fikra tunduizi na kujifunza kwa vitendo.
Somo la Biashara, ambalo limeingizwa katika mtaala wa elimu ya sekondari, limetajwa na wanafunzi kuwawezesha kuona uhusiano kati ya elimu wanayopata darasani na fursa za kuanzisha shughuli za ujasiriamali.
Mwalimu mmoja wa somo hilo mkoani Morogoro amewaambia watafiti kuwa mbinu za ufundishaji kwa vitendo zinawasaidia wanafunzi kuelewa dhana mbalimbali na kushiriki kikamilifu zaidi katika masomo.
Akizungumzia umuhimu wa elimu ya sekondari, Rais na Mtendaji Mkuu wa Mastercard Foundation, Sewit Ahderom, amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa kwa vijana wengi barani Afrika ndiyo fursa ya mwisho ya kupata elimu rasmi kwa kiwango kikubwa.
“Kwa vijana wa leo, hasa katika ngazi ya sekondari, elimu lazima iwe na mwelekeo na iwawezeshe kufikia mahali fulani. Kwa vijana wengi wa Afrika, shule ya sekondari ndiyo fursa ya mwisho kwa mfumo wa elimu kuwafikia kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha vijana wanapata ajira zenye staha na zinazowaridhisha. Tanzania ni miongoni mwa nchi saba zilizofanyiwa uchunguzi wa kina kupitia tafiti maalumu na mashauriano na vijana, pamoja na Ethiopia, Ghana, Malawi, Rwanda, Senegal na Sierra Leone.
Theluthi moja vijana hawajahi kufanya ngono ila wanatazama ponografia - Utafiti

Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti umebaini kuwa watu nchini Uingereza, hususan vijana walio balehe, na watu wazima ambao umri wao haujaenda sana, wanashiriki ngono kwa kiwango cha chini au hawafanyi kabisa ikilinganishwa na vizazi vilivyotangulia.
Hata hivyo, wengi wao wanatazama ponografia na kutumiana picha za kingono kupitia simu.
Hii ni mara ya kwanza kwa utafiti wa kitaifa kuhusu mitazamo na mienendo ya kingono iitwayo National Survey of Sexual Attitudes and Lifestyles, kuchunguza tabia za watu zinazohusiana na ngono kupitia mitandao ya intaneti.
Utafiti huo umebaini kuwa nusu ya watu wenye umri wa miaka 16 hadi 24 wametuma au kupokea picha za kingono kupitia simu zao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Aidha, mwanamke mmoja kati ya wawili na takriban wanaume tisa kati ya 10 katika kundi hilo la umri wanasema wamewahi kutazama ponografia.
Hata hivyo, theluthi moja ya watu katika kundi hilo la umri hawajawahi kufanya ngono, ikilinganishwa na asilimia 20 katika utafiti uliofanyika miaka 12 iliyopita.
Utafiti huo pia umebaini kuwa watu wazima walio chini ya umri wa miaka 45 wanafanya ngono kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Kwa wastani, wanafanya ngono mara mbili kwa mwezi, ikilinganishwa na mara moja kwa wiki mwaka 1990.
Soma pia:
Wanajeshi wa Libya wauawa katika shambulizi la Ukraine bandari ya Benghazi

Chanzo cha picha, Reuters
Libya imesema kuwa wanajeshi wake wawili, waliuawa katika shambulizi la ndege isiyo na rubani la Ukraine dhidi ya meli ya Urusi katika bandari ya Benghazi siku ya Jumapili.
Takriban watu 10 pia walijeruhiwa katika shambulizi hilo.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, alilitaja shambulizi hilo kuwa la "mfano wa kuigwa", licha ya kufanyika umbali wa kilomita 2,400 kutoka eneo la mapigano nchini Ukraine.
Operesheni hiyo inasemekana haikulenga tu kuharibu meli nyingine ya kivita ya Urusi bali kuonyesha uwezo wa Ukraine kushambulia mali za kijeshi za wanamaji wa Urusi katika maeneo yaliyo mbali zaidi na Bahari Nyeusi.
Shambulizi hilo limekashifiwa vikali na maafisa wa Libya na ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo.
Soma pia:
Chombo cha Shenzhou-24 cha China charushwa angani na mwanaanga wa kwanza wa Pakistan

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanaanga kutoka Pakistan, Zeeshan Ali, anatarajiwa kuwa raia wa kwanza wa kigeni kupanda kituo cha anga za juu cha Tiangong cha China, hatua inayoweka historia katika azma ya Pakistan kuendeleza sayansi na juhudi za Beijing kupanua ushirikiano wake wa kidiplomasia kupitia sekta ya anga za juu.
Chombo cha anga za juu cha Shenzhou-24 kilitia nanga katika kituo cha Tiangong saa saa tisa alfajiri hii leo, takriban saa tatu na nusu baada ya kurushwa kutoka kituo cha kurushia vyombo vya anga cha Jiuquan, kaskazini-magharibi mwa China, kwa kutumia roketi ya Long March-2F.
Rubani huyo mwenye umri wa miaka 40, ambaye amekuwa raia wa kwanza wa Pakistan kwenda kwenye obiti ya dunia, atafanya kazi ya kusimamia vifaa na majaribio ya kisayansi na anatarajiwa kukaa katika kituo hicho kwa siku tano hadi 10.
Ameandamana na kamanda wa chombo hicho cha China, Tang Hongbo, pamoja na mhandisi wa safari za anga, Wu Yi.
Katika kujiandaa kwa safari hiyo, Ali alifanya mafunzo kwa muda wa miezi saba mjini Beijing. Katika kipindi hicho, alipata mafunzo ya kina ya lugha ya Kichina, alijifunza nyimbo za Kichina na kusoma mashairi ya lugha hiyo. Pia alijifunza sanaa ya uandishi wa Kichina na kucheza mchezo wa tenisi ya mezani.
"Sisafiri kwa ajili yangu mwenyewe. Nimebeba jina la Pakistan begani mwangu," Ali aliwaambia waandishi wa habari hapo jana.
Soma pia:
CIA na taasisi ya ujasusi ya Marekani ODNI zadukuliwa

Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa (ODNI) zimebaini kuwa mifumo yao ya usalama wa mtandao ilikuwa imedukuliwa, na kusababisha baadhi ya taarifa zao zisizo za siri kuvuja.
Udukuzi huo uliathiri mtandao unaotumika kutafuta na kuchambua taarifa za kijasusi kutoka kwenye vyanzo vya wazi na visivyo vya siri, kulingana na gazeti la New York Times, ambalo lilikuwa la kwanza kuripoti kuhusu tukio hilo.
Hata hivyo, haijabainika wazi ni taarifa zipi hasa zisizo za siri zilizofichuliwa. Gazeti hilo pia lilisema kuwa taarifa katika taasisi nyingine za serikali ya Marekani zimeathirika kutokana na udukuzi huo.
Ilipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa (ODNI) ilisema kuwa hakukuwa na hitilafu katika uwezo wa kiutendaji wala mifumo yake inayohifadhi taarifa za siri.
Tukio hilo ni la hivi karibuni katika mfululizo wa hitilafu za kiteknolojia na matukio ya ukiukaji wa usalama wa mtandao nchini Marekani, yakiwemo mashambulizi ya mtandao yaliyoripotiwa katika Wizara ya Kilimo ya Marekani.
Awali, matukio mawili tofauti ya udukuzi pia yaliripotiwa katika Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), huku Wizara ya Ulinzi (Pentagon) na Wizara ya Usalama wa Ndani pia zikikumbwa na matukio ya mashambulizi ya mtandaoni
Soma pia:
Rais wa zamani wa Ufaransa na mkewe washtakiwa kwa kuifadhili Libya

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, na mkewe Carla Bruni-Sarkozy Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, na mkewe Carla Bruni-Sarkozy, watafikishwa mahakamani mwaka ujao, ili kujibu tuhuma za kutoa ufadhili wa kifedha kinyume cha sheria kufadhili kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2007 ya aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.
Sarkozy na mkewe Bruni wamekanusha madai hayo.
Mwezi Septemba 2025, Sarkozy alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela katika kesi hiyo hiyo, na kuwa rais wa kwanza wa zamani wa Ufaransa kufungwa gerezani.
Hata hivyo, alikaa gerezani kwa siku 20 pekee kabla ya kuachiliwa.
Uamuzi kuhusu rufaa yake pia unatarajiwa kutolewa wiki ijayo.
Soma pia:
Tetesi za Soka: Arteta asema Arsenal inahitaji bahati zaidi ili kumaliza mechi zake kwa ushindi

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika wiki za hivi karibuni Arsenal imekuwa ikishindwa kumaliza mechi kwa ushindi hata pale inapokuwa na udhibiti wa mchezo huo.
Katika mechi zake tisa zilizopita katika mashindano yote, ni mara moja pekee ambapo The Gunners wamefanikiwa kushinda kwa tofauti ya zaidi ya bao moja.
Changamoto hiyo imejitokeza tena hapo jana baada ya Arsenal kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Borussia Dortmund.
Licha ya kutawala na kudhibiti sehemu kubwa ya michezo yao, Arsenal imekuwa na vipindi ambavyo kiwango chake cha kucheza hushuka na kuruhusu wapinzani wao kuwatawala
Katika mechi ya ugenini dhidi ya Slavia Prague kwenye Ligi ya Mabingwa, baada ya kufunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza, kiwango cha Arsenal kilishuka.
Hali kama hiyo ilijitokeza pia katika mechi dhidi ya Newcastle kwenye Ligi Kuu ya England mwishoni mwa wiki iliyopita. Arsenal iliongoza wakati wa mapumziko, lakini ikajikuta ikifungwa mabao 2-1 katika kipindi cha pili kabla ya kupata sare ya mabao 2-2.
Baada ya kukamilika kwa mechi ya Borussia Dortmund ,Kocha Mikel Arteta aligusia kushindwa kwa timu yake kutumia vyema nafasi ilizopata, ingawa alisifu kiwango kizuri cha wachezaji wake.
Arteta alisema, "Kuna kipengele cha bahati, lakini pia kuna umuhimu wa sisi kumalizia vyema zaidi katika nafasi tunazopata. Tunapaswa kuendelea kujitahidi kwa sababu naamini kile ambacho timu imeonesha leo ni mwelekeo sahihi."
Bajeti ya kuendeleza vita dhidi ya Iran ipo - Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump, amesema kuwa bajeti ya kuendesha vita dhidi ya Iran inajitosheleza hadi mwisho wa Januari 2027.
Katika mahojiano na gazeti la New York Post, Trump alisema kuwa wanachama wa Democrat katika bunge la Congress,wanaweza kugeuza ‘ushindi’ wao kuwa ‘kushindwa’ iwapo watajaribu kusitisha vita dhidi ya Iran.
Trump aliongezea kuwa wameliharibu jeshi la wanamaji la Iran Pamoja na mifumo yake ya ulinzi wa anga.
"Tunaweza kumaliza vita hivi wakati wowote tunapotaka,"alisema Trump.
Wiki iliyopita, Seneti ya Marekani ilipinga mswada uliolenga kuweka mipaka kwa mamlaka ya Trump ya kuendeleza vita dhidi ya Iran.
Mswada huo ungehitaji Rais wa Marekani ama kusitisha vita dhidi ya Iran au kupata idhini ya Congress ili kuendelea na operesheni za kijeshi.
Soma pia:
Thomas Markle akabiliwa na mashtaka ya kumiliki picha za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto

Chanzo cha picha, Pinellas County Sheriff's Office
Thomas Markle, babake Meghan Markle, amefunguliwa mashtaka na baraza kuu la mahakama mjini Los Angeles, Marekani, kwa tuhuma za kumiliki picha na video za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.
Markle, ambaye bado anazuiliwa katika jimbo la Florida, anadaiwa kumiliki kanda hizo zilizojumuisha angalau picha moja ya mtoto ambaye hajafikia umri wa kubaleghe na mwingine mwenye umri wa chini ya miaka 12, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizowasilishwa California.
Markle mwenye umri wa miaka 82 amekanusha kumiliki picha za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani mjini Los Angeles katika wiki zijazo ili kujibu mashtaka hayo.
Wiki iliyopita, mahakama ya Florida ilitangaza kuwa baba mkwe wa Prince Harry ana uwezo wa kiakili wa kuelewa mashtaka yanayomkabili na kushiriki katika kesi yake.
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilimkamata Markle tarehe 6 Novemba, katika makazi ya wazee katika jimbo la Florida.
Wakili wa serikali ya Marekani, Bill Essayli, alisema kuwa iwapo atapatikana na hatia, Markle anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela kwa kila shtaka.
