Mambo 6 yanayopigiwa chapuo kwa Tanzania kuipiku Kenya na nchi nyingine kiuchumi

Chanzo cha picha, BOT
- Author, Beatrice Kimaro
- Nafasi, Mchambuzi
Kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), pato la Taifa la Tanzania limeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni $85.42 (Shilingi 200 trilioni za Tanzania) kwa mwaka huu wa 2023.
Hiyo inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi sita Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi. Imeshazipiku nchi kama Ghana na Ivory Coast zilizokua juu yake.
IMF inasema kufikia mwaka 2028 uchumi wa taifa hilo la Afrika Mashariki utazidi kukua na utafikia dola $136 billioni (Shilingi 318.8 trilioni za Tanzania) na pato la mtu mmoja mmoja litakua hadi kufikia dola 1,860 (Shilingi 4.3milioni) kutoka dola $1,350 za sasa (Sawa na 3.15milioni za Tanzania).
Kwa tathimini ya ripoti hiyo na kwa makadirio yaliyopo, si muda mrefu Tanzania huenda ikaipiku Kenya kiuchumi, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiongoza Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa IMF uchumi wa Kenya kwa mwaka 2023 umefikia dola $118.1billioni.
Wachumi wanabashiri pia Tanzania itaziacha kwa mbali pia nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na nchi zingine za ukanda huu. Huku ikizifukuzia kwa karibu nchi zinazofanya vizuri za Kusini mwa janga la Sahara kama Ethiopia, Afrika Kusini na Nigeria yenye uchumi mkubwa Afrika unaofikia dola $506.6 billioni.
Nini siri ya mafanikio ya Tanzania kiuchumi?
Kwa muongo mmoja uliopita, Tanzania kasi ya ukuaji wa kiuchumi wa nchi hiyo umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka. Pamoja na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 na vita vya Ukraine, uchumi wa nchi hiyo umepaa kutoka dola $69.9 bilioni mpaka dola $85.42 bilioni.
Siri kubwa katika mafanikio haya kwa muda mfupi huu moja kubwa ni uwekezaji mkubwa kwenye biashara unaosukumwa na Rais Samia Suluhu.
Amepokea wawekezaji wengi toka nje, ameruhusu uwekezaji mkubwa na mdogo, ameingiza matrilioni ya pesa toka nje kwa njia ya misaada na mikopo. Pesa zinazosaidia kuongeza mzunguko na kuchagiza shughuli za kiuchumi.
‘Usisahau wakati wa Corona, Tanzania iliendelea na shughuli za uzalishaji, haikufunga shughuli zake, huu ndio wakati ambao Tanzania iliziacha nchi nyingi za Afrika kiuchumi’, anasema Hasina Masaninga mtaalam wa maendeleo ya uchumi wa Jamii kutoka Tanzania.
Mambo 6 yatakayofanya Tanzania kuipiku Kenya na nchi zingine kiuchumi

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
Ripoti ya IMF inagusa makadirio katika kipindi cha miaka 10 kati ya mwaka 2018 mpaka 2028, kipindi ambacho kwa tathimini ya kiuchumi imeibeba zaidi Tanzania kuliko Kenya na nchi zingine zenye rasilimali nyingi kama DRC, Ivory Coast, Uganda na Ghana.
Haitashangaza kuiona ikiipiku Kenya katika kipindi hicho cha miaka 10. Haitashangaza kuona pia ikiipiku Angola yenye uchumi unaofikia dola $117.8 bilioni au hata Ethiopia yenye uchumi wa dola $156 bilioni.
IMF imezingatia masuala kadhaa ambayo pia uchambuzi wa kiuchumi unayabainisha kama mambo muhimu ambayo yanaipa Tanzania nafasi kubwa ya kuipiku Kenya kiuchumi inayoongoza Afrika Mashariki na ikitarajiwa pia kuipiku nchi kama Angola inayoshika nafasi ya Tano Afrika, kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.
1: Uwekezaji na Sekta binafsi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika kipindi cha miaka 2 iliyopita Tanzania imejenga mahusiano muhimu ya kidiplomasia na mataifa ya kigeni kuruhusu wageni na biashara za kigeni kufanyika zaidi na kwa njia nyepesi. Uwekezaji umeomgezeka na ameithaminisha sekta binafsi.
Hili halikuonekana kati ya mwaka 2010 na 2021 wakati wa utawala wa Rais John Magufuli ambaye hakuwahi kufanya ziara yeyote ya nje ya bara la Afrika kwa miaka zaidi ya mitano ya utawala wake.
Samia alikwenda Ufaransa, nchi yenye pato la taifa linalokadiriwa kuwa ya dola za Kimarekani $2.6 Trilioni na kusaini mikataba 6 muhimu ukiwemo wa Euro 178 milioni za kuendeleza mradi wa ujenzi wa barabara za mwendokasi (BRT), akaenda Ubelgiji na akaenda Marekani kukutana na makamu wa rais Kamala Harris ambaye aliitembelea pia Tanzania na kuhaidi msaada wa dola milioni 560 mwaka 2024.
Ukiacha IMF yenyewe, Benki ya dunia imeitengea Tanzania dola za kimarekani bilioni 2.1 kati ya 2022- 2025.
‘Tanzania inapoingiza kwenye mzunguko wake wa fedha nyingi za kigeni kama hizi hasa za msaada ama mikopo yenye masharti nafuu, ni kuchochea uchumi, ni kuchagiza uchumi,na hilo linafanyika sana katika utawala wa sasa’, anasema Masaninga.
2: Bandari

Chanzo cha picha, Tanzania Ports Authority
Bandari hii mojawapo ya lango la kuu la kibiashara, ambapo asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania inahudumiwa na Bandari hii. Inauwezo wa kuhudumia tani za metriki milioni 14 za shehena kavu na tani milioni 6.0 za vimiminika. Ukweli bandari hii ni silaha muhimu ya uchumi kwa Tanzania.
Ukiacha bandari ya mpya ya Bagamoyo iliyo katika hatua ya ujenzi, bandari ya Tanga na Mtwara, bandari yake ya Dar es Salaam inafaida kubwa ya kijiografia, inayotegemewa na nchi karibu 6 za Afrika.
Kwa ripoti za hivi karibuni usafirishaji wa mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa 21% wakati bandari ya Mombasa, Kenya umeshuka kwa 6.2%. Uganda ambaye ni moja ya nchi zinazotumia sana bandari ya Mombasa, wafanyabiashara wake wengi wameanza kutumia bandari ya Dar es Salaam. Maboresho ya bandari hii itaendelea kuitishia ile ya Kenya kwenye mchango wake kiuchumi.
3: Madini adimu na ya kimkakati

Chanzo cha picha, Wizara ya Madini Tanzania
Wiki hii, Tanzania imesaini mikataba na kampuni tatu za ubia kutoka Australia kwa ajili uwekezaji kwenye uchimbaji wa madini adimu kwenye mikoa ya Morogoro, Lindi na Songwe, mkataba wenye thamani ya dola za kimarekani 667 milioni kufuatia utafiti ulioanza miaka zaidi ya 20 iliyopita.
‘Nimearifiwa kutokana na utafiti huo hadi sasa kuna tani milioni 67 zenye wastani wa asilimia 5.4 ya madini ya Kinywe yaliyogundulika katika kijiji cha Chilalo ambayo yatachimbwa kwa miaka 18.
‘Hili ni eneo lingine ambalo Tanzania itakwenda kufanya vizuri na kimapato kuliko Kenya’, anasema Dokta Barnos Willium, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi.
Mchango wa Sekta ya madini nchini Tanzania kwa sasa kwenye pato la taifa ni 9.7% nchi hiyo ikilenga kuliongeza mpaka 10% ifikapo 2025.
4: Gesi asilia, Bwawa la Nyerere na Reli ya kisasa (SGR)

Chanzo cha picha, Michuzi Blog
Achilia mbali uwepo wa gesi wenye ujazo wa futi zafi ya trilioni 60, Kitakachoibeba Tanzania katika miaka 10ijayo ni reli ya kisasa inayojengwa kwa awamu kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza na kigoma. hiyo kuunganishwa na bandari ya Dar es Salaam inayohudumia nchi jirani zisizo na bandari kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.
‘Kama unataka kufanikiwa kiuchumi ni kuwa na miundo mbinu thabiti inayounganisha kila sehemu, hasa sehemu za uchumi chochezi, hili litaipaisha Tanzania zaidi kibiashara na cnhi jirani’, Mchumi Willium.
Mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) ambalo litakuwa moja ya mabwawa makubwa duniani, litazalisha megawati 2,115 za umeme, ambao mbali na kusaidia viwanda na kuuzwa nje, pia utatumiwa kuendeshea mitambo ya SGR.
5: Kilimo cha Mashamba makubwa ya Pamoja
Machi 20, 2023 Rais wa Tanzania Samia Suluhu alizindua kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja (Block Farming) chini ya mpango wa Building a Better Tomorrow Youth Initiative for Agribusiness Program (BBT-YIA).
Mpango huu wa miaka 8 utakuza sekta ya kilimo mpaka asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.
‘Huwezi kuwekeza dola $148mil kwenye mpango usio na mchango kwa uchumi, Kenya wanafanya lakini nimeuona mpango huu utaleta mapinduzi makubwa kwa namna ulivyoandaliwa’, anasema Masaninga
6: Amani na Utulivu
Masuala yote matano niliyoyataja, lakini hili la amani na Utulivu ni la kipekee kabisa na kinaitofautisha Tanzania na nchi zingine shindani kiuchumi hasa Kenya.
Kwa sasa Kenya inapitia kipindi kingine cha wasiwasi kiuchumi hasa baada ya kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kuitisha maandamano nchi nzima pamoja na mambo mengine wanataka serikali ishughulikie suala la ugumu wa maisha.
Kawaida ghasia za maandamano zinazuia shughuli nyingi za kiuchumi. Unaonekana kuwapo kwa mvutano mkubwa wa kisiasa kati ya Serikali ya William Ruto na upinzani nchini Kenya. Kama wapinzani wataendelea na maandamano itafifisha uchumi wa taifa hilo ambalo mara kwa mara limekuwa likikumbwa na ghasia za uchaguzi ama za baada ya uchaguzi.
Je ni 'Mashindano ya vibushuti'
Wapo wenye mtazamo tofauti kuhusu uwezo wa Tanzania kuipiku Kenya kiuchumi kama makadirio ya IMF yanavyoonyesha.
Wanaweza kuwa na majibu, lakini lililo wazi ni kujidhatiti kwa taifa la Kenya kwenye eneo la miundo mbinu, ukuaji wa biashara za nje, uzalishaji wa mazao na bidhaa ambazo zina soko kubwa Tanzania, Uganda na nchi zingine za duniani.
Taarifa za Benki kuu ya Kenya zinaonyesha mauzo ya nje yaliongezeka hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 1.09 katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2022 kutoka dola milioni 865 katika kipindi kama hicho Mwaka 2021, kati ya mauzo hayo, dola milioni 226 yalikuwa mauzo kwenda nchini Tanzania.
Tanzania ni mnunuzi mkubwa wa bidhaa za Kenya kama sabuni, mafuta ya kupikia, vifaa vya umeme na dawa.
Pengine Tanzania ijizalishie yenyewe bidhaa za aina hii, ili kuzuia kuwa soko la Kenya ambalo linaiongezea mapato muhimu kiuchumi taifa hilo.
Haya ni 'Mashindano ya vibushuti', ni kauli ya mmoja ya wafuatiliaji wakubwa wa masuala ya uchumi, siasa na maendeleo Afrika Mashariki, Mohamed Warsame kupitia mtandao wake wa twitter.
Warsame kama walivyo baadhi ya wakosoaji wengine wanaoona Tanzania kuipiku Kenya au Kenya kuipiku Tanzania ni sawa na kushindanisha watu wote wafupi na kuuliza nani mfupi zaidi, au mrefu kuliko mfupi mwenzie. Maana isiyo rasmi ni kwamba zote ni nchi dhoofu kiuchumi.
Na mfano anaosimama nao kutetea hoja yake ni kufananisha uchumi wa New Zeeland yenye watu 5.1milioni ambao ni dola $250bilioni wakati nchi zote za Jumuia ya Afrika Mashariki zenye watu 312milioni uchumi wake ni dola $333bilioni.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Ripoti ya IMF inasemaje kwa muelekeo wa uchumi wa dunia?
Ingawa tumeitazama Tanzania kwa mizania ya Kenya na nchi zingine za Karibu. Ripoti ya mwaka huu ya IMF inaonyesha kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia utasalia kuwa wastani wa asilimia 3% katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Ingawa unatazamiwa kutereka kutoka 3.4% mwaka 2022 hadi 2.8 mwaka 2023 lakini utapanda tena mwaka 2024 hadi kufikia 3%.
Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Niger inatarajiwa kufanya vizuri zaidi kiuchumi, kwa kasi ya ukuaji wake ikitarajiwa kupanda hadi 13% mwakani 2024 kutoka 10.1% mwaka 2022, Senegal utapanda mpaka 10.6% mwakani kutoka 4.7 mwaka 2022.
Moja ya nchi zitakazokuwa na hali mbaya zaidi kiuchumi, pato lake likitetereka Equatorial Guinea. Kasi ya ukuaji wa uchumi kwa taifa hili la magharibi inatarajiwa kushuka mpaka (-.8.2%) mwaka 2024 kutoka 1.6% mwaka jana, ingawa mwaka huu pia imeshuka mpaka (-1.8%).
Nchi nyingi zimekumbwa na mdodoro kwa sababu ya vita vya Ukraine na ugonjwa wa Covid-19. Lakini zilizosalia kuzalisha kipindi cha Covid 19 na zile zilizo na sera himilivu za kifedha hasa wakati wa kuathirika na viwango vya kubadilishia dola zimeonekana kuendelea kufanya vyema ikiwemo Tanzania.












