Jinsi benki kuu ya Ghana ilivyopoteza $5bn kwa mwaka mmoja

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Thomas Naadi
- Nafasi, BBC News, Accra
Ghana - ambayo wakati mmoja ilijivunia kuwa mafanikio ya kiuchumi barani Afrika - inakabiliwa na mzozo wa kifedha ambao haujawahi kutokea.
Wiki hii, mamia ya waandamanaji waliingia barabarani katika mji mkuu wa Accra, wakitoa wito kwa gavana wa Benki kuu ya Ghana na manaibu wake wawili kujiuzulu kutokana na hasara ya takriban cedis bilioni 60 za Ghana sawa na dola bilioni 5.2 katika mwaka wa fedha wa 2022.
Maandamano hayo yaliyopewa jina la #OccupyBoG, yaliongozwa na chama cha upinzani cha National Democratic Congress (NDC). Waandamanaji, wakiwa wamevalia mashati mekundu, jitambaa na kofia, waliimba nyimbo na kuinua mabango - yaliyoandikwa "komesha uporaji, tunateseka".
Upinzani unadai benki hiyo ilichapisha pesa kinyume cha sheria ili kuikopesha serikali, na kusababisha kushuka kwa thamani ya sarafu hiyo na kulemaza mfumuko wa bei.
Pia umeikosoa benki hiyo kwa kutumia zaidi ya dola 762,000 kwa usafiri wa ndani na nje, ongezeko la 87% kwa mwaka uliopita, na $250m katika jengo jipya la ofisi. Upinzani unasema takwimu hizi zimerekodiwa katika ukaguzi wa ndani.
NDC imemshutumu gavana wa benki kuu, Dkt Ernest Addison, kwa uzembe na usimamizi mbaya. Na wakati benki hiyo imeshutumiwa kwa usimamizi mbaya siku za nyuma, hasara ya ukubwa huu haijawahi kutokea.

Chanzo cha picha, Reuters
"Hatujawahi kuona kitu kama hiki katika historia yetu. Ikiwa Benki Kuu ya Ghana inataka kupata ahueni kutokana na hasara hii... itawachukua zaidi ya miaka 45," anasema mwanauchumi Profesa Godfred Bokpin, kutoka Chuo Kikuu cha Ghana.
Benki hiyo inakanusha mashtaka ya usimamizi mbaya na inasema hasara hiyo ilitokana na kushuka kwa kiwango cha ubadilishaji na kwa sababu ya kutolipwa kwa mikopo na taasisi za serikali.
Pia inasema uamuzi wa serikali wa kukopa dola milioni 700 kutoka kwake na kutolipa kikamilifu umechangia mzozo huo.
Waimamizi wa benki hiyo pia wameshutumiwa kwa kuendeleza mfumuko wa bei na matatizo ya kiuchumi kutokana na hatua zao. "Wakati walipokuwa wakichapisha mabilioni kwa serikali, hawakujua kuwa itakuwa na athari?" anauliza wakili Martin Kepbu
Kwa nini hii imetokea?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ghana kwa sasa inakabiliwa mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kutokea katika historia yake. Mwaka jana, mfumuko wa bei ulifikia 54% kiwango cha juu zaidi kurekodiwa- na bado unaendelea kwa zaidi ya 40%. Mashirika mengi ya kukadiria mikopo yamelishusha hadhi taifa, na kulizuia kukopa pesa kimataifa.
Kufikia Septemba 2022, jumla ya deni la Ghana lilikuwa limepanda hadi dola bilioni 55. Hii ilimaanisha kuwa serikali ilihitaji zaidi ya asilimia 70 ya mapato yake kulipia deni hilo, jambo ambalo haikuweza kufanya. Baadaye ilishindwa kulipa sehemu kubwa ya malipo yake ya deni.
Serikali ililazimika kuwasiliana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa usaidizi. Ili kupata dhamana ya $3bn mapema mwaka huu, serikali ilibidi kukubali kutimiza masharti kadhaa.
La muhimu zaidi kati ya haya lilikuwa kupunguza malipo ya riba ya deni la taifa hadi kiwango kinachoweza kudhibitiwa ifikapo 2028. Hili lingewaacha na fedha za kutosha kuendesha uchumi.
Ili kufanikisha hili, serikali ya Ghana ilianza urekebishaji wa deni kwa kujadiliana upya masharti na wakopeshaji wake, na kupendekeza viwango vya chini vya riba kwa mikopo yao na kurefusha muda wa kulipa ili kupunguza shinikizo kwa fedha za umma.
Hata hivyo, baadhi ya wakopeshaji walikataa kushiriki katika mpango huu wa kubadilishana madeni.
Tarehe 9 Agosti Benki Kuu ya Ghana ilitoa taarifa ikisema serikali ilikuwa imeiambia kuwa haina pesa za kutosha kukidhi matakwa ya IMF na hivyo basi haitalipa nusu ya $700m ilizokopa kutoka kwake.
Badala yake pesa zingeenda kwenye urekebishaji wa deni. Pia ilisema haitalipa riba yoyote kutokana na benki hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Benki hiyo ndiyo inayotoa mikopo ya mwisho na wataalamu wanasema hadhi yake imetumiwa vibaya na serikali inayoongozwa na Rais Nana Akufo-Addo na sheria za benki hiyo zimevunjwa.
"Sheria ya Benki Kuu ya Ghana iko wazi kabisa kwamba uchapishaji wa pesa au kufadhili serikali ni mdogo kwa 5% ya mapato ya mwaka uliopita, ambayo ina maana kwamba kimsingi kusaidia serikali sio uhalifu lakini usizidi 5%," Anasema Profesa Bokpin.
Maafisa wa benki hiyo wameagizwa kisheria kuripoti bungeni ikiwa kiwango cha 5% kimepitwa. Kukiuka agizo hilo kunaweza kusababisha faini au kifungo kisichozidi miaka miwili.
Athari kwa benki
Hii haimaanishi kuwa Benki Kuu ya Ghana imefilisika. Sio benki ya biashara ambayo inapaswa kupata faida, kwa hivyo hasara haipaswi kuathiri shughuli zake za kawaida na kama mkopeshaji wa hatua ya mwisho inaweza kuunda pesa zake.
Lakini kulingana na wataalam, hasara ya benki kuu ina athari kubwa.
Inadhoofisha mamlaka ya kimaadili ya benki kusimamia benki za biashara za Ghana. Pia inaathiri imani katika mfumo wa fedha wa nchi.
Ingawa benki kuu nyingine duniani kote zimekabiliwa na changamoto kama hizo, tofauti ya Ghana ni kiasi cha pesa kilichopotea ikilinganishwa na ukubwa wa uchumi.
Nchini Uingereza, Benki ya Uingereza itakuwa ikifanya hasara ya takriban $180bn katika kipindi cha miaka 10 ijayo ambayo itafadhiliwa na serikali ya Uingereza. Lakini ukubwa wa uchumi wa Uingereza ni wa matrilioni ya dola.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ripoti ya Benki ya Dunia mwezi uliopita ilikadiria kuwa Waghana 850,000 wameingia kwenye umaskini kwa sababu ya mfumuko mkubwa wa bei.
Mapato ya Waghana yamedorora, na kuathiri uwezo wao wa kununua. Bei za vyakula, mafuta na huduma zinaendelea kuwa kupanda, na familia nyingi zinatatizika kujikimu kimaisha.
Na licha ya hayo yote benki kuu sasa iko chini ya uangalizi kutoka ndani ya nchi na IMF.
Chini ya masharti ya mkopo wa IMF, ikiwa serikali itaomba msaada zaidi, benki hiyo haitakuwa na budi ila kukataa.












