Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, M23, jeshi la Rwanda walifanya mauaji na ubakaji DR Congo - Human Rights Watch

Shirika hilo limesema makumi ya raia waliuawa katika kipindi cha mwezi mmoja ambapo waasi wa M23 walidhibiti mji wa Uvira, mashariki mwa DR Congo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Asha Juma

  1. Israel na Lebanon wakutana kwa duru ya tatu ya mazungumzo ya kusitisha vita

    Wajumbe kutoka Serikali ya Israel na Lebanon wameanza duru ya tatu ya mazungumzo mjini Washington, Marekani, siku chache kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano kukamilika.

    Israel imeendelea kufanya mashambulizi hasa kusini mwa Lebanon licha ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi uliopita ikisema inazilenga ngome za wanamgambo wa kundi la Hezbollah.

    Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran halishiriki katika mazungumzo hayo na limepinga mchakato huo.

    Israel inataka Hezbolah kuweka chini silaha huku serikali ya Lebanon ikiitaka Israel kukomesha mapigano yote nchini humo.

    Mamia ya watu wameuawa kusini mwa Lebanon katika kipindi cha mwezi mmoja.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Wes Streeting ajiuzulu kama waziri wa afya Uingereza

    Waziri wa afya wa Uingereza Wes Streeting amejiuzulu kutoka Serikali ya Waziri Mkuu Keir Starmer.

    Bwana Streeting amesema hana imani na uongozi wa Sir Starmer kama Waziri Mkuu na kuongeza kuwa ni bayana kuwa Bwana Starmer hatakiongoza chama cha Labour kuelekea Uchaguzi Mkuu.

    Bwana Streeting anatarajiwa kutangaza nia ya kuwania uwaziri mkuu dhidi ya Starmer.

    Washirika wake wameiambia BBC kuwa ana kiwango cha uungwaji mkono kutoka kwa wabunge wa chama tawala kutia nia ya kuwa kiongozi ajaye.

    Keir Starmer amewaonya mawaziri wake kuwa mabadiliko ya uongozi yatalitumbukiza taifa hilo katika vurugu.

  3. Mashambulizi mapya yatokea kwenye meli karibu na Hormuz

    Rais wa Marekani Donald Trump alijadili vita vya Iran na Rais wa China Xi Jinping huko Beijing siku ya Alhamisi, huku mashambulizi mapya dhidi ya meli karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz yakikumbusha gharama zilizotokana na mkwamo wa muda mrefu, huku mazungumzo ya amani yakikwama.

    Baada ya Trump na Xi kukutana, afisa wa Ikulu ya White House alisema viongozi hao walikuwa wamekubaliana kwamba mlango-bahari huo unapaswa kuwa wazi, na kwamba Iran haipaswi kamwe kupata silaha za nyuklia.

    China iko karibu na Iran na mnunuzi mkuu wa mafuta yake.

    Katika mahojiano na CNBC huko Beijing, Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema anaamini China "itafanya wawezavyo" kusaidia kufungua mlango-bahari huo, ambao alisema "unawanufaisha sana".

    Diplomasia kwa ajili ya kukomesha vita imesitishwa tangu wiki iliyopita wakati Iran na Marekani kila mmoja ilipokataa mapendekezo ya mwingine ya hivi karibuni, zikishikilia madai ya awali ambayo kila moja inayaona kuwa "tahadhari"

    Iran imefunga kwa kiasi kikubwa Mlango-Bahari wa Hormuz kwa meli za nchi zingine tangu Marekani na Israeli zilipoanzisha vita miezi miwili na nusu iliyopita, na kusababisha usumbufu mkubwa zaidi kuwahi kutokea kwa usambazaji wa nishati duniani.

    Katika tukio la hivi punde katika njia ya biashara, meli ya mizigo ya India iliyokuwa imebeba mifugo kutoka Afrika kwenda Umoja wa Falme za Kiarabu ilizama siku ya Alhamisi katika maji ya pwani ya Oman.

    Soma zaidi:

  4. Mkutano wa Mawaziri wa Nje wa BRICS waanza nchini India

    Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa ya BRICS ikiwa ni pamoja na Iran na Urusi, walikutana mjini New Delhi siku ya Alhamisi, ambapo India ilionya juu ya "mabadiliko makubwa" na migogoro inayosababisha kutokuwa na uhakika wa kiuchumi na ukosefu wa usalama wa nishati.

    Vita nchini Iran na mzozo wa mafuta vimetawala mijadala katika mkutano huo wa siku mbili.

    India, ambayo ni mwenyekiti wa kundi la mataifa la BRICS mwaka huu, ilikuwa mwenyeji wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka kundi hilo lililopanuliwa ambalo kwa sasa linajumuisha Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, nchi ambazo hazielewani kuhusu mzozo ulioanzishwa na Marekani na Israel Februari 28.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa India Subrahmanyam Jaishankar alisema, katika hotuba yake ya ufunguzi, kwamba mkutano unafanyika wakati wa mabadiliko ya haraka na yasiyotabirika.

    "Tunakutana wakati wa mabadiliko makubwa katika mahusiano ya kimataifa, migogoro inayoendelea, kutokuwa na uhakika wa kiuchumi, na changamoto katika biashara, teknolojia, na hali ya hewa kimataifa," alisema Jaishankar.

    Miongoni mwa mawaziri wa mambo ya nje waliohudhuria ni pamoja na Abbas Araghchi wa Iran na Sergei Lavrov wa Urusi.

    Jaishankar alisema msukosuko katika njia za meli za Ghuba na Mlango Bahari wa Hormuz unaendelea kufanya hali kuwa tete katika soko la mafuta na gesi, na kuongeza shinikizo kwa uchumi unaoagiza nishati, ikiwa ni pamoja na India.

    BRICS iliundwa mwaka wa 2009 kama kongamano la mataifa makubwa yanayoibukia kiuchumi yanayotafuta ushawishi mkubwa katika taasisi zinazotawaliwa na mataifa yenye nguvu za Magharibi.

    Kundi hilo mwanzoni ilikuwa na Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini limepanuka, huku wanachama wakijaribu kuongeza ushawishi wa kisiasa na kiuchumi wa umoja huo kimataifa.

    Sasa inajumuisha Misri, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia, Indonesia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

  5. M23, jeshi la Rwanda walifanya mauaji na ubakaji DR Congo - Human Rights Watch

    Shirika la kutetea haki za binadamu ( Human Rights Watch), limebaini kuwa kundi la waasi la M23 na Jeshi la Rwanda walitekeleza mauaji makubwa ya raia, unyanyasaji wa kingono na utekaji nyara katika kipindi ambacho walikalia mji wa Uvira, mashariki mwa Congo mwishoni mwa mwaka 2025 na mapema 2026.

    Shirika hilo limesema makumi ya raia waliuawa katika kipindi cha mwezi mmoja ambapo waasi wa M23 walidhibiti eneo hilo.

    Uchunguzi huo unajumuisha simulizi kutoka kwa manusura wanaosema walishuhudia ukatili uliofanywa na wanajeshi wa Rwanda waliovalia sare. Rwanda imekuwa ikikanusha kila mara kwamba wanajeshi wake wako nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

    Maelfu ya watu walitoroka mji wakati M23 ilipochukua udhibiti wa eneo hilo.

    Uchunguzi wa Human Rights Watch unaangazia kile ambacho baadhi ya wale waliobaki walisema kilitokea baadaye.

    Ripoti ya kundi hilo inajumuisha simulizi za mauaji ya kinyama, ukatili wa kingono, utekaji nyara na watu kutojulikana walipo.

    Wachunguzi walipata ushahidi wa makaburi matatu ya halaiki na walisema raia 53 waliuawa, miongoni mwao watoto sita.

    Rwanda inakanusha madai ya kuisaidia kundi la waasi wa M23 na inasema kuwa wanajeshi wake hawajavuka mpaka kuingia katika nchi jirani.

    Lakini ripoti hii inajumuisha simulizi kutoka kwa mashahidi wanaosema waliona maafisa waliovalia sare wakifanya uhalifu dhidi ya raia.

    M23 ilidhibiti eneo la Uvira kwa mwezi mmoja kabla ya kuondoka kutokana na shinikizo la kidiplomasia kutoka kwa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani ambayo ilisaidia kufanikisha makubaliano ya amani.

    Licha ya makubaliano hayo, waasi bado wanaendelea kudhibiti maeneo makubwa na mapigano yanaendelea.

    Kundi la waasi wa M23 na serikali ya Rwanda hawakujibu maombi ya BBC kuhusiana na suala hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Waziri wa zamani wa Nigeria ahukumiwa kifungo cha miaka 75 jela

    Mahakama nchini Nigeria imemhukumu aliyekuwa Waziri wa Nishati, Saleh Mamman, kifungo cha miaka 75 jela baada ya kupatikana na hatia ya kutakatisha fedha kiasi cha naira bilioni 33.8 sawa na dola milioni 24.7 za Marekani.

    Uamuzi huo ulitolewa Jumatano katika mji mkuu wa Abuja baada ya mahakama kumtia hatiani mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 68 bila yeye kuwepo mahakamani.

    Mapema mwezi huu, Saleh Mamman alipatikana na hatia kwa makosa 12 yanayohusiana na udanganyifu na utakatishaji fedha katika kesi iliyowasilishwa na shirika la kupambana na ufisadi nchini Nigeria, la Economic and Financial Crimes Commission (EFCC).

    Mahakama iliamuru vifungo hivyo vya gerezani kutumikia kwa mfululizo. Pia ilimtaka Mamman kurejesha naira bilioni 22 zinazohusishwa na miradi ya umeme ya Mambilla na Zungeru, ambayo alikuwa akiisimamia alipokuwa madarakani.

    Wiki chache kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Mamman alikuwa amechukua fomu za kuwania uteuzi wa uchaguzi wa ugavana katika jimbo la Taraba kupitia chama tawala cha All Progressives Congress kabla ya uchaguzi wa mwaka 2027.

    Hajulikani alipo kwa sasa na hajatoa tamko lolote hadharani kuhusu hukumu hiyo.

    Mamman aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Nishati chini ya rais wa zamani wa Nigeria, Muhammadu Buhari, ambaye serikali yake iliingia madarakani kwa ahadi ya kupambana na ufisadi.

    Hukumu hiyo imewashangaza Raia wengi wa Nigeria, kwani kutiwa hatiani kwa maafisa wakuu wa serikali kwa makosa ya ufisadi bado ni jambo lisilo la kawaida nchini humo.

    Kesi hiyo ni sehemu ya kampeni pana ya EFCC dhidi ya maafisa wa zamani wa serikali wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

    Uchunguzi mwingine mkubwa umehusisha aliyekuwa Waziri wa Sheria, Abubakar Malami, pamoja na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kibinadamu, Sadiya Umar Farouq, ambaye hivi karibuni alitangazwa kusakwa na shirika hilo.

    Hukumu hiyo pia imefufua hasira za wananchi kuhusu mgogoro wa muda mrefu wa umeme nchini Nigeria — hasa ikizingatiwa kuwa Mamman aliwahi kuahidi kuwa wizara yake ingeboresha usambazaji wa umeme kwa wananchi.

    Licha ya kuwa mmoja ya wazalishaji wakubwa wa nishati barani Afrika, Nigeria bado inakabiliwa na uhaba mkubwa wa umeme, huku kukatika kwa umeme mara kwa mara kukiathiri biashara kote nchini.

    Familia nyingi pamoja na kampuni hutegemea jenereta zinazotumia mafuta ili kupata umeme, huku kupanda kwa bei ya mafuta kukiwaacha mamilioni ya watu wakihangaika kumudu gharama za vyanzo mbadala vya nishati.

  7. Urusi yaanzisha mashambulizi makubwa nchini Ukraine

    Maafisa wamesema watu watano wameuawa, akiwemo msichana wa miaka 12, baada ya Urusi kuanzisha wimbi kubwa la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya Ukraine usiku kucha.

    Polisi walisema watatu kati ya waliokufa walitolewa kutoka kwenye kifusi cha jengo la ghorofa lililoharibiwa kwa kiasi fulani huko Kyiv, ambapo operesheni ya uokoaji inaendelea kwa karibu watu 10 wanaohofiwa kutoweka baada ya mji mkuu kushambuliwa kwa bomu.

    Meya wa jiji hilo alisema makumi ya wengine wamejeruhiwa katika shambulio hilo kubwa, wakiwemo watoto wawili. Watu ishirini na mmoja wanatibiwa hospitalini.

    Hii ni siku ya tatu mfululizo Ukraine kuripoti vifo, huku Urusi ikiongeza mashambulizi yake baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya siku tatu kuisha siku ya Jumatatu.

    Rais Volodomyr Zelensky alisema shambulio hilo la usiku kucha lilishuhudia zaidi ya ndege zisizo na rubani 670 na makombora 56 yakilenga nchi hiyo.

    Hili ni miongoni mwa mashambulizi makubwa zaidi ambayo Urusi imeyafanya tangu kuanza kwa uvamizi wake mwaka wa 2022.

    Zelensky aliongeza kuwa mashambulizi hayo yaliathiri zaidi ya maeneo 180 kote Ukraine, na kusababisha uharibifu wa majengo zaidi ya 50 ya makazi.

    "Lazima kuwe na jibu la haki kwa mashambulizi haya yote," alisema, akitoa wito kwa washirika kuiwajibisha Urusi na kutekelezwa kwa vikwazo vya kimataifa.

    Huko Kyiv, operesheni ya utafutaji na uokoaji ilianza mapema Alhamisi ili kutafuta watu chini ya vifusi vya jengo la ghorofa tisa refu, ambalo lilikuwa limeshambuliwa usiku kucha.

    Soma zaidi:

  8. Madonna, Shakira na kundi la K-pop kuongoza onyesho la Kombe la Dunia wakati wa mapumziko

    Madonna, Shakira na bendi ya wavulana ya K-pop BTS wataongoza onyesho la wakati wa mapumziko katika fainali ya Kombe la Dunia ya msimu huu wa joto.

    Mashindano hayo, ambayo yataandaliwa kwa ushirikiano na Marekani, Canada na Mexico, yanamalizika kwa fainali jijini New Jersey tarehe 19 Julai.

    BBC inafahamu kuwa kipindi hicho kitakuwa cha dakika 11.

    Maonyesho ya kabla ya mechi katika hafla za maonyesho kama vile fainali ya Ligi ya Mabingwa yamekuwa ya kawaida, lakini hii itakuwa onyesho la kwanza la wakati wa mapumziko katika fainali ya Kombe la Dunia.

    Nyota wa pop kutoka Colombia Shakira atatoa wimbo wake rasmi wa Kombe la Dunia Dai Dai - msemo wa Kiitaliano unaomaanisha "twende" au "njooni" na pia atamshirikisha mwimbaji wa Nigeria Burna Boy - siku ya Alhamisi.

    Mwimbaji huyo wa Hips Don't Lie mwenye umri wa miaka 49 pia alitoa wimbo wa Waka Waka (This Time for Africa) kwa ajili ya mashindano ya mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

    'Malkia wa Pop' Madonna ndiye msanii wa muziki wa kike ambaye amekuwa na mauzo mazuri wakati wote na anajiandaa kutoa albamu yake ya 15, Confessions II, tarehe 3 Julai.

    Wakati huo huo, wanachama saba wa BTS ndio kundi la wanamuziki walioweka rekodi katika historia ya Korea Kusini, huku zaidi ya albamu milioni 45 zikiuzwa.

    Mnamo Machi, rais wa Fifa Gianni Infantino alisema onyesho hilo "litaweka historia katika mashindano ya Kombe la Dunia la Fifa, na kuwa tukio kubwa zaidi katika michezo duniani".

    Onyesho hilo la wakati wa mapumziko limeandaliwa na Chris Martin wa kundi la muziki la Coldplay na litachangisha pesa kwa ajili ya Mfuko wa Elimu ya Raia Duniani wa Fifa, mpango unaolenga kuchangisha dola milioni 100 (£73m) kwa ajili ya watoto duniani kote.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Marekani yatoa visa za kuingia nchini bila malipo

    Marekani imetangaza kuwa mashabiki watakaonunua tiketi za Kombe la Dunia 2026 hawatalazimika kulipa dhamana ya dola 15,000 ili kupata visa ya kuingia Marekani.

    Mwaka jana, raia wa takriban mataifa 50 walitakiwa na utawala wa Rais Donald Trump kuweka dhamana ya dola 15,000 kabla ya kuomba visa ya kuingia Marekani, kwa mujibu wa afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

    Mashabiki kutoka mataifa hayo sasa wataruhusiwa kuingia bila kulipa dhamana hiyo, mradi wawe na tiketi halali za mechi za Kombe la Dunia.

    Miongoni mwa mataifa hayo, Algeria, Cape Verde, Ivory Coast, Senegal na Tunisia tayari yamefuzu kwa mashindano hayo yatakayofanyika kwa ushirikiano kati ya Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11.

    Wachezaji na makocha walioshiriki mashindano hayo tayari walikuwa wameondolewa kwenye masharti ya dhamana hiyo.

    Mpango huo wa majaribio wa miezi 12 ulianza Agosti mwaka jana ukiwa sehemu ya sera pana ya udhibiti wa uhamiaji ya utawala wa Trump.

    Mpango huo mpya wa dhamana ya visa, unaowataka wageni kulipa dola 15,000 kupata visa za biashara au utalii aina ya B1 na B2, unatarajiwa kuanza kutekelezwa Aprili 2. Maafisa wa Marekani wanasema hatua hiyo inalenga kuzuia wageni kukaa nchini humo baada ya muda wa visa zao kuisha.

  10. Mlolongo wa ushuru kati ya Marekani na China

    Viwango vya ushuru kati ya Marekani na China vimekuwa vikibadilika na kuwa changamano zaidi kwa miaka mingi, kutokana na mabadiliko ya sera na hatua zinazofuatana tangu muhula wa kwanza wa Donald Trump. Hali ilivyo hadi sasa ni kama ifuatavyo:

    2018 Rais Donald Trump alitangaza ushuru mpya kwa bidhaa kutoka China kwa lengo la kurejesha ajira za viwanda nchini Marekani na kuhakikisha biashara ya haki. Ushuru wa Marekani kwa bidhaa za China ulisalia karibu asilimia 20 na uliendelea hivyo hadi kipindi cha utawala wa Joe Biden.

    Aprili 2025 Trump, akiwa amechaguliwa tena kuwa rais, alitangaza kile alichokiita “Liberation Day tariffs”. Alitishia ushuru kwa karibu washirika wote wa biashara wa Marekani na kuongeza ushuru wa bidhaa za China hadi karibu asilimia 50. China ilijibu kwa hatua za kulipiza, na kuanzisha vita vya biashara vilivyopandisha viwango vya ushuru hadi zaidi ya asilimia 100 kwa pande zote.

    Mei 2025 Maafisa wa Marekani na China walifanya mazungumzo ya kupunguza mvutano. Ushuru wa bidhaa za China ulipunguzwa kutoka asilimia 145 hadi 30, huku ushuru wa China kwa bidhaa za Marekani ukishuka kutoka asilimia 125 hadi 10.

    Oktoba 2025 Trump na Xi Jinping Xi Jinping walikutana moja kwa moja kujadili mvutano wa kibiashara. Marekani iliweka vizuizi vya uuzaji wa semikondakta kwenda China, hatua iliyosababisha Beijing kuongeza udhibiti wa usafirishaji wa madini muhimu adimu. Baadaye, China ilisitisha vizuizi vya usafirishaji wa madini hayo na kukubali kununua bidhaa za kilimo kutoka Marekani, huku Washington ikiondoa sehemu ya ushuru uliowekwa kutokana na fentanyl.

    2026 Mahakama Kuu ya Marekani ilibatilisha ushuru wa “Liberation Day” wa Trump. Ikulu ya Marekani ilitangaza hatua ya muda ya ushuru kwa bidhaa zote za kimataifa zinazoingia Marekani chini ya sheria nyingine, hatua iliyofanya kiwango cha jumla cha ushuru kwa bidhaa za China kushuka hadi karibu asilimia 10.

  11. Ni wakurugenzi wakuu gani walio sehemu ya ujumbe wa Marekani nchini China?

    Ujumbe wa Rais wa Marekani kuelekea Beijing ulijumuisha viongozi wakuu wa kampuni kubwa wanaoendesha biashara zilizo katika maeneo nyeti ya mvutano wa kiuchumi kati ya Marekani na China, ikiwemo magari ya umeme na teknolojia.

    Ikulu ya Marekani ilitoa orodha kamili ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo:

    • Tim Cook (Apple)
    • Stephen Schwarzman (Blackstone)
    • Kelly Ortberg (Boeing)
    • Brian Sikes (Cargill)
    • Jane Fraser (Citigroup)
    • Henry Lawrence Culp (GE Aerospace)
    • David Solomon (Goldman Sachs)
    • Jacob Thaysen (Illumina)
    • Michael Miebach (Mastercard)
    • Sanjay Mehrotra (Micron Technology)
    • Jensen Huang (Nvidia)
    • Cristiano Amon (Qualcomm)
    • Elon Musk (SpaceX na Tesla)
    • Ryan McInerney (Visa)

    Viongozi wengine wa kampuni mbalimbali wanatarajiwa kujiunga na ujumbe huo baadaye mchana wa leo.

    Trump atakuwa China kwa ziara rasmi hadi Ijumaa, kikao kikielezwa kitabadilisha uhusiano wa nchi hizo mbili ambazo zimekuwa mahasimu hivi karibuni.

  12. Man City yailaza Crystal Palace na kuweka shinikizo kwa Arsenal

    Manchester City wameibuka na ushindi wa uhakika dhidi ya Crystal Palace na kupunguza pengo hadi pointi mbili nyuma ya vinara wa ligi ya mabingwa Ulaya Arsenal, na hivyo kuendeleza ushindani mkali wa ubingwa kuelekea wiki ya mwisho ya msimu.

    Pep Guardiola alifanya mabadiliko sita kwenye kikosi chake, akiwapumzisha mastaa akiwemo Erling Haaland, Rayan Cherki na Jeremy Doku, akilenga mchezo wa fainali ya FA Cup dhidi ya Chelsea.

    Mabadiliko hayo yaliifanya City kuanza kwa taratibu, lakini Phil Foden aliibadilisha kabisa kasi ya mchezo kwa ubunifu wake.

    Foden alitoa pasi ya kisigino iliyomuweka Antoine Semenyo ana kwa ana na lango, na Mghana huyo akafungua ukurasa wa mabao kwa ustadi mkubwa.

    Baadaye Omar Marmoush aliongeza la pili kwa City kwa kumalizia kwa ustadi baada ya pasi ya Foden.

    Tyrick Mitchell aliishia kugonga shuti kali lililookolewa na Gianluigi Donnarumma, likiwa nafasi bora ya Palace, kabla ya Savinho kufunga la tatu na kukamilisha ushindi huo wa kishindo.

    Soma zaidi:

  13. Mama aliyemuua mumewe kwa sumu ahukumiwa kifungo cha maisha

    Mama mmoja kutoka jimbo la Utah nchini Marekani ambaye aliandika kitabu cha watoto kuhusu huzuni baada ya kifo cha ghafla cha mumewe, amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani bila nafasi ya kuachiliwa huru baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mume wake.

    Majaji wa mahakama mwezi Machi walihitimisha kuwa Kouri Richins alimuua mumewe mwaka 2022 kwa kumpa kinywaji kilichochanganywa na dawa ya fentanyl.

    Waendesha mashtaka walisema Richins mwenye umri wa miaka 36 alikuwa na madeni ya mamilioni ya dola, alikuwa amechukua bima za maisha kwa jina la mumewe, na pia alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa.

    Akitoa hukumu Jumatano, siku ambayo marehemu Eric Richins angefikisha miaka 44, Jaji Richard Mrazi alisema:

    “Mtu aliyepatikana na hatia ya makosa haya ni hatari mno kuachiwa huru tena.”

    Mama huyo wa watoto watatu, ambaye hakutoa ushahidi wakati wa kesi yake, alizungumza kwa takriban dakika 30 mahakamani, akielekeza maneno yake zaidi kwa watoto wake.

    “Ninaelewa kuwa leo hamtaki kuzungumza nami na mnanichukia. Hilo ni sawa. Mtakapokuwa tayari, nitakuwa hapa kwa ajili yenu,” alisema.

    Richins pia alipatikana na hatia ya kudanganya ili kupata fedha za bima baada ya kifo cha mumewe nyumbani kwao karibu na mji wa mapumziko wa Park City.

    Waendesha mashtaka walisema aliamini angeurithi utajiri wa mumewe uliokadiriwa kuwa zaidi ya dola milioni nne baada ya kifo chake.

    Mahakama pia ilielezwa kuwa Richins alikuwa akipanga maisha ya baadaye na mwanaume mwingine aliyekuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi.

    Aidha, alipatikana na hatia ya kujaribu kumuua mumewe katika tukio la awali ambapo alidaiwa kuweka sumu kwenye mkate wa nyama aliokuwa akiula.

    Richins alikamatwa Machi 2023, miezi miwili baada ya kuchapisha kitabu cha picha cha watoto kiitwacho Are You With Me?, ambacho alisema kililenga kuwasaidia watu, akiwemo watoto wake watatu, kukabiliana na huzuni ya kumpoteza mpendwa wao.

    Katika mahojiano aliyowahi kufanya na kituo cha redio cha KPCW kabla ya kukamatwa kwake, alisema alikuwa na matumaini kuwa kitabu hicho kingewafariji familia zinazopitia maumivu ya kumpoteza mtu wa karibu.

    Pia alimuelezea marehemu mumewe kama “mume mzuri na baba bora.”

    Soma zaidi:

  14. Xi atoa wito China na Marekani kuwa 'washirika badala ya wapinzani'

    Rais wa China Xi Jinping ametoa wito kwa nchi yake na Marekani kushirikiana kama washirika badala ya kuwa wapinzani, akisisitiza haja ya utulivu katika uhusiano wa mataifa hayo mawili yenye ushawishi mkubwa duniani.

    Akizungumza katika hotuba ya ufunguzi, Xi amesema dunia nzima inafuatilia mazungumzo yao, akibainisha kuwa mabadiliko makubwa ya kimataifa yasiyo ya kawaida yanaendelea kwa kasi na hali ya kimataifa iko katika mzunguko wa mabadiliko na misukosuko.

    Aliongeza kuwa dunia imefika katika njia panda mpya, akihoji iwapo China na Marekani zinaweza kuepuka kile kinachoitwa “mtego wa Thucydides” na badala yake kuanzisha mfumo mpya wa mahusiano unaoweza kuleta utulivu wa kimataifa.

    Xi amehoji pia iwapo mataifa hayo mawili yanaweza kushirikiana kukabiliana na changamoto za dunia na kujenga mustakabali bora wa mahusiano yao kwa maslahi ya watu wao na binadamu kwa ujumla.

    Pia amewapongeza Marekani na Rais Donald Trump kwa kuadhimisha miaka 250 ya uhuru, akisema nchi hizo mbili zina maslahi mengi yanayofanana kuliko tofauti.

    Amesisitiza kuwa mafanikio ya upande mmoja yanaweza kuwa fursa kwa mwingine, na kwamba uhusiano thabiti kati ya China na Marekani ni muhimu kwa utulivu wa dunia.

    “China na Marekani zinanufaika na ushirikiano na hupoteza kupitia migogoro,” amesema, akihitimisha kwa wito wa mataifa hayo kuwa washirika na kusaidiana kufanikiwa katika enzi mpya ya mahusiano ya kimataifa.

    Soma zaidi:

  15. Mazungumzo ya Trump na Xi yaanza rasmi Beijing huku ishara za ukaribu zikionekana

    Ingawa tayari Donald Trump amewasili nchini China, shughuli kuu za ziara yake zimepangwa kufanyika Alhamisi na Ijumaa.

    Hapa ni baadhi ya ratiba muhimu wakati wa ziara hiyo:

    Alhamisi

    Rais wa China Xi Jinping atampokea Rais Trump katika Ukumbi Mkuu wa Watu mjini Beijing.

    Viongozi hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi ya pande mbili.

    Pia kutakuwa na karamu ya chakula cha jioni baadaye usiku.

    Ijumaa

    Kutakuwa na picha ya pamoja na kupeana mkono kati ya Rais Xi na Rais Trump katika bustani ya Zhongnanhai mjini Beijing, ambayo ni makao makuu ya Chama cha Kikomunisti cha China.

    Kualika viongozi wa kigeni katika eneo hilo mara nyingi huchukuliwa kuwa ishara ya ukaribu wa kidiplomasia.

    Baadaye, Trump na Xi watafanya kikao kingine cha mazungumzo ya pande mbili wakinywa chai. Pia kutakuwa na chakula cha mchana kabla ya Rais Trump kuagwa rasmi katika uwanja wa ndege.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Iran yaonya UAE baada ya taarifa za ziara ya siri ya Netanyahu

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameibua hisia kali kufuatia taarifa za ziara ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, nchini United Arab Emirates, akisema hatua hiyo ilikuwa tayari imefahamika na vyombo vya usalama vya Iran muda mrefu uliopita.

    “Netanyahu sasa ameweka hadharani kile ambacho taasisi za usalama za Iran zilikuwa tayari zimewasilisha kwa viongozi wetu,” Araqchi amesema.

    Katika kauli kali zinazoonekana kuelekezwa kwa UAE na mataifa mengine ya Ghuba, Araqchi amesema:

    “Uadui dhidi ya taifa kubwa la Iran ni kamari ya kipumbavu, na ushirikiano au njama na Israel katika mwelekeo huo hauwezi kusameheka. Wale wanaoshiriki kushirikiana na Israel kuleta mgawanyiko wanapaswa kuwajibishwa.”

    Kauli hiyo imekuja wakati taarifa kuhusu ziara ya siri ya Netanyahu nchini UAE wakati wa vita dhidi ya Iran zikiendelea kuzua mjadala mkubwa wa kimataifa.

    Katika siku za hivi karibuni pia, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti madai kuhusu mashambulizi ya siri ya kijeshi yaliyofanywa na UAE pamoja na Saudi Arabia dhidi ya Iran, taarifa ambazo zimevuta uangalizi mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Soma zaidi:

  17. UAE na Israel zatofautiana kuhusu ziara ya siri ya Netanyahu nchini humo

    UAE imekanusha taarifa zinazoeleza kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alifanya ziara ya siri nchini humo wakati wa vita kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE, serikali hiyo ilisema: “Umoja wa Falme za Kiarabu unakanusha taarifa zilizochapishwa kuhusu ziara ya Waziri Mkuu wa Israel au kupokea ujumbe wa kijeshi wa Israel.”

    Wizara hiyo iliongeza kuwa uhusiano kati ya UAE na Israel uko wazi na unategemea makubaliano ya Abraham Accords, hivyo ziara zote rasmi na mikutano hutangazwa hadharani na kufanyika kwa uwazi.

    Kauli hiyo imekuja baada ya vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa, vikiwemo Reuters na CBS News, kuripoti Jumatano kwa kunukuu Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel kwamba Netanyahu alifanya ziara ya siri nchini UAE wakati wa vita dhidi ya Iran na kukutana na Rais wa UAE Mohammed bin Zayed Al Nahyan.

    Awali, Ofisi ya Netanyahu ilikuwa imesema ziara hiyo iliashiria “hatua ya kihistoria” katika uhusiano kati ya Israel na UAE.

    Wakati huo huo, gazeti la Israel Hayom liliripoti kuwa Israel iliipatia UAE mfumo wa ulinzi wa anga wa Iron Dome wakati wa vita vya karibuni, madai yaliyonukuliwa kutoka kwa Mike Waltz ambaye alisema UAE ilionekana kutumia mfumo huo uliotolewa na Israel.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 14 mwezi Mei 2026.