Waziri mkuu
wa kwanza mwanamke nchini Bangladesh Khaleda Zia amefariki dunia akiwa na umri
wa miaka 80 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Zia alikuwa
mwanamke wa kwanza kuongoza serikali nchini Bangladesh mwaka 1991 baada ya
kukiongoza chama chake kupata ushindi katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia
nchini humo katika kipindi cha miaka 20.
Madaktari
walisema Jumatatu kuwa hali yake ilikuwa "mbaya sana."
Licha ya
afya yake mbaya, chama chake kilisema hapo awali kwamba Zia atagombea urais
katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Februari, uchaguzi wa kwanza tangu
mapinduzi yaliyosababisha kuondolewa madarakani kwa mpinzani wake Zia, Sheikh
Hasina.
Siasa za
Bangladesh kwa miongo kadhaa zilikuwa zikiogozwa na wanawake hao wawili.
"Kiongozi
wetu tunayempenda hayupo tena," Chama cha Kizalendo cha Bangladesh (BNP)
cha Zia kilitangaza kwenye mtandao wa Facebook siku ya Jumatatu.
Zia
alionekana hadharani kwa mara ya kwanza kama mke wa rais wa zamani wa
Bangladesh Ziaur Rahman. Lakini baada ya kuuawa kwake katika mapinduzi ya kijeshi ya
1981, Zia aliingia katika siasa na baadaye akapanda cheo na kuiongoza BNP.
Baada ya
muhula wa pili mwaka 1996 uliodumu kwa wiki chache tu, Zia alirudi katika
wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2001, akajiuzulu Oktoba 2006 kabla ya uchaguzi
mkuu.
Kazi yake ya
kisiasa ilikumbwa na madai ya ufisadi na ushindani wa kisiasa wa muda
mrefu na kiongozi wa Awami League, Sheikh Hasina, ambaye aliondolewa kutoka
wadhifa wa uwaziri mkuu mwaka jana.
Zia
alifungwa jela kwa ufisadi mwaka 2018, chini ya utawala wa Hasina.
Zia alikana kutenda makosa na akasema mashtaka hayo yalikuwa ya kisiasa.
Aliachiliwa
huru mwaka jana, muda mfupi baada ya maandamano makubwa ya kupinga serikali
nchini Bangladesh kumpindua Hasina, na kumlazimisha kukimbilia uhamishoni.
Chama cha
BNP kilisema mwezi Novemba kwamba Zia atafanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi
mkuu ujao.
Chama cha
BNP kinatazamia kurejea madarakani, na ikiwa hilo litatokea, mwana wa Zia,
Tarique Rahman, anatarajiwa kuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo.
Rahman,
mwenye umri wa miaka 60, amerejea Bangladesh wiki iliyopita tu baada ya
miaka 17 ya kuishi uhamishoni jijini London.
Zia alikuwa
hospitalini tangu mwezi uliopita, akipokea matibabu ya figo, ugonjwa wa moyo na
nimonia, miongoni mwa magonjwa mengine.