Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashambulizi ya Israel-Hezbollah yaanza tena
Hezbollah imerusha roketi zaidi kuelekea kaskazini mwa Israel, huku jeshi la Israel likifanya mashambulizi kusini mwa Lebanon.
Muhtasari
- Israel yasema shambulizi lake liliua wanachama 16 wa Hezbollah
- Moshi unaopaa wazidi kuongezeka kusini mwa Lebanon
- Vita vyapamba moto El Fasher
- Shambulizi la Israel kwenye shule ya Gaza laua 22 - Hamas
- Mshtuko nchini Lebanon: 'Je kuna mahali ambapo ni salama?,'
- Ndege yaelekezwa kwingine baada ya abiria kupata panya aliyehai kwenye chakula
- Kamanda mwingine mkuu aliuawa - Hezbollah
- Japan yaamuru watu kuhama makazi yao kutokana na tishio la mafuriko
- ‘Sitagombea urais 2026’- Jenerali Muhoozi Kainerugaba
- Mwanajeshi mtoro wa Marekani aliyekimbilia Korea kaskazini ahukumiwa
- Israel inachunguza wanajeshi wake waliopigwa picha wakirusha miili juu ya paa
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Israel yasema shambulizi lake liliua wanachama 16 wa Hezbollah
Jeshi la Israel limetoa taarifa kuhusu shambulio la jana kusini mwa Lebanon, likisema kuwa limewaua makamanda waandamizi 16 katika kikosi cha wasomi cha Hezbollah cha Radwan.
Katika kile inachoeleza kama "shambulizi sahihi", Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema lilimuua Ibrahim Aqil - mkuu wa operesheni na kamanda wa Radwan - na wanachama wengine 15 wa Hezbollah.
Kundi hilo lilikuwa likikutana huko Dahieh, ngome inayojulikana ya kundi linaloungwa mkono na Iran katika mji mkuu wa Lebanon, IDF inaongeza.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, msemaji wa IDF anaongeza kuwa 12 kati ya wale waliouawa katika shambulizi hilo huko Beirut walikuwa wanachama waandamizi wa kundi linaloungwa mkono na Iran "juu ya uongozi wa Hezbollah".
Moshi unaopaa wazidi kuongezeka kusini mwa Lebanon
Shirika la habari la Reuters limetoa picha zinazoonyesha moshi ukipaa juu ya eneo la Jabal Al Rihan kusini mwa Lebanon - karibu na mpaka na Israel.
Muda mfupi uliopita, tumekufahamisha kuhusu Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) likisema lilikuwa linashambulia tena maeneo lengwa ya Hezbollah nchini Lebanon.
Hezbollah inasema ilishambulia maeneo ya kijeshi kaskazini mwa Israel - AFP
Wakati huohuo, Hezbollah imesema imerusha makombora katika maeneo mawili ya kijeshi kaskazini mwa Israel, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
Katika taarifa tofauti, kulingana na AFP, kundi linaloungwa mkono na Iran limesema lilirusha "safu ya roketi za Katyusha" kwenye kambi mbili za Israel.
Vita vyapamba moto El Fasher
Mapigano yamepamba moto katika eneo la Darfur nchini Sudan ambako vikosi vya RSF vinaendelea na shambulio lao katika mji wa El Fasher – kufyetua makombora dhidi ya maeneo yenye watu.
Jeshi nalo limejibu kwa kuyashambulia maeneo yanayodhibitiwa na RSF kutoka angani.
Onyo linazidi kutolewa la uwezekano wa kuwepo mauaji ya kimbari iwapo mji huo utapoteza udhibiti.
Zaidi ya raia milioni kumi wamepoteza makazi yao huko Sudan tangu vita vizuke mnamo Aprili mwaka jana.
Mashahidi huko El fasher wanasema kombora la RSF limetua katika soko kuu la mji huo Ijumaa na kusababisha vifo vya angalau watu watatu na makumi wengine kujeruhiwa.
Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuiwa mauaji ya kimbari anasema RSF imekiuka mpaka wa ulinzi na wanashiriki mapambano makali.
Alice Wairimu Nderitu amesema hili limesababisha hofu miongoni mwa raia katika eneo hilo.
Soma zaidi:
Shambulizi la Israel kwenye shule ya Gaza laua 22 - Hamas
Shambulio la Israel laua watu 22 katika shule ya Gaza, yasema wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas
Shambulizi la anga la Israel katika shule moja kwenye mji wa Gaza limewauwa takriban Wapalestina 22, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema lililenga kituo cha komandi cha Hamas katika shule ya al-Falah, ambayo Israel ilisema kundi hilo la wanamgambo lilikuwa likikitumia "kupanga na kutekeleza mashambulizi ya kigaidi dhidi ya wanajeshi wa IDF na taifa la Israel".
Shule hiyo, iliyofungwa wakati wa vita, ilikuwa ni makazi ya watu waliohamishwa, wizara ya afya ilisema.
IDF imesema ilichukua hatua za kupunguza hatari ya kuwadhuru raia, ikiwa ni pamoja na kutumia silaha sahihi na ufuatiliaji wa angani, na ikashutumu Hamas kwa kutumia miundombinu ya kiraia.
Hamas imekanusha kutumia shule na maeneo mengine ya kiraia kwa madhumuni ya kijeshi.
Ofisi ya vyombo vya habari vya serikali inayoongozwa na Hamas ilisema watu waliouawa katika shambulizi la siku ya Jumamosi eneo la al-Zaytoun ni pamoja na watoto 13 - mmoja mtoto wa miezi mitatu - na wanawake sita.
Shirika la ulinzi wa raia la Gaza liliripoti idadi hiyo hiyo ya vifo na kuongeza kuwa mmoja wa wanawake hao alikuwa mjamzito.
Pia unaweza kusoma:
Mshtuko nchini Lebanon: 'Je kuna mahali ambapo ni salama?,'
Huko Dahieh, vitongoji vya kusini mwa Beirut, shughuli ya utafutaji na uokoaji inaendelea.
Watu bado wako kwenye mshutuko.
Familia chache zinazojulikana na wanahabari wa BBC kutoka Dahieh zilisema kwamba wote wamehamia "vitongoji salama" eneo jirani.
Kitongoji hicho chenye ngome nyingi kinadhibitiwa na Hezbollah, lakini sio watu wote wanaoishi Dahieh ni wafuasi wa Hezbollah au Washia.
"Vyombo vyote vya Habari vinakosa kuelewa hivi," rafiki yangu Nour, anayeishi huko, anasema.
Yeye ni wa upande wa Washia na anasema familia yake inajitambulisha kama watu wa mrengo wa kushoto na mambo ya kidunia.
Nour anafanya kazi katika shirika la kimataifa la kutoa misaada na aliagizwa kuondoka Dahieh na kuhamia kitongoji kingine baada ya shambulio la Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lililomuua kamanda mkuu wa Hezbollah Fuad Shukr tarehe 30 Julai.
Lakini dada na wazazi wake wazee walikataa kwenda naye wakati huo.
Sasa ameandikia BBC akisema kwamba hatimaye waliamua kuondoka na wanahamia anakoishi yeye.
"Lakini je, kuna mahali popote ambapo ni salama?," ananiuliza.
Swali ambalo sasa wengi huko Beirut na Lebanon wanauliza, baada ya kushuhudiwa kwa ndege zisizo na rubani na jeti zinazotembea juu ya anga.
Ndege yaelekezwa kwingine baada ya abiria kupata panya aliyehai kwenye chakula
Shirika la ndege la Scandinavia (SAS) limesema moja ya ndege zake iliyokuwa safarini ililazimika kutua kwa dharura baada ya panya kutoroka kwa haraka kutoka kwa mlo wa abiria ndani ya ndege siku ya Jumatano.
Ndege hiyo ilikuwa ikitoka mji mkuu wa Norway Oslo kuelekea Malaga nchini Uhispania na ililazimika kutua kwa dharura huko Copenhagen, Denmark.
Kutua huko kwa ghafla kulifuata taratibu za kampuni kwa sababu panya huyo alikuwa anahatarisha usalama, msemaji wa shirika la ndege Oystein Schmidt aliliambia shirika la habari la AFP.
Mashirika ya ndege huwa na sheria kali kuhusiana na panya kwenye ndege ili kuzuia nyaya za umeme kutafunwa.
"Hili ni jambo ambalo ni nadra sana kutokea," Bw Schmidt alisema.
Jarle Borrestad aliyeshuhudia kisa hicho, aliambia BBC News Channel katika video iliyorekodiwa kwamba panya huyo alitoroka kutoka kwenye sanduku la chakula ambalo mwanamke huyo aliketi karibu nalo.
Soma zaidi:
Kamanda mwingine mkuu aliuawa - Hezbollah yasema
Asubuhi ya leo, Hezbollah inasema kamanda wake mwingine mkuu aliuawa katika shambulio la Israel kwenye kitongoji cha Beirut hapo jana.
Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa Ahmed Wahbi alisimamia operesheni za kijeshi za vikosi vya Hezbollah vya Radwan kwa muda hadi mapema 2024.
Makamanda hao wakuu wa Hezbollah miongoni mwa 37 waliouawa katika shambulio la Israel huko Beirut
Hezbollah walithibitisha vifo vya Ibrahim Aqil na Ahmed Wahbi baada ya Israel kusema kuwa shambulio lililolenga vikosi vya Radwan pia liliwauwa "viongozi wengine".
Wizara ya afya ya Lebanon inasema idadi ya watu waliouawa katika shambulio la Israel huko Beirut siku ya Ijumaa imeongezeka hadi 37, wakiwemo watoto watatu.
Je! IDF imesema nini kuhusu shambulio la Ijumaa huko Beirut?
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema kuwa vikosi vyake "vilifanya shambulizi katika eneo lengwa huko Beirut".
IDF inasema kamanda mkuu wa Hezbollah Ibrahim Aqil alikuwa miongoni mwa waliouawa, pamoja na wapiganaji wengine "waandamizi" katika Kikosi cha Radwan cha kundi linaloungwa mkono na Iran - bila kuwataja.
Katika taarifa ya video, msemaji wake Daniel Hagari alisema watu hao walikuwa "wamekusanyika kwenye jengo la makazi" chini ya ardhi huko Dahiyah na kuwatumia raia wa Lebanon kama "ngao".
Soma zaidi:
Japan yaamuru watu kuhama makazi yao kutokana na tishio la mafuriko
Makumi ya maelfu ya watu katika miji minne katikati mwa Japani wameagizwa kuhama baada ya watabiri wa hali ya hewa kuonya kuhusu mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa.
Takriban watu 18,000 katika jiji la Wajima na wengine 12,000 huko Suzu wametakiwa kutafuta hifadhi katika mkoa wa Ishikawa, kisiwa cha Honshu.
Wakaazi wengine 16,000 katika wilaya ya Niigata na Yamagata kaskazini mwa Ishikawa pia wametakiwa kuhama, shirika la habari la AFP lilisema.
Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japani imetoa dharura ya mvua kubwa - kiwango cha juu zaidi cha tahadhari – katika sehemu za eneo hilo.
Shirika la utangazaji la umma la Japan NHK lilinukuu maafisa wa serikali wakisema mito 12 imevunja kingo zake.
NHK pia imepeperusha picha zinazoonyesha mtaa mzima wa Wajima ukiwa umezama chini ya maji.
Mito mitatu huko Ishikawa imefurika katika jamii za karibu, afisa wa eneo hilo aliambia shirika la habari la AFP.
‘Sitagombea urais 2026’- Jenerali Muhoozi Kainerugaba
Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi nchini Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museven ametangaza kwamba hatogombea katika uchaguzi wa rais wa 2026.
"Ningependa kutangaza kwamba sitakuwa kwenye uwaniaji uongozi wa uchaguzi wa 2026," Jenerali Muhoozi aliandika ujumbe huo kwenye mtandao wa X (ambao zamani ulijulikana kama Twitter).
"Mwenyezi Mungu ameniambia nizingatie masuala ya Jeshi lake kwanza. Kwa hivyo, ninamuunga mkono kikamilifu Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi ujao," aliongeza.
Katika ujumbe mwingine, alisisitiza ahadi yake ya kutumikia Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF).
Tangazo hilo linawadia wakati ambapo ushawishi wa Jenerali Muhoozi kama kiongozi wa kijeshi na mwasiasa unaendelea kuongezeka.
Muhoozi, Jeneral mwenye utata ambaye mara kwa mara amekuwa akiibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kauli zake, aliwahi kutoa tangazo katika ujumbe wake wa Twitter, akisema kuwa atagombea kiti cha urais mwaka 2026.
Kama nchi nyingine yeyote, uchaguzi wa mwaka 2026 nchini Uganda, unatarajiwa kuvutia pia wagombea wengine kuwania nafasi ya urais.
Pia unaweza kusoma:
Mwanajeshi mtoro wa Marekani aliyekimbilia Korea kaskazini ahukumiwa
Travis King, mwanajeshi wa Marekani aliyetoroka Korea kusini na kuingia Korea kaskazini mwaka jana 2023 kabla ya kurudishwa nyumbani – amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na kutimuliwa jeshini bila ya heshima.
Alikabiliwa na mashtaka yakiwemo kutoroka jeshini Julai 2023 na kumshambulia afisa wa jeshi.
Kutokana na kwamba tayari amekuwa kizuizini na kudhihirisha tabia nzuri, King mwenye umri wa miaka 24 alitoka akiwa huru, mawakili wake wameiambia BBC.
Alikiri mashtaka kwa makosa matano kati ya kumi na nne yaliowasilishwa dhidi yake katika kesi hiyo iliosikilizwa Ijumaa huko Fort Bliss, Texas. Mashtaka mengine yalitupiliwa mbali.
King alijiunga katika jeshi Januari 2021 na alikuwa Korea Kusini kama sehemu ya kitengo cha jeshi kilichokuwa kwenye mzunguko wakati alipovuka na kuingia Korea kaskazini.
King alimwambia jaji wa kijeshi Ltn Knl. Rick Mathew kwamba aliamua kutoroka jeshi la Marekani kwasababu hakuridhishwa na kazi na alikuwa akiwaza kutoroka kwa takriban mwaka mmoja kabla ya kuelekea Korea kaskazini.
King amekuwa raia wa kwanza wa Marekani kuzuiwa Korea kaskazini katika takriban miaka mitano.
Soma zaidi:
Israel inachunguza wanajeshi wake waliopigwa picha wakirusha miili kutoka juu ya paa
Jeshi la Israel limeanzisha uchunguzi baada ya wanajeshi wake kupigwa picha wakitupa miili ya Wapalestina watatu kutoka juu ya paa wakati wa uvamizi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Picha za tukio hilo, zilizopigwa katika mji wa kaskazini wa Qabatiya, karibu na Jenin, kisha zinaonekana kuonyesha tingatinga la kijeshi la Israel likichukua na kutoa miili hiyo.
Picha hizo zimesababisha hasira kubwa. Kikosi cha Ulinzi cha Israel (IDF) kilisema Ijumaa kuwa ni "tukio kubwa" ambalo "halikuendana" na maadili yake na kile kinachotarajiwa kutoka kwa vikosi vyake.
Maafisa wa eneo la Palestina wanasema kuwa takriban watu saba waliuawa na wanajeshi wa Israel huko Qabatiya siku ya Alhamisi.
Chini ya sheria za kimataifa, wanajeshi wanalazimika kuhakikisha kwamba miili, ikiwa ni pamoja na ya wapiganaji wa adui, inapewa heshima.
IDF ilisema ilifanya operesheni ya kukabiliana na ugaidi huko Qabatiya, ambapo wanamgambo wanne waliuawa katika "makabiliano ya risasi" na wengine watatu waliuawa baada ya shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye gari.
Mwandishi wa habari mjini Qabatiya aliambia BBC kuwa siku ya Alhamisi asubuhi wanajeshi wa Israel walikuwa wamezingira jengo moja mjini humo.
Alieleza jinsi watu wanne waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walipotoroka hadi kwenye paa na wanajeshi walenga shabaha.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 21/9/2024