Ghislaine Maxwell, mshirika na swahiba wa mfanyabiashara wa ngono aliyetiwa hatiani Jeffrey Epstein, aliwaambia maafisa wa Marekani kwamba “orodha ya wateja” inayozungumziwa sana haipo, kulingana na nakala ya mahojiano yake iliyowekwa wazi.
Katika mahojiano hayo ya Julai na Naibu Mwanasheria Mkuu Todd Blanche, Maxwell alisema kuwa hakujua chochote kuhusu vitisho vya kutumika kama “Msaliti” na hakushuhudia mwenendo wowote usiofaa kutoka kwa Rais Donald Trump au Rais wa zamani Bill Clinton.
Alizungumzia pia uhusiano wake na Epstein pamoja na Prince Andrew, na akaita madai kwamba alijihusisha na ngono na msichana mdogo nyumbani kwake kama jambo “lisilowezekana kabisa kufikirika.”
Maxwell anatafuta msamaha kutoka kwa Trump na ameshtumiwa kwa kudanganya maafisa.
Mahojiano hayo yalifanyika wakati serikali ya Trump ilikuwa chini ya shinikizo la kuendelea kufichua taarifa zaidi kuhusu Epstein ambaye Trump alikuwa na urafiki naye kabla ya urafiki wao kufa mwaka 2004, kwa mujibu wa rais huyo.
Muda mfupi baada ya mahojiano na Blanche ambaye hapo awali alikuwa wakili binafsi wa Trump Maxwell alihamishwa kutoka gereza la Florida hadi gereza jingine lenye ulinzi mdogo huko Texas. Haijajulikana ni kwa nini uhamisho huo ulifanyika.
Ikulu ya White House imesisitiza kwamba “hakuna upendeleo unaotolewa au kuzungumziwa” katika kesi ya Maxwell.
Kwa sasa, Maxwell anatumikia kifungo cha miaka 20 kwa makosa ya ulanguzi wa ngono, na ameomba Mahakama Kuu ya Marekani kufuta hukumu yake. Wakili wake amesema wangepokea kwa mikono miwili msamaha kutoka kwa rais.
Shinikizo pia limekuwa likiongezeka kutoka ndani ya chama cha Republican cha Trump kwa ajili ya uwazi zaidi kuhusu uchunguzi wa Epstein. Lakini rais amewashutumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kutumia kesi hiyo kuondoa umakini kutoka kwenye kile anachokiita mafanikio ya serikali yake.
Katika nakala za mahojiano zenye kurasa 300, baadhi zikiwa zimefichwa sehemu, Maxwell alisema kwamba ingawa anaamini Trump na Epstein walikuwa marafiki “katika mikusanyiko ya kijamii”, haoni kama walikuwa karibu sana.
Pia alisema hakumbuki Trump kutuma ujumbe wa heri za siku ya kuzaliwa kwa Epstein mnamo 2003, uliokuwa gumzo baada ya kuripotiwa na jarida la Wall Street Journal hivi karibuni.
Katika mahojiano hayo, Blanche pia alimuuliza Maxwell kuhusu “orodha ya wateja” yenye majina makubwa ambayo imekuwa kiini cha nadharia za njama kwa miaka ya hivi karibuni.
Maxwell aliulizwa kuhusu watu mashuhuri wengine, akiwemo Bill Gates, Elon Musk, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Ehud Barak, Waziri wa Afya na Huduma za Binadamu Robert F. Kennedy Jr, mwigizaji Kevin Spacey, mwanamitindo Naomi Campbell na Prince Andrew ambapo alikanusha kuwa ndiye aliyemtambulisha Andrew kwa Epstein.
Orodha ya marafiki wake mashuhuri imekuwa kitovu cha nadharia za njama, zikidaiwa kufichwa na “deep state” ili kulinda wahusika wakuu katika uhalifu wa Epstein.
Viongozi kadhaa wa serikali ya Trump akiwemo Mkurugenzi wa FBI Kash Patel na naibu mkurugenzi Dan Bongino waliwahi kurudia madai hayo zamani, ingawa sasa wameyakanusha.
“Hakuna orodha,” Maxwell alisema.