Elon Musk ananunua Twitter: Je jukwaa hilo litabadilika vipi?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Elon Musk amefikia makubaliano ya kununua mtandao wa Twitter kwa ahadi ya kupunguza udhibiti kwenye jukwaa, na kuzua maswali kuhusu mbinu yake itamaanisha kwa 'mitandao ya kijamii.'

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameibua wasiwasi kwamba kukosekana kwa usawa kunaweza kusababisha kuongezeka kwa matamshi ya chuki.

Watumiaji wengi wa mtandao wa Twitter pia wanauliza ikiwa hii inamaanisha kuwa akaunti zilizosimamishwa na kampuni zitaruhusiwa kurudishwa.

Mtu mashuhuri zaidi kusimamishwa kazi alikuwa Donald Trump.

Baada ya habari za mpango huo kutangazwa, mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliibua wasiwasi kuhusu matamshi ya chuki kwenye Twitter na uwezo ambao ungempa Bw Musk, ambaye anajieleza kuwa ''anayependelea uhuru wa kujieleza''.

Amekuwa akisema katika ukosoaji wake wa sera za jukwaa kuhusu kudhibiti maudhui, akisema kuwa Twitter inahitaji kuwa jukwaa la kweli la uhuru wa kujieleza.

Katika taarifa baada ya kufikia makubaliano hayo alielezea uhuru wa kujieleza kama ''msingi wa demokrasia inayofanya kazi.''

Katika mtandao wa Twitter, Shirika la Amnesty International lilisema: ''Tuna wasiwasi na hatua zozote ambazo Twitter inaweza kuchukua ili kukomesha utekelezwaji wa sera na mifumo iliyoundwa kulinda watumiaji.''

''Jambo la mwisho tunalohitaji ni Twitter ambayo inafumbia macho kwa makusudi matamshi ya jeuri na matusi dhidi ya watumiaji, hasa wale walioathiriwa zaidi, ikiwa ni pamoja na wanawake, watu wasio na mahusiano yanayokubalika katika jamii na wengine.''

Hata hivyo, Twitter haikujibu mara moja ombi la BBC la kutoa maoni yao kuhusu wasiwasi huo.

Je Trump atarudi?

Akaunti ya Donald Trump ilifutwa kabisa mwaka jana kufuatia ghasia za Januari 6 katika jengo la Capitol huko Washington.

Lakini hata ikiwa marufuku yake ya Twitter itabatilishwa, Bw Trump anasema hana mpango wa kurejea Twitter, badala yake ameamua kutumia jukwaa lake binafsi la, Truth Social.

''Siendi kwenye Twitter, nitabaki kwenye Ukweli,'' Bw Trump aliambia Fox News.

Aliongeza kuwa anaamini Bw Musk, ambaye alimwita ''mtu mwema'', ''ataboresha'' jukwaa la mtandao huo.

Wawakilishi wa Bw Trump hawakujibu mara moja ombi la BBC la kutaka maoni yao.

Ming-Chi Kuo, mchambuzi wa teknolojia katika kampuni ya usimamizi wa uwekezaji ya TF International Securities, aliambia BBC kwamba Bw Trump anaweza kuamua kurejea jukwaani iwapo atashiriki uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2024.

''Twitter bado ni chaguo bora kwake kuwa na sauti, ikiwa Twitter iko tayari kurejesha akaunti yake,'' Bw Kuo alisema.

''Siyo rahisi kujenga jukwaa lenye ushawishi zaidi kuliko Twitter kabla ya uchaguzi ujao wa urais.''

Je, watu wataondoka Twitter?

Bw Musk alisema anatumai kuwa hata wakosoaji wake wakuu watasalia jukwaani ''kwa sababu hiyo ndiyo maana ya uhuru wa kujieleza''.

Walakini, watumiaji wengine wametishia kuacha kutumia mtandao wa Twitter, wakati wengine tayari wameacha.

Muigizaji wa Uingereza Jameela Jamil, ambaye anajulikana zaidi kwa uhusika wake katika kipindi cha televisheni cha 'The Good Place', alisema anatarajia jukwaa hilo ''kuwa eneo lisilo na sheria zaidi, lenye chuki, chuki dhidi ya wageni, chuki kubwa na chuki dhidi ya wanawake''.

''Ningependa hii iwe... tweet yangu ya mwisho,'' Bi Jamil aliwaambia wafuasi wake milioni moja.

Wakati huo huo, Caroline Orr Bueno, mwanazuoni mtafiti wa katika Chuo Kikuu cha Maryland, alisema kuwa kwa sasa atakaa kwenye jukwaa la mtandao huo, ambapo ana wafuasi zaidi ya 450,000.

Bi Bueno alisema ''hatujui itakuwaje chini ya uongozi wa Elon Musk''.

''Tunachojua ni kwamba ikiwa watu wote wenye heshima wataondoka, itakuwa mbaya hapa tena kwa haraka sana,'' aliongeza.

Dan Ives, mchambuzi katika kampuni ya uwekezaji ya Wedbush Securities, aliiambia BBC kwamba anatarajia watumiaji wengi ''kuchukua mbinu ya kusubiri-na-kuona''.

''Sasa ni kuhusu kuwavutia watumiaji wapya na kuwakomesha waasi kwenye jukwaa,'' Bw Ives alisema.

Kutokuwa na uhakika kwa siku za usoni

Bodi ya wanachama 11 ya Twitter ilikubali kwa kauli moja ofa ya Bw Musk ya $44bn (£34.5bn).

Jack Dorsey, ambaye alianzisha mtandao wa Twitter na bado yuko kwenye bodi yake, alisema alikuwa na furaha jukwaa hilo ''litaendelea kuhudumia mazungumzo ya umma'', ingawa haamini ''mtu yeyote anafaa kumiliki au kuendesha mtandao wa Twitter.

''Inataka kuwa nzuri kwa umma katika kiwango cha itifaki, sio kampuni,'' Bw Dorsey alisema kwenye ujumbe wa Twitter Jumanne.

''Kutatua tatizo la kuwa kampuni hata hivyo, Elon ndiye suluhisho la pekee ninaloamini,'' Bw Dorsey aliongeza.

''Ninaamini dhamira yake ya kupanua mwanga wa fahamu.''

Mtendaji mkuu wa Twitter Parag Agrawal pia amehutubia wafanyakazi katika mkutano, ambapo alisema mustakabali wa kampuni hiyo haujulikani, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

''Makubaliano yanapofungwa, hatujui jukwaa litaelekea upande gani,'' inasemekana Bw Agrawal alisema.

Mwitikio wa wanasiasa

On Siku ya Jumatatu, msemaji wa Ikulu ya White House Jen Psaki aliwaambia waandishi wa habari kwamba Rais wa Marekani Joe Biden ''kwa muda mrefu amekuwa na wasiwasi kuhusu nguvu za mitandao mikubwa ya kijamii'', yeyote anayemiliki au kuendesha mtandao Twitter.

Seneta wa chama cha Democrat Elizabeth Warren alisema mpango huo ulikuwa ''hatari kwa demokrasia yetu'', huku akishinikiza kutozwa ushuru wa mali na ''sheria kali za kuwajibisha kampuni kubwa za teknolojia.''

Wakati huo huo, Seneta wa Republican Marsha Blackburn alifurahishwa na makubaliano hayo na kuyachukulia kama ''siku ya kutia moyo kwa uhuru wa kujieleza''.

Pia unaweza kutazama: