Waridi wa BBC : 'Picha zangu za utupu zilivyosambazwa mitandaoni'

Chanzo cha picha, Queenter Wambulwa
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Alipoanza mahusiano ya kimapenzi na aliyekuwa barafu ya moyo wake Queenter Wambulwa hakuona dalili za makovu makubwa ya baadaye ambayo mahusiano hayo yangeacha baada ya mapenzi hayo kufika mwisho wake.
Quenteer ambaye ni mkazi wa jiji la Mombasa nchini Kenya , amekuwa kwenye vyombo vya habari nchini Kenya akizungumza kuhusiana na jinsi aliyekuwa mpenzi wake alimgeuka na kuweka picha za utupu wake alizokuwa akimtumia wakati wako kwenye mahusiano .
Ni sehemu moja ya maisha yake iliyomvuta chini sana lakini pia alitumia uchungu wake katika kuwa mstari wa mbele kuzungumzia kuhusiana na magonjwa ya kiakili na jinsi ambavyo huathiri watu kutokana na sababu moja au nyengine.
Mahangaiko yalianzaje
Alipokuwa Chuo kikuu , uhusiano huo wa kimapenzi ulipofika kikomo , Quenteer allikiwa bado anapitia maumivu ya kuachwa na pia msongo wa kiakili.
"Wakati huo nilikuwa ninaishi na shangazi yangu , nilikuwa naendelea kupona katika maumivu ya Moyo, na pia kujikakamua kufanya kazi kwa bidii angalao kujenga jina langu "anasema Quenteer
Kwa hiyo alikuwa ameanza kujitokeza hadharani kuzungumzia umuhimu wa kuwa mwangalifu na afya ya kiakili hapo hapo chuo kikuu .Wakati huo alikuwa hata ameangaziwa kwenye gazeti moja nchini Kenya ambapo alizungumzia athari za afya ya kiakili , na harakati zake kama mwanamke kijana chuo kikuu.

Chanzo cha picha, Queenter Wambulwa
Kwa hiyo baada ya kuangaziwa kwenye vyombo ya habari, haikuchukua muda kwa maoni mengi kuanza kujitokeza, Quenteer anakumbuka alikuwa na simu ndogo tu ila alichambua hisia kutoka kwa simu hio . moja kati ya jumbe hizo nusura impe mshtuko wa moyo ,pamoja na kwamba alipokea simu nyingi watu wakimuuliza kuhusu picha za utupu hakuelewa hadi alipoyashuhudia, yalimpa tumbojoto alipoziona picha na Video zake akiwa uchi zikiwa katika mitandao tofauti .
Picha za utupu zasambaa
Kumbe kule kuonekana kwenye vyombo vya habari, kulikuwa chanzo cha masaibu mabaya yaliomfuata.
"Wakati nilipoangaziwa kwenye gazeti moja mnamo Novemba 2018, yule mpenzi wangu wa zamani alitoa video pamoja na Picha za maumbile yangu . Alizituma kwa wazazi wangu, kwa wenzangu na kikundi cha WhatsApp cha kanisa ambalo baba yangu alihudumu kama mzee wa kanisa. Baba yangu pia ni mkuu wa shule ya upili. Mama yangu ni mwanasiasa. Kwa hivyo tunatoka katika familia inayoheshimika sana na kuwa mzaliwa wa kwanza na binti pekee, ilisababisha vurumai kuu," Queentah anasema.
Mwanamke huyu anasema kwamba picha za utupu mikononi mwa aliyekuwa mpenzi wake , ni zile alikuwa anamtumia , kama njia ya kukoleza mahusiano, kando na hayo anasema kwamba walikuwa na mahusiano ya mbali .

Chanzo cha picha, Queenter Wambulwa
Kukubaliana na hali
Anaeleza kwamba uvujaji wa picha hizo za utupu wake zilimrejesha tena kwenye shimo lenye giza, na kumpa mawazo ya kujiua.
Alilia kwa uchungu asijue cha kufanya, aligundua kwamba picha hizo hizo zilikuwa zimevuja hadi kwenye mitandao ya Facebook .
Katika mtandao huo kulikuwa na eneo ambalo wengi wa watu kutoka kijiji chao walikuwa washirika, kumaanisha kwamba watu wengi walizitazama.
"Nilifahamu kwamba wengi katika kijiji changu walikuwa wameona picha hizo, wasiwasi wangu ulikuwa Je wazazi wangu wangesema nini ? Wangenifanyia nini kutokana na aibu hii"aliwaza Quenteer
Mrembo huyu alisema kwamba , hisia baada ya picha hizo kusambaa hasa kutoka kwa wazazi wake ziliwapa hofu, yaani anasema kwamba hakuamini kwamba angewahi kuwa na mdahalo kuhusu utupu wake, na hasa jinsi picha hizo zilipigwa na kuwa mikononi mwa mwanamume. ila alijikakamua na kueleza wazazi ukweli wote.
"Kwangu nilihisi kama nimewakosea sana, na kwamba hawastahili aibu niliyoizua. Ulikuwa wakati mgumu sana kwa Kweli."
Walimpa nafasi ya kujieleza japo ilikuwa ni hali ya aibu walivyomuoelewa.

Chanzo cha picha, Queenter Wambulwa
"Ilifedhehesha sana na pia iliniathiri kisaikolojia kwa sababu hatuwezi kamwe kurudisha video na picha Kwa hio na lazima niishi na ukweli huo. Kwa upande wa wazazi wangu waliniunga mkono na kunilinda, wakanirudisha kwa matibabu, na kunishawishi nizingatie masomo yangu. ," anasema Queentah.
Quenteer alilelewa katika familia iliyompenda sana , kando na kwamba wazazi walihimiza nidhamu na maswala ya kanisa ndio yalipewa kipaumbele. Anasema kwamba hata yeye na kaka zake hawakuwa na ruhusa ya kusikiliza au kuzitizama nyimbo za kimapenzi au zenye maadili ya dunia. Queenter anaongeza kwamba walikuwa 'watoto washamba' kwani hawakuwa na hata televisheni nyumbani na basi ulimwengu kwao ulikuwa mdogo sana na hawakuelewa kuhusiana na uovu mwingi uliopo.
Kutokana na hayo anasema ilikuwa rahisi kutekwa kimapenzi, kwani alikutana na mwanamume ambaye alimnunulia chochote alichokitamani, na hata simu ya mkononi, kifaa ambacho kwao kilikuwa marufuku. Kwa hio anaona uhuru alioupata ulilegeza maadili ya nyumbani
"Wajua Baba hakukubali niwe na simu. au hata kutembea nje ? Kwa hio nilipokutana na jamaa huyu alinionyesha ulimwengu, alikuwa ananipeleka sehemu zilizonipumbaza, hata alikuwa wa kwanza kunipeleka maduka makubwa makubwa(supermarket) . " Quenteer anasema.

Chanzo cha picha, Queenter Wambulwa
Ila anasema kwamba licha ya kuwa na mpenzi aliyependa, bado alikuwa ameona bendera nyekundu za mpenzi aliyekuwa na wapenzi wengine.na hatimaye mapenzi yao yalifika kikomo baada ya kumfumania. Baada ya mahusiano kuisha ndipo msongo wa mawazo ulipoanza na akawa anapambana na magonjwa ya kiakili .
Nyumbani changamoto zilikuweko, baba na mama pia walikabiliana na watu waliowahukumu kutokana na kusambaa kwa picha za binti wao . Kuna wale waliohoji ni wazazi ambao wanamlea mwana kwa njia zisizofaa. Kwa mwanadada huyu anasema kwamba kosa lake ilikuwa kuamini mpenzi wake hadi kiwango cha kumtumia picha za utupu wake. Anasema kwamba alihisi kusalitiwa.
"Licha ya kwamba nilimsamehe, sijasahau na kwa hio natumia kila nafasi kuzungumzia hali hii kama njia ya kuelimisha umma , ilikuwa salama mtu asitumie yeyote picha za ndani huenda siku moja zikavuja hata kwa bahati mbaya, ni muhimu kuwa na uangalifu "Quenteer alisema
Alirudi shuleni kusomea saikolojia na ushauri nasaha na alihitimu mwaka jana kama mwanasaikolojia aliyeidhinishwa kutoa huduma hasa kwa maswala yanayohusu afya ya kiakili , msongo wa mawazo na kadhalika.
Quenteer ni mwandishi wa vitabu viwiili , kitabu kimoja kinaangazia simulizi za jinsi ya kusambazwa kwa picha za utupu wake zilimpa aibu na kupelekea afya yake ya kiakili kuathirika, na pia jinsi alivyojinasua.
Kitabu Cha pili kinaangazia afya ya kiakili na jinsi ya kukabiliana na hali hio.
Sheria inasema nini kuhusu usambazaji wa picha za aibu ?
Sheria ya matumizi mabaya ya utandawazi na makosa ya mtandao ya mwaka 2018 nchini Kenya , inasema lengo kuu la Sheria hiyo ni kuweka masharti ya makosa yanayohusiana na mifumo ya kompyuta; kuwezesha ugunduzi, upigaji marufuku, uzuiaji kwa wakati unaofaa.
Sheria hiyo imefanya kuwa hatia kutuma picha fulani kwenye mtandao bila idhini inayokusudiwa kusababisha mfadhaiko wa kihisia unaojulikana kama 'Kisasi cha ponografia'. Huu ni ushiriki wa nyenzo za kibinafsi, za ngono, ama picha au video, za mtu mwingine bila ridhaa yake na kwa madhumuni ya kusababisha aibu au dhiki.
Picha hizo wakati mwingine huambatanishwa na maelezo ya binafsi kuhusu mhusika, ikijumuisha jina lao kamili, anwani na viungo vya wasifu wao wa mitandao ya kijamii.
Sheria chini ya kifungu cha 37 ambacho kinaunda kosa kinaeleza mengi kuhusu mtu akipatikana na hatia
Vile vile Ulimwenguni nchi mbali mbali kimataifa zina sheria kali kuhusiana na wahalifu wanaosambaza picha za utupu za watu bila idhini yao, hali kadhalika mikakati ya jinsi ya kuwasaidia waathiriwa wanaojipata wakiwa kwenye mitandao hasa afya yao ya kiakili .












