Freeman Mbowe:Nini maana ya kuachiwa kwa kiongozi wa upinzani Tanzania Freeman Mbowe?

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

KATIKA siku yake ya kwanza madarakani kama Rais wa Tanzania kufuatia kifo cha mtangulizi wake hayati John Magufuli Machi mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan, alikutana na orodha ya masuala ambayo yalielezwa na wasaidizi wake kama "miiba" kwenye utawala wake.

Mojawapo lilikuwa ni mgawanyiko uliopo baina ya Watanzania kutokana na tofauti za kisiasa zilizotokana na miaka mitano ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli. Hata hivyo, kitendo cha kukamatwa na kufunguliwa kesi dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, mwaka jana kulichafua taswira ya kisiasa ya utawala wa Samia ambao ulikuwa umeanza kuonekana nafuu kulinganisha na mtangulizi wake.

Wakati utawala wa Rais Samia ukielekea kutimiza mwaka jana mmoja madarakani, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) juzi iliamua kutoendelea na kesi hiyo na hivyo kumwachia huru mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro baada ya takribani siku 221 za kukaa jela kutokana na kushitakiwa kwa makosa yasiyo na dhamana.

Unaweza pia kusoma:

Kitendo cha Mbowe kukamatwa na kufunguliwa kesi - kwa namna zaidi ya moja, kulifanana na namna ilivyokuwa wakati wa Magufuli. Kwanza alikamatwa wakati akifanya shughuli za kisiasa ambazo zilianza kuonekana si halali wakati wa Magufuli, alifunguliwa kesi kwa makosa yasiyodhaminika na kwa muibu wa maoni ya baadhi ya raia, wachambuzi na wanaharakati kesi ilikuwa ikionekana kuwa ya kisiasa zaidi kuliko kisheria.

Mbowe tayari yuko uraiani na katika tukio ambalo halikutarajiwa na wengi na kushangaza hadi baadhi ya viongozi wenzake wa Chadema, ni kitendo cha Rais Samia kukutana ana kwa ana na Freeman Mbowe Ikulu Dar es salaam. Na walizungumza kuhusu umuhimu wa "kuaminiana baina ya viongozi wa kisiasa na kufanya siasa za kistaarabu".

Swali kubwa ambalo Watanzania na pengine wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wanajiuliza kwa sasa ni je nini maana ya hatua hii ya Mbowe kuachiwa? Na mkutano wake na Rais unamaana gani?

'Mfupa' umetemwa

Kwa vile suala la Mbowe lilichukuliwa kama mfupa kwenye utawala wa Rais Samia, kuachiwa kwake maana yake ni kuwa serikali imefanikiwa kuutema. Ilianza kama ibada kwa baadhi ya wana Chadema kwenda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kufuatilia mwendendo wa kesi hiyo na kisha taarifa zake kusambazwa mitandaoni na katika vyombo vya habari.

Kesi hiyo ilifuatiliwa kiasi kwamba wako maofisa ubalozi kutoka baadhi ya nchi za magharibi nao walikuwa wakionekana mahakamani kufuatilia kesi hiyo. Ni kesi ambayo haikuwa inaleta taswira njema kwa serikali wala kwa Rais Samia ambaye anajenga taswira yake kisiasa kama Rais mpenda demokrasia, haki na maendeleo ya watu wake.

Kutemwa kwa 'mfupa' kuna maana nyingi kwa Rais na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Muhimu ni kwamba sasa wapinzani wa serikali wataanza kujielekeza kukosoa masuala kwa kujenga hoja za masuala yanayowahusu watu na chama tawala kuwa na majibu kuhusu hoja hizo. Lakini maana nyingine ni kwamba kwa kukaa kwake jela, Mbowe sasa moja kwa moja anaonekana atakuwa mshindani wa Samia kisiasa.

Kihistoria, Tanzania haijawahi kutengeneza kiongozi mkubwa wa upinzani- wa aina ya Jomo Kenyatta wa Kenya au Nelson Mandela wa Afrika Kusini, baada ya kuwa ametoka jela. Wengi wa waliokaa jela wakiwa viongozi wakubwa walitoka jela au vizuizini wakiwa hawana tena nguvu au ushawishi waliokuwa nao awali. Mbowe ana bahati ya kuwa kiongozi wa kwanza wa ukubwa wake - kwa maana ya kiongozi mkuu wa chama cha upinzani kukaa jela katika nyakati za mitandao ya kijamii. Wafuasi wake hawakuwahi kuacha kupiga kelele za kumtetea na kufanya jina na ushawishi wake usipotee.

Hakuna shaka yoyote kwamba kitendo cha Mbowe kukaa jela kwa muda aliokaa kumemuongezea sifa kama kiongozi wa upinzani na kumuondolea nakisi ya kisiasa iliyokuwa daima ikitembea juu ya kichwa chake.

Mbowe ni mwanasiasa aliyekuwa na bahati mbaya ya kuonekana kila wakati kuna mwanachama mwenye sifa kumzidi wakati linapokuja suala la kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu. Mwaka 2005 aligombea urais kwa shinikizo ikijulikana asingeweza kumzidi aliyekuwa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba. Ulikuwa zaidi ni mkakati wa kukitangaza chama kupitia kampeni kuliko yeye kutaka kushinda.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Chadema ilimpitisha Dk. Wilbrod Slaa kuwa mgombea urais wake. Ndani ya Chadema, ilionekana kwamba Slaa ndiye aliyekuwa anafaa kwa nafasi hiyo kumzidi Mwenyekiti wake. Katika uchaguzi wa mwaka 2015, Chadema ilikuwa inaelekea kumpitisha Slaa kuwania tena nafasi hiyo kabla ya uamuzi mashuhuri wa 'kubadili gia angani' uliompa nafasi hiyo Edward Lowassa na kumtema Slaa.

Mwaka 2020, Chadema haikumpa Mbowe nafasi ya kuwania urais na badala yake ikaonekana Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, ndiye aliyekuwa na nafasi nzuri zaidi ya kumpa ushindani zaidi Magufuli. Lissu aliingia katika uchaguzi huo akiwa ametoka kuuguza majeraha ya risasi yaliyosababishwa na tukio la kutaka kumuua lilitokea Septemba mwaka 2017.

Katika siasa za Tanzania, si kawaida kwa Mwenyekiti wa chama kikubwa cha kisiasa kuachia mtu mwingine kuwania urais. Lakini wanachama wa Chadema hawakuona tatizo kwa Mwenyekiti wao kugombea kwa sababu mara zote ilionekana kuna mtu mwingine ana uwezo na ushawishi kumzidi Mwenyekiti. Na Mbowe mwenyewe mara zote akiwa mstari wa mbele kupiga kampeni za kumsaidia mgombea.

Kitendo cha Mbowe kukaa jela na hatimaye kutoka kunampa sifa ya "mteswa wa utawala (victim)" ambayo ni muhimu kwa upinzani katika siasa za nchi zinazoendelea. Lissu alikuwa na sifa hiyo mwaka 2020 na Mbowe hakuwa nayo. Mara baada ya matukio haya kwenye utawala wa Rais Samia, Mbowe hana tena nakisi hiyo na badala yake amebeba faida hiyo.

Jambo hili pia linaibua uwezekano wa kuwa na "mafahari wawili" - kwa maana ya Mbowe na Lissu, ndani ya zizi moja. Wawili hawa ni wanasiasa wenye haiba tofauti na mwelekeo tofauti kiitikadi ingawa wako ndani ya chama kimoja. Unaweza watofautisha kwa kusema, Mbowe ni mwerevu na mwanasiasa halisi huku Lissu akiwa mwenye ulimi mkali na mwanaharakati halisi. Chadema kinakwenda kuwa chama cha kwanza kikubwa cha kisiasa hapa nchini ambacho Mwenyekiti na Makamu wake wanaweza kujidai kuwa na ngome zao wenyewe ndani na nje ya chama.

Siasa za kistaarabu

Taarifa ya Ikulu haikufafanua kuhusu maana ya "siasa za kistaarabu" zilizokubaliwa kufanywa baina ya Mbowe na Samia. Lakini inafahamika kwamba Chadema imekuwa ikidai kuwepo kwa Katiba Mpya na mabadiliko mengine ya kisheria ili kuwepo kwa Uchaguzi Mkuu huru mwaka 2025.

Tayari Rais Samia ameteua timu inayohusisha viongozi wa serikali, asasi za kiraia, wasomi na viongozi wa vyama vya siasa kwa ajili ya kupendekeza mabadiliko yanayoweza kufanywa kuelekea mwaka 2025. Chadema iligomea mchakato huo lakini sasa kuna dalili ya kuingia kwa sababu ya mikutano ya hivi karibuni kati ya Rais Samia na viongozi wawili wakuu wa Chadema.

Kama Chadema itaingia katika mchakato huo, kutakuwa na nafasi ya kufanya siasa kupitia mikutano. Lakini, kama Chadema itaendelea na msimamo wake wa kutaka Katiba Mpya kwanza na kugomea uchaguzi ujao, subra italeta majibu kuhusu siasa zitakazofaa wakati huo.

Lakini kwa sasa, walau nchi imepumua na mfupa uliokuwa umekaa kooni kwa Rais Samia umeondolewa. Pasi na shaka yoyote, bila kujali chama washindani kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 sasa wanaweza kuanza jaramba. Chuma kimeanza kupata moto taratibu.