Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Almasi ya Bluu: Wizi uliotatiza uhusiano kati ya Saudia na Thailand kwa miaka 33
Saudi Arabia na Thailand zilifikia makubaliano ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati yao, zaidi ya miaka thelathini na tatu baada ya kuzuka kwa mgogoro wa "almasi ya bluu" kati ya nchi hizo mbili. Hadithi ya almasi hii ni ipi na sasa iko wapi ?
Mwanzo
Mnamo mwaka wa 1989, wakati mtunza bustani Kithai Kriangkray Techamong alipokuwa akifanya kazi katika kasri la mwanamfalme Faisal bin Fahd kama mlinzi, macho yake yaliangukia kiasi kikubwa cha vito vya thamani vilivyokuwa mikononi mwa mfalme huyo. Kwa hiyo alipanga kuiba baadhi yao, akifikiri kwamba mwanamfalme hatatambua.
Mtunza bustani alikuwa amepata imani ya wafanyakazi wa ikulu, akamwendea mlinzi wa ikulu ya Ufilipino huku akiingia na kukariri namba za siri wa kengele.
Alianza kuiba vito kwa awamu, wakati mtoto wa mfalme na familia yake walikuwa likizo nje ya Riyadh. Wanaporudi, wanagundua kwamba vito hivyo havipo, na kujua kwamba ni mtunza bustani aliyefanya hivyo.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulidorora kwa kasi kutokana na wadhifa wake Prince Faisal, kwani baba yake, Mfalme Fahd, alikuwa akichukua kiti cha ufalme wakati huo. Kesi hiyo imekuwa kama eneo la Bermuda Triangle, ikimeza mtu yeyote anayeikaribia.
Wizi
Mtunza bustani alifanikiwa kujipenyeza ndani ya vyumba vya kulala wakati wa kutokuwepo kwa wamiliki wake, na kuiba vito vya mapambo kwenye awamu, vyenye jumla ya kilo 90 za shanga, pete na bangili zilizotengenezwa kwa vito vya thamani, dhahabu na saa zilizojaa rubi na almasi.
Miongoni mwa vito vya thamani alivyoiba, kulikuwa na almasi ya bei ghali na adimu ya bluu yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 20.
Mtunza bustani huyo alituma bidhaa zilizoibwa kwa makundi nchini mwake kabla ya kuchukua kundi la mwisho na kukimbia nalo kutoka Saudi Arabia.
Haikupita muda mwanamfalme na familia yake kujua kwamba baadhi ya vito vyao vilikuwa vimepotea. Waliwasiliana na viongozi wa Thai, ambao waliahidi kutatua kesi hiyo haraka iwezekanavyo na kurudisha vito kwa mwanamfalme.
Kudanganywa
Lakini mwanamflame aligundua kuwa ni asilimia 20 tu ya vito vya thamani vilivyorudishwa kwake ndivyo vilikuwa vya kweli, vingine vilikuwa bandia.
Kwa miaka miwili, Thailand ilijaribu kudumisha uhusiano mzuri na Saudi Arabia, kwa hivyo iliendelea kuchunguza kesi hiyo, na afisa mashuhuri alishtakiwa kwa ubadhirifu wa vito kadhaa, na vilipatikana kutoka kwake na kurudishwa kwa mwanamflame mnamo 1991, lakini kiasi kilikuwa kidogo, na almasi ya bluu haikuwa miongoni mwa vito vilivyopatikana.
Kesi hiyo ilizidi kuwa ngumu, baada ya mke na mtoto wa sonara walionunua vito vilivyoibiwa kutoka kwa mtunza bustani kutishiwa na kutekwa nyara, na baadaye kukutwa wamekufa ndani ya gari lao.
Mauaji yote yaliyokuwa yanahusiana na kesi ya vito vya Prince Faisal yalihusishwa na mtu asiyejulikana, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa mfanyabiashara wa Saudia ambaye alikuwa akifanya uchunguzi maalum katika kesi hiyo, na wanadiplomasia wanne wa Saudia. Wataalamu walidokeza kuwa mauaji hayo yalifanywa na maafisa wakuu katika mamlaka hiyo.
Kesi hiyo iliamsha hasira ya Saudi Arabia, na ikachukua hatua za kidiplomasia dhidi ya Thailand, ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha ujumbe wake wa kidiplomasia hadi ngazi ya chini kabisa. Mamia ya maelfu ya wafanyakazi wa Thailand walipoteza kazi nchini Saudi Arabia, na kurejea nchini mwao. Saudi Arabia ilisitisha kwa muda kutoa visa kwa raia wa Thailand.
Wakati Wasaudia wakiendelea kutafuta vito vyao vilivyopotea, wake za maafisa wakuu wa Thailand walionekana kwenye hafla rasmi wakiwa wamevalia vito vipya vilivyofanana sana na vya mwanamfalme Faisal.
Bangkok: "Mtego wa Kifo"
Mji mkuu wa Thailand ulikuwa kama mtego wa kifo kwa kila mtu ambaye alichangia katika kutafuta ukweli, kwani wale wote waliojaribu kufikia ukweli na kufichua walengwa wa kweli wa vito vilivyoibwa waliuawa katika mazingira ya kutatanisha.
Wasaudi walisema kuwa maafisa wakuu wa Thailand walihusishwa na wizi na mauaji yaliyofuata ya wachunguzi. Kulikuwa na maoni yaliyokinzana kuhusu washukiwa wa mauaji hayo. Uchunguzi wa Marekani mwaka 2010 ulionyesha kuwa kundi la Hezbollah la Lebanon ndilo lililohusika na mauaji hayo nchini Thailand, lakini uchunguzi haukuweza kutatua suala hilo, na wezi na wauaji hawakujulikana.
Muhammad Saeed Khoja (mwanadiplomasia mashuhuri wa Saudi aliyekuwa akiishi Thailand) aliliambia gazeti la New York Times mwaka 1994: "Polisi hapa ni wakubwa kuliko serikali yenyewe. Ninahisi kwamba kama Mwislamu lazima nipigane na mapepo hapa."
Mnamo 2015, Saudi Arabia iliwafungulia mashtaka maafisa watano wakuu wa Thailand kwa kuhusika na wizi huo, lakini hawakushtakiwa kwa sababu ya kutokuwa na ushahidi wa kutosha.
Mkuu wa polisi wa Thailand, Saung Teraswat, alijumuishwa katika orodha ya washukiwa na akasema alibadilisha na kuzuia uchunguzi kwa kuweka shinikizo kwa sonara ambaye awali alikiri kwamba "maafisa wengi wa polisi waliovalia sare ni wezi".
Ilisemekana kuwa mke wa Tiraswat alionekana wakati akiwa amevalia mkufu wa almasi, ambao ulionekana kufahamu sana na wa mwana mfalme wa Saudia, lakini Tiraswat alikanusha kuwa mkufu huo ulikuwa sawa na mkufu uliopotea.
Kesi hiyo ilisababisha Thailand kupoteza takriban dola bilioni 10 kila mwaka kwa muda wa miaka 20 kutokana na marufuku ya Ufalme kwa wafanyakazi wa Thailand na kupungua kwa utalii wa Saudia nchini Thailand. Licha ya haya yote, hatima ya almasi ya bluu bado haijulikani.
Kukubali hatia
Mwizi huyo aliachiliwa baada ya kukaa gerezani kwa takriban miaka mitatu kati ya mitano, baada ya kusamehewa kwa tabia yake nzuri gerezani.
Alisema wakati huo akisikitika, "Nina hakika kwamba masaibu yangu yote yalisababishwa na laana ya vito vya mwana mfalme Faisal nilivyoiba, hivyo niliamua kuwa mtawa wa Kibudha maisha yangu yote na kukiri hatia yangu hadharani. "
Baada ya kuachiliwa, alichukua jina jipya linalomaanisha "mmiliki wa bendera ya almasi".