Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania: 'Hatujapokea taarifa za meli yenye taka za nyuklia'
Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa haina taarifa yoyote rasmi kuhusu meli ya mizigo iliyotia nanga Bandari ya Mombasa, Kenya ikiwa imebeba taka za nyuklia ambayo inaripotiwa kuwa ipo njiani kuelekea katika Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo ameiambia BBC kuwa Serikali haina taarifa za kushikiliwa kwa meli ya mizigo iliyobeba taka za nyuklia nchini Kenya ikitokea Mumbai, nchini India.
Alisema, "Hatujapokea taarifa zozote rasmi kuhusu meli hiyo, lakini nimeskia tu kwenye vyombo vya habari mbalimbali. Pia hatuna taarifa juu ya meli hiyo kuja nchini Tanzania.
Waziri huyo alisema kuwa kabla ya kitu chochote kuingizwa au kusafirishwa nje ya nchi ni lazima sheria zifuatwe na kwamba jambo lolote ambalo pengine ni hatari kwa maisha na mazingira ya Tanzania halitakubaliwa kuingia Tanzania.
Aliongeza kuwa Jeshi la Wanamaji la Tanzania limekuwa likifanya doria katika bahari ikiwa ni hatua za kuhakikisha nchi iko salama na kila kinachoingia nchini kinakuwa hakina madhara kwa wananchi na mazingira kwa ujumla.
"Meli zozote zinazotaka kutia nanga katika bandari za Tanzania lazima zizingatie sheria za nchi na hata zile zinazokatisha kwenye imaya yetu lazima zizingatie sheria zetu, " alisema.
Wakati huo huo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi nchini Tanzania imeeleza kuanza kufanya mawasiliano na mamlaka za Kenya kwa kwaajili ya kupata maelezo zaidi kuhusu suala hilo.
Katibu Mkuu Wizara hiyo, Gabriel Migire alisema kuwa wanafuatilia sakata hilo kwa kuwasiliana na mamlaka za Kenya kwa maelezo yoyote kuhusu suala hilo.
Vyombo vya habari vya Kenya juzi viliripoti kuwa meli hiyo ilitia nanga katika Bandari ya Mombasa, ikiwa imesheheni taka hatari za nyuklia ambazo zilipaswa kutupwa katika pwani ya Afrika Mashariki, na hivyo kuhatarisha afya za mamilioni ya watu katika eneo hilo.
Shehena iliyokuwemo kwenye meli ya MV Piraeus Voy ilikuwa na makufuli na vifaa vingine vya ujenzi, na ilizuiliwa baada ya Wizara ya Afya ya Kenya kutoa tahadhari kwamba ilikuwa imebeba nyenzo za mionzi.
Maofisa wanaochunguza suala hilo, walisema meli hiyo ilisafiri hadi Kenya ikitokea Mumbai, India na ilikuwa ikielekea nchini Tanzania.
Mamlaka ya Kudhibiti Nyuklia nchini Kenya (KNRA) juzi ilithibitisha kuwa meli hiyo ipo salama mjini Mombasa, baada ya wiki iliyopita Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliamuru izuiwe.
Mkurugenzi mkuu wa KNRA, Joseph Maina alisema mamlaka hiyo inaongoza ukaguzi na uhakiki wa kontena iliyo kwenye meli ya MV Piraeus Voy.