Ninaweza kujitunza nyumbani iwapo nitapata Covid?

Nitajitunza vipi baada ya kupata Covid?

Ninaweza kujitunza nyumbani iwapo nitapata Covid?

Ni lini inafaa kuondoka kwenye kiti au kitanda ?

Kwa hiyo mfano una Covid. Ni nini la kufanya sasa?

Bila shaka, kaa mbali na watu wengine ili kuepuka kuwaambukiza

Kuhusu hali yako, huu ndio ushauri unaotolewa na wataalamu:

Wafahamishe familia na marafiki

Usiumie kimya. Acha watu wajue kwamba una Covid. Wanaweza kusaidia kukupatia chakula kwenye mlango wako na kukujulia hali kufahamu unaendeleaje.

Katika nchi nyingi kuna watu wanaojitolea ambao wanaweza kukusaidia wakati umejitenga nyumbani, kwa kukuletea vitu kama bidhaa za mahitaji ya kila siku na kukuletea dawa.

Pumzika

Hata kwa aina mpya zaidi ya virusi kama vile Omicron na Delta, watu wengi huwa na dalili ndogo au hata huwa hawana dalili na wataweza kupona salama maambukizi wakiwa nyumbani.

Dalili kuu, linasema shirika la afya duniani(WHO) bado ni:

  • Kikohozi kipya, kinachoendelea
  • Viwango vya juu vya joto la mwili
  • Kupoteza au kubadilika kwa harufu au ladha

Lakini watafiti ambao wamekuwa wakikusanya mrejesho kutoka kwa maelfu ya watu kuhusu uzoefu wao wa Covid unaonyesha kuwa dalili kuu tano zinafanana na zile za mafua:

  • Kutoka na makamasi ya maji maji
  • Maumivu ya kichwa
  • mchoko (kiasi au mkubwa)
  • kupiga chafya
  • kuvimba kwa koo

Iwapo utahisi kuumwa vibaya, kuna mambo unayoweza kuyafanya ambayo yanaweza kukusaidia.

Pumzika sana, kunywa maji mengi na meza paracetamol au ibuprofen ili zikusaidie kujihisi vyema zaidi.

Kuhusu kikohozi, jaribu kulala upande at keti wima kuliko kuegamia nyuma.

Kaa wima, badala ya kulala, pia itakusaidia iwapo unahisi kutopumua vyema.

Unaweza pia kujaribu:

  • vuta pumzi taratibu kupitia pua na utoe pumzi kupitia mdomo, huku midomo ikiwa imekaribiana sawa na unavyofanya unapozima mshumaa
  • legeza mabega, ili yasiumie, inama mbele kidogo huku mikono yako ikiwa kwenye magoti
  • Punguza joto kiasi na uingize hewa safi ndani ya nyumba na mwili wako

Baadhi ya watu huenda wana kifaa au wanaweza kupenda kuwa na kifaa kinachoitwa pulse oximeter ambacho kinaweza kupima kiwango cha hewa ya Oksijeni katika damu.

Kinawekwa kwenye kidole na kinaweza kuwa kipimo kinachofaa sana kukuwezesha kujua , au hata kufuatilia joto lako la mwili kwa kutumia thermometer.

Viwango vya chini vya oksijeni katika damu yako inaweza kuwa dalili kwamba hali yako inakuwa mbaya zaidi.

Kipimo cha 95 au juu yake ni cha kawaida. Lakini kikishuka hadi 93 au 94 na kubakia hivyo kwa saa moja baadaye, wasiliana na daktari ili kupata ushauri . Iwapo ni chini ya 92 au chini yake nenda hospitali au ita gari la wagonwa likupeleke hospitali.

Fahamu ni lini unafaa kupata usaidizi

Iwapo unataka ushauri wa ziada , unaweza kupiga simu kwenye duka la dawa au kuwasiliana kwa njia ya mtandao na duka la dawa. Wavuti wa WHO pia unazo taarifa nyingi sana kuhusu Covid.

Baadhi ya watu wenye Covid wanahitaji usaidizi wa kimatibabu, ambao unaweza kuwa ni pamoja na kulazwa hospitalini.

Huduma za afya katika baadhi ya nchi hutoa pia tembe kwa baadhi ya wagonjwa waliomo hatarini, ambayo wanaweza kuimeza wakiwa nymbani ili kusaidia kupunguza hatari ya maambukizi na kuyazuwia yasiwe mabaya zaidi.

Pata ushauri kutoka kwa daktari wako iwapo:

  • Unahisi hali yako ya kiafya ikiendelea kuzorota au kupungukiwa na uwezo wa kupumua
  • Unapopata ugumu wa kupumua wakati umesimama au kutembea
  • Unapohisi mdhaifu, maumivu au mchovu
  • Unapotetemeka au kuhisi baridi mwilini kupita kiasi
  • Unapopoteza hamu ya kula
  • Kama huwezi kujihudumua-kwa mfano, kufanya kazi kama kufua nguo au kujivalisha au kujipikia chakula ni vigumu sana
  • Kama unaendelea kuhisi kuumwa baada ya wiki nne-hii inaweza kuwa ni Covid ya muda mrefu

Nenda hospitali mara moja, au ita gari la wagonjwa(ambilansi), iwapo:

  • Unahisi kukosa pumzi kabisa kiasi kwamba huwezi kutamka maneno ya sentensi fupi wakati umetulia
  • Kama uvutaji wako wa pumzi umekuwa mbaya zaidi ghafla
  • Kama unakohoa makohozi yenye damu
  • Kama unahisi baridi na kutoka jasho, na ngozi yako kuwa na muongekano chakavu
  • Iwapo mwili wako utatoka vipele vinavyoonekana kama vina damu ndani yake au kama unatoka damu chini ya ngozi ya mwili
  • Iwapo utaanguka au kuzimia
  • Kama utahisi mwenye hasira, kukanganyikiwa na kujihisi mwenye kizunguzungu
  • Iwapo umeshindwa kupata haja ndogo au unakwenda haja ndogo mara chache kuliko kawaida

Iwapo una wasi wasi kuhusu mtoto mchanga au mtoto mdogo, usichelewe kupata usaidizi. Iwapo wanahisi kuugua, wana hali mbaya, au unafikiria kuna kitu ambacho hakiko sawa, ita gari la wagonjwa.