Kwanini simu mbovu husafirishwa maelfu ya maili kutoka Afrika kwenda Ulaya?

Eric Arthur hana muda mwingi wa mambo anayopenda - hutumia wikendi nyingi akiendesha gari kote Ghana kukusanya simu za mkononi zilizoharibika.

Kutoka nyumbani kwake huko Cape Coast anaweza kutembea zaidi ya maili 100 (km 160) katika wikendi moja akitembelea maduka ya kutengeneza simu na mahali popote ambapo kuna vifaa vilivyoharibika.

Katika wikendi nzuri anaweza kukusanya simu mbovu 400.

Zaidi ya hayo, anasimamia timu ya mawakala sita wanaofanya kazi sawa katika maeneo mengine ya nchi, na kati yao wanatarajia kukusanya karibu simu 30,000 mwaka huu.

Bw Arthur na mawakala wake hulipa kiasi kidogo kwa wauzaji kwa kila simu, cedis za Ghana 2.5-2.7, au karibu senti 44 za Marekani.

Ingawa simu haziwezi kurekebishwa, wakati mwingine huwashawishi ili waweze kuziachia.

''Simu [mpya] ya Android inauzwa kama $150 na ninawapa chini ya $1 kwa kuipata Ingawa haitumiki tena, huwa wanasema: 'Lakini niliinunua kwa bei hii. Kwa nini nitoe kwa bei nafuu kama hiyo?'"

Joost de Kluijver, ambaye alianzisha kampuni ya Closing the Loop na Reinhardt Smith, anasema jibu ni rahisi.

Afrika bado haina mitambo ya kisasa ya kuyeyusha kupata kiasi kidogo cha madini ya thamani sana ambayo hutumika kutengeneza simu za mkononi.

"Kila kitu unachohitaji kuwa nacho katika kiwanda ambacho ni endelevu kifedha, hakipo,"anasema.

"Hakuna sheria,miundombinu na hakuna ufahamu kwa watumiaji. Matokeo yake,huna pesa za kufadhili ukusanyaji na urejelezaji ufaao."

Wakati huohuo takriban simu milioni 230 huuzwa barani Afrika kila mwaka.

Wakati hazihitajiki tena, nyingine huchukuliwa na tasnia isiyo rasmi ya kuchakata tena, lakini nyingi hutupwa.

Pia unaweza kusoma

Kwa mujibu wa Global E-waste Monitor, Afrika ilizalisha tani milioni 2.9 za taka za elektroniki mnamo 2019, ambayo ni 1% tu ndiyo iliyokusanywa na kusindikwa tena.

"Nchi za Kiafrika ni wataalam katika upanuzi wa mzunguko wa maisha, ukarabati na pia kwa kiasi fulani katika kuchakata tena. Kwa hivyo mawazo tayari yapo lakini zana zinazofaa hazipo, haswa kwa aina hii ya taka," anasema Bw de Kluijver.

Ili kulipia mkusanyiko wa simu barani Afrika, kampuni ya Closing the Loop hujishughulisha na makampuni na mashirika ambayo huilipa Closing the Loop karibu Euro 5 ($ 5.60; £ 4.20) kwa kila simu mpya wanayonunua au kukodisha kutoka kwa yeyote anayetoa teknolojia yao.

Kwa kila kifaa kipya cha mahali pa kazi, Closing the Loop hurejesha kiasi sawa cha taka za kielektroniki katika nchi ambazo hazina uwezo rasmi wa kuchakata tena.

Euro 5 kwa kila simu hugharamia ukusanyaji, usafirishaji na urejelezaji wa simu barani Afrika, pamoja na faida fulani kwa kampuni ya Closing the Loop.

Orodha inayokua ya wateja ni pamoja na serikali ya Uholanzi na kampuni ya huduma za kifedha, KPMG. Kwa wateja ni uwekezaji mdogo lakini una faida kubwa ya kimazingira.

Bw de Kluijver anakosoa baadhi ya juhudi za hivi karibuni za kuanzisha miradi ya kuchakata taka barani Afrika.

Anasema kuwa bila mipango endelevu ya kifedha na sheria inayotekelezwa itakuwa vigumu kupiga hatua.

Simone Andersson anafahamu vyema changamoto hizo. Yeye ndiye afisa mkuu wa biashara wa Waste Electrical and Electronic Equipment Center (WEEE) ambayo husafisha bidhaa hizi nchini Kenya.

Kenya haina mfumo wa kitaifa wa kuchakata taka unaoendeshwa na serikali, ni huduma ya kukusanya taka katika baadhi ya maeneo.

Wazo la Kituo cha WEEE lilitokana na Shirika la Computers For Schools Kenya, shirika lisilo la faida ambalo hutoa kompyuta zilizorekebishwa mashuleni.

Kazi yake na shule ilionesha kuwa kulikuwa na haja ya kukabiliana na taka za elektroniki zisizohitajika na mnamo 2012 kampuni ya kuchakata ilizinduliwa.

Mwaka huu, Kituo cha WEEE kinatarajia kukusanya tani 250 za taka za elektroniki, haswa kupitia mikataba na makampuni makubwa kama Total Energies na Absa.

Lakini hii ni sehemu ndogo tu ya makadirio ya tani 50,000 za taka za kielektroniki ambazo Kenya huzalisha kila mwaka.

Bi Andersson ana mipango kabambe ya kuweka vituo vya kukusanya bidhaa kote nchini ambapo watu wataweza kuviacha vifaa vyao vya kielektroniki visivyohitajika.

Anasema kuwa Wakenya wanafahamu zaidi matatizo ya kimazingira yanayosababishwa na taka za kielektroniki na wangependa kufanya jambo kuhusu hilo.

"Watu wengi wanafahamu sana matatizo ya jumla ya taka. Wengi wangependa kubadili njia zao, kama kungekuwa na baadhi ya miundombinu, kusaidia - tunataka kuwa sehemu ya kutatua hilo linapokuja suala la taka za kielektroniki," anasema.

Serikali ya Kenya inachukua baadhi ya hatua kusaidia: kuna mpango unaendelea wa kuanzishwa kwa sheria ya Uwajibikaji wa Mzalishaji (EPR), ambayo itawapa watayarishaji au waagizaji wa bidhaa za kielektroniki mzigo wa kifedha wa kuchakata tena.

"Tunaisukuma kwa sababu tunaona inahitajika katika nchi hii," anasema Bi Andersson. "Na pia tunataka Kenya iwe mfano mzuri kwa wengine barani Afrika.

"Kuwa na EPR kutasaidia kama tutaweka sheria. Labda si mara moja, lakini kwa uhakika itaweka mawazo tofauti kabisa na itakuwa na athari kubwa kwa malengo na miundo."

Timu ya Kituo cha WEEE ya mafundi 10 hupanga na kubomoa kwa uangalifu vifaa vya kielektroniki.

Baadhi ya metali - chuma na shaba - zinaweza kupatikana ndani ya nchi, lakini madini ya thamani kama dhahabu, platinum na paladium ambayo yamepachikwa kwenye mbao za saketi yanaweza kupatikana tu na makampuni maalum ya kuyeyusha huko Ulaya au Asia.

Siku moja Bi Andersson angependa kujenga kiwanda cha kuchakata nchini Kenya: "Tunapopanuka, bila shaka tunataka kuleta teknolojia hiyo barani Afrika.

Kwa nini tusiilete Afrika mashariki? Kwa nini tusifanye Kenya na Nairobi? Hiyo ni sehemu moja ya maono yetu."

Bw de Kluijver pia anatumai kuwa Closing the Loop itaweza kufadhili mitambo ya kuchakata na kuyeyusha vyuma barani Afrika, lakini hadi wakati huo, chaguo bora zaidi ni kusafirisha simu hadi Ulaya.

Huko Cape Coast nchini Ghana, Eric Arthur ameona maboresho katika utunzaji wa taka za kielektroniki katika miaka ya hivi karibuni, lakini anafikiri zaidi jitihada zinapaswa kufanywa. "Kwa elimu zaidi, ninaamini kwamba watu watakuja kupata uelewa kuhusu kutupa taka za kielektroniki," anasema.