Mfahamu Malcom X na sababu zilizomfanya awe maarufu?

Ni miaka 95 tangu Malcolm X azaliwe tarehe 19 Mei 1925.

Alikuwa manaharakati wa kisiasa na alifahamika zaidi kwa kazi yake ya uongozi katika asasi za harakati za kupigania haki nchini Marekani.

Lakini alikuwa nani? na kwanini alikuwa mtu muhimu kwa watu wengi?

Malcolm X ni nani?

Alizaliwa tarehe 19 mwezi Mei mwaka 1925 huko Nebraska, Marekani, Malcolm Stuart Little, alikuwa mtoto wa nne kati ya watoto nane.

Wakati alipokuwa mdogo Malcolm na familia yake walikabiliana na unyanyasaji wa kibaguzi kutoka kwenye kundi la Ku Klux Klan - hivyo iliwabidi wahamehame ili kuepuka ubaguzi na kudhuriwa na kundi hilo la kibaguzi .

Alipokuwa na miaka sita, baba yake aliuawa , huku wengi wakihisi kuwa alishambuliwa kwa sababu ya ubaguzi wa rangi.

Maisha aliyoishi akiwa mdogo ndio yalimuhamasisha kuingia katika harakati za kutetea haki.

Haki ya mtu katika jamii inaitwa haki ya raia.

Haki ya raia inajumuisha masuala ya haki ya uhuru, haki ya elimu, haki ya kupiga kura na hukumu iliyo ya haki.

Kwa muda mrefu nchini Marekani, Wamarekani wenye asili ya rangi nyeusi walikuwa wananyimwa haki ya raia.

Walilazimishwa kuwa watumwa, walikuwa wakinunuliwa na kuuzwa kwa fedha, kama ilivyo wanyama na bidhaa zinavyonunuliwa. Maisha ya utumwa yalikuwa magumu sana kuyatafakari sasa.

Watumwa wengi wallikuwa wanatishiwa na wamiliki wao wazungu na hawakuwa na haki yeyote. Wengi iliwabidi wabadili majina yao - mara nyingine kwa kutumia majina ya wanao wamiliki.

Ingawa biashara ya utumwa ilitokomezwa nchini Uingereza mwaka 1833, na Marekani mwaka 1865, bado watu weusi walikuwa hawapewi haki zao kwa usawa kwasababu ya sheria - au kanuni zilizokuwepo - ubaguzi bado uliwatenganisha watu weusi na watu weupe.

Unyanyasaji wa watu weusi au mtu yeyote ambaye alichukuliwa kuwa si mzungu , aliongoza harakati za haki za raia mwaka 1960s - wakati Wamarekani weusi walipoanza kupambania usawa. Walitaka kupata haki sawa na wazungu.

Maandamano makubwa ya makumi, mamia na maelfu ya watu, yaliweka shinikizo kwa serikali kubadili sheria zisizo za haki, zenye ubaguzi wa rangi.

Viongozi mashuhuri wa haki za kiraia wakati huo walikuwa pamoja na Martin Luther King Jr.

Malcolm X alishiriki vipi kutetea haki ya mtu mweusi?

Malcolm alitaka kupambania haki ya watu weusi kwa sababu ya ubaguzi ambao yeye na familia yake walipitia na kuteseka sana.

Alizungumza kwa hisia katika mikutano ya hadhara - mikusanyiko mikubwa - na matukio mengi ambayo watu wengi walikusanyika kusikiliza ujumbe wake.

Lakini ujumbe wake ulikuwa tofauti na ule wa Martin Luther King Jr. - mtu mwingine muhimu aliyepigania usawa wa watu weusi huko Marekani.

Tofauti na Martin Luther, ambaye alihimiza maandamano yasio na vurugu, Malcolm X alisema kwamba watu weusi wanapaswa kujilinda "kwa njia yoyote muhimu".

Na pia hakukubaliana na azma ya Martin Luther King Jr ya Marekani ambayo watu weusi na weupe wanaishi kwa pamoja - Malcolm hakuamini katika maono hayo na alitaka taifa tofauti kwa ajili ya watu weusi tu.

Malcolm X alipataje jina lake?

Malcolm X alikulia mazingira magumu na alihisi kuwa hakuwa na fursa yeyote.

Baba yake aliuawa alipokuwa mdogo na familia ya Malcolm haikuwa na pesa nyingi na akawa muhalifu.

Alipelekwa gerezani kwa kukamatwa na bidhaa za wizi.

Alipokuwa gerezani, kaka yake alimtumia barua kuhusu kikundi cha kisiasa na kidini alichojiunga nacho kiitwacho Nation of Islam.

Malcolm aliamua kujiunga pia, na akabadilisha jina lake kuwa Malcolm X ili kuashiria mabadiliko haya.

Watu walifikiri nini kuhusu hilo?

Taifa la Uislamu liliongozwa na mtu anayeitwa Eliya Muhammad. Washiriki wa Nation of Islam waliamini kwamba watu weusi walikuwa bora kuliko watu weupe.

Pia walifikiri kuwa Uislamu ndio dini ya kweli ya watu weusi.

Watu wengi walipata utata huu - baadhi ya watu walisema inaenda kinyume na wazo la usawa - ambalo walisema lilimaanisha kuwa lilikuwa linaenda kinyume na harakati za haki za kiraia pia.

Malcolm X alikutwa na nini?

Ilitokea tu, Malcolm aliliacha Taifa la Uislamu baada ya kutofautiana na baadhi ya washiriki wa hapo, lakini akabakia kuwa Muislamu.

Alifanya safari ya kwenda Mecca, mji mtakatifu zaidi wa Uislamu, na aliporudi alianza kufanya kazi na viongozi wengine wa haki za kiraia kama Martin Luther King Jr. juu ya njia za kupata haki sawa kwa amani.

Malcolm alitengeza maadui wengi ndani ya Taifa la Uislamu, na mnamo Februari 14, 1965 nyumba yake ilishambuliwa na kuchomwa moto.

Siku chache baadaye, alipoanza kutoa hotuba katika Jiji la New York, alipigwa risasi na kuuawa.

Urithi

Ubaguzi wa rangi uliisha Marekani kati ya miaka ya 1950 na 1960.

Mwaka 1964, Sheria ya Haki za Kiraia hatimaye zilifanikiwa kuweka sheria kwa umma za kutobaguana kutokana na misingi ya rangi, dini au taifa ulilotoka, atakayekiuka atakuwa amevunja sheria.

Umuhimu wa kubadilika kwa sheria hiyo ni kuzingatia mafanikio makubwa ya harakati za haki za raia za Malcolm X ambaye aliongoza vuguvugu hizo.

Vitabu vingi na filamu vimeandika kumuhusu ikiwemo filamu ambayo ilichaguliwa katika tuzo za Oscar- mwaka 1992 ambayo iliongozwa na Spike Lee, ambapo muigizaji maarufu wa Hollywood, Denzel Washington alicheza kama Malcolm X.