Raia wa Japan aliyevalia sare za mchekeshaji na kubeba kisu awajeruhi watu 17 katika treni mjini Tokyo Japan

Mtu mwenye umri wa miaka 24 aliyekuwa amevalia vazi la mchekeshaji amewashambulia abiria katika treni moja mjini Tokyo Jumapili jioni.

Zaidi ya watu 17 walijeruhiwa walipokuwa wakielekea katika sherehe za Haloween katika mji huo. Mashahidi wanasema mshukiwa alikuwa amevalia shati ya kijani na koti la zambarau.

Alimwaga mafuta fulani katika mojawapo ya mabehewa na kuwasha moto. Kanda ya video iliwaonesha abiria wakikimbia katika mabogi hayo ili kukwepa huku wengine wakilazimika kutoroka kupitia madirisha ya treni hiyo.

''Nilidhani ni kiroja tu cha Halloween, mmoja ya mashihidi aliambia gazeti la Yomiuri kuhusu shambulio hilo. Baadaye nikamuona mtu akitembea kuelekea tuliko, polepole akionesha kisu kirefu.

Shambulio hilo lilitokea mwendo wa saa mbili karibu na kituo cha reli cha Kokuryo katika makaazi ya magharibi mwa mji huo . Vyombo vya habari vinasema kwamba mtu huyo alikamatwa na maafisa wa polisi hapo kwa hapo.

Kulingana na chombo cha habari cha Kyodo, aliambia maafisa wa polisi alikuwa akimuigiza muigizaji vichekesho wa Batman Comics.

Joker ni mhalifu mkuu katika katuni na adui mkuu wa Batman. Filamu hiyo ya mwaka 2019 ya Joker, iliyoigizwa na mwigizaji Joaquin Phoenix, iliangazia tukio ambapo aliwashambulia wanaume kadhaa kwenye treni baada ya kunyanyaswa nao mara kwa mara. Ni wakati muhimu, unaoashiria mwanzo wa mabadiliko ya mhusika Joker.

Shirika la habari la NHK lilinukuu polisi wakisema kuwa mwanamume huyo alisema "alitaka kuua mtu tangu Juni" kwa sababu alikuwa ameacha kazi na kuwaona marafiki zake wengi wakisambaratika .

Iliongeza kuwa alivaa kama Joker kwa sababu "alimuenzi sana Joker".

Ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinasema kuwa mshukiwa aliambia mamlaka kuwa alitaka kuua watu ili ahukumiwe kifo.

Shirika la habari la AP, likinukuu Idara ya Zimamoto ya Tokyo, likisema watatu kati ya waliojeruhiwa walikuwa na majeraha mabaya. Vyombo vya habari vya eneo hilo vinaripoti mzee mmoja alikuwa amepoteza fahamu baada ya kuchomwa kisu katika shambulio hilo.

Video kutoka eneo la tukio inaonyesha abiria wakimtoroka mshambuliaji, wakijikwaa kupitia mlango unaounganisha mabehewa na kutoka kupitia madirisha baada ya treni hiyo kusimama kwa dharura.

Shunsuke Kimura, ambaye alirekodi moja ya video hizo, aliambia shirika la utangazaji la taifa la NHK kwamba tukio hilo lilikuwa "la kuogofya". "Milango ya treni ilifungwa na hatukujua kinachoendelea, na tukaruka kupitia madirishani," alisema.

Uhalifu wa kikatili ni nadra sana nchini Japani lakini kumekuwa na idadi ya mashambulizi ya visu ya hali ya juu katika miaka ya hivi karibuni.

Watu kumi walijeruhiwa na mtu aliyekuwa amebeba kisu kwenye treni nyingine huko Tokyo mwezi Agosti. Mnamo mwaka wa 2019, mwanamume mmoja alishambulia kundi la watoto wa shule waliokuwa wakisubiri basi huko Kawasaki, na kuua wawili na kuwajeruhi wengine 18.