Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afghanistan: Fahamu aina ya silaha wanazomiliki wapiganaji wa Taliban kutoka kwa serikali ya Marekani
Video iliyochapishwa hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha wapiganaji wa Taliban wakitazama kipande cha picha cha silaha ya Marekani (silaha za kijeshi) - helikopta ya Black Hawk - ilifanyiwa majaribio kwenye uwanja wa ndege wa Kandahar.
Ndege aina ya helikopta zenye mabapa manne zilikuwa tu zinaonekana kwenye barabara ya kupaa na kutua ndege, lakini hatua hiyo ilituma ujumbe kwa ulimwengu: Taliban hawakuwa tena kundi la wanajeshi wahuni na wachafu waliotumia bunduki za Kalashnikov kushambulia alori yaliyozeeka.
Mahali pengine, tangu kuanguka kwa Kabul mnamo 15 Agosti, kundi lenye msimamo mkali wa Kiislam, wapiganaji wa Taliban waekuwa wakipigwa picha wakionyesha silaha na magari yaliyotengenezwa na Marekani.
Baadhi yao walionekana wakiwa na vifaa kamili vya kupigana kwenye mitandao ya kijamii na hawangeweza kutofautishwa na vikosi vingine maalum kutoka ulimwenguni kote.
Hakukuonekana kama ilivyozoeleka na ndevu ndefu, mavazi ya jadi ya salwar kameez, na silaha za kutu.
Walichukua silaha hizo kutoka kwa wanajeshi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Kitaifa vya Afghanistan waliokuwa wanajisalimisha kutoka mji mmoja baada ya mwingine.
Wengine kwenye mitandao ya kijamii walisema hii ilifanya Taliban kuwa kundi pekee lenye msimamo mkali lenye jeshi la anga.
Je Taliban ina ndege ngapi?
Kikosi cha Anga cha Afghanistan kilikuwa kikiendesha ndege 167, pamoja na helikopta za kushambulia na ndege mwishoni mwa Juni, kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu Maalum wa Marekani wa Ujenzi wa Afghanistan (Sigar)
Lakini haijulikani ni ngapi kati ya hizo 167 zimechukuliwa na Taliban.
Picha za setilaiti za uwanja wa ndege wa Kandahar, zilizopewa BBC na Planet Labs, zinaonyesha ndege kadhaa za jeshi la Afghanistan zilizokuwa zimeegeshwa kwenye barabara ya ndege.
Picha kutoka siku sita baada ya mji kuchukuliwa na Taliban inaonyesha ndege tano - angalau helikopta mbili za MI-17, Hawks mbili nyeusi (UH-60) na helikopta ya tatu ambayo inaweza pia kuwa UH-60, kulingana na Angad Singh, mtaalam wa anga za jeshi huko Delhi.
Kwa upande mwingine, ndege 16 - pamoja na 'Black Hawks' tisa na helikopta mbili za MI-17 na ndege tano aina ya fixed-wing - zinaweza kuonekana kwenye picha nyingine ya setilaiti iliyochukuliwa mnamo Julai 16.
Inamaanisha kwamba baadhi ya ndege hizo zilikuwa ama zimesafirishwa nje ya nchi au kuhamishiwa kwenye vituo vingine vya kijeshi.
Taliban pia imekamata ndege tisa zilizokuwa zimesalia katikakambi ya jeshiya Afghanistan, pamoja na zile zilizokuwa Herat, Khost, Kunduz na Mazar-i-Sharif - lakini haijulikani ni ndege ngapi ambazo zimekamatwa kutoka hapo kwani picha za setilaiti hazipatikani kutoka viwanja hivyo vya ndege.
Wapiganaji wa Taliban na vyombo vya habari vya eneo wamekuwa wakionesha picha za ndege zilizochukuliwa na ndege zisizo na rubani kutoka viwanja hivyo vya ndege.
Tovuti zingine huru pia zimepata ndege kadhaa.
Lakini pia kuna maoni kwamba ndege zingine zilisafirishwa nje ya Afghanistan kabla ya kuangukia mikononi mwa wapiganaji waasi.
Uchambuzi wa picha za setilaiti zilizochukuliwa mnamo Agosti 16 kutoka uwanja wa ndege wa Termez wa Uzbekistan zinaonyesha helikopta zaidi ya dazeni mbili, pamoja na MI-17, MI-25, 'Black Hawks' na pia ndege kadhaa za A-29 na ndege ya C-208, kulingana na mtaalam wa masuala ya anga huko Delhi ambaye hakutaka kutajwa.
Wataalam wa jopo la ushauri juu ya usalama CSIS wanasema ndege hizi na helikopta zinaweza kuwa za Kikosi cha Anga cha Afghanistan.
Je! Taliban imerithi silaha gani nyingine?
Wakati kuna maswali juu ya nguvu ya anga ya Taliban, wataalam wanakubali kwamba wana uzoefu wa kushughulikia bunduki za kisasa, bunduki na magari ya kivita.
Na wapo wengi tu nchini Afghanistan.
Kati ya mwaka 2003 na mwaka 2016, Marekani ilipakua silaha nyingi za kijeshi kwa vikosi vya Afghanistan waliokuwa wanashirikiana katika vita, silaha hizo ikiwa ni pamoja na: bunduki 358,530 za aina tofauti tofauti, zaidi ya bunduki 64,000 za rashasha, mabomu 25,327 na (magari ya ardhi yote) 22,174, kulingana na Ripoti ya Uwajibikaji kwa Serikali ya Marekani.
Baada ya vikosi vya Nato kumaliza jukumu lao la mapigano mnamo mwaka 2014, jeshi la Afghanistan lilipewa jukumu la kuilinda nchi hiyo.
Ilipokuwa ikijitahidi kukabiliana na Taliban, Marekani ilitoa vifaa zaidi vya kupigana vilivyochukua nafasi ya silaha za zamani za kijeshi.
Ilitoa karibu bunduki 20,000 za M16 mnamo mwaka 2017 pekee.
Katika miaka iliyofuata, ilichangia angalau bunduki za M4 3,598 na magari ya kivita 3,012 miongoni mwa vifaa vingine kwa wanajeshi wa Afghanistan kati ya mwaka 2017 na mwaka 2021, kulingana na Sigar.
Jeshi la Afghanistan pia lilikuwa na magari yanayohama kwa urahisi kutoka sehemu moja hadi nyingine, ambayo yanatumika kusafirisha wanajeshi ndani ya kipindi kifupi. Magari haya ya ukubwa wa 4x4 yanaweza kutumika kubeba watu au vifaa.
Je! Taliban inaweza kufanya nini na ghala lake jipya la silaha?
Hiyo inategemea na walichopata.
Kukamata au kutwaa ndege inaweza kuwa rahisi kwa Taliban, lakini kuziendesha na kuzitunza itakuwa kibarua kigumu, anasema Dkt. Jonathan Schroden, mkurugenzi wa kikundi cha ushauri cha CNA na mshauri wa zamani wa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan.
Mara nyingi kuna sehemu za vifaa hivyo zinazohitaji kuhudumiwa na wakati mwingine kubadilishwa, na jeshi la anga hutegemea timu ya mafundi wanaofanya kazi kudumisha ubora wa kila ndege.
Ndege nyingi zilitunzwa na wakandarasi wa kibinafsi wa Marekani ambao walikuwa wameanza kuondoka hata kabla ya shambulio la Taliban kwenye miji na majimboni kuanza mnamo mwezi Agosti.
Jodi Vittori, profesa wa siasa na masuala ya usalama ulimwenguni katika Chuo Kikuu cha Georgetown na mkongwe wa jeshi la anga la Marekani ambaye aliwahi kuwa Afghanistan, anakubali kwamba Taliban wanakosa utaalam wa kuzifanya ndege hizi kufanya kazi.
"Kwa hivyo, hakuna hatari ya sasa hivi ya Taliban kutumia ndege hizi", anasema, akionesha ndege kuwa ndege hizo zingeweza kuondolewa baadhi ya vipuri kabla ya majeshi ya Afghanistan kujisalimisha."
Hata hivyo, Taliban watajaribu kulazimisha marubani wa zamani wa Afghanistan kuziendesha ndege hizi, anasema Jason Campbell, mtafiti wa Rand Corporation na mkurugenzi wa zamani wa Afghanistan katika Ofisi ya Waziri wa Ulinzi wa Sera wa Marekani.
"Watawatishia wao na familia zao. Kwa hivyo, wanaweza kuendesha baadhi ya ndege hizo angani, lakini matarajio yao ya muda mrefu yanaonekana kuwa kufifia."
Na Taliban wanaweza kuwa na uwezo wa kuendesha ndege aina ya MI-17 zilizotengenezwa na Urusi kama walivyokuwa nchini humo kwa miongo kadhaa.
Kwa ndege nyengine, wanaweza kutegemea huruma kutoka kwa nchi zingine zenye huruma katika matengenezo na mafunzo.
Silaha zingine zitakuwa rahisi zaidi kwa waasi kuzitumia.
Hata wanajeshi wa Taliban wanaotembea kwa miguu wanaonekana kufurahia vifaa na silaha walizokamata.
Kwa miaka mingi, vituo vya ukaguzi vilivyokamatwa na wanajeshi waliowanyanganya silaha kumekuwa chanzo cha wanamgambo hao kupata silaha hizo.
Aidha, kuna hofu kwamba silaha ndogo ndogo zinaweza kuanza kuonekana kwenye soko la magendo na kuchochea makundi mengine ya wanamgambo duniani.
Sio hatari inayoweza kujitokeza kwa haraka, lakini usambazaji wake unaweza kuenea katika miezi ijayo.
Jukumu la kukomesha hili ni kwa nchi jirani kama Pakistan, China na Urusi.
Umoja kati ya Taliban ni jambo lingine muhimu ambalo litakuwa na sehemu muhimu katika jinsi silaha hizi zinatumiwa.
Bi Vittori anasema kuna uwezekano kwamba vikundi vya ndani ya muungano wa Taliban vinaweza kuamua kuondoka, na kuondoka na silaha hizo.
Kwa hivyo, mengi yatategemea uongozi wa kundi hilo utakavyokuwa.