Manny Pacquiao: Kutoka Ulingo wa masumbwi mpaka siasa: Je atauweza ulingo wa Ikulu?

Manny Pacquiao, bingwa wa dunia mara nane na seneta nchini Philippines, anawaza urais na kipigo alichokipata jumamosi usiku dhidi ya Yordenis Ugás kutoka Cuba huko Las Vegas Marekani kunaweza kuongeza kasi ya safari yake ya kuwania urais wa nchi yake katika uchaguzi mkuu ujao.

Pacquiao, 42 amekuwa akijikita zaidi kwenye siasa katika miaka miwili iliyopita, kipigo alichokipata toka kwa Ugás huenda kukatoa ishara ya namna gani safari yake ya kuingia Ikulu itakua, ikiwa ni bondia wa kihistoria katika taifa hilo lenye uwekezaji mkubwa kwenye michezo na sanaaa hasa ya uigizaji.

"Kuzichapa ulingoni kama jambo la ziada tu," Monico Puentevella, msemaji wa Pacquiao katika masuala ya siasa, aliiambia Al Jazeera.

"Baada ya pambano hili la Las Vegas fight, atakuwa na pambano lake kubwa kuwahi kupigana katika maisha yake, hapo Mei mwakani".

Raia wa Philippines wanatarajia kupiga kura na kumchagua rais mpya wa taifa hilo mwezi Mei, 2022 kuchukua nafasi ya Rais mtata Rodrigo Duterte. Ingawa mwenyewe Pacquaio hajatoka hadharani na kusema anataka kuwania urais, lakini nia na dhamira yake hiyo imekuwa siri ya wazi kwa muda mrefu, kila mtu akimtaja na kumzungumzia kwamba anautaka uraia.

"Anajiandaa kugombea. Amekua akiitamani fursa hii kwa muda mrefu, anataka kwamba amaliza pambano lake hili na aanze harakati. Ameniambia niwaamaba wazi kwamba atawania urais," alisema Puentevella.

Je itakuwa kazi rahisi kwa Pacquiao kuingia Ikulu?

Pacquiao anajua anachokifanya, mpaka kufikia sasa amejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutimiza ndoto zake hizo. Disemba 2020 aliukwaa urais wa chama cha Rais Duterte, cha PDP-Laban, na anaonekana kuitumia fursa hiyo ingawa kwa muda mfupi kujiweka sawa kwenye uchaguzi ujayo. Na Bondia huyo anaonekana kama mtu muhimu kwenye siasa za nchi hiyo . Kuna wakati Duterte, alitoka hadharani na kusema bondia huyo anamuona kama "rais ajaye wa Philippines".

Duterte, kikatiba anaruhusiwa kuwania kipindi kimoja cha miaka 6, na inaelezwa huenda akakutana na mkono wa sheria atakapoachia madaraka, kutokana na tuhuma mbalimbali.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC) inamtuhumu Rais huyo kwa uhalifu dhidi ya binadamu, na kwamba mahakama hiyo huenda ikaamuru akamatwe. Watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakimpinga rais huyo hasa kupitia vita yake dhidi ya dawa za kulevya" , ambao pia wameeleza watamshitaki kwa tuhuma hizo hizo, mara tu baada ya kutoka madarakani na kukosa kinga ya kushitakiwa.

Kwa sababu hana uwezo wa kuwania awamu nyingine, Duterte alisema anataka kuwania umakamu wa rais, na kwa namna anavyoonekana angependa nafasi ya urais iende kwa mmoja wa watu wa familia yake na labda ikishindikana kwa watu wake wa karibu sana, ili kuendelea kuwa salama na tuhuma zinazomkabili akiamini atalindwa na rais.

"Rais anawasiwasi na mtu yeyote ambaye sio binti yake akiwania urais na kushinda, Rais anajua kwamba atashitakiwa kwenye mahakama ya ICC," alisema Puentevella.

Hofu hii huenda ikamnyima usingizi Pacquiao, anayeutaka urais na huenda ikawa ni kikwazo kikubwa , kwa sababu Ras Duterte ana nguvu kubwa na mbinu za kufanya analoweza ili jambo lake litimie.

"kwa sasa anataka kuhakikisha kuwa, haendi jela, kwa hivyo hakuna mtu wa kumsaidia hilo isipokuwa ni binti yake tu."

Kuondolewa nafasi ya Rais wa chama

Mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu, wajumbe wa PDP-Laban ambao wanamuunga mkono rais Rodrigo Duterte wameanza kumpigia chapuo binti wa rais huyo, Sara Duterte, kugombea urais wa chama hicho. Pacquiao akapinga wazo hilo, kwa sababu inaonekana Sara Duterte hakuwa mwanachama wa chama hicho.

"Tuwape nafasi watu wengine," Pacquiao alisema kwenye moja ya mahojiano yake na ABS-CBN News, hata hivyo hajathibitisha kwamba atawania tena urasi wa chama hicho ama la.

Katikati ya mwezi Julai, Pacquiao aliondoka nchini kwake na kwenda Hollywood, Marekani kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na pambano lake la usiku wa jumamosi alilopoteza dhidi ya Ugás. Akiwa huko, wanachama wa chama chake cha PDP-Laban 'maswahiba' wa rais Duterte walikusanyika nje ya jiji la Manila na kutangaza kwamba nafasi ya rais wa chama iko wazi, wakimuondoa Pacquiao kwenye nafasi hiyo. Pacquiao hata hivyo alisema mkutano huo haukuwa halali.

"Haya ni kama matumizi ya mabavu, wakati wanachama hao [wanaomuunga mkono Duterte] wakikutana kwenye hotel za kisasa, maelfu ya wanachama wanakutana nchi nzima, wengine mitaani, wengine chini ya miti, wengine kwenye viukumbi vidogo," anasema mtendaji mkuu wa chama hicho cha PDP-Laban Ron Munsayac, anayemuunga mkono Pacquiao.

"Tumeonyesha kwamba wanachama walio chini kabisa mashinani wapo na wananguvu, wanataka sauti zao kusikikia. wanabahati ya kuwa na kiongozi kama Manny Pacquiao ambaye anawapa nafasi ya kusikilizwa ndani ya chama," aliongeza.

Vyovyote itakavyokuwa ndani ya chama hicho, tayari Pacquiao ameshapoteza uungwani mkono na rais Duterte na hilo huenda likatingisha kampeni yake ya kwenda Ikulu.