Hakuna tena magauni na vipodozi kwa wanawake wa Afghanistan

Muda wa kusoma: Dakika 3

Kuwasili kwa Taliban huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, kuliamsha hofu kwa raia, hasa wanawake.

Pamoja na kurejeshwa kwa Taliban madarakani miaka 20 baadaye, wanawake nchini Afghanistan wana hofu ya kupoteza haki za kijamii na kiuchumi walizozishinda kwa miaka miwili hadi miaka kumi.

Taliban huweka tafsiri kali na ya kizuizi ya sheria ya Kiislamu ambayo inazuia sana haki za wanawake.

Haya ni baadhi ya mabadiliko ambayo tayari yameonekana huko Kabul dhidi ya wanawake katika siku za mwanzo za udhibiti wa Taliban.

Hakuna wanawake kwenye televisheni

Chaneli kuu za televisheni za Afghanistan zinaendelea kutangaza baada ya Taliban kuingia madarakani.

Hatahivyo, kuna tofauti kubwa, kama vile ukweli kwamba hakuna watangazaji wa kike tena kwenye vioo vya runinga kwa mujibu wa BBC Monitoring.

Inabainishwa pia kuwa kuna ongezeko kubwa la maoni mazuri na ukosoaji mdogo sana wa Taliban kwenye vituo kama vile runinga inayomilikiwa na serikali National Afghanistan TV na Tolo News ya binafsi, Ariana, Shamshad na 1TV.

Televisheni ya serikali, inayoendeshwa na Taliban tangu usiku wa Agosti 15, imekuwa ikitangaza vipindi vya kidini.

Kwa upande wake, gridi nyingi za Tolo News na 1TV imekuwa ikirudia vipindi vinavyorushwa Jumapili, labda kwa sababu ya ugumu kazini.

Hatahivyo, Saad Mohseni, mmiliki wa Moby Group, ambayo inahusisha Tolo TV na Tolo News TV, alisema kwenye tweet: "Ninaweza kukuhakikishia kuwa watu wetu wanaendelea vizuri na kwamba tumeendelea na matangazo yetu ambayo hayajakatika wakati ''huu wa mpito''.

Kikundi cha Moby ndio kitovu kikubwa zaidi cha burudani, habari na siasa nchini Afghanistan.

Pia, Shamshad TV, inayomilikiwa na msaidizi wa rais wa zamani, ilikuwa ikitangaza maudhui yanayounga mkono Taliban.

Katika kipindi kimoja, mwandishi wa idhaa hiyo aliwaonesha wakazi wa Kabul wakisherehekea kuwa kikundi hicho kitaleta usalama na umoja nchini.

Hakuna magauni, hakuna vipodozi

Kufuatia kusonga mbele kwa Taliban nchini Afghanistan, haki nyingi za kijamii na kiuchumi zilizopatikana katika kipindi cha miaka 20 iliyopita zilimalizika ghafla, raia kadhaa wa Afghanistan waliiambia BBC.

Na ripoti za kupunguzwa kwa uhuru wa wanawake zimekuwepo

"Kuna vizuizi vingi sasa. Wakati ninatoka nje, lazima nivae burqa (vazi linalofunika mwili wa mwanamke kikamilifu), kama ilivyoamriwa na Taliban, na mwanaume lazima aandamane nami," alisema Ishkamish mkunga.

Katika siku mbili za kwanza baada ya Taliban kuwasili Kabul, mitaa ya mji mkuu pia ilianza kuonesha dalili za mabadiliko haya kwa wanawake.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha kuwa madirisha yenye picha za wanawake wasio na ushungi, na vipodozi na nguo za sherehe zikichanwa au kufunikwa na rangi.

"Sijui mustakabali wetu ni upi "

Wanawake wengi huko Kabul wanahisi hofu na kukosa matumaini.

Binti mmoja - ambaye alipendelea kutojitambulisha - aliuelezea mji huo kuwa "kimya." Taliban wanatawala jiji hilo na kila mtu yuko nyumbani, aliiambia BBC.

"Nilikuwa na mipango mingi ya maisha yangu ya baadaye, lakini sasa siwezi kwenda kazini au chuo kikuu," akaongeza.

"Sijui hali yetu ya baadaye itakuwaje. Hii imenifanya nipoteze matumaini. Ninatafuta njia ya kutoka Afghanistan kwa sababu hakuna tumaini kwa wanawake."

Kwa upande wake, Aisha Ahmad, ambaye anasoma sayansi ya kompyuta katika Chuo Kikuu cha Kabul, aliishia kupigwa Jumapili na umati wa watu waliojaribu kupanda ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamid Karzai.

"Umati ulisukumwa na polisi, watoto na wanawake walikuwa chini, niliumia mikono, miguu na magoti," kijana huyo wa miaka 22 aliliambia shirika la habari la PA.

Baada ya kutoweza kupanda ndege, Ahmad aliuliza kwenye mitandao ya kijamii kwamba nchi mojawapo impe hifadhi ili aweze kumaliza masomo yake, ambayo haamini tena kuwa inawezekana.

"Nimepoteza tumaini na nadhani haitakuwa barabara rahisi," alisema. "Ninahisi kama niko kwenye handaki ... siwezi kuona taa yoyote angavu na sijui handaki lina urefu gani handaki," akaongeza.

Mahbouba Seraj, mwanaharakati wa haki za wanawake na watoto huko Kabul aliambia BBC kwamba haikuwa na faida kwa mtu yeyote ikiwa wanawake wote wataondoka nchini, na kuongeza kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na kufanya kazi na Taliban.

"Ikiwa wanawake wa Afghanistan, wale ambao wanahusika na wamekuwa wakifanya kazi, wangeweza kukaa mezani na kuzungumza na watu hawa, wangeweza kuwa werevu na kujua rasilimali ambazo wanazo kwa wanawake wa Afghanistan," alisema.

"Kwa sababu kabla ya hii, mbele ya Taliban, sio ulimwengu wala jamhuri yetu wenyewe waliona nguvu za wanawake wa Afghanistan."