Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ghasia za Afrika Kusini:Ndani ya wiki ya machafuko na uporaji jijini Durban
Wiki mbili baada ya Afrika Kusini kukumbwa na wimbi la ghasia na uporaji - matukio mabaya zaidi ya vurugu tangu ujio wa demokrasia mnamo 1994 - vizuizi vya muda mfupi na majaa ya takataka katika jiji la bandari la Durban vimeondolewa.
Lakini wanajeshi wanaendelea kufanya doria katika vitongoji vilivyoharibiwa na wiki ya machafuko ambayo iliwaacha watu zaidi ya 300 wakiwa wamekufa.
"Kila kitu kimeenda. Sina bima. Nina wasiwasi juu ya siku zijazo za Afrika Kusini. Nina wasiwasi juu ya maisha ya baadaye ya watoto wangu," alisema mjasiriamali Dawn Shabalala, ambaye maduka yake manne madogo yaliporwa - hadi bomba la maji na nyaya za umeme
Alikumbuka kutazama kwa hofu na kuchanganyikiwa wakati polisi wa eneo hilo waliozidiwa idadi na nguvu na waporaji - hawakujaribu kuzuia uharibifu.
"Ninaogopa inaweza kutokea tena. Lakini niende wapi? Nifanye nini? Nilikuwa na wafanyikazi 12 ambao sina uwezo wa kulipa. Serikali haikugundua jambo hili," alisema, akiwa amesimma ndani ya saluni yake iliporwa katika barabara ambayo kila duka liliporwa na kuteketezwa
Vurugu 'zilipangwa'
Akioka kwenye mkutano wa dharura na viongozi wa kitaifa na mkoa, waziri mkuu wa mkoa wa KwaZulu-Natal, Sihle Zikalala, alielezea hali hiyo kama "janga."
Bwana Zikalala hapo awali alikuwa amekosolewa kwa kupendekeza kwamba ili kutuliza hali hiyo, mamlaka inapaswa kumwachilia Rais wa zamani Jacob Zuma kutoka gerezani.
Ilikuwa kukamatwa kwa Zuma, kwa kosa la kukaidi korti, ambao ndio chanzo cha machafuko, na kusababisha madai kwamba washirika wake walikuwa wakitaka kuipindua demokrasia changa ya Afrika Kusini.
Lakini baadaye Bw Zikalala alibadilisha msimamo na kuanza kuegemea upande wa serikali akikiri kwamba vurugu katika mkoa wake na katika ngome ya uchumi ya Gauteng "zilianza kama lalama dhidi ya kukamatwa kwa Zuma , lakini baadaye likawa jambo lisilodhibitiwa".
"Ilianzishwa na kupangwa kwa makusudi… na ilikuwa na lengo la kudhoofisha serikali - uasi," Bw Zikalala aliongeza.
Ingawa "watu wengi, wengi hawafurahii juu ya kifungo cha [Zuma]," Bw Zikalala alisema, "mtu yeyote anayehusika katika kuchochea au kupanga au kuunga mkono usumbufu lazima akamatwe na kushtakiwa".
Inafanana na eneo la vita
Katika mojawapo ya vitongoji vilivyoathiriwa sana, Phoenix, wengi wanaoishi hapa ni watu wa asili ya India walionyesha wasiwasi wao kuwa mivutano ya kikabila na kwa msingi wa rangi ilikuwa imechochewa kwa makusudi na wale wanaofanya vurugu, na vikosi vya usalama vimeshindwa kulinda jamii.
"Ilikuwa kama eneo la vita. Ilikuwa kitu kilichopangwa. Kitu kibaya. Hawa walikuwa watu wenye mafunzo. Walikuwa wakijaribu kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hii. lilikuwa shambulio la moja kwa moja - kwa jamii ya Wahindi," alisema Marvin Govender , kutoka muungano wa wakaazi.
Lakini alionyesha kuridihika kwamba "jamii ziliishia kujilinda".
Hata hivyo, kumekuwa na tuhuma za kushambuliwa kwa watu kwa msingi wa rangi na hata mauaji.
Kuongeza wasiwasi juu ya suala hilo, Waziri wa Polisi wa Afrika Kusini Bheki Cele alitolea mfano kisa cha msichana mweusi ambaye alikuwa amesimamishwa kwenye kizuizi kisicho rasmi.
"Aliniambia kuwa aliposimamishwa na gari lake kukaguliwa kila mahali, magari mengine, yaliyokuwa yakiendeshwa na Wahindi, yalikuwa yakipita na hayakuzuiliwa. Alipelekwa kwenye mto uliokuwa karibu na, baada ya kushambuliwa, kulikuwa na mjadala kuhusu ikiwa lazima auawe au la. Gari lake pia liliteketezwa, "Bw Cele alisema.
Maandamano ya kumuunga mkono Zuma
Wahindi - ambao walifika kwanza Afrika Kusini mwishoni mwa miaka ya 1800 kama wafanyikazi wasio na dhamana - hufanya asilimia 2.6 ya idadi ya watu wa Afrika Kusini. Wengi wao wanaishi KwaZulu-Natal.
Katika kitongoji cha Wahindi katika mji wa Verulam, Nasreen Peerbhay alisema mumewe, Mohammed Rahoff Sathar, aliuawa katika kizuizi kisicho rasmi kilichowekwa kulinda jamii.
Picha za video kutoka eneo hilo, kwenye barabara kuu karibu na biashara ya familia hiyo, zilionyesha gari jekundu likiingia moja kwa moja kwenye umati.
"Kulikuwa na wavulana watano weusi ndani ya gari.
Aliendesha kwa mwendo wa kasi sana , akiwaangamiza wavulana wanane, watano walijeruhiwa vibaya. Mume wangu alikuwa miongoni mwa waliouawa. kilikuwa kitu kibaya sana.Maisha mengi yameangamizwa kwa siku chache, "alisema.
Katika mahakama ya karibu, askari na polisi walisaidia kutenganisha umati wa Wahindi na Waafrika wakiandamana kulalamikia kukamatwa kwa washukiwa kadhaa.
Thobile Mkhize, mfanyakazi wa ujenzi, alisimama katika umati mdogo wa waandamanaji, akiwa amevaa mashati yenye picha za Zuma, na akiimba nyimbo ambazo zilikuwa maarufu wakati wa mapambano dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi, ambao ulimalizika mnamo 1994 na kuibuka kwa African National Congress ( ANC) - wakati huo ikiongozwa na marehemu Nelson Mandela - kuingia madarakani.
"Hatuamini mahakama," Bi Mkhize alisema kwa kishindo huku akipata vigelegele vya kuunga mkono kauli hiyo nakufuatwa na kutajwa kama "Zuma!"
Kabla ya kufungwa, rais huyo wa zamani alikuwa akihoji mara kwa mara uadilifu wa majaji wakuu wa nchi hiyo, akiwashutumu kwa upendeleo wa kisiasa dhidi yake, na kusababisha Mahakama ya Katiba kumshtaki Zuma kwa kutaka "kuvuruga utawala wa sheria".
Umaskini walaumiwa kwa ghasia
Watu wengi katika jiji kuu la KwaZulu-Natal, Durban - walioshtushwa na kiwango cha machafuko - walionekana kusadikika kuwa sasa kutakuwa na kisasi dhidi ya Zuma na washirika wake ndani ya chama tawala cha ANC.
"Walishindwa. Hawakuharibu jamii. Ilikuwa njia ya kuhamasisha jamii kuwa na nguvu, na kutoka nchi zote tofauti," alisema Anthony Kirkwood, mkurugenzi wa wa mauzo katika eneo hilo
"Nadhani hilo ndilo jambo la busara zaidi ambalo tumeshuhudia."
Lakini Nkosentsha Shezi, mwanaharakati anayeongoza kundi jipya la uanaharakati linalofanya kazi kuunga mkono wito wa Bwana Zuma wa "mabadiliko makubwa ya uchumi", alisema hakuna ushahidi wa kumhusisha rais wa zamani na wafuasi wake na vurugu hizo, na akasema kuwa ni Waafrika Kusini weusi , waliozongwa na umaskini wa kimfumo, ambao walikuwa wahanga wa kweli.
"Watu wako tayari kutoa maisha yao kutetea maadili ambayo Rais wa zamani Jacob Zuma anasimamia. Hivi sio vita dhidi ya watu weupe. Hivi sio vita dhidi ya watu wa India. Ni juu ya kumaliza ubaguzi wa rangi wa kikoloni.
"Wengi walio weusi ... ambao walikwenda kwenye maduka makubwa na kila mahali kupora, hawana mikuki, hawakuwa na bunduki. Kwa kweli, wao ndio waliokua wahanga wa vita, wahasiriwa wa watu ambao wanawapiga risasi kwa kisingizio cha kulinda mali za kibinafsi , "alisema Bw Shezi.