Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jovenel Moise: Wanajeshi wa zamani wa Colombia walijua kuhusu njama ya kumuua rais wa Haiti
Rais wa Colombia Ivan Duque anasema kwamba baadhi ya washukiwa wa Colombia katika mauaji ya rais wa Haiti Jovenel Moise walikuwa na ufahamu kuhusu njama ya kumuua kiongozi huyo.
Bwana Moise alipigwa risasi hadi kufa wiki iliopita nyumbani kwake na mkewe akajeruhiwa.
Maafisa wa polisi wa Haiti wanasema kwamba kundi la mamluki lililowashirikisha wanajeshi wa zamani wa Colombia lilimuua bwana Moise.
Bwana Duque alisema kwamba wengi wa raia wa Colombia walidanganywa baada ya kuambiwa kwamba wangefanya kazi kama walinzi nchini Haiti.
Lakini kulikuwa na kundi dogo miongoni mwao ambalo lilikuwa na habari kuhusu operesheni hiyo , aliambia kituo cha redio.
Kati ya wanaume 28 waliodaiwa kuwa katika kundi lililomuua bwana Moise , wote isipokuwa wawili walikuwa raia wa Colombia huku wengine wawili wakiwa raia wa Marekani walio na mizizi yao nchini Haiti.
Idara ya ulinzi nchini Marekani imefichua kwamba baadhi ya raia hao wa Colombia walipokea mafunzo ya kijeshi nchini Marekani wakati wakiwa katika jeshi la Colombia.
Kitengo cha kukabiliana na dawa za kulevya DEA kiliambia chombo cha habari cha Reuters kwamba mmoja ya washukiwa hao raia wa Haiti mwenye mizizi yake Marekani alikuwa chanzo chake cha siri.
Maafisa wa Haiti wanasema kwamba washukiwa hao walijifanya kuwa mawakala wa DEA.
Katika kanda ya video iliochukuliwa muda mfupi kabla ya shambulio hilo nje ya makao ya rais, mtu mmoja alisikika akisema ''hii ni operesheni ya DEA, kila mtu alale chini!".
Polisi wa Haiti pia walimkamata daktari mmoja wa Haiti, Christian Emmanuel Sanon , ambaye walimtaja kuwa mshukiwa muhimu wa mauaji hayo.
Mkazi huyo wa Florida aliwasili nchini Haiti kupitia usafiri wa ndege ya kibinfasi mnamo mwezi Juni na maafisa wa polisi walisema kwamba walipata kofia ya DEA pamoja na silaha chini ya umiliki wake .
Uchunguzi wa gazeti la The New York Times unasema kwamba bwana Sanon na baadhi ya washukiwa wengine walikutana kuzungumzia kile ambacho kitafanyika Haiti wakati huu ambao bwana Moise hayupo tena madarakani.
Lakini mtu mmoja aliyekuwa katika mkutano huo aliambia NYT kwamba mauaji ya bwana Moise hayakujadiliwa.
Maafisa wa polisi bado wanawasaka wale wanaodaiwa kupanga njama hiyo.